Ayafanyayo Mzazi Huamua Atakavyokuwa Mtoto

PICHA: Pinterest


'Mwanangu ni mtundu haijapata kutokea’ alilalamika msomaji mmoja wa safu hii. Sikuelewa ana maana gani aliposema mwanae ni mtundu. Nikaomba ufafanuzi. ‘Hasikii. Jeuri asikwambie mtu. Usipomfanyia purukushani huwezi kumwambia kitu akasikia.’ Kwa mujibu wa maelezo yake, kuna nyakati hubidi amtishe, amwadhibu vikali na hata kumtukana ikibidi.

‘Hao watoto unaowaongelea sio huyu wangu. Huyu ni mkorofi. Ukisema nimsikilize kama unavyoshauri ndio unaharibu […] Akiona fimbo ndio kinaeleweka.’ Nilitamani kujua kama mbinu hizo anazotumia zimesaidia.

‘Kidogo. Nikimshikia fimbo ndio tunaelewana. Ukienda hivi hivi hana anachoelewa […] Shida yake kubwa ni utukutu. Ni mwongo sijapata kuona.’

Mzazi huyu anawakilisha mtazamo wa wazazi wengi. Imejengeka imani kuwa watoto wanazaliwa na tabia zao. Wapo watoto kwa ‘asili’ ni wakorofi na watundu wakati wapo pia watoto wapole na wasikivu.

Ni dhahiri kuwa vinasaba vina mchango wake kwenye kuumba tabia zetu.  Kama ambavyo huwezi kuamua kimo cha mwanao, huwezi pia kuamua mustakabali wa tabia fulani za mtoto kwa asilimia mia moja.

Tunafahamu, kwa mfano, kuna watu wana ukali usioelezeka. Pamoja na kulelewa kwenye familia yenye watu wapole, anaweza kutokea mtu mwenye hasira kali. Ukimgusa anawaka kwa ghadhabu. Katika mazingira kama haya, inaonekana upo uwezekano wa kurithi tabia fulani fulani.

Hata hivyo, watafiti wa tabia za mwanadamu wanakubaliana kuwa mazingira ya kimalezi anamokulia mtoto nayo yana mchango mkubwa katika kuchonga tabia zetu. Hata pale inapoonekana watoto wamerithi tabia kwa wazazi wao, kimsingi wanakuwa wanaakisi kile wanachokiona kwa wazazi wao.

Makala haya yanaangazia makundi manne ya tabia za watoto yanayotokana na mazingira ya kimalezi. Kimsingi, hoja ni kuwa hulka anazokuwanazo mzazi ndizo zinazochangia kutengeneza tabia ya mtoto. Lengo si kujenga hatia kwa wazazi bali kutusaidia kuelewa mchango wa yale anayoyafanya katika kujenga mustakabali wa mtoto kitabia.

Mtoto mtulivu mwenye uchangamfu

Huyu ni mtoto mwenye utulivu na kwa hakika anajiamini. Huwa ni mchangamfu kwa watu kwa sababu anapenda watu. Ukitaka kupima upendo wa mtoto huyu kwa watu, mpe kitu. Ni mwepesi kuwapa wenzake. Ingawa kuna umri fulani kila mtoto huwa na ubinafsi, mtoto wa kundi hili anapozidi miaka miwili, anakuwa mwepesi kuwapa watu kile alichonacho. Sababu ni kuwa anawaona wengine kuwa bora kama alivyo yeye.

Pia, hana ugomvi wala usumbufu. Tangu anapokuwa mdogo, huwezi kusikia akilia lia bila sababu. Hata pale anapolia ni rahisi kumtuliza. Kwa mfano, anapoachwa na mzazi wake, anaweza kulia kama watoto wa makundi mengine tutakayoyaona lakini ni mwepesi ‘kusahau’ na kuendelea kucheza. Mama anaporudi baadae, mtoto huyu humchangamkia.

Kwa ujumla, utulivu wa mtoto huyu si wa kuzaliwa. Ni matokeo ya malezi yanayomwelewa, yanayomshirikisha, yanayomkubali vile alivyo na yanayomweka karibu. Kisaikolojia tunasema mtoto huyu ana nafsi iliyotulia. Anajisikia kama mtu aliyeshiba asiye na njaa ya ‘kueleweka’, ‘kushirikishwa’ ‘kukubaliwa’ na ‘kupendwa.’

Mtoto mkimya ‘asiyependa’ watu

Huyu ni mtoto anayejiamini kama yule wa kundi la kwanza lakini ana tatizo la kujiona bora kuliko wengine. Kwa kawaida hana tabia ya ugomvi, lakini hupenda kujitenga na watu kufanya mambo yake. Kinachomfanya apende kuwa ‘kivyake’ ni kutokuamini uwezo wa watu wengine. Hana imani watu wanaweza kuwa na msaada wowote kwake. Ndani yake anajiona yuko sahihi mara nyingi, anajitosheleza na hahitaji sana msaada wa wengine.

Mara nyingi ni mkimya na hana maneno mengi sana, ingawa wakati mwingine akimzoa mtu na kumwamini anaweza kuwa mwongeaji. Shauri ya kupenda kuzingatia kile anachokifanya, anaweza kuwa na uwezo mzuri kiakili wazazi wakimwelekea mazingira sisimushi.

Unaweza kumgundua mtoto wa kundi hili tangu akiwa mdogo. Si mtoto wa kulia lia bila sababu kama yule wa kwanza, lakini sababu yake kuu ni kutokujali ukaribu wake na watu wa karibu. Anapoachwa anaweza kulia kama watoto wengine, lakini mama anaporudi, huwa haoenekani kujali.

Tabia hii ni matokeo ya mchanganyiko wa malezi yasiyojali (yanayopuuza) hisia zake lakini yenye kumshirikisha kwa namna fulani. Kwa mfano, mtoto anapokuja kukulalamikia, huonekani kujali hisia zake. 

Mzazi unapokuwa huna tabia ya kuonyesha kuelewa hisia za mtoto kwa hakika unamfanya mtoto aamini watu hawaelewi hisia zake. Mara nyingi atajijitetea kwa kupenda kuwa kivyake vyake. Kukosa uchangamfu na watu ni lugha ya kusema kuwa watu hawamwelewi.

Mtoto ‘mpenda watu’ asiyejiamini

Huyu ni mtoto anayependa watu kama mtoto wa kundi la kwanza. Tatizo lake ana hulka ya kuwaona wengine kuwa bora kuliko yeye. Ndani yake anajisikia kukosa kitu fulani na anaamini watu wengine watamsaidia kukipata hicho anachokikosa. Kwa hiyo, anapenda sana michezo na kuwa na marafiki zake. 

Mtoto wa namna hii anaweza kuonekana mpole na mwenye haya (aibu) anapokuwa na watu anaoamini hawamwelewi. Lakini anapokutana na watu wanaomwelewa, ni mchangamfu na mwongeaji kuliko kawaida. 

Wapo wa kundi hili, hawana uwezo wa kuwachangamkia watu hata kama ndani wanatamani kuchangamka. Wanatamani marafiki lakini hawawezi kuwakaribia. Kimsingi mtoto wa kundi hili anajisikia upweke ndani yake na anajaribu kufidia hisia za upweke ndani yake ama kwa kujichanganya na watu au kwa kutamani kujichanganya na watu.

Huyu ni mtoto aliyeathirika na tabia ya utoro wa wazazi (wasiopatikana kimwili.) Mtoto wa kundi la pili, ana wazazi wanaopatikana lakini hawaelewi hisia zake. Huyu wa kundi hili ni tofauti. Wazazi wake wanaonekana kuelewa hisia zake na anajua wanampenda, lakini muda mwingi hawapo.

Kwa sababu mtoto angependa kuwa karibu na wazazi wake, ndani yake anajisikia kukosa kitu muhimu anachojua kinapatikana kwa watu wengine. Hii ndiyo sababu ya yeye kupenda ‘kujichanganya’ sana na watu wengine. Uzungumzaji na kupenda watu unamsaidia kufidia hali ya kukosa uwepo wa mzazi.


Mtoto mkorofi na mgomvi

Huyu ni mtoto asiyejielewa. Hujiona hana thamani na wengine wanaomzunguka hawana maana pia kama alivyo yeye. Ni mtoto anayejidharau na kudharau wengine. Hana hisia na haelewi hisia za wengine na ndio sababu huwa mgomvi na mtundu.

Ukimchunguza mtoto huyu ni kama anafurahia kuwaona wengine wakiumia. Huwachokoza wengine na hata kuwatukana almuradi ajisikie ‘mbabe.’ Ni mchoyo hasa kama amekulia kwenye mazingira ya umasikini na huwa ni mbinafsi.

Kimsingi huyu ni mtoto anayelelewa kwenye mazingira ya mabavu na udhalilishaji. Mfano wazazi walevi wenye tabia ya kupigana na kutukanana mbele yake. Pia wazazi wakali kupindukia wanaangukia kwenye kundi hili.

Aidha, wakati mwingine wazazi hawatambui kuwa wanawalea watoto wao kimabavu. Ndani yao mna hasira na maumivu wasiyoyatambua na huwatumia watoto kama namna ya kufidia maumivu waliyonayo. Matokeo yake, wanakuwa wepesi hutukana na kutumia nguvu kubwa kuwaadhibu watoto bila kung’amua wanachokifanya.  


Inaendelea

Maoni

  1. Ni kweli kabisa mwalimu, maana wazazi wengi kutumia hasira katika kuwaonya watoto, kumbe tatizo ni wao, laiti wangejua/tambua tatizo ni wao, hakika malezi mabovu ya watoto yangepungua.Ahsante maana umenifungua akili japokua zipo katika ndoa.

    JibuFuta
  2. Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.

    JibuFuta
  3. Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?