Wajibu wa Wamiliki wa Shule za Msingi za Bweni

PICHA: BORGEN Magazine

TUMESHAURIANA mambo kadhaa ya kuzingatia tunapolazimika kuwapeleka watoto wadogo kwenye shule za msingi za bweni. Kubwa zaidi ni mzazi kujiridhisha na namna shule inavyomwekea mtoto mazingira mazuri yanayofanana na yale ya nyumbani.

Katika makala haya, tunazishauri menejementi za shule zinazotoa huduma za bweni kwa ngazi ya shule ya msingi.  Ushauri huu unatokana na uchambuzi wa matokeo ya tafiti mbalimbali za malezi ya watoto wanaolelewa vituoni (institutionalized child care).

Huduma za msingi

Shule zihakikishe huduma zinazingatia ubora kwa kuyafanya mazingira ya shule yawe na sura ya nyumbani. Watoto wadogo wasichanganywe na watoto wa umri mkubwa katika chumba/bweni moja. 

Mtoto asichangie kitanda na wenzake; aishi na majirani wachache chumbani wanaolingana nae kiumri; apate uangalizi wa karibu kwa mlezi mwenye sifa na anawasiliana kwa karibu na wazazi wake.

Idadi nzuri kwa watoto wa darasa la kwanza mpaka la saba ni watoto wanne kwa chumba kimoja bwenini. Mlezi mmoja aangalie vyumba viwili mpaka vinne kwa watoto wa madarasa ya awali, na vyumba vinne mpaka sita kwa madarasa ya juu. Kufanya hivi kunawawezesha walezi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mtoto mmoja moja kama inavyokuwa nyumbani.

Sifa za walezi

Si kila mtu anaweza kuwa mlezi wa watoto wadogo. Ni muhimu, basi, kupata mtu mwenye moyo wa kuwapenda, kuwajali na kuwatunza watoto bila mtoto kujisikia kusumbuliwa.

Mara nyingi walezi wa kike ambao ni wazazi hufanya vizuri zaidi ya walezi wa kiume. Walezi hawa wanakuwa na uelewa mzuri wa mahitaji mahususi ya watoto kuliko walezi wasio wazazi.

Kadhalika, walezi wasibadilike badilike mara kwa mara. Watoto wanahitaji kuwa na mtu waliyemzoea na kumwamini, waweze kuwa huru naye.  Unapobadili mlezi mara kwa mara, unawapa kazi watoto kumzoea upya hali inayoweza kuwafanya wakakosa amani kuona mtu waliyemwamini anaachana nao.

Pia menejimenti zitambue kuwa uzoefu pekee hautoshi. Ni muhimu kuwaandalia walezi semina za mara kwa mara kuwasaidia kuboresha uelewa wao kuhusu mahitaji ya watoto kiumri.

Utaratibu wa mawasialiano

Mtoto aliyetengwa na familia yake anapungukiwa kitu muhimu kwenye maisha yake. Ukaribu wa kifamilia unamsaidia mtoto kujisikia salama kisaikolojia.

Shule itengeneza utaratibu mzuri wa wazazi kuwasiliana na watoto wao mara kwa mara. Kwa watoto wa madarasa ya awali, ni vyema wazazi wapate fursa ya kuwaona watoto angalau mara moja kwa juma. Kufanya hivi kutawaruhusu watoto kuendelea kuwa karibu na wazazi wao hata katika mazingira ya shule.

Sambamba na hili, wazazi waelimishwe na kimsingi walazimike kuwatembelea watoto wao wanaoishi bweni. Kwa kuwa wapo wazazi wanaoweza kuwatelekeza watoto shuleni kwa miezi kadhaa, shule zinaweza kuweka kigezo cha kumtembelea mtoto kama kigezo cha kuendelea kupata huduma hiyo ya bweni.

Mazingira sisimushi

Shule iweke mazingira sisimushi kwa mtoto. Sambamba na vifaa vya kujifunzia vinavyopatikana kwenye shule nyingi, ni muhimu kuhakikisha watoto wanapata muda mzuri wa kucheza na kufurahia muda wa mapumziko. Shule nyingi zinaweka msisitizo kwenye taaluma na kusahau michezo.

Pia katika kuhakikisha mtoto anajenga uwezo wa kujimudu, shule iwe na ratiba ya kuwawezesha watoto kushiriki kazi za mikono. Badala ya kuwa na watu maalum wa kufanya kazi za nje, ni muhimu mtoto ashiriki kikamilifu. Shughuli kama kufua nguo nyepesi, kusafisha maeneo anayoishi, kutunza bustani, kusafisha vyombo na shughuli nyingine kama hizo.

Kama tulivyoona, wazazi wengi wanakuwa na matarajio makubwa kitaaluma kwa watoto wao. Hali hii inakuwa shinikizo kwa walimu kuweka msisitizo wa kitaaluma ambao wakati mwingine haulingani na uwezo wa mtoto.

Wazazi waelimishwe hasara za kuwa na matarajio makubwa kitaaluma kwa watoto. Hatua hiyo inaweza kuzisaidia shule kuongeza muda wa michezo ambayo nayo ni muhimu kwa ukuaji wa watoto.

Haya yakifanyika, shule za bweni zinaweza kuwa na faida kwa watoto ambao kwa namna moja au nyingine wanalazimika kuondoka kwenye mazingira ya nyumbani kwenda kupata elimu katika shule za bweni.


Makala haya yalichapishwa awali kwenye Jarida la Kisima cha Maarifa linaloandaliwa na Gazeti la Mtanzania.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Haiba ni nini?