Haiba ni nini?

Sipendi kutumia kiingereza kwa sababu kwanza ninadhani kiswahili kinanitosha kabisa kuelezea kile ninachotaka kusema. Hata hivyo najua pia matumizi ya kiswahili chetu hayajawa katika kiwango kile kilichokusudiwa. Kuna maneno mengi yasiyoeleweka vizuri katika kiswahili cha kitabuni. Moja wapo ya maneno hayo ni hili ninalolitumia leo hii. Haiba. Pengine niweke msisitizo kwa faida ya wale wasiolifahamu neno hili vizuri. Personality. Wengine wanasema maana ya hichi kinachoitwa personality ni utu kwa kiswahili. Ni bahati mbaya kwamba niliyakimbia masomo ya lugha siku nyingi. Ila nimejiridhisha kwamba haiba ndiyo tafsiri muafaka kabisa.

Haiba ni nini? Watu wengine watafikiria tunazungumzia mwonekano wa mtu kimavazi. Lakini haiba ni neno pana zaidi ya mwonekano wa mtu kwa nje. Haiba ni jumla ya tabia za mtu zinazotokana na kile anachofikiri, anachopenda, anavyojichukulia yeye mwenyewe, anavyowachukulia watu wengine na kadhalika. Haya yote hujenga mwonekano wa mtu unaopimika (tabia) kama vile anavyoongea na watu, anavyodhibiti hasira zake, anavyofanya maamuzi, anavyoweza kuwa mwaminifu, anavyoweza kutunza siri moyoni, anavyoweza kukabiliana na changamoto, anavyovaa na mambo kama hayo mengi mengi mengi.

Haiba hii tunayoizungumzia hujengwa na mambo mengi. Tunaweza kutaja kurithi kama sehemu muhimu ya utengenezaji wa haiba. Hapa tunazungumzia kemikali zinazoongoza mienendo ya mwili ama homoni (kwa kutohoa). Ujue wingi ama uchache wa homoni fulani huchangia kujengeka kwa tabia fulani. Pia mazingira alimokulia mtu, kwa maana ya watu na malezi aliyopata na kadhalika.

Vile vile ni vyema kujua kuwa haiba ya mtu hubadilika kuendana na umri. Kila umri unazo changamoto zake zinazoathiri haiba ya mtu husika. Haiba yangu nilipokuwa na umri wa miaka mitano siyo niliyokuwa nayo nikiwa na umri wa miaka kumi na mitano na siyo niliyo nayo hivi sasa. Kwa sababu haiba yangu inabadilika kwa umri. Nikioa haiba yangu pia itabadilika.

Na tunajua kuwa kila mtu hurithi kitu tofauti kutoka kwa wazazi wake. Maana hata ndugu wa damu wnaatofautiana uthirishwaji huu wa kibaolojia. Mazingira yanayomzunguka mtu nayo ndiyo usiseme. Tunatofautiana kupindukia. Ni kwa sababu hiyo tunaweza kusema kuwa haiba hutofautiana kati ya mtu na mtu.

Haiba ziko nyingi -tutaziangalia mbeleni- lakini ninachotaka kusema hapa ni kwamba tusithubutu kufanya majumuisho kwa kuwaweka watu katika makundi fulani ya jumla jumla ya kinadharia. Kwa mfano kusema kuwa wanawake wote wanatabia fulani, ama wanaume wote wanatabia fulani ni makosa ya kiufundi.

Sababu si kila mwanamke ana haiba inayofanana na mwanamke mwingine. Na pia haiba ya mwanamke huweza kubadilishwa kutokana na haiba ya mume aliyenaye. Yaani kama mwanamke huyo angeolewa na mwanamme mwenye haiba nyingine, mwanamke huyo huyo angekuwa na haiba nyingine kabisa.

Au niseme, tabia ya mwanamke wa ndoa fulani inatokana na jinsi haiba yake iliyoingiliana na ile ya mume wake. Mke huyo japo anaonekana kuwa na haiba isiyoridhisha katika ndoa B angeweza kuwa na haiba njema zaidi laiti kama angekuwa na ndoa C na mume mwingine kabisa.

Upo hapo? KUmbe kabla hujaamua kuishi na mtu, wapaswa kupima hata suala la haiba zetu wawili! Umuhimu wa haiba ndugu msomaji. Nitarudi kukudadavulia ei to zii.

Maoni

  1. Kaka,

    Kiswahili chako nimekipenda kwakweli unajitahidi sana.
    Pia nimepita hapa nimejifunza mengi sana.

    Kazi njema

    JibuFuta
  2. Kaka Mbilinyi karibu sana. Tena na tena. Kutembeleana ni utamaduni wa mwafrika. Au sio>

    JibuFuta
  3. safi sana ndugu bwaya.
    haiba ni bonge la matatizo tunayokutana nayo na mwishowe hujikataa na kutaka tuwe vinginevyo na wakati mwingine huishia kubaya.

    wengine huita ego kwa kiingereza na wengine huihusisha na tamaa, kiburi, majivuno, majigambo, uchoyo nk.

    blog hii ni nzuri kutembelea na sitosita kutembelea, kuisoma na kuacha maoni. ahasante

    JibuFuta
  4. Kamala karibu mno. Nafurahi kupata wageni wa maana kama wewe. Karibu tena na tena.

    JibuFuta
  5. Imenipa utata mkubwa na kunifanya niwe mwenye kukosa amani hapa na pale nikizani na kuamini kwamba bahati mbaya ipo na mimi kumbe nilikuwa nakosea sana, HAIBA sikuwa najua chochote kuhusu hili ,ahsante kaka umenifumbua macho, akili na mawazo, tupo pamoja

    JibuFuta
  6. ahsante kwa kutuelimisha ndugu

    JibuFuta
  7. Karibuni sana Zaituni na ndugu asiye na jina. Tunaelimishana kwa pamoja!

    JibuFuta
  8. Nimekusoma vizuri kaka. saikolojia ni moja wapo ya stadi nyingi zilizonitatiza nikiwa mdogo, lakini saizi naona nimeanza kupata mwanga. Moses toka dodoma

    JibuFuta
  9. Asante sana kwa Kiswahili na staili ulioitumia. Pia nimejifunza mengi hasa neno nilikuwa na myezi kama sio myaka nikijiuliza maana yake: Compatibility of personalities = Muingiliano wa haiba. Ao sio?

    JibuFuta
  10. nimeelewa mambo mengi na mazuri

    JibuFuta
  11. Safi sana

    JibuFuta
  12. Asante sana dokta.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging