Tufanye nini Kukuza Udadisi kwa Wanafunzi Wetu?

PICHA: Fernando Díez Gallego

UDADISI ni uwezo wa kuhoji mazoea. Udadisi ni kiu ya kujiuliza maswali yanayolenga kutafuta majibu ya changamoto zilizopo. Mtu mdadisi lazima atakuwa na uchunguzi ndani yake. Haiachi akili yake itulie. Haridhiki na majibu yaliyozoeleka. Mdadisi hupembua taarifa kumwezesha kuelewa ujumbe uliojificha kwenye taarifa hizo.

Kwa hakika udadisi una nafasi muhimu katika kuleta maendeleo katika jamii. Ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu kwa kiasi kikubwa unategemea na uwezo wa raia kujiuliza na kusaka majibu ya maswali ya msingi.

Dhima kuu ya elimu iliyo bora ni kuzalisha raia wenye sifa ya udadisi. Hawa ni raia wanaofikiri kwa bidii, wanaohoji mazoea, wasioridhishwa na majibu yaliyozoeleka, wanaotumia muda mwingi kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili. Mambo kadhaa yanaweza kuchangia upatikanaji wa elimu yenye sifa hizo. 

Mitalaa yenye ubora

Mitalaa ni mkusanyiko wa mambo yote, ndani na nje ya darasa, yanayomwezesha mwanafunzi kupata maarifa na ujuzi unaomsaidia kujitambua kibinafsi na kuitambua jamii anamoishi.

Mtalaa ni mwongozo wa jumla, wenye malengo mapana ya kumwuumba raia mwenye sifa fulani zinazokidhi mahitaji ya jamii husika. Kimsingi, mtalaa hubeba matamanio ya jumla ambayo, ili yawe na maana, lazima yakutane na vipaji binafsi vya mwanafunzi kumsaidia kutambua wajibu alionao katika jamii sawa sawa na vipaji alivyonavyo.

Pamoja na ukweli kuwa mtalaa unahitaji kumwekea kijana mazingira ya kutambua vipaji vyake na nafasi aliyonayo katika jamii, ni vigumu mtalaa kukidhi mahitaji mahususi ya kila mtu. Ni hivyo kwa sababu, kama tulivyodokeza hapo juu, mtalaa kwa asili yake hubeba malengo mapana yanayoifikiria jamii kwa ujumla wake.

Wadau wengi wa elimu wamekuwa wakilalamikia ubora wa mtalaa wa nchi yetu. Hata hivyo, watalaamu waliolinganisha maudhui ya mtalaa wa nchi yetu na mitalaa ya nchi nyingine wanaonesha kuwa hatuna matatizo makubwa na mitalaa. Kimsingi tunashindana kwa ubora barani Afrika. Hiyo, hata hivyo, haimaanishi kuwa mitalaa yetu haina kasoro. Hakuna mtalaa usio na kasoro. Lakini mapungufu yaliyopo hayaweza kuhalalishi ukosefu wa udadisi miongoni mwa vijana wetu. 

Kwamba tunazalisha watoto wasio na udadisi, jibu haliwezi kuwa udhaifu wa mitalaa. Tunaweza kutumia mitalaa ya vyuo vikuu kama mfano dhahiri. Ukisoma mitalaa hiyo unaweza kushangazwa na tofauti kubwa iliyopo kati ya maudhui ya mitalaa na aina ya wahitimu wanaofuzu kupitia mitalaa hiyo. 

Mwanafunzi anayepata alama A, kwa mfano, hana tofauti na mwenzake aliyefaulu kwa kurudia mitahani. Tafsiri yake ni kuwa ubora wa mitalaa hautuhakikishii wahitimu wenye ubora. Lazima iwepo  sababu ya ziada. 

Mwalimu aliyefuzu

Kwangu, naamini, changamoto ni namna gani malengo na maudhui yaliyoanishwa kwenye mtalaa huo yanatafsirika katika maisha halisi ya mwanafunzi.

Hapa ndiko uliko umuhimu mkubwa wa mtu anayeitwa mwalimu. Kazi kuu ya mwalimu ni kutafsiri malengo hayo mapana yaliyoainishwa katika mtalaa na kuyahusianisha na mazingira halisi anayoishi mwanafunzi. Bila mwalimu, mwanafunzi ataishia kupata maarifa na ujuzi wa jumla usiomsaidia kuona mchango wake mahususi katika jamii. Mwalimu, kwa nafasi yake, ndiye anayebeba dhamana ya kujenga udadisi kama tutakavyoona mbeleni.

Ili mwalimu aweze kufanya kazi hiyo nyeti lazima awe na sifa fulani. Sifa ya kwanza na muhimu ni kuelewa malengo mapana ya mtalaa. Tunahitaji mwalimu mwenye weledi na ari ya kumjengea mwanafunzi uwezo wa kudadisi. Bila mwalimu mwenyewe kuwa mdadisi haiwezekani kutarajia kitu tofauti kwake. 

Mazingira ya ujifunzaji

Ndio kusema, haitoshi kuwa na mtalaa mzuri kwa maana ya kuwa na malengo mazuri yanayogusa matatizo halisi ya jamii. Tunahitaji kuwa na utaratibu mzuri wa kusimamia utekelezaji wa mtalaa tukilenga kumsaidia mwanafunzi kujenga shauku ya kujifunza, kiu ya maarifa na njaa ya kudadisi. Mazingira wezeshi, ambayo kimsingi yanayofahamika, ni suala la lazima. Tunazungumzia miundo msingi, zana za kujifunzia na kufundishia.

Katika eneo hili, haihitaji utafiti mkubwa kujua kuwa shule zetu zinakabiliwa na mazingira yenye changamoto kubwa. Mazingira ya shule zetu si tu hayakuzi udadisi, bali hata kuwezeshi upatikanaji wa maarifa ya msingi imekuwa changamoto. 

Hata hivyo, zipo shule (mfano binafsi) zenye mazingira mazuri ya kujifunzia. Kila anachokihitaji mwalimu ili aweze kufanya kazi yake kinapatikana lakini bado wanafunzi wanaopita kwenye mazingira hayo mazuri hawana tofauti yoyote ya msingi na wenzao wanaosoma kwenye mazingira magumu.

Tafsiri yake ni kuwa mazingira, pamoja na umuhimu wake katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji, bado hayawezi kutuhakikishia ubora wa kile wanachojifunza wanafunzi. Kama nitakavyoonesha kwenye makala inayofuata, udadisi wa mwanafunzi unaweza kukuzwa hata katika mazingira ya kawaida kabisa.

Upimaji makini

Jambo la nne linalotajwa kuwa na nafasi ya pekee katika utoaji wa elimu bora ni umakini wa mchakato wa upimaji.  Mchakato madhubuti wa ujifunzaji na ufundishaji lazima uwekewe utaratibu makini wa tathmini. Hapa tunazungumzia mitihani inayopima uelewa (udadisi) wa wanafunzi. Ili mitihani iaminike kuwa na ubora, lazima itoe taswira inayokadiria uwezo halisi alionao mwanafunzi. 

Mitihani inayotolewa na Baraza la Mitihani inakidhi viwango hivyo. Pamoja na changamoto zake, aina ya maswali yanayoulizwa na Baraza la Mitihani kwa kiasi kikubwa inakidhi viwango vya upimaji bora. Maswali mengi yanalenga kupima kiwango cha juu cha maarifa pamoja na ujuzi anaohitajika kuwa nao mwanafunzi. Hata hivyo, pamoja na upimaji mzuri, bado wahitimu wengi wenye ufaulu mzuri hawajawa na udadisi ndani yao. 

Wahitimu wengi waliofaulu wanakuwa na uwezo mkubwa wa kukumbuka maarifa waliyofundishwa kuliko kuhoji, kuchambua, kutafsiri taarifa wanazokutana nazo. Ndio kusema, tunaweza kuwa na utaratibu mzuri wa upimaji lakini bado tusiweze kuwa na wahitimu wanaoweza kutusaidia kutatua matatizo yanayolikabili taifa letu.

Ninachojaribu kukionesha hapa ni kwamba mwalimu mwenye sifa anaweza kubeba jukumu la kuratibu mchakato wa ujifunzaji unaoibua udadisi ndani ya wanafunzi kwa kutumia mitalaa hii hii inayolalamikiwa katika mazingira haya haya tunayoyajua wote kuwa yana changamoto kubwa.

Inaendelea

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia