Kumsaidia Mtoto Asiyejiamini, 'Anayeogopa' Watu

PICHA: Blend Images

KUTOKUJIAMINI ni kutokuwa na ujasiri, kutokuwa na imani na uwezo wako mwenyewe. Mtu asiyejiamini anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya vitu. Tatizo lake ni kujishuku. Vijana wa mjini wanaita ‘kujistukia.’ 

Huenda umewahi kukutana na mtu anayefanya kitu kwa umahiri mkubwa lakini ana wasiwasi. Pengine na wewe ni mmoja wapo. Unafanya kitu vizuri tu lakini bado unahisi hujafanya ipasavyo. Wanaokuona wanaweza kukupongeza kwa kazi nzuri lakini ndani yako bado unahisi wanakudanganya. Huamini unachoambiwa. Hii ndio hali ya kutokujiamini.

Unapokosa imani na uwezo wako mwenyewe unajiweka kwenye hatari ya kushindwa katika maisha. Huwezi kufanikiwa kama huna hakika na uwezo wako mwenyewe. Maisha yanakuhitaji ujiamini. Watu huwa na mashaka na mtu ambaye yeye mwenyewe haonekani kujiamini.

Aidha, unaweza usiwe na uwezo mkubwa lakini kujiamini kukakubeba. Ukijiamini, watu watakuamini. Kujiamini kunaongeza uwezekano wa watu wengine kuwa na imani na wewe. Kwa hakika kuaminiwa ni jambo la muhimu katika maisha. Wapo watu wanakosa kazi kwa sababu tu wameshindwa kuonyesha kujiamini kwenye usaili. Wapenzi, hali kadhalika, wanaweza kufarakana kirahisi kwa sababu tu kuna mmoja wao hajiamini. Mtu asiyejiamini hujaa wivu usio na sababu na humchosha mwenzake. Kujiamini, kwa kweli, ni tunu muhimu kwenye maisha.

Jambo la kuzingatia ni kwamba hatuzaliwi na hali ya kutokujiamini. Kujiamini kunajengwa. Kila mtu anaweza kujenga hali ya kujiamini ndani yake. Wazazi wanaweza kujifunza kuwajengea watoto kujiamini. Ili uweze kufanikiwa kumjengea mtoto imani na uwezo wake mwenyewe, ni muhimu kuelewa viashiria vya mtoto asiyejiamini na chanzo chake.

Viashiria vya kutokujiamini

Unaweza kumfahamu mtoto asiyejiamini tangu akiwa mdogo. Kwanza, ana tabia ya ‘kumganda’ mzazi/mlezi kupita kiasi. Anapohisi dalili za kuachwa, hali ya hewa hubadilika. Kwa mfano, katika umri wa miezi kadhaa tu, hapendi kabisa kuachwa. Ingawa mtoto anayejiamini naye atalia kama huyu, tofauti yao ni kwamba itamchukua muda huyu asiyejiamini kunyamaza.  

Pili, ni mdekaji na muda mwingi analia lia bila sababu ingawa si mgomvi wala mkaidi. Wakati mwingine huwa ni mtoto mwenye mashitaka mengi dhidi ya wenzake. Kinachomsumbua ni haja ya kusikilizwa.

Pia katika umri wa kuanzia miaka sita na kuendelea, mtoto asiyejiamini anaweza kuwa mkimya. Ingawa si kila mtoto mkimya hajiamini, mara nyingi, ukimya unaashiria woga na wasiwasi wa kutokueleweka na watu. Mtu mkimya ni nadra kujichanganya na watu.

Kinachomfanya ashindwe kujichanganya na wenzake ni kujistukia. Nafsi yake haiamini watu. Ndani yake kuna sauti inayomnong’oneza, 'Walimwengu hawaaminiki. Usimwamini mtu!'.

Hata hivyo, wapo watoto wasiojiamini wanaokuwa na tabia ya kupenda kuwa na watu. Kinachofanya wapende ‘kujichanganya’ na watu, si upendo walionao kwa watu bali ni ile hali ya kuwaamini wengine kuliko wanavyojiamini wao. Mioyo yao haijisikii utoshelevu bila kuwa na watu wanaowaamini na hivyo wanakuwa na shauku kubwa ya kutaka kuwapendeza na kuwaridhisha wengine. Hali hii huwafanya wawe na ‘umaarufu’ fulani.

Mtoto asiyejiamini anaweza kupatwa na ‘dhoruba’ anapoingia kwenye kipindi cha balehe. Kwanza, hana imani na kile anachoambiwa na mzazi wake. Kichwani kwake anaamini mzazi hamtendei haki. Kwa hiyo hata anapoelekezwa jambo si mwepesi kuzingatia. Katika mazingira haya, kugombana na wazazi ni jambo la kawaida kwake.

Katika uhusiano wa kimapenzi, mtu asiyejiamini huwa na wivu uliopitiliza. Wivu humfanya awe na matarajio mengi yasiyo halisi na hutamani kumdhibiti mpenzi wake. Ingawa anaweza kuonekana kama mtu anayejua kupenda, ukweli ni kuwa wasiwasi alionao humfanya awe karibu sana na mwenzake kwa lengo la kumlinda.

Chanzo cha kutokujiamini

Kutokujiamini kunachangiwa na mambo kadhaa kwa pamoja. Kwanza, ni mchanganyiko wa malezi yaliyojaa upendo yasiyo na kelele wala mabavu lakini yasiyotabirika. Mtoto huyu kwa hakika anaelewa kuwa wazazi wake wanamthamini na kumpenda. Ingawa mzazi si mtu mkali mwenye ghasia, changamoto ni kuwa mtoto anakuwa hana hakika afanya nini kuupata upendo huo unaopatikana kwa nadra. Sababu ni kuwa mzazi kimsingi ana utoro wa kutokupatikana nyumbani.

Kwa upande mwingine, inawezekana mzazi huyu mpole anapatikana kimwili, lakini kihisia ni kama vile hayupo. Muda mwingi anakuwa hajali kile anachojisikia mtoto au inawezekana ameweka ukuta mnene kati ya yake na mtoto. Mazingira haya yanamchanganya mtoto asielewe ni wakati upi anaweza kubahatisha ‘urafiki’ usiojulikana utapatikana lini.

Lakini pia inawezekana mzazi huyu ni mkosoaji kupindukia. Ingawa ni mzazi mwenye utulivu na asiyetumia nguvu, ana viwango vya juu mno ambavyo humwia mtoto vigumu kuvifikia. Huyu ni mzazi mgumu kumridhisha kwa sababu usipofikia viwango vyake, ni sawa na hujafanya kitu.

Sambamba na hilo, inawezekana pia mzazi anamdekeza mno mtoto na hajampa nafasi kufanya vitu bila msaada kwa imani kuwa ‘mtoto hawezi kuteseka wakati mimi nipo.’ Huyu ni mzazi anayeamini mtoto kufanya vitu fulani ni kumsumbua. Mtoto asiyepewa fursa ya ‘kuhangaika kidogo’ huishia kukosa imani na uwezo wake.

Msaada unaohitajika

Kwanza, hakikisha unapatikana kimwili na kihisia. Hata katika mazingira ambayo umebanwa na shughuli nyingi, tengeneza utaratibu wa kutabirika wakati upi unakuwepo. Unapopatikana, hakikisha unapatikana kweli kihisia. Mpe mtoto nafasi ya kukupata kwa mazungumzo na michezo. Usimfanye mtoto afanye kazi ya ziada ‘kukupata’ wakati upo.

Lakini pia usimdekeze mtoto. Mzazi utambue kuwa unapomdekeza mtoto unamnyang’anya ujasiri wake. Kumdekeza kunamfanya asijiamini. Punguza kumwonea huruma mtoto. Mpe fursa mtoto kujifunza maisha kwa kumshirikisha kwenye shughuli ndogo ndogo. Mwache afanye vitu kwa uhuru wake bila kumpa msaada mkubwa.

Pia, epuka kumkosoa mtoto kupindukia. Punguza matarajio. Mpe mtoto nafasi ya kukosea na msaidie kujiwekea malengo yanayosadifu uwezo alionao. Hata pale anaposhindwa kuyafikia, mtie moyo. Anapofanikiwa, hata kwa sehemu, tambua na mpongeze.


Maoni

  1. Ahsante sana Barikiwa Mr. Christian Bwaya

    JibuFuta
  2. Ahsante sana Barikiwa Mr. Christian Bwaya

    JibuFuta
  3. Ahsante sana bwaya kwa makala nzuri ningependa kujua inakuwaje kwa mtoto wa namna ya kutojiamini akiishi kwenye mazingira ya shida je anaweza kuwa mbunifu na kujiamini au kwake itabaki hivyo muda wote wa changamoto zake?

    JibuFuta
  4. Mtoto wangu mimi anaweza kufanya mambo mengi mazuri lakini hajiamin ,anawoga anapokuwa shuleni, na hata mbele za watu hiyo inampelekea kutokufanya vizur. Naomba ushauri nifanye nini?

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi