Nidhamu ya Mtoto Bila Viboko Inawezekana

PICHA: Pinterest
Adhabu ya bakora ni utamaduni. Kwa wengi wetu bakora ni imani. Tunaziamini kiasi cha kuwa tayari kuzirithisha kwa wanetu kama ambavyo na sisi tumeziridhi kwa wazazi wetu. Kwa hiyo tunapopendekeza mbadala wa bakora kama adhabu iliyozoeleka tunaelewa hili haliwezi kuwa jambo jepesi.

Kama tulivyoona, wazazi tunapowachapa watoto tunaamini lengo ni kuwasaidia wawe na nidhamu. Hata hivyo, kwa kutazama mazingira yanayoambatana na adhabu hii ni dhahiri bakora haiondoi tatizo linalokusudiwa.

Kwanza, hutumika kama njia ya mkato ya kujenga nidhamu ya woga ambayo hata hivyo haidumu. Pili, mara nyingi bakora hutolewa kwenye mazingira ya hasira yasiyokwenda sambamba na mbadala wa tabia inayoadhibiwa.

Kwa kuwa bakora hutolewa kwa msukumo wa hasira, ni rahisi mtoto kuitafsiri kama ugomvi binafsi kati yake na mzazi. Hali hii, kama tulivyoona, hujenga imani potofu kuwa mabavu ndiyo namna sahihi ya kutatua matatizo. Tuone mfano wa Diana.

Ukomo wa bakora

Diana ni mama wa watoto wawili. Frank, mwanae wa pili, ni mkorofi kuliko Salome, mwanae wa kwanza. Salome kwa kawaida ni msikivu na Diana anampenda. Kwa Salome, Diana anasema, fimbo si lazima. Ni mwepesi kusikia na hana ubishi anapoelekezwa kufanya jambo.

Shida iko kwa Frank. Kwa mujibu wa Diana, kila siku lazima angalau amtishie Frank kumlazimisha kuoga, kumlisha na hata kumlaza. Hata nyakati za asubuhi wakati wa kumwandaa kwenda shule, Diana hulazimika kushika fimbo kumtisha Frank achangamke kujiandaa.

Karibu kila anachomwambia Frank kinatanguliwa na fimbo –iwe ni kwa namna ya kitisho au kwa kumchapa kabisa. Wazazi wengi tunaweza kuelewa hali hii. Tumeamini bila bakora mambo hayawezi kwenda.

Ninapomwuuliza Diana kujua kama kweli fimbo zinasaidia, jibu lake lina utata. Ingawa kwa haraka inaonekana Frank hupata usikivu anaposhikiwa fimbo, kimsingi fimbo zimemjenga utegemezi fulani.

Frank anaendelea kuzoea fimbo. Kadri anavyoziona zikitumika ndivyo anavyokuwa jasiri. Amejenga ujasiri kujilinda na maumivu ya kihisia na kimwili. Ili kukabiliana na hali hii, Diana atalazimika kuendelea kushika fimbo kwa muda mrefu ikiwa anataka kuendelea kutumia njia ya hofu na vitisho kama namna ya kupata usikivu wa Frank.

Ingawa njia hii inaweza kuonekana kuwa na ufanisi, kiukweli haiwezi kuwa na msaada wa muda mrefu. Frank atajenga nidhamu ya woga kumridhisha mama yake. Lengo la nidhamu hii bandia atakayoijenga Frank ni kujinasua na matatizo kati yake na mama.

Kwa upande mwingine, Frank anaweza kuamini katika ubabe na matumizi ya nguvu kama namna ya kumsaidia anapokuwa na matatizo na watu. Kadri anavyokuwa mtu mzima, Frank ataendelea kuamini maisha ni mapambano.

Ukikosewa, ni lazima kutumia nguvu kumtisha au kumwuumiza anayekukosea. Matokeo yake Frank anaweza kuwa mwanaume mgomvi kwa familia yake mwenyewe. Yote haya chimbuko lake ni nguvu anazotumia Diana kumrekebisha mwanae kwa nia njema ya kumrekebisha.

Bakora haiwezi kuwa jibu la nidhamu ya mtoto. Maumivu anayoyapata mtoto kwa bakora hayawezi kukupa heshima yako kama mzazi. Kama tulivyoona, kumchapa mtoto huishia kuumiza hisia na mwili wake. Maumivu ya namna hii hayawezi kumfanya mtoto awe na msukumo wa dhati ya kukusikiliza.

Elewa kinachomsumbua

Ni rahisi kuchukua hatua bila kujua msukumo ulio nyuma ya tabia anayoionesha mwanao. Badala ya kumtisha na kumchapa mtoto, jaribu kumwelewa. Naam, mwelewe. Fanya jitihada za kujua kwa nini hasikii unachomwambia. Pengine unatumia vitisho na maumivu kama njia ya mkato kwa sababu haujawa tayari kuingia kwenye ulimwengu wake.

Frank, kwa mfano, hamsikilizi mama yake pengine kwa sababu mama hajawa tayari kujua namna bora ya kuwasiliana nae. Pengine mama amemkatia tamaa Frank na anaonyesha wazi kuwa mwanae hana usikivu. Frank naye anaamua kufanya kama mama yake anavyoamini. Frank kichwani anafikiri, ‘kwa kuwa unaniona mjeuri, basi sina namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuwa mjeuri kama unavyotaka.’

Vipi kama mama yake Frank atamfanya mwanae aamini, ‘mbona kama mama ananiona msikivu?’ Kwa nini mama yake Frank asioneshe matarajio yaliyo kinyume na kile Frank anachokifanya?

Unapomjengea imani mtoto kuwa unamwona kama mtu msikivu, na akakuamini kuwa kweli ndivyo unavyomwona, inaweza kuwa rahisi kwake kubadilika na kupunguza upinzani.

Kwa kutumia mfano wa Frank, kama ataamini mama anamchukulia kama mtu msikivu, hiyo inaweza kubadili mwelekeo wake. Kama tulivyosema, watoto wengi wanapenda kushirikiana na wazazi. Unapomwaminisha kuwa unamtazama kwa jicho chanya, anaweza kabisa kukuthibitishia kuwa hujakosea kumwona hivyo. Huo unaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko.

Ukimheshimu, atakuheshimu

Sambamba na kumwelewa mwanao, fanya juhudi za kumwonyesha kuwa unamheshimu kama binadamu. Kwa mzazi mwingine, hili si jepesi kutekeleza. Wakati mwingine tunafikiri watoto ni wadogo mno kustahili heshima yoyote ya mtu mzima. Hata hivyo, ukweli ni kwamba unapomheshimu mwanao, na akajua hivyo, atakuwa tayari kushirikiana na wewe.

Heshima ni pamoja na kuepuka kuchokoza hisia za mtoto bila sababu za msingi; kutokumdhalilisha mbele za wenzake kwa kumkemea, kumtukana na kumdhalilisha. Heshima ni kumpa muda wako na kutokuonekana ukithamini vitu vingine kuliko yeye. Unapomfanya mtoto aamini unamheshimu, hatakuwa na sababu ya kupambana na wewe na ukalazimika kumchapa.

Kadhalika, mheshimu mwanao kwa kujua msukumo ulio nyuma ya madai yake. Tulishajadili namna kisasi, kutafuta usikivu, kukosa ushawishi na hata kujiona hawezi kuvyoweza kuchangia utovu wa nidhamu. Mpe nafasi ya kuona anaweza kusikika. Mruhusu kuongoza utendaji wa shughuli ndogo ndogo hapo nyumbani kulingana na umri wake.


Mpe nafasi ya kuongoza sala kabla ya kula; mwache aongoze ibada zenu hapo nyumbani; mruhusu kupendekeza mahali pa kutembelea; mtamkie kuwa unampenda; mkumbatie ajisikie yu salama mikononi mwako; weka utaratibu wa kumwezesha kufanya vitu kwa uhuru unaoweza kuudhibiti bila yeye kughamua. Ukiyaratibu vizuri mambo haya na mengine yanayofanana na hayo, utamjenga mtazamo tofauti. Hatakuwa na sababu ya kufanya vituko.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia