Desturi Zetu Zilivyosaidia Malezi Bora ya Watoto -2


NIMEJARIBU kubainisha baadhi ya desturi zilizosaidia kukuza watoto wanaojitambua. Unaweza kusoma makala ya kwanza hapa. Kwa kuanzia, tuliona namna familia zilivyowajibika kumtunza mama aliyejifungua. Mtoto na mama walipata muda wa kutosha kujenga mahusiano ya karibu.

Ukaribu huu kati ya mama na mtoto haukuishia kwenye kipindi cha uzazi pekee. Hata baada ya mama kupata nguvu na kuendelea na shughuli nyingine za kawaida, bado mtoto aliendelea kuwa na nafasi muhimu kwenye ratiba za mama. Ilipolazimu, mama alifanya shughuli zake akiwa amembeba mwanae mgongoni. Kumbeba haikuwa na maana ya mama kujichosha bali kumwangalia mwanae kwa karibu.

Nyakati za jioni zilikuwa fursa ya wazazi na watoto kukaa pamoja. Watoto walikusanyika kusikiliza hadithi, methali na vitendawili. Desturi hii ilikuwa darasa muhimu lililokuza ufahamu wa mtoto na kumfunza kuhusu jamii yake na wajibu alionao kama sehemu ya jamii.

Sambamba na hayo, michezo ilikuwa sehemu muhimu ya maisha ya mtoto. Jamii iliheshimu hitaji la mtoto kucheza na wenzake. Katika michezo, watoto hawakutegemea vifaa vilivyotengenezwa tayari kwa matumizi kama ilivyo leo. Vifaa vingi vilitengenezwa kwa kutumia vitu vya kawaida vinavyopatikana kwenye mazingira yao.

Nakumbuka nilipokuwa mtoto, tulitumia maboksi na gundi za asili kutengeneza magari ya kuchezea. Tulicheza mpira kwa kutumia mpira uliotengenezwa kwa mchanganyiko wa nguo kuu kuu na makaratasi. Tuliruka kamba, tulichora kwa kumtumia mikaa na chokaa na bado tulifurahia michezo.

Watafiti wengi, akiwemo Christine Tamis-LeMonda, wanatuambia kwamba mtoto anapotengeneza vifaa vyake mwenyewe kwa ajili ya michezo au shughuli nyingine, anajenga uwezo mkubwa wa kufikiria na ubunifu.

Katika makala haya, tunaangalia desturi nyingine nne zinazoweza kutukumbusha wajibu wetu katika ulimwengu wa sasa.

Kushiriki kazi za mikono

Mtoto wa ki-Afrika alishiriki kazi za mikono tangu akiwa mdogo. Kazi zilikuwa sehemu ya maisha ya kila mtu katika familia. Mama, kwa mfano, alihakikisha watoto wanaanza kutumwa kufanya shughuli ndogo ndogo za nyumbani tangu kungali mapema. Watoto walifagia nyumba, waliosha vyombo, walikaa na wadogo zao. Baba naye aliwashirikisha watoto wa kiume kwenye majukumu ya kuchunga au kutafuta majani ya mifugo inayofugwa nyumbani.

Kufanya hivi haikumaanisha wazazi hawakuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo. Hapana. Lengo lilikuwa kuwafundisha watoto tabia ya uwajibikaji. Kupitia ushiriki wa kazi za mikono tangu wakiwa wadogo, watoto walijifunza ujuzi mwingi bila kutumia mtalaa rasmi.

Profesa Bame Nsamenang wa Cameroon, anatuambia utamaduni huu umeanza kufifia katika jamii nyingi za ki-Afrika. Wazazi wameanza kuwatenga watoto na kazi za ndani na kuwakabidhi watu wengine shughuli hizo. Matokeo yake watoto wengi wanakosa ujuzi wa maisha ya kawaida.

Familia tandaa

Jamii zetu zilithamini sana uhusiano na ukoo wa pande zote mbili. Wazazi, wajomba, akina shangazi, mama na baba wadogo, binamu, wapwa, bibi na babu walikuwa sehemu muhimu katika uhusiano wa familia.  Kufahamiana na kuitambua familia tandaa lilikuwa ni sharti la msingi kwa kila mtoto.

Wakati mwingine, kulikuwa na mwingiliano wa kimaisha baina ya familia na familia. Ndugu walisaidiana kwa shida na raha. Kadhalika, ndugu walitembeleana mara kwa mara. Binamu, kwa mfano, angeweza kwenda kuishi kwa baba mdogo, shangazi, bibi na babu kwa muda fulani. Shangazi, naye angeweza kufunga safari kwenda kuwaona ndugu wengine walioishi sehemu nyingine.

Mwingiliano huu ulisaidia kuimarisha mahusiano ya karibu katika jamii. Mtoto alishuhudia uhusiano wa namna hii na kuuchukulia kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku. Pia, ilimsaidia kuuelewa ukoo wake na hivyo alijitambua mapema.

Kwa bahati mbaya tumeanza kuipa mkono desturi hii ambayo imekuwa sehemu ya utambulisho wa jamii yetu kwa muda mrefu. Uhusiano na familia tandaa umeanza kufifia. Watoto wa siku hizi wananyimwa fursa ya kufahamiana kwa karibu na familia tandaa. Hawaoni wazazi wakitembeleana na ndugu wengine wa ukoo. Hawaoni mawasiliano ya karibu na ndugu wengine. Hali hii inawazoeza kuwa mbali na ndugu zao.

Mtoto alikuwa wa kijiji

Mbali na familia tandaa, malezi ya mtoto hayakuwa jukumu la familia pekee. Mtoto alikuwa mali ya jamii nzima. Kila mwanajamii alijiona ana wajibu katika malezi. Ushiriki huu wa kijiji chote katika malezi ulisaidia kurahisisha kazi ya kuchunga mwenendo wa watoto wanapokuwa mbali na nyumbani.

Mtoto aliyekwenda kutafuta kuni, kwa mfano, hakuwa na uhuru wa kufanya chochote alichotaka. Macho yaliyomtazama yalikuwa mengi. Ikiwa mtu angemwona mtoto anakosa nidhamu njiani, hakusubiri kuomba ruhusa ya wazazi wake kumwonya. Alijua mtoto ni mali ya kijiji kizima na jukumu la malezi ya watoto kijijini ni la kila mtu.

Imani hii, kwa kiasi kikubwa, ilisaidia kuwafanya watoto wawajibike kuonesha mwenendo mwema kwa kila mwanakijiji. Hapakuwa na fursa ya kukwepa adhabu kwa kile alichokifanya hata kama alikuwa mbali na wazazi wake.

Jando na unyago

Jamii zetu zilikuwa na mfumo rasmi wa mafundisho maalum kwa ajili ya watoto wanaopevuka kimwili. Balehe haikuachwa ipite hivi hivi. Watoto wa kiume, kwa mfano, wafanyiwa tohara iliyoambatana na utaratibu wa kuwafunza kuelewa nafasi yao kama wanaume wanaotegemewa na jamii.

Pia, katika jamii nyingine, kipindi cha tohara kilikuwa ni fursa ya kuwafundisha watoto wa kiume ujasiri. Mtoto alitakiwa kuthibitisha kuwa yeye ni mwanaume anayeweza kugemewa katika jamii.

Mtoto wa kike naye hakuachwa nyuma. Ingawa hatuungi utamaduni wa tohara kwa wanawake, kazi ya kumfundisha binti majukumu yake kama mwanamke anayejitambua ilikuwa muhimu. Katika kipindi cha mpito kuelekea utu uzima, msichana alisaidiwa kujua yeye  ni nani na jamii ina matarajio gani kwake.


Kwa ujumla destruri kama hii ilisaidia kuwaandaa vijana timamu, wanaojielewa na kufahamu wajibu walionao katika jamii. 

Maoni

  1. Ni kweli kabisa mwalimu wangu hili limekuwa tatizo kubwa kwa kizazi chetu ,nakumbuka nikiwa nyumbani kwetu kijijini niliwahi kuadhibiwa barabarani nikiwa darasa LA tatu kwa kutoroka shuleni na kuingia mtaani nikiamini wazazi hawataniona badala yake nilikutana na mwanakijiji mmoja akanihoji kidogo alipoona sina hoja alinitandika viboko na kunirejesha shuleni na kunikabidhi kwa mwalimu .
    Sitaweza kusahau tukio hilo ambalo nililiona kama LA ajabu kipindi hicho nashukuru umenikumbusha tena Leo .kwa kweli jamii yetu ilikuwa na uwajibikaji sana siuoni tena uwajibikaji kama huo kwa sasa, ubarikiwe sana mwalimu wangu

    JibuFuta
  2. Ahsante Sana Mr Christian Bwaya Hii Ni dhahiri kweli kutoshirikishwa kwa watoto katika kufanya mambo ya ubunifu kunarudisha Rate na mbinu za kujifunza maarifa Shukrani kwa kuielimisha jamii na Umma

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi