Ufanye Nini Mtoto Anapokuwa Mkorofi?

PICHA: JGI/Jamie Grill

Pengine una mtoto unayefikiri ameshindikana. Unamwita mtundu, mtukutu, asiyeambilika, mbishi, mkaidi na majina mengine. Kikubwa ni tabia yake ya kupenda kushindana. Katika makala haya tunamwita mtoto mkorofi. Huyu ni mtoto anayeweza kukukatalia kitu bila kupepesa macho na ukajikuta ukifedheheka.

Unaweza kumwagiza afanye kitu na akabaki akikuangalia. Hajigusi. Wakati mwingine ni mtoto mwepesi kurusha rusha mikono na miguu kama namna ya kupinga unachomwelekeza. Anapoamua jambo, anakuwa na msimamo imara. Ukimlazimisha kufanya asichokitaka yeye unaambulia vilio na vurugu.

Mtoto wa namna hii pia huwa mgomvi anapokuwa na wenzake. Tabia yake ya kushindana na kila anayekuwa naye inamfanya ajikute kwenye migogoro ya mara kwa mara.

Mbali na kusumbuana naye hapo nyumbani, inawezekana pia ni msumbufu hata shuleni. Pengine umepokea malalamiko kwa walimu wake kuwa hafanyi kazi anazopewa, hatulii darasani na muda mwingi anautumia kugombana na wenzake bila sababu za msingi. Inawezekana tabia ya usumbufu imechangia matokeo yake shuleni yasiwe mazuri.

Pia, ukorofi unakwenda sambamba na tabia ya kupenda kujiona ni mtawala anapokuwa na wenzake. Anaweza kuwa mwongeaji au mkimya lakini anafurahia kuona wenzake wakifanya kile anachokitaka yeye. Ni aina fulani ya hulka ya uongozi iliyochanyikana na kutokuelewa wengine wanataka nini. Upofu wa hisia.

Athari za ukorofi

Ni vizuri kuzingatia kuwa si kila ubishi ni ukorofi. Kila mtoto kwa wakati fulani hujaribu kupigana na maagizo ya mzazi. Ubishi ni sehemu ya udadisi wa mtoto hasa pale anapofikiri kile anachoambiwa hakiendani na anachotamani. Usichukulie kuulizwa maswali mengi na mwanao kama ubishi au ukorofi.  Mtoto mwenye akili nzuri mara nyingi hapokei kirahisi kile anachoambiwa bila kukitafakari.

Ingawa kila mwanadamu anahitaji kiasi fulani cha ukorofi kwa maana ya msimamo wa kile tunachokiamini, tabia hii ya misimamo inayoongozwa na upofu ikiachwa imee inaweza kuwa kikwazo kwa mafanikio ya mwanao.

Ukubwani, ukorofi unahatarisha –na hata kuvunja– uhusiano baina ya watu. Unapokuwa mtu mkorofi, huwezi kujisikia hatia kumwumiza mwezako. Tena wakati mwingine furaha yako inaweza kuwa kuona wenzako wanaumia. Hakuna mzazi anatamani kukuza mtu wa namna hii.

Kinachosababisha ukorofi

Ukorofi wa mtoto ni ujumbe. Ni muhimu uuelewe ujumbe huu kabla hujachukua hatua za kuushughulikia. Ukorofi ni lugha ya kusema ndani anajisikia utupu. Ni sawa na mtu aliyeshinda njaa siku kadhaa. Kwa vyovyote vile ni dhahiri atakosa utulivu. Mwili wake unahitaji chakula.

Mtoto mkorofi kimsingi anaamini watu wanaomzunguka hawajatambua nafasi yake ipasavyo. Ndani yake mna sauti inayomwaminisha kuwa hatambuliki. Imani hiyo potofu huchochea jitihada za kutafuta kutambulika kwa namna isiyokubalika.

Ubishi na ukaidi anaoufanya –wakati mwingine bila hata yeye kung’amua– ni namna ya kujirudishia mamlaka anayoamini hana. Anapobishana na mzazi, anapogombana na wenzake, kimsingi anajaribu kujirejeshea ushawishi ambao anaamini hana.

Mambo mengi yanaweza kuzaa ukorofi. Wapo baadhi ya wanataaluma wanaamini mtu huzaliwa na ukorofi. Inawezekana. Lakini kwa sehemu kubwa tafiti zinaonyesha kuwa ukorofi ni zao la malezi.

Hapa kuna mambo makubwa matatu. Kwanza, inawezekana kwa sababu ya kutamani mtoto ‘anyooke’ umekuwa na sheria kali mno. Unaamini mtoto hawezi kufanya kitu bila kuamrishwa. Kwa sababu ya kuamini hivyo, umejikuta ukijenga mazingira ya mapambano yasiyo na sababu. Mtoto mkorofi ni ama anakuiga vile ulivyo au basi anapambana na wewe.

Lakini pili, inawezekana una ukali uliopitiliza. Huwezi kuongea bila kufoka na kupaza sauti. Huna sauti ya upole inayoleta taswira ya mtu mwelewa, anayejali, na mtulivu. Unaamini bila kelele hakuna nidhamu.

Aidha, inawezekana mtoto amekuwa akishuhudia vitendo vya ukorofi katika mazingira ya familia au jirani. Kwa kawaida, watoto wananasa kwa haraka sana mambo yanayogusa hisia zao. Wanapoona mtu mzima anafanya jambo fulani na watu anaowaamini wanalichukulia kawaida, wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya kile kile wakati fulani.  

Mbinu za kumrekebisha

Jambo la kuzingatia ni kuwa ukali na mapambano yanakomaza ukorofi. Badilika na amua kuwekeza katika kujenga urafiki kabla hujatarajia kusikilizwa. Hatuzungumzii urafiki wa siku mbili au tatu. Hapana. Tunazungumzia urafiki wa kudumu ambao mtoto hatakuwa na sababu ya kuwa na mashaka nao. Kama tulivyoona, mtoto mkorofi kimsingi anahitaji uhusiano wa karibu na wewe mzazi. 

Hata katikati ya urafiki huo, usishangae mwanzoni bado mtoto akaendelea kuwa mkaidi vile vile. Usikate tamaa. Mpe nafasi ya kukuamini kwa kujenga urafiki imara. Sambamba na urafiki, punguza amri na kelele zisizo za lazima. Kumbuka kuwa amri bila urafiki huchochea uasi.

Badala yake jenga tabia ya mazungumzo ya utulivu unaposhughulika naye. Badala ya kuagiza, jaribu kushirikiana naye. Mwonyeshe kuwa unajali na kuthamini kile anachokipenda. Huna sababu ya kushindana naye. Katika mazungumzo, mpe nafasi ya kusema. Mwache aongee yaliyoujaza moyo wake na usiwe mwepesi kukosoa hisia zake wala kujitetea. Kumbuka kuwa ukorofi wake unatokana na kujisikia kutokueleweka.

Mpe uzingativu kwa kuacha shughuli unazofanya kwa ajili yake. Ushirikiano wa kiwango hiki utamchangamsha. Ukiweza kufanya hivi bila unafiki, mtoto ataanza kukuamini. Kidogo kidogo atabadilika.

Kadhalika, mheshimu kama mtu mwingine yeyote unayemheshimu. Heshima ina mambo mengi. Usimdhalilishe mbele ya wenzake kwa maneno au vitendo. Kama kuna sababu ya kumwadhibu, fanya hivyo kwa staha. Kumheshimu mtoto hakukuondolei mamlaka yako kama mzazi.

Pia, tengeneza mazingira ya kufanya maamuzi shirikishi yanayoheshimu matakwa yake. Kwa sababu tayari ana ukorofi, mweke karibu unapotaka atekeleze jambo. Badala ya kumwambia ‘kafanye,’ badili lugha iwe, ‘tufanye’ hata kama hulazimiki kufanya. Inapobidi, hasa kwenye hatua za mwanzo, shirikiana nae kufanya hicho unachotaka akifanye.

Vile vile, tambua kizuri kipya anachojifunza. Kama, kwa mfano, ameweza kuacha kubishana unapomwagiza kufanya kitu, usikae kimya. Tambua mabadiliko hayo hata kama ni madogo. Fahari ya mtoto ni kuona jitihada zake zinatambuliwa. Kadri unavyomfanya ajisikie kutambuliwa, ataendelea kufanya bidii ya kukupendeza na hatimaye ukorofi aliokuwa nao utapungua.


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi