"Ningerudia ujana tena, kipaumbele changu kingekuwa familia!"

Re-living my life? " anauliza halafu anajijibu mwenyewe, "Ningebadili mtazamo wa tafsiri ya mafanikio. Mafanikio yangemaanisha ubora wa mahusiano yangu na familia yangu. Hivyo, ningewajibika zaidi kujenga na kuilea familia yangu kwa karibu. Ningetumia muda mwingi na wanangu na mke wangu. Ningepunguza ukali usio  na sababu kwa mke wangu na wanangu. Ningewafanya wanangu wajisikie kuwa na baba anayewaelewa na anayejua mahitaji yao. Ningepatikana zaidi. Ningemfanya mke wangu ajione ni kipaumbele cha maisha yangu.
 __________________________________________________________________________
NINACHOKIPENDA kwa rafiki yangu huyu, mzee aliyestaafu, ni uwazi na uwezo wa kutumia upungufu wake kama somo kwa wengine. Hana aibu kuyataja mapungufu yake wazi wazi. Ni mzee aliyeheshimika kwa mafanikio ya kimaisha. Safari hii kwa kuhisi ana muda wa kusema nami, nikamwuuliza, "Baba, kama ungepata fursa ya kuyaishi maisha yako upya kitu gani ungekifanya tofauti?"

"Kuyaishi maisha yangu upya?", alisita kidogo. Akatafakari na kisha akasema moja kwa moja bila kumumunya maneno, "Ningetumia muda mwingi zaidi na familia yangu". Suala nyeti. Nikastuka. Nikaona haya kuona machozi yalimlenga lenga machoni kwa mbali. Alijikaza na kutabasamu kwa kujilazimisha, akanyoosha maelezo, "Ningemtendea haki mke wangu na wanangu wanne".

 Alirekebisha miwani yake na kunitazama kwa kuniangalia machoni huenda akipima yanavyoniinga yale anayoyasema, kisha akaendelea kwa Kiingereza chake chenye lafudhi yake ya ki-Irishi, "Nilikuwa mjinga kipindi hicho ninaanzisha familia. Niliingia kwenye maisha ya ndoa nikiamini mimi ndiye mnufaika mkuu wa ndoa. Sikujua napaswa kuwekeza. Nilimdai mke wangu vingi kuliko nilivyowekeza. Hapa, bwana mdogo, ningepabadilisha."

"Nilikuwa busy sana kutafuta maisha enzi za ujana wangu. Nilitafuta pesa usiku na mchana. Nilisafiri huko na kule nikitafuta maisha. Wakati mwingine nilihamia nchi nyingine na kuwaacha wanangu na mke wangu peke yao nyumbani. Sikujali.  Niliamini familia yangu ilihitaji kutimiziwa mahitaji ya kiuchumi. Nilituma fedha nyingi nyumbani nikiamini hiyo ndiyo ilikuwa namna ya kuonesha upendo wangu kwao".

Nini maana ya mafanikio? Picha Na Khadija Atkinson
"Kimaisha tulifanikiwa. Si mbaya," anajigamba kwa dakika kadhaa na kutaja nchi alizowahi kufanya kazi, mashirika aliyowahi kuajiriwa, baada ya kuridhika, akaendelea, "Lakini nilishangaa namna ambavyo mke wangu alizidi kuwa mbali na mimi. Hatukuweza kuwasiliana vizuri.
Tuligombana mara nyingi na wakati mwingine mbele ya watoto. Nilimwona mke wangu kama mwanamke jeuri na mkaidi. Sikuwajibikia makosa yangu hata siku moja zaidi ya kumbebesha yeye lawama siku zote kila tulipogombana", anasimulia.

"Nilianza kukosa hamu ya kuwa nyumbani kukwepa matatizo. Nilijua tuna matatizo ingawa hadharani tuliigiza hali kuwa shwari. Kidogo kidogo nilianza ulevi kujiliwaza na kujisahalisha matatizo. Baadae tabia yangu ilianza kubadilika. Nikaanza kuwa na mahusiano na wanawake wengine. Nikapoteza interest na mke wangu nikalowea kwa nyumba ndogo. Uhusiano wetu ukabaki kulinda heshima ya wanetu ambao kwa kipindi hicho walikuwa watu wazima lakini hapakuwa na mahusiano yenye furaha tena".

"Ninapoangalia nyuma sijivunii maisha yangu ya ndoa. Sina ujasiri wa kuwakemea wengine ingawa kwa upande mwingine najua sina la kufanya. Kama ninge-rewind miaka, basi ningempenda zaidi mke wangu na kujali mahitaji yake mengine ukiachilia pesa na mali ambazo hazijasaidia. Ningejiepusha na wanawake wengine wote na kuhakikisha nalinda kiapo changu cha ndoa". anajiapiza kwa ujasiri.

Vipi kwa upande wa malezi ya watoto?

"Ningetumia muda zaidi na wanangu wanne. Sasa hivi wamekua, ni watu wazima wana maisha yao ambayo siwezi kuyaingilia lakini najua nilikosea kama baba aliyekuwa mbali na wanae hata wakati nilipoishi nao. Yupo mmoja wa kike naweza kusema yuko karibu na mimi. Nampenda. Lakini wengine sifurahii wanavyoishi na vile tunavyohusiana kama baba na wanae".

"Maisha yangu hayakuwa na ukaribu na watoto. Nilimwachia mama (mke wake) jukumu la kuwalea ingawa nae alikuwa na mengi ya kufanya kazini kwake. Watoto walinikosa katika sehemu kubwa ya maisha yao ya utoto. Sikuweza kujua wanafikiri nini, wanaendeleaje na kadhalika. Nilidhani kufanya hivyo ni kuwaingilia maisha yao. Lakini sasa najua sikutimiza vizuri wajibu wangu kama baba yao".

"Nilikosoa kuliko nilivyoelekeza. Nilikemea kuliko nilivyotambua. Nilikuwa baba mbinafsi. Matokeo yake? Watoto walianza kujenga ukuta na mimi. Hawakutaka kuwasiliana na mimi. Nilitamani kujua mambo yao binafsi lakini hawakunipa ushirikiano. Nilianza kuonekana kulazimisha mahusiano yasiyo kuwepo. Jambo hili lilinishangaza na kuniumiza sana kwa sababu, kwa kweli, niliamini niliwapa kila walichotaka. Lakini kinyume na matarajio yangu, ndiyo hivyo, walionesha hasira na dharau."

"Nilikasirika. Nikajikuta nakuwa mkali sana. Niliona hawanitendei haki. Niliwacharaza sana. Nilidhani mke wangu anahusika kuwachochea kunichukia, hivyo ndoa yetu iliendelea kwenda mrama. Nilifikiri anawatumia kama sehemu ya kujilipiza kisasi na matatizo yetu. Lakini sasa najua nilipata mshahara unaonistahili kwa ujinga wangu. Watoto walianza kuharibika. Mmoja alianza kuvuta bangi. Mwingine ana watoto wawili wa baba tofauti. Mwingine ana maisha yake mazuri tu lakini hatuelewani. Nimebahatisha mmoja wa kike".

"Re-living my life? " anauliza halafu anajijibu mwenyewe, "Ningebadili mtazamo wa tafsiri ya mafanikio. Mafanikio yangemaanisha ubora wa mahusiano yangu na familia yangu. Hivyo, ningewajibika zaidi kujenga na kuilea familia yangu kwa karibu. Ningetumia muda mwingi na wanangu na mke wangu. Ningepunguza ukali usio  na sababu kwa mke wangu na wanangu. Ningewafanya wanangu wajisikie kuwa na baba anayewaelewa na anayejua mahitaji yao. Ningepatikana zaidi. Ningemfanya mke wangu ajione ni kipaumbele cha maisha yangu. Hilo sikufanikiwa", alimaliza na masikini hakujua ningeyaandika haya niliyoyaandika.

christianbwaya@gmail.com

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Uislamu ulianza lini?

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)