Msomaji anauliza, 'Nilipenda pesa zake, naweza sasa kumpenda mwenyewe?'

Wapo watu hujikuta wameingia kwenye mahusiano na watu wasiowapenda kwa sababu kadha wa kadha. Katika makala haya, tunajaribu kuonesha kwamba kisaikolojia, upo uwezekano mkubwa wa watu hao kuingia kwenye mapenzi ya dhati na wenzi hao ikiwa mambo kadhaa yatafanyika. Ni mambo gani hayo?
__________________________________________________________________________
NIMEPATA swali zuri kutoka kwa msomaji wangu. Swali lenyewe linahusiana na maudhui ya makala yaliyopita. Hapa namnukuu:

“ Habari mwana saikolojia! Kwanza story ndefu. Nilikiwa nalipia vitu supermarket leo. Sasa huyo cashier akaniangalia mkononi (sijui ndio aliona pete?) akaniuliza, 'dada umeolewa?' Nkamwambia,  ndio! Ananiuliza, 'Eti waweza olewa na mtu humpendi kabisa baada ya muda ukampenda?' Nkamwambia, 'Ndio, labda ulichodhani umekuta sivyo or kilichokuwa kinazuia usimpende kimeisha au kilikuwa superficial.'

 Nilimjibu hivyo huku nikimshangaa (kwani) hanijui kwanini ananiuliza swali kama hilo? Then nkamuuliza, yamekukuta??? Akasema, 'Hapana. Rafiki yangu alikuwa na wachumba watatu na huyo aliyemuoa yeye alikuwa hampendi ila mamake ndio alikuwa anampenda. Kwanza ni mzee!'

Nkamuuliza so aliolewa na chaguo la mama? Akasema ndio. Kwa hiyo ndo amefika mwisho wa reli. Akacheka nkamtania, 'uzee mwisho Msata, mjini kila mtu bebi, kama una mshiko hamna uzee mjini.' Akacheka akasema kweli mumewe ana hela sana.

Swali linakuja nililoulizwa. Hivi unaweza kuolewa na mtu usiempenda then ukafa ukaoza later au ndo mtu anapenda mali?" Anamalizia swali lake.

Pesa zimekuwa sababu ya watu kuvalishana pete. Picha: Kwestro
Tafiti zinasemaje kuhusu mahusiano?

Kwanza nikushukuru sana msomaji wangu kwa kufuatilia mijadala ya blogu yetu na kutoa maoni yako. Ni jambo la faraja kuona mchango wako, naamini na wasomaji wengine wataiga mfano wako wa kuendeleza mijadala. Twende moja kwa moja kwenye swali lako.

Kama ambavyo wapenzi wanaopendana leo wanaweza kujikuta wakichukiana, ndivyo ambavyo wasiopendana leo wanavyoweza kujikuta wakiwa wapenzi wa dhati bila hata kutarajia. Nilieleza katika makala iliyopita kwamba uhusiano una tabia ya kuchipua katika mazingirayasiyotarajiwa. Ni kama nasibu fulani hivi.

Tulisema, na tunarudia, kwamba unapokuwa katika mazingira ya kuonana na mtu mara kwa mara, proximity, hatua kwa hatua hisia za kumpenda hujiumba. Na unaweza kujikuta, hata kama mwanzoni ulidhani hakufai, iwe kwa mwonekano au tabia, kadri unavyoonana naye, ndivyo unavyojikuta ukibadili mtazamo. Unajikuta ukianza kum-rate vizuri. Ndio maana tunawajua watu waliokuja kujikuta wakiwaoa watu ambao awali walikuwa wakiwaponda.

Tulitaja sababu kadhaa. Kubwa ni kwamba mbali ni hulka ya mwanadamu kupenda anachokijua  vizuri, vile vile inategemeana na namna huyo unayekutana naye anavyojibu matarajio yako ya kihisia. Akikupenda, ni vigumu kumchukia maana katika hali ya kawaida, binadamu hatuwezi kuvumilia kuwachukia  wanaotupenda. Akifanana na wewe mtazamo, ndivyo unavyozidi kuvutiwa nawe maana binadamu tunapenda watu wanaofanana na sisi. Akionesha kukuamini, ndivyo unavyoendelea kumpenda. Na kadhalika.

Unawezaje kumpenda anayekupenda?

Sasa katika mazingira ya kuolewa na mtu usiyempenda, iwe kwa kuwapendeza wengine, au kwa sababu zisizo za kuhisia kama fedha, bado kabisa inawezekana kujikuta ukimpenda. Lakini hiyo inategemeana na namna mtu huyo uliyejikuta unaishi naye anavyojitahidi kujibu mahitaji yako ya hisia. Unaweza kusoma hapa kujua hisia kuu za mwanamke ni zipi.

Kadhalika, nikukumbushe mjadala wetu kuhusu pembetatu ya mahusiano au mapenzi. Tulisema mahusiano yana ingredients zatu; hisia za kimapenzi, ukaribu na maamuzi.

Kwa uhusiano usioanza na mapenzi, maana yake ni kwamba kilichoanza hapo kwenye pembetatu yetu ni maamuzi, yaani ile basi tu mtu anaamua kuingia kwenye mahusiano na mtu asiyempenda. Ni kama ilivyokuwa enzi za wazee wetu kwamba binti anakamatwa na kujikuta anaishi na mtu asiyemtarajia. Baadae binti alijikuta akimpenda mtu huyo huyo aliyemkamata kwa nguvu. Hiyo ni kusema, maamuzi bila mapenzi yanaweza kabisa kuwa msingi wa ukaribu/intimacy ikiwa huyo uliyeoana naye bila mapenzi anayo jitihada ya kujibu mahitaji yakoya kihisia kama tulivyopata kueleza huko nyuma.

Kwa hiyo kadri anavyokufanya ujisikie kupendwa, ujisikie wa thamani, ndivyo hisia zinazokuvuta kwake na kujenga intimacy, ukaribu. Ukaribu ukiendelea, ndio msingi wa hisia za kimapenzi ambazo hapo awali hazikuwepo.

Ndio kusema, ikiwa umeolewa na mtu ambaye hukuwa na hisia za kimapenzi kwake, iwe kwa sababu ya kupenda fedha zake au umaarufu wake, au kulazimishwa, bado upo uwezekano mkubwa wa kujikuta ukimpenda kama naye, kwa nafasi yake, atakuwa na jitihada ya dhati ya kutambua na kujibu mahitaji yako.

Lakini asipoweza kulipa gharama za kujenga mahusiano na wewe, kama ilivyo kawaida ya wanaume wengi wababe wa ki-Swahili, inawezekana kabisa mahusiano hayo yakaendelea kuwa mechanical, yaani ndoa ikabaki kuwa arrangement ya kukuwezesha kupata fedha au mahitaji mengine yasiyo na uhusiano na mapenzi. Labda kama huyu aliyeolewa na asiyempenda ataamua kuwekeza vya kutosha na kumfanya mwanaume aone tofauti ya kihisia, tofauti itakayomvuta kumpenda kama anavyotarajia. 

Kwa ujumla mapenzi ni matokeo ya imani, mtazamo na tabia. Unachokifikiri ndicho unachokipata. Na wala sio matokeo ya kuonana na mtu sahihi kama wengi wanavyofikiri. Kumbe ukibadili mtazamo na imani unaweza kabisa kumpenda yeyote.

Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia