Unavyoweza Kutumia Mshahara Kujikwamua Kiuchumi


Wapo watu wanawakejeli wafanyakazi kwa kuajiriwa. Kwamba kama mtu asiye na elimu anaweza ‘kuosha magari mtaani’ na akakuzidi kipato kuna sababu gani kuishi maisha magumu ofisini?

Upo ukweli wa namna fulani. Wafanyakazi wengi wanaishi maisha ya ukata. Kazi yao kubwa ni kupambana kuhakikisha kuwa mishahara inakutana. Katika mazingira ya namna hii, inakuwa vigumu kupiga hatua za maana kimaisha.

Ukweli huo, hata hivyo, hauondoi umuhimu wa kuajiriwa na kufanya kazi chini ya mtu mwingine. Kila mtu ana wito wake katika maisha. Wapo watu wanaoweza kufanya kazi bila kuajiriwa. Kimsingi, watu wa aina hii wana uwezo wa kubuni na kuendesha biashara zao wenyewe. Furaha yao ni kujitegemea na kutengeneza ajira kwa watu wengine.

Lakini pia wapo wenye wito wa kuuza ujuzi kwa wengine. Furaha yao ni kutumia ujuzi walionao kutatua matatizo ya watu katika jamii. Kinachompa daktari utosholevu, kwa mfano, ni kuona anaokoa maisha ya wagonjwa. Mwalimu naye anafurahi kuelimisha jamii.

Mafanikio ya watu hawa ni vile wanavyouza na kutumia ujuzi wao kwa manufaa ya wengine. Unapowashauri waache kazi wakafanye biashara nyingine, kimsingi unawanyang’anya thamani waliyonayo kwa jamii.

Pamoja na umuhimu wa mtu kutambua na kuheshimu wito wa maisha yake, bado fedha ina nafasi kubwa kwenye maisha. Tunahitaji fedha kutatua matatizo mengi. Kwa kuzingatia kuwa hakuna wakati kila mtu atajiajiri, makala haya yanaangazia namna mwajiriwa anavyoweza kujikwamua kiuchumi kwa kutumia mshahara wake.

Mafanikio hayategemei kipato

Wapo wafanyakazi wanafikiri ugumu wa maisha wanaokabiliana nao unasababishwa na udogo wa kipato. Kwamba wangelipwa mshahara mkubwa, basi maisha yao yangebadilika. Dhana hii haina ukweli mkamilifu kama nitakavyofafanua.

Wapo watu wanaolipwa mshahara mkubwa lakini haukutani na mshahara unaofuata. Kinyume na hao, wapo wafanyakazi wanaolipwa mishahara midogo, lakini wanaweza kufanya mambo yanayoonekana.

Tofauti ya makundi haya mawili si kipato bali namna wanavyotumia kile wanachokipata. Unapoelekeza kipato chako kwenye matumizi ya kila siku ni dhahiri utahitaji kiasi kikubwa cha fedha ili ufanikiwe kuweka akiba. Maisha yasiyolingana na kile unachopata hayawezi kukutoa kwenye umasikini.

Kwa mfano, mtu mwenye mshahara wa Tsh milioni moja kwa mwezi anapoamua kuishi kwenye nyumba inavyomgharimu Tsh 200,000 kwa mwezi; akatumia Tsh 200,000 kuendesha gari la mkopo; akatumia Tsh 300,000 kulipa mkopo kila mwezi mtu huyu atakuwa anaishi maisha yasiyolingana na kipato chake. Kwa hakika ataishi katika ‘umasikini wa kisomi’ kwa muda mrefu.

Kwa nje, kijana huyu anaweza kuonekana ‘mambo safi.’ Jamii inaweza kumheshimu kwa sababu kwa haraka haraka mafanikio yake yanaonekana. Anaendesha gari (ya mkopo); anaishi mitaa wa wenye hadhi; anapumzika kwenye maeneo ya gharama kubwa lakini katika hali halisi ‘mafanikio’ hayo hayapo.

Tunasema hana mafanikio kwa sababu mbili. Kwanza, kipato kinaishia kugharamia mahitaji ya msingi katika maisha. Pili, kipato hicho hakiwezi kutosha kuweka akiba itakayowekezwa kwa ajili ya kuzalisha.

Mazingira ya namna hii yanaweza kumshawishi kukopa kwa watu (mara nyingi wenye kipato kama chake) ili asukume maisha. Matokeo yake ni kuendelea kujididimiza kwenye kifungo cha madeni zaidi yatakayomnyima amani.

Pia, katika mazingira haya, mtu huyu anaweza kukosa utulivu kazini na kufanya maamuzi ya kuacha kazi katika jitihada za kutafuta kipato zaidi. Lakini hata anapopata kazi nyingine, maisha yanaweza kubaki kuwa yale yale kwa sababu tatizo linaweza kuwa namna anavyotumia kidogo anachokipata.

Mbinu za kujikwamua

Tunahitaji elimu ya msingi ya fedha ambayo pengine ni vigumu kuipata kupitia mfumo rasmi. Fedha, kwa kawaida, inaongozwa na kanuni zake. Ukiziheshimu, unaweza kuimudu fedha na ikakufuata. Unapozivunja kanuni hizo,unaweza kutumia muda mrefu kuitumikia fedha.

Kinachoongoza kanuni hizi, kwa mujibu wa wataalam wa uchumi binafsi, ni nidhamu ya fedha. Bila kujali kiasi cha fedha unachokipata kwa mwezi, unahitaji uwezo wa kutokukubali mtindo wako wa maisha ubalishwe na ongezeko lolote la kipato.

Ukifanikiwa kuwa na nidhamu hiyo, kiasi chochote cha fedha kinaweza kukupa usalama wa kipato. Hapa kuna mambo kadhaa ya kuzingatia.

Jifunze kuweka akiba. Usifanye matumizi ya kawaida kabla hujaweka akiba. Unapopata mshahara elekeza asimilia fulani kwenye akiba na kinachobaki kipangie matumizi. Unapoweka akiba kwa mtindo huu, ni sawa na kujilipa ili ufanye mambo ya maendeleo.

Pili, punguza matumizi ya kila siku kwa kujiruhusu kuishi maisha ya kawaida kwa kipindi fulani. Wafanyakazi wengi hutamani kutetea hadhi za ofisi wanazofanyia kazi kwa kuishi maisha ya hadhi kubwa. Matokeo yake wanajikuta wakifanya maamuzi yanayoweza kuwagharimu.

Mfano, kijana anapoanza kazi anakuwa na shauku ya kujenga taswira ya mtu aliyefanikiwa. Shauku hiyo itamsukuma kutamani kuendesha gari ili awe na hadhi inayolingana na kazi anayoifanya. Kwa hiyo anapopata fursa ya mkopo kazini, kijana huyu kwa haraka atawaza kununua gari.

Anaweza kuwa na sababu nyingi za kuhalalisha maamuzi yake hayo. Labda atasema gari itamsaidia kutatua tatizo la kuchelewa kazini. Lakini ukweli halisi ni kwamba angeweza kuendelea kutumia usafiri wa umma kwa muda fulani wakati akijenga misingi imara ya kiuchumi.

Changamoto anayoweza kukabiliana nayo kijana huyu inaweza kuwa kubwa kuliko faida ya ‘kutatua tatizo la usafiri.’ Kwanza atalazimika kulipa mkopo na riba yake kwa muda mrefu hali inayoweza kumfanya asiweze kufanya chochote kwa miaka kadhaa. Maamuzi ya namna hii huchangia umasikini wa wafanyakazi.

Tatu, fikiria kuwekeza ujiongezee kipato. Tumia ujuzi wako kujiongeza kiujasiriamali. Maarifa na ujuzi ni mtaji. Si lazima ufanye uchuuzi. Tumia ujuzi wako kufanya kitu cha ziada. Usikae ukimlilia mwajiri akuongezee kipato. Jiongoze.

Faida waliyonayo wafanyakazi wengi ni mikopo. Kama sio kupitia mwajiri, kuna vyama vya kuweka na kukopa. Tumia fursa za mikopo kwa faida. Wekeza unachokopa badala ya kununua vitu visivyokuzalishia. Hiyo ndiyo namna rahisi ya kujikwamua.


Kisingizio cha wafanyakazi wengi ni kukosa muda wa kufanya mambo mengine. Ni suala la kubadili mtazamo tu. Hulazimiki kuacha kazi ili ukafanye biashara. Unaweza kufikiri kufanya kazi kwa kushirikiana na watu wanaofanya biashara tayari. Ukiwekeza hatua kwa hatua, unaweza kupata mafanikio ukiwa kazini. 

Makala haya yamechapishwa awali kwenye Jarida la Ajira na Kazi linaloandaliwa na gazeti MWANANCHI kila Ijumaa.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia