Unavyoweza Kumfundisha Mtoto Kuwa Mkweli

PICHA: Heaths Haven

Fikiria uko jikoni ukiandaa chakula cha jioni. Watoto wako wawili wadogo Fred na Joe wanacheza sebuleni. Salome yuko mezani akifanya kazi za shule.
Mara unasikia mlio wa kitu kuvunjika sebuleni. Unapatwa na wasiwasi. Unakwenda haraka kujua kilichotokea. Maji yanatiririka sakafuni. Chupa ya chai imedondoka na kupasuka. Unakasirika.

Fred, mwanao mdogo, haonekani kuwa na wasiwasi. Haraka anamsemea mkubwa, ‘Sio mimi mama…ni Joe!’ Kwa hasira unamtazama Joe. Uso wake kweli unaonyesha wasiwasi.  Kwa ukali unamwuuliza, ‘Wewe ndo’ umevunja chupa?’
Anasita. Amejaa wasiwasi. ‘Nauliza ni wewe?’ unarudia. Kwa haraka anajibu huku akitikita na kichwa, ‘A-a-a! Sio mimi mama!’
‘Nani amevunja chupa?’ Unauliza kwa hasira kali. Mdogo anasisitiza, ‘Ni Joe!’ Unamshika mkono kwa ghadhabu kubwa huku ukilalamika, ‘Kwa nini umevunja chupa?’
Salome anaona aokoe jahazi. ‘Usimchape Joe mama. Aliyevunja chupa ni Fred!’ ‘Fred?’ Unakasirika kudanganywa na mtoto wa miaka miwili. Mbaya zaidi haonekani kujutia anachokifanya.

Hatari ya uongo

Kwa nyakati na sababu tofauti watoto wote hudanganya. Kudanganya ni kusema uongo. Ni kutoa habari zisizo za kweli.

Uongo ni dhambi. Uongo huumiza watu. Uongo unaharibu uhusiano wetu na watu. Mtu mwongo haaminiki.  Hakuna mzazi anaweza kuvumilia kuona analea mtu ambaye hataaminika kwa jamii.

Tabia ya uongo ikiachwa ikomae ni hatari kwa mstakabali wa mtoto. Kama mzazi unayetamani kukuza mtoto mwadilifu atakayeaminiwa na watu ni lazima kuushughulikia mapema.

Sababu za watoto hudanganya

Hatuzaliwi na tabia ya kudanganya. Tunajifunza. Bahati mbaya, tunapoanza kujifunza uongo, nia huwa ni ‘njema.’ Mtoto wa miaka miwili, kwa mfano, hajui maana ya kusema uongo. Anapodanganya, akili yake haikusudii kudanganya.

Fred tuliyemwona hapo juu hakuwa na lengo la kudanganya. Mazingira yalimlazimisha kudanganya. Kimsingi kwa umri wake, hana uwezo wowote wa kutunga uongo.

Fred anatamani angechukua nafasi ya Joe. Anajua kabisa kuvunja chupa ni kosa kwa sababu mama amekasirika. Hatamani kuwa upande wa kumwuudhi mama yake.

Kwa sisi watu wazima Fred anadanganya. Lakini yeye haoni hivyo. Anatumia ‘uongo’ kusema matamanio yake. Anaposema, ‘Ni Joe’ maana yake anatamani angekuwa Joe. Hapendi matokeo ya kile alichokifanya.

Sababu ya pili, mtoto hutumia uongo kama namna ya kulinda uhusiano wake na mzazi. Kwa mtoto, uhusiano na mzazi ni kitu cha maana kuliko kitu kingine chochote kinachostahili kulindwa kwa gharama yoyote.

Kufanya kosa maana yake ni kuhatarisha uhusiano wake na mtu wa muhimu zaidi kwenye maisha yake. Kwanza, anajua matokeo ya kukiri kosa maana yake ni kukaribisha adhabu. Ili awe salama lazima aseme kile anachojua ndicho mzazi anachokinatarajia. Kudanganya ni kuepusha shari na mzazi wake.

Pia mtoto mkubwa kidogo huweza kutumia uongo kama silaha ya kupambana na wabaya wake. Hudanganya kama namna ya kumwuumiza mtu mwingine.

Kwa mfano, anapoamini mdogo wake anapata upendeleo, anaweza kutumia uongo kujaribu kumwingiza mwenzake kwenye matatizo. Anachoamini ni kuwa wazazi wanapokosa imani na mwenzake, yeye anakuwa kwenye nafasi nzuri.

Tufanyeje kuondoa tabia ya uongo kwa watoto? Tuangazie kanuni nne kubwa.

Usimfanye akudanganye

Unaweza kuchochea tabia ya uongo bila kujua kwa kuuliza maswali yanayoweza kumfanya mtoto ashawishike kukudanganya.  Kwa mfano, unamwona mtoto anakula bila kuombea chakula kama ulivyomwelekeza. Usiombe akudanganye kwa kumwuuliza kama ameshaombea chakula.

Kumbuka kuwa fahari ya mtoto ni kukupendeza wewe mzazi. Unapomwuuliza swali kama hilo unamshawishi kukudanganya ili asipoteze sifa za kuwa ‘mtoto mzuri kwako.’

Badala ya kuomba kudanganywa kwa maswali ya uchokozi, shughulika na kosa moja kwa moja. Mwonyeshe kosa lake na mwelekeze afanye nini. Ikiwa kosa linastahili adhabu fanya hivyo.

Mrekebishe anapodanganya

Kupuuza uongo ‘mdogo’ unaoubaini kwa mwanao ni kukomaza tabia ya uongo wa makusudi mbeleni. Shughulika nao kila unapojitokeza. Hapa kuna njia mbili.

Mosi, kama mwanao tayari ana uelewa, zungumza nae kirafiki uelewe kwa nini amekudanganya. Ikiwa anadanganya kwa lengo la kukupendeza, pengine shida ni namna unavyoshughulikia makosa yake. Jifunze kumrekebisha kwa njia za kirafiki.

Pili, ikiwa mwanao anadanganya kwa nia ya kuwakomoa wengine, mwadhibu. Jambo la kuzingatia ni kwamba si wakati wote adhabu husaidia. Mtoto anaweza kukwepa ghadhabu zako kwa kukudanganya. Jirekebishe.

Hata anapokuwa amekudanganya, tumia lugha inayoonyesha kuwa bado una matarajio chanya na yeye. Epuka kumwita majina kama ‘mwongo wewe’ ‘nilijua utanidanganya.’ Unapofanya hivyo anaona tayari umemweka kwenye kundi la waongo. 

Usimwadhibu kwa kusema ukweli

Unafanyaje mtoto anapokwambia ukweli unaothibitisha kuwa amekosea? Mfano, mtoto amekiri kuwa ndiye aliyevunja sahani. Unamwadhibu kwa sababu alichofanya ni kosa?

Katika mazingira haya unalazimika kufanya mazungumzo ya kirafiki kuliko kuadhibu. Unapoadhibu fikiria ujumbe usiowazi unaoutuma kwake. Adhabu inaweza kuwa na maana, ‘ni hatari kuwa mkweli.’ Siku nyingine atakudanganya kuepusha shari.

Badala ya kutumia adhabu kama suluhisho, zungumza nae ajue kosa lake. Kisha onyesha kuelewa kwa nini amefanya kosa na mpongeze kwa kuwa mkweli. Unapofanya hivyo hulei makosa yake bali unampa motisha ya kuwa mkweli.

Onyesha mfano mzuri

Mtoto hawezi kuwa tofauti na mzazi wake. Usipokuwa na tabia ya kusema ukweli hata katika mazingira magumu, unamfundisha mtoto kudanganya. Unapoahidi jambo kwa mwanao, tekeleza. Ikitokea umeshindwa kutekeleza, omba msamaha.

Usitumie uongo kufunika makosa yako. Anapouliza swali gumu, mpe maelezo rahisi ya kweli badala ya uongo ‘mzuri’ ambao, hata hivyo, anaweza kuugundua baadae.

Kadhalika, usiwadanganye watu mbele yake. Usimpe mtu majibu ambayo mtoto atajua ni ya uongo. Mfano, uko nyumbani umepigiwa simu na mkuu wako wa kazi akiuliza uliko. Unaposema uko ofisini na mtoto anakusikia, mtoto ataona uongo ni sehemu ya maisha. Usishangae akikudanganya na wewe siku nyingine.  


Maoni

  1. Asante mwalimu.Wazazi tuwe wakweli ili watoto nao watuige

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Pay $900? I quit blogging