Mafanikio Hayamfanyi Mwanamke Anayejitambua Kuacha Wajibu Wake


PICHA: RealClearPolitics

USAWA wa kijinsia katika dunia ya leo si suala linalohitaji mjadala. Tunakubaliana kimsingi kuwa hakuna jinsia bora kuliko nyingine na pia hakuna jinsia inayohitaji kulipa gharama ya kulinda hadhi ya jinsia nyingine. Mwanamke, anayo haki ya kupata elimu kulingana na uwezo wake, kufanya kazi anayoiweza, kumiliki na hata kurithi mali sawa na mwanaume.

Hata hivyo, mabadiliko haya kimsingi yanakuja na gharama zake. Kwa mfano, mwanaume aliyezoea kutumia udhaifu wa mwanamke kama ngazi ya kujihakikishia mamlaka yake katika familia lazima akubali kubadilika. Badala ya kutegemea uduni na unyonge wa mwanamke, lazima aanze kuchukua hatua za kujitambua.  

Kama tulivyodokeza kwenye makala iliyopita, mwanaume anapojitambua hawezi kutishwa na mabadiliko yanayomruhusu mwanamke kuwa na haki ambazo hapo awali hakuwa nazo. Hiyo hata hivyo, haimaanishi kuwa mwanamke hana gharama anayohitaji kuilipa. Hapana. Mwanamke naye anahitaji kujitambua kwa kuelewa kuwa mafanikio ya kielimu, kiuchumi na kijamii hayamfanyi asahau wajibu wake kama mwanamke. Nitaeleza.

Tofauti ya majukumu kijinsia

Mila na desturi zetu ziligawa majukumu fulani fulani kwa kigezo cha jinsia. Ingawa ni kweli mgawanyo huu wa kimajukumu wakati mwingine uliigharimu jinsia moja kwa faida ya jinsia nyingine,  bado ulisaidia kuondoa mgongano wa kimajukumu usio wa lazima.

Tofauti hii, hata hivyo, ilikuwa na msingi wa kimaumbile. Kwa mfano, maumbile ya mwanaume yanamruhusu kufanya kazi ngumu kuliko mwanamke. Kwa sababu ya maumbile yake, mwanaume alifanya kazi za suluba kuhakikisha chakula cha familia kinapatikana. Ndiye aliyewinda wanyama pori kuiletea familia yake kitoweo. Maumbile yake, kadhalika yalimpa wajibu wa kumlinda mke na familia yake kwa ujumla. Huo, kwa hakika, haukuwa upendeleo bali wajibu wa mwanaume kimaumbile.

Sambamba na shughuli nzito, mwanaume alikuzwa kuwa kiongozi wa familia. Uongozi wa familia haikuwa suala la kimadaraka bali majukumu mazito ya kuelewa familia yake inaelekea wapi na nini kifanyike kuelekea huko.

Mwanamke, kwa upande wake, hakuwa na haja ya kujipatia majukumu haya ambayo kimsingi alijua si yake. Mwanamke, tofauti na mwanaume, alikuzwa kuamini kuwa yeye ndiye msaidizi wa mume wake. Kuwa msaidizi maana yake ni kukubali kuwa chini ya mamlaka ya mwanaume. Mwanamke aliheshimu nafasi ya mume wake kama kiongozi wa familia.

Kazi yake kubwa ilikuwa ni kuelea watoto na kutunza familia. Hatuwezi kudhihaki jukumu hili nyeti. Kazi ya kulea haikuwa ‘shughuli’ ndogo. Ilihitaji moyo wa upendo na kujituma kwa hali ya juu kuhakikisha kuwa watoto wanapata malezi yanayostahili.

Kuyasema hayo hatupendekezi mwanamke asifanye kazi nje ya familia. Hapana. Hoja tunayoijenga ni kwamba mwanaume na mwanamke walikuwa na majukumu yasiyoingiliana. Mume alijua kazi yake na mke naye alifahamu kazi yake katika familia. Hapakuwa na mgongano wa kimajukumu kama ilivyo leo.

Tofauti ya mahitaji kijinsia

Mahitaji ya mwanamke kimsingi ni tofauti na mahitaji aliyonayo mwanaume kisaikolojia. Tuliwahi kuzungumzia suala hili. Kwa ufupi, mamlaka na heshima ni hitaji la kisaikolojia la kila mwanaume. Ndani ya kila mwanaume kuna kiu ya kuheshimiwa kama kiongozi wa taasisi ya familia.

Mwanamke wa asili hana hitaji hili. Kwake, kilichomuhimu ni kupendwa. Mwanamke wa kawaida anahitaji mtu atakayemhakikisha mapenzi ya dhati. Hata kama anaweza kuwa na kila kitu, bado mwanamke anauhitaji wa mwanaume atakayempenda kwa dhati.
Tofauti hizi zinafanya uhusiano wa mwanamke na mwanaume kuwa wa nipe nikupe. Wakati mwanaume anafanya kazi ya kumpenda mke wake, mwanamke naye anafanya kazi ya kumpa mwanaume heshima anayoihitaji. Utegemeano huu wa kijinsia ndio unaoimarisha uhusiano wa mwanamke na mwanaume.

Usawa wa jinsia si kufanana

Dhana ya usawa wa kijinsia, kwa bahati mbaya, inachukuliwa na wengi kama kufanana kijinsia. Tunafikiri kwa sababu mwanamke ana haki ya kufanya kazi ambazo hapo awali zilifanywa na mwanaume basi maana yake ni kuwa kihisia, kiufahamu, kimatamanio, mwanamke ni sawa na mwanaume. Mtazamo huu unaoendelea kupata umaarifu katika jamii za kileo unaathiri namna mwanaume na mwanamke wanavyohusiana.

Inapotokea, kwa mfano, mwanamke anapata mafanikio ni rahisi kwake kujichukulia kama mtu anayeweza kufikiri na kutenda kama mwanaume. Mafanikio yanampa nguvu ya kuanza kuhoji uhalali wa mamlaka ya mwanaume. Hufanya hivyo akiamini mafanikio ya kielimu, kiuchumi na kijamii yanampa uhuru wa kujinasua na ‘utumwa’ wa kuwa chini ya mwanaume.

Changamoto ni kwamba mwanaume aliyelelewa katika mila na desturi zinazomtambua kama kichwa cha familia, hutishika anapoona mamlaka yake yanapinduliwa. Kuhoji uhalali wa yeye kuwa kichwa ni tishio la wazi wazi la ‘mapinduzi.’ Ni sawa na mkuu wa ofisi anayeshuhudia wafanyakazi waliochini yake wakipanga kumng’oa. Hawezi kuwa na amani.

Ndivyo inavyokuwa kwa mwanaume anapoona mwanamke anataka kuwa na mamlaka kama alivyo yeye. Inapofikia hapa, uhusiano kati ya mume na mke huanza kuingia dosari zinazoweza kuzaa misuguano isiyo ya lazima.

Nguvu ya mwanamke

Kunusuru dosari hii katika mahusiano ni muhimu (soma lazima) mwanamke uliye na mafanikio ufahamu iliko nguvu yako. Kuwa na fedha, elimu, madaraka havikupi nguvu kwa mwanaume. Hivyo vyote, kama tulivyoona, vinakupunguzia ushawishi wako kwa mwanaume. Nguvu uliyonayo inayoweza kumkamata mwanaume ni kujitambua kwa maana ya kuelewa mahitaji halisi ya mwanaume.

Kujitambua ni kuelewa kuwa mafanikio yako kielimu, kifedha na kijamii hayapaswi kukushawishi kujiondoa chini ya mwanaume. Kujitambua ni kumhakikishia mume wako –bila kujali elimu yake, uwezo wake wa kiuchumi wala hadhi yake– kuwa hana sababu ya kuwa na wasiwasi na mamlaka yake katika familia.


Pamoja na uwezo ulionao, jifunze kuwa mnyenyekevu kwa mwanaume unayempenda. Rekebisha tafsiri yako ya usawa wa kijinsia na usitamani kuwa ‘mwanaume’ kwa sababu ya mafanikio. Vitendo na kauli zako zioneshe kuwa wewe bado ni mwanamke anayejua mipaka ya majukumu yake kwa kuwa anatambua nafasi ya mwanaume katika familia. 

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi