Namna ya Kuutambua Wito wa Maisha Yako

PICHA: Baha'i Blog

Umewahi kufanya kazi zenye heshima lakini hujisikii ridhiko ndani yako? Unapata kipato kizuri na watu wengine wanatamani kufanya unachokifanya lakini wewe mwenyewe hufurahii. 

Unakuta umesoma vizuri lakini huoni thamani ya kile ulichokisoma. Zaidi ya kutaja chuo ulichosoma na ngazi ya elimu uliyofikia huoni namna gani elimu yako inakusaidia kutoa mchango kwa jamii.

Lakini pia inawezekana umejitahidi kupenda hicho ulichokisoma. Ni kawaida ukifanya kitu kwa muda fulani akili inaweza kukulazimisha kukipenda. Shida ni ubunifu. Unapofanya kitu ambacho sio wito wako huwezi kuwa na ubunifu zaidi ya kukariri kile ulichofundishwa na mwalimu wako. Unakuwa kama umefungwa na nadharia.

Katika maisha mazingira yana nafasi kubwa ya kutulazimika kufanya kisichotoka ndani. Tunajikuta tukifanya mambo yasiyoendana na wito wetu. Tunakuwa wepesi sana kusikiliza maoni ya watu wengine kuliko kujua kile kilichojificha ndani yetu.

Matokeo yake tunaishi maisha ya wengine. Tunawaiga wale tunaodhani wanaheshimika kwenye jamii. Tunafanya tunachofikiri watu wanakitarajia kwetu. Tunasoma kozi fulani kukidhi matakwa ya watu. Tunajikuta tunataka kufanya kazi zinazotarajiwa na jamii. Tunaishi wiito ya watu wengine.

Tunasahau kuwa mwanadamu ni mtu wa pekee. Wewe unayesoma hapa ni mtu wa pekee. Mungu ameweka vitu vya pekee ndani yako. Unahitaji kuvijua ili vikuongoze kufanya maamuzi ya msingi katika maisha.

Tufanye nini kutambua vitu alivyoviweka Mungu ndani yetu? Kuna mambo mengi ya kuzingatia. Hapa naleta kwako maswali matatu unayohitaji kuyajibu.

Una vipaji gani?

Kila mtu ana vipaji vyake. Unaweza usikifahamu kipaji chako lakini hiyo haimaanishi huna. Tunapoongelea kipaji usifikiri vitu vikubwa ukachanganyikiwa.

Kipaji ni ule uwezo wa kufanya vitu kwa namna rahisi ambayo watu wengine hawawezi. Ni ule ujuzi unaokuwa nao bila hata kufundishwa sana.

Kwa mfano mwimbaji. Hahitaji kwenda kusomea ili ajue namna gani aimbe. Ni uwezo wa kuzaliwa nao. Akienda shule kujinoa zaidi inakuwa vizuri. Lakini elimu inakuwa kama inajazia kitu ambacho tayari anacho tayari. Asiye na kipaji anapokwenda kusomea kitu inakuwa kama kumfundisha sungura namna ya kupaa angani kama kunguru.

Tafakari vipaji alivyokupa Mungu. Pata nafasi ya kujikagua ndani yako. Una kipaji gani? Je, ni kuwashawishi watu? Kuchora? Mbunifu? Fundi? Mwandishi? Mwalimu? Biashara? Tambua kipaji chako.

Kitu gani kinakuvutia?

Pengine kujua kipaji inaweza kukuwia vigumu kwa sasa. Najua si kazi rahisi na wakati mwingine inahitaji muda. Lakini angalau kila mmoja wetu anaweza kujua kile anachopenda kukifanya. Nikikuuliza unavutiwa na nini kwenye maisha huwezi kupata shida.

Kila mtu ana vitu vinavyomvutia. Ndivyo hata wewe ulivyo. Kuna vitu vinakuvutia. Unapenda kuvifanya vitu fulani kwenye muda wako wa ziada. Mfano mimi hapa napenda kuandika. Nikiwa kwenye mapumziko kuandika. Ndiyo furaha yangu kujieleza. Kuandika ni moja wapo ya vitu vinavyovipenda.

Kipimo kuwa unapenda kitu fulani ni utayari wako wa kukifanya bila malipo. Unaridhika tu kukifanya hata bure. Nikijitolea mfano mwenyewe, sisubiri kulipwa ili niandike. Navutiwa na maandishi.

Mwimbaji hali kadhalika maisha yake ni kuimba. Huhitaji kumlipa ili aimbe. Mwalimu naye huhitaji kumlipa ili akuelekeze kitu. Kufundisha ndiyo maisha yake. Wewe unavutiwa na nini? Lazima ukifahamu.

Kusema hivi haimaainishi tusilipwe kwa sababu tu tunapenda tunavyovifanya. Hapana. Tunachokisema ni kupenda kitu kwa dhati kabisa.

Labda mpaka hapa bado huelewa unavutiwa na nini. Nikupe kipimo kingine. Hebu  fikiria watu maarufu wanaokuvutia. Nani unampenda?  Mimi nawapenda wengi. Mmoja wao anaitwa Rick Warren. Nimejifunza vingi kwake. Mwingine Stephen Covey. Nimesoma mawazo yao mengi.

Usiishie kusema nampenda fulani. Nenda hatua moja mbele. Tafuta sababu kwa nini unawapenda watu hao. Kwa mfano mimi hao jamaa niliokutajia nawapenda  kwa sababu ya misimamo yao kwenye maisha. Kila nikisoma na kusikiliza mawazo yao kuna kitu wanachokisema hakibadiliki. Kinanivutia kwao.

Na wewe lazima ujiulize kwa nini unavutiwa na hao uliowafikiri hapo juu. Hicho kinachokuvutia chaweza kuwa ndio ni sehemu ya kitu unachokipenda kwenye maisha. Huo ndio wito wako.

Maamuzi gani yanakupa kuridhika?

Kwa kuwa zipo sababu nyingi zinaweza kukufanya ukavutiwa na kitu lazima kuongeza kipimo cha kupima udhati wa msukumo ulio ndani yako. Hapa tunaongelea kuchukua hatua ngumu lakini zinazokupa kuridhika.

Kuridhika ni kujisikia utoshelevu na kitu unachokifanya.  Hapa hatuongelei utoshelevu wa kuwaridhisha watu. Hatuongelei kuamua kufanya kitu fulani unachojua kuna watu wanatarajia ukifanye. Hatuongelei msukumo wa kuridhisha watu unaowapenda.

Tunaongelea msukumo wa kimaamuzi unaoanzia ndani yako kukushawishi kufanya vitu unavyodhani ni vya muhimu kwako bila kuangalia wengine wanasemaje. Hiki ndicho kipimo cha juu cha wito wako. Utayari wa kulipa gharama za kuutumikia wito wako.

Maamuzi  haya mara nyingi ni yale yatakayobadili maisha yako. Mfano kuacha kazi na kubadili fani uliyosomea. Si jambo jepesi. Inahitaji moyo. Fikiria mtu anayeweza kuamua kuacha kazi. Lazima awe na sababu kubwa kiasi cha kutokuwa na woga na changamoto zinazoweza kuambatana na maamuzi yake.

Maamuzi haya yanaweza kuwa na changamoto kadhaa. Changamoto ya kwanza ni kupishana na hata kuachana na baadhi ya watu wa muhimu kwenye maisha yako. Mara nyingi si kila mtu atauelewa wito wako. Watu hawataelewa mantiki ya unachokifanya. Watu wanakuona kituko. Lakini ndani yako unajua unafanya kitu sahihi.

Hata hivyo si mara zote unapouendea wito wako mambo yatakuwa mepesi. Unakumbata na changamoto nyingi. Lakini kama umeupambanua wito wako vizuri hutarudi nyuma hata kama mambo yatakuwa magumu namna gani. Utaendelea kusimama imara huku ndani yako ukiwa na amani.

Kama bado hujaweza kufanya maamuzi mazito kwenye maisha yako; kila mtu anaelewa kile unachokifanya; unapend kufanya kitu kwa sababu tu wengi wanakipendekeza; unafanya kufanya kitu usichokipenda au unajaribu kufanya vitu vingi kwa wakati moja, inawezekana kabisa bado hujautambua wito wako. 

Rudi ndani yako tafakari wito wako. Jielewe. Fanya maamuzi ya kuufuata wito wako. Ukifanya kitu ulichopaswa kukifanya, utakuwa mtu mwenye utoshelevu mkubwa. 

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Kama sio utumwa ni nini hiki?