Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini
Ufanisi kazini, kwa kiasi kikubwa, unategemea uwezo alionao kiongozi. Huyu ni mtu mwenye mamlaka yanayompa sauti ya kuhamasisha watu kujiwekea dira na utaratibu wa kuifikia dira hiyo. Kiongozi anatambulishwa na uwezo wake wa kuwavuta na kuwashawishi watu makini kutumia vipawa , ujuzi na uzoefu walionao katika kuwezesha kufikia malengo mapana ya kampuni, taasisi au kikundi husika.

 Tunaweza kusema mengi yanayohusu wajibu wa mfanyakazi lakini bila kiongozi makini itakuwa vigumu kupata ufanisi unaotakikana. Haiwezekani, kwa mfano, kuwa na wafanyakazi waliohamasika bila kuwa kiongozi anayejua kuibua hamasa hiyo kwa watu. Utendaji wa watu unategemea aina ya sauti inayowaongoza kufanya kazi.

Kama wewe ni kiongozi wa idara, ofisi, kampuni au taasisi yoyote ikiwemo familia, makala haya yanakuhusu. Ingawa ni kweli tunaweza kuzaliwa na siha ya uongozi,  kiongozi makini hachoki kujifunza namna bora ya kuwaongoza waliochini yake. Tuangalie sifa nne muhimu kuwa nazo wewe kama kiongozi.
Kujenga hamasa
Kiongozi mzuri ana tabia ya kuwafanya watu wakajisikia fahari kufanya kitu bila kusukumwa. Hapa tunazungumzia kuwa na sauti inayosikika mioyoni mwa wale unaowaongoza. Kinyume chake ni kuwatawala watu kwa maana ya kuwalazimisha kufanya kitu wasichojisikia kukifanya.
Unaweza kujenga hamasa kwa namna kadhaa. Kwanza, kuwafahamu waliochini yako kwa majina yao. Kama kiongozi unapokuwa na desturi ya kuongea na kuwasiliana na watu kwa kuwaita majina yao unawafanya waone unawathamini. Kuthaminiwa kunaongeza hamasa.
Pili, kutambua  kazi na jitihada zinazofanywa na waliochini yako. Kuna ukweli kuwa zaidi ya mshahara mzuri watu wanatamani kuona kazi wanazofanya zinatambuliwa na kiongozi wao. Ukijifunza kutambua jitihada za watu wako utawajengea hamasa ya kujituma zaidi. Kuwa na utaratibu wa kuwaita wale wanaofanya vizuri zaidi utambue kazi zao. Itisha vikao si kwa lengo la kuwagombeza watu kwa makosa yao bali kusikiliza maoni yao na kuwapa mrejesho wa kazi nzuri ulizoziona. Utawaongeza hamasa.
Kujali ndoto za unaowaongoza

Moja wapo ya sifa mbaya zinazotajwa kwa viongozi wengi ni tabia ya kupuuza maslahi na mustakabali wa watu wanaowaongoza. Kuwachukulia watu wako kama mashine zisizo na hisia wala malengo ni namna moja wapo ya kuonyesha unavyowapuuza.

Jambo moja la kuzingatia ni kwamba mafanikio ya taasisi au kampuni unayoiongoza yanachangiwa na bidii ya watu unaofanya nao kazi. Ukishindwa kulitambua hilo utakuwa huna sifa za kiongozi anayeweza kuhamasisha watu kufikia malengo ya kampuni au taasisi unayoiongoza.

Katika mazingira hayo hutafikiria mahitaji ya watu wako kama binadamu badala yake utatumia muda mwingi kujifikiria wewe na utakuwa mwepesi kufurahia kuona unaowaongoza wakitaabika na kulalamika.

Ukitaka kufanikiwa kama kiongozi, jifunze kujali utu wa watu unaowaongoza. Jali maslahi yao badala ya kuwakamua kutumikia maslahi yako binafsi. Tengeneza mipango ya wazi ya kuwaendeleza kadri ya uwezo wao. Fikiria unavyoweza kuwasaidia kufikia ndoto zao.

Ukiweza kuwathamini watu wako kwa kauli na matendo, wataheshimu kazi. Ari na motisha ya wafanyakazi kufikia malengo ya kampuni au taasisi yako, kwa kiasi kikubwa inategemea kiwango cha imani waliyonayo kuwa unawajali.

Kujiamini na kujifunza

Kiongozi anayejiamini hana wasiwasi na kile anachokifanya. Kujiamini kunamfanya awe na uhakika kwamba anaiweza kazi yake. Kipimo cha kujiamini kwako kama kiongozi ni uvumilivu unaposikia mawazo mbadala. Kiongozi unayejiamini huwezi kuchukulia mawazo tofauti na yako kama uadui. Hutishwi na uhuru wa waliochini yako kushauri jambo kwa nia ya kuboresha. 

Kadhalika, kujiamini kunakwenda sambamba na tabia ya kusema ukweli. Kiongozi anayejiamini hadanganyi. Inahitaji kujiamini ili uweze kuwaambia wale unaowaongoza vile mambo yalivyo hasa katika mazingira ambayo kuficha ukweli kuna madhara kwao.

Kiongozi asiyejiamini, kwa upande mwingine, hujilinda kwa kuwa mkali bila sababu ya msingi. Hufikiri ubabe na kufoka ndio ujasiri kumbe ni kuficha udhaifu anaousikia ndani yake.

Pia, kutokujiamini kunamfanya asiruhusu waliochini yake kusema tofauti na vile anavyofikiri. Kiongozi anapokosa hali ya kujiamini huwa na shughuli ya kutengeneza makundi ya kimaslahi kazini kwa lengo la kuwa na vibaraka wanaomsaidia kujua wabaya wake wanafikiri nini.

Ili uweze kujiamini kama kiongozi lazima kweli uwe na uwezo. Ingawa si lazima uwazidi unaowaongoza, lakini ni muhimu kwako kama kiongozi kuwekeza kwenye weledi na maarifa. Kuwa kiongozi haimaanishi unajua kuliko unaowaongoza. Hiyo ikupe unyenyekevu wa kujifunza na kuwa msikivu kwa wanaokuzidi.

Jiulize ni lini ulijiongezea maarifa kwenye eneo lako la utaalamu kama kiongozi? Unapata muda wa kusoma vitabu na kuhudhuria semina za kujinoa kiweledi? Unapokuwa mwanafunzi wa kudumu unajiongeza hali ya kujiamini.
Ujasiri wa maamuzi

Unapokuwa kiongozi maana yake unaijua njia. Waliochini yako wanategemea maongozi yako uwaonyeshe wapi pa kupita. Hapa tunazungumzia uwezo wako wa kuona mbali. Kiongozi lazima uwe na maono mapana. Unapokuwa na maono yanayoakisi malengo na dira ya taasisi au kampuni unayoiongoza, utakuwa na ujasiri wa kuwashawishi waliochini yako kukufuata. Huwezi kuwa kipofu na ukawa na ujasiri.

Ujasiri ni uwezo wa kuthubutu kufanya maamuzi yenye maslahi ya wengi. Kama kiongozi, lazima ujitokeze kuwa mtu wa kwanza kugundua viashiria vya tatizo na kuwaalika wale unaongoza katika kutafuta ufumbuzi. Unaowaongoza wanakuwa na ujasiri wanapoona na wewe kama kiongozi wao unao ujasiri huo. Hulazimiki kuongea ili watu waone kuwa wewe ni jasiri bali namna unavyoongea, unavyoonekana, unavyowasiliana na watu.

Kinyume cha ujasiri ni kiongozi anayejificha nyakati za matatizo akisubiri wengine watangulie. Kiongozi dhaifu huogopa kufanya maamuzi mara nyingi kwa sababu hana hakika na kile anachokisimamia. Kinachompa wasiwasi ni namna anavyoweza kuonyesha njia ambayo yeye mwenyewe hana hakika nayo. Usiwe kiongozi wa namna hii.

Maoni

  1. Asante kwa somo zuri sana
    Na hii ni changamoto kubwa sana kwa viongozi Mungubakubariki

    JibuFuta
  2. Kiongozi bora anasiniliza mawazo ya wenzake nakuyachakata

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu