Mwanaume Anayejitambua Hatishwi na Mafanikio ya Mwanamke

PICHA: Ayo Martins

Upo ukweli usiosemwa wazi kuwa wanaume wengi wanawaogopa wanawake wenye mafanikio. Wanawake waliosoma, wenye mali na fedha, wenye madaraka makubwa katika jamii, wanakuwa na mtihani mkubwa kuanzisha na kudumisha uhusiano na wanaume.

 Hali hii inachangiwa na mambo kadhaa. Kwanza, hulka ya wanaume kuwa kichwa cha familia.  Ni dhahiri wanaume wengi wanapenda kujihakikishia hadhi ya juu kuliko wanawake. Kwa mfano, mwanaume wa kawaida anatamani kujihakikishia nafasi yake kama kiongozi wa familia kwa uwezo wake wa kumwongoza, kumwamrisha na kumdhibiti mwanamke.

Katika kuhakikisha kuwa hilo linawezekana mwanaume huyu hujitahidi awe na sifa za ziada kama vile kuwa na umri mkubwa zaidi, fedha zaidi na madaraka zaidi. Haya yote kwa pamoja yanajenga utamaduni wa kutafuta mwanamke dhaifu asiye na sifa alizonazo yeye ili kujihakikishia madaraka zaidi.

Lakini pili, kwa upande mwingine, baadhi ya wanawake nao wana hulka ya kupenda kupambana na mamlaka ya wanaume. Pengine kwa kuchoka kunyanyasika na kuwa chini ya udhibiti wa wanaume , inapotokea wanapata mafanikio kuwazidi waume zao, huanza kutishia heshima  na hadhi ya mwanaume.  

Kwa mfano, mwanamke mwenye uwezo mkubwa wa kifedha kuliko mumewe anaweza kuanza kujiona hana sababu ya kumsikiliza mume wake. Fedha zinakuwa ni fursa ya ‘kujikomboa’ dhidi ya utawala wa mwanaume jambo ambalo linaweza kuwatisha wanaume.

Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa  katika siku za nyuma, tofauti ya kijinsia ilikuwa dhahiri. Mila na desturi za wakati huo, kwa mfano, zilimnyima mwanamke fursa ya kujengewa uwezo sawa na mwanaume. Katika familia nyingi, mtoto wa kiume ndiye aliyepewa upendeleo kielimu na kijamii. Upendeleo huo ulimwezesha mtoto wa kiume kuwa na nafasi nzuri ya kupata mafanikio zaidi ya mwanamke. Katika mazingira hayo, haikuwa ajabu kwa mwanaume kumzidi mwanamke.

Mambo yamebadilika. Wanawake wa kileo wanayo fursa sawa na wanaume katika maeneo yote muhimu ya maisha. Wanawake wanakwenda shule sawa na wakati mwingine hata kuwazidi wanaume. Fursa ya kusoma imewafungulia milango wanawake kuajiriwa na kupata nafasi ambazo hapo awali zilikuwa haki ya wanaume.

Hapa tunapata masomo mawili makubwa. Mosi, mwanaume wa sasa hawezi kuendelea kutegemea udhaifu wa mwanamke kama kigezo cha kujihakikishia hadhi ya kuwa kichwa cha familia. Kuendekeza ukandamizaji dhidi ya wanawake kama namna ya kulinda heshima ya mwanaume ni jambo lisilowezekana.

Tulikofika haiwezekani tena kurudi nyuma. Mwanaume mwenye mawazo ya kumzidi mwanamke kielimu, kifedha, kimadaraka kama mbinu ya kujihakikishia heshima ya kichwa cha familia anaweza asifanikiwe.

Somo la pili ni haja ya kuondoa utata wa kimajukumu baina ya wanawake na wanaume. Mambo yamebadilika kiasi cha kufanya iwe vigumu kujua wajibu wa wanaume ni upi na kipi ni wajibu wa mwanamke. Mume, kwa mfano, anafikiri kazi yake kubwa ni kutoa fedha. Fedha zinampa ujasiri. 

Changamoto inakuja pale anapokutana na mwanamke asiye na shida na hizo fedha zake. Anachanganyikiwa hasa pale anapojikuta pamoja na kutoa fedha zake bado hapati yale mamlaka anayotamani kuwa nayo. Asichokijua ni kwamba shida ya mwanamke sio fedha kama anavyoamini bali kutokufanya wajibu wake asioufahamu. 

Mwanamke naye anafikiri akishafanikiwa basi hana haja ya kumpa mwanaume nafasi yake. Kimsingi, kusema 'hampi nafasi' ni kumwonea kwa sababu hajui kwa hakika nafasi ya mume wake ni ipi. Mazingira haya ya kuchanganyikiwa yanafanya iwe lazima kuzitambua nafasi zetu katika familia.

Tukianza na upande wa mwanaume, kujitambua ni muhimu. Huwezi kujiamini kama hujitambui. Mwanaume anayejiamini anaelewa fika kuwa kichwa cha familia maana yake ni uwezo wa kuelewa majukumu. Kichwa cha familia ni kuwa kiongozi. Kiongozi hujitoa, huipa familia nafasi ya kwanza, kuheshimu mahitaji halisi ya mke na watoto wake.

Mwanaume anayejiamini hana haja ya mwanaume kumshusha mwanamke ili yeye anufaike na udhaifu wa mke wake. Mwanaume asiyejitambua hufikiri kumfokea, kumpiga, kumdhalilisha, kumwamrisha na hata kumdhibiti mwanamke ndio kuwa kichwa cha familia. Hii si kweli. Huwezi kuwa kichwa cha familia kwa kutegemea uduni wa unayemwongoza.


Mwanaume wa sasa anahitaji kuelewa kuwa yeye mwenyewe ndio tishio la kweli kweli la hadhi yake. Asipojiamini na kuelewa nafasi yake atakuwa anahatarisha nafasi yake kama kichwa cha familia. Ndio kusema mwanaume imara, mwanaume anayejiamini, anayejitambua na kuelewa wajibu wake, hatishwi na uimara wala mafanikio ya mwanamke. 

Inaendelea 

Maoni

  1. tatizo kubwa wanaume walio wengi wamejenga mtazamo hasi kwamba mwanamke akiwa na mafanikio zaidi ya mume wake hujenga kiburi na dharau kwa mumewe, ila kama ulivyosema hii ni kutokana na kutojiamini kwa mwanaume na kutoelewa nafasi yake katika familia ndio huona kuwa wanadharaulika kwa wake wao.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi