Mwalimu Anavyoweza Kukuza Udadisi kwa Wanafunzi

PICHA: OBrown & Associates Education Consulting


Mara nyingi tumesikia watu wakilaumu mtalaa wetu kwamba unafunga fahamu za wanafunzi wetu. Wenye madai haya wanafikiri bila mtalaa kufanyiwa marekebisho makubwa, haiwezekani elimu yetu ikamnufaisha mwanafunzi. Hata hivyo, tulisema wiki iliyopita, kazi ya mtalaa ni kutoa diraya jumla ya aina ya raia wanaotarajiwa kufundwa kupitia mtalaa husika.

Mwalimu ndiye mwenye kazi kubwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaelewa kile kinachokusudiwa kufikiwa na mtalaa. Katika makala haya ninalenga kuonesha namna gani mwalimu aliyefuzu anaweza kutumia mtalaa huu unaolalamikiwa kujenga tabia ya udadisi kwa wanafunzi wake.

Ningependa nitumie mfano wa Shirika lisilo la Kiserikali liitwalo Opportunity Education. Shirika hili linaendesha mradi unaoitwa Next Generation Learning (NGL) ambao kimsingi unajaribu kutafsiri maudhui ya mtalaa katika mazingira halisi ya mwanafunzi. Kazi hii inafanywa na walimu wa shule zetu waliopata mafunzo maalum kuandaa mfululizo wa masomo yanayoandaliwa kutokana na mtalaa wetu.

Sambamba na kutafsiri maudhui ya mtalaa wetu, NGL wametengeneza mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji wanaousimamia wao wenyewe kwenye shule teule. Mradi huu ambao tayari umeshaonesha mafanikio, unatumia kanuni kuu tano ambazo naamini mwalimu yeyote anaweza kuzitumia.

Kwanza, kuhakikisha kuwa mwanafunzi anaelewa kwa nini anahitaji kujifunza kile anachojifunza. Hili kwa hakika limekuwa changamoto ya ufundishaji wa kimazoea.

Tumekuwa tukifundishwa maudhui ambayo kwa kweli hatuelewi tutayatumia wapi. Nakumbuka kwa mfano, nikiwa kidato cha V kwenye somo la Fizikia tulifundishwa hesabu ndefu za namna ya kutafuta muda utakaotumiwa na tone la mwisho kudondoka kwenye bomba la maji linalofungwa.

Hatukuelewa kwa nini ilikuwa ni lazima kusumbua akili kufanya hesabu hizi ngumu zisizotatua tatizo lolote kwenye maisha yetu. Ufundishaji wa namna hii, kwa hakika, unamkatisha tamaa mwanafunzi. Mwanafunzi asiyeelewa kwa nini anasoma kitu hawezi kuwa na udadisi. NGL wameonesha mfano wa namna tunavyoweza kuondoa hitilafu hii.

Kupitia mfumo wao wa ujifunzaji, NGL wanajaribu kufikiri namna gani kile kinachofundishwa kinagusa maisha ya kawaida ya mwanafunzi. Kujua uhusiano wa maudhui na maisha yake kunamwongezea mwanafunzi ari ya kujifunza kwa sababu anaelewa thamani ya kile anachotarajiwa kujifunza.

Mwalimu anapata somo muhimu hapa. Kwamba ni muhimu atafute namna ya kuhusianisha somo lake na maisha ya mwanafunzi. Kwa mfano, mwalimu wa Kemia anapofundisha somo la Mada (matter) anahitaji kufanya kazi ya ziada kumsisimua mwanafunzi kuona namna maarifa ya mada yanavyoweza kumsaidia katika maisha yake ya kila siku. Kazi hii haifanywi na mtalaa bali mwalimu.

Kanuni ya pili inayotumiwa na NGL, ni kuhakikisha mwanafunzi anajenga uwezo wa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu hicho anachojifunza badala ya kutegemea majibu yaliyopikwa na mwalimu anayeonekana kuwa mjuzi na mmiliki wa maarifa.

Kwa hakika madarasa yetu yanafanya kinyume. Kazi ya walimu imekuwa ni ‘kuhubiri’ maarifa kwa mwanafunzi. Mwanafunzi anachukuliwa kama mtu anayesubiri kupikiwa kila kitu na kazi yake ni ‘kumeza’ kile anachoambiwa. Hana fursa ya kuuliza wala kuhoji.

Shule zetu ‘zinazofaulisha sana’ kimsingi zinajitahidi kuhakikisha mwanafunzi anafahamu kwa hakika nini cha kukariri. Walimu wa shule hizi wanafanya bidii kubwa kuwaimbisha wanafunzi kile wanachojua kitaulizwa kwenye mtihani.

Somo tunalopewa na Opportunity Education ni kwamba mwanafunzi anayewekewa mazingira ya kujiuliza maswali na kushiriki moja kwa moja katika kutafuta majibu, anakuwa na uwezo wa kudadisi kuliko mwenzake anayeshiriki ‘kumeza’ maarifa.

Mwalimu lazima afanye kazi kubwa ya kuibua maswali yanayohusiana na kile anachokifundisha ili wanafunzi waweze kujifunza kwa mfumo wa kutafuta majibu wao wenyewe. Mradi wa NGL unatuthibitishia kuwa mwalimu akiwezeshwa anaweza kutafsiri mtalaa huu unaodaiwa kuwa haufai kuibua kiu ya kutafuta majibu.

Kanuni ya tatu ni kumtarajia mwanafunzi kutumia maarifa yake kutengeneza ujuzi. Mwanafunzi wa NGL si tu anahitajika kujibu maswali ya kufikirisha, bali kuonesha ujuzi mahususi. Mathalani, baada ya mwanafunzi kujifunza namna mimea inavyotengeneza sukari kwa kutumia mwanga wa jua, lazima aoneshe anavyoweza kutumia maarifa hayo kutatua matatizo katika mazingira yake.

Inaendelea

Maoni

  1. Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.

    JibuFuta
  2. Ni kweli Mwalimu, lazima tuwashirikishe wanafunzi nao ktk kufikiri na Kutafiti na si kuwamezesha tuu .

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu