Mbinu Nne za Kukuza Ubunifu wa Mtoto
Ubunifu ni uwezo wa kufikiri, kutafuta majibu au
kutatua changamoto kwa namna isiyotarajiwa. Mtu mbunifu hufanya mambo kwa namna
isiyo ya kawaida. Hafanyi vitu fulani kwa sababu ameona watu wakifanya. Hafuati
mazoea wala uzoefu. Huwa tayari kufanya mambo mapya.
Ingawa kuna uhusiano mdogo kati ya ubunifu na uwezo
wa jumla wa akili, kwa kawaida, mtu mwenye akili si lazima awe mbunifu. Unaweza
kuwa na akili ya kuchambua, kuelewa, kukumbuka na kueleza mambo unayojifunza
lakini usiweze kufanya mambo kinyume na mazoea.
Ubunifu unaonekana kwa namna mtu anavyoweza kufikiri
na kupendekeza njia mbalimbali za kutatua tatizo. Kwa mfano, mtu mbunifu
anapokutana na changamoto ya kukosa chakula, anaweza kufikiri mbinu mbalimbali
za kumsaidia kupata chakula anachokihitaji. Mwenzake asiye mbunifu, huwa na
mbinu moja na ikishindikana hana namna ya kujinasua.
Elimu rasmi inayopatikana darasani, kwa kawaida,
haikusudiwi kumjengea mwanafunzi uwezo wa kubuni mambo mapya. Mitaala yetu
inafundisha kufikiri kwa namna inayofanana, kutoa majibu yale yale na wakati
mwingine kufumbua matatizo yanayoyofahamika tayari.
Mitihani inayopima uelewa wa mwanafunzi, kwa mfano,
inatafuta majibu yanayotarajiwa. Kwamba mwanafunzi hatarajiwi kufikiri kinyume
na matarajio ya mwalimu wake maana yake ni vigumu kwa uwezo wa kubuni kukuzwa kupitia
mitaala rasmi.
Hata hivyo, ubunifu ni muhimu katika maeneo karibu
yote ya kimaisha. Taaluma. Uhusiano. Kazi. Uongozi. Maeneo karibu yote
yanahitaji majibu mapya yasiyotegemea uzoefu.
Ubunifu unamsaidia mtu kupambana na changamoto zake
kwa namna nyepesi. Ubunifu si tu ni muhimu kwenye sanaa, lakini pia unayo
nafasi yake katika kila nyanja ya maisha yetu ya kila siku. Bila ubunifu ni
vigumu kwa mtu kuendana na mabadiliko tunayokabiliana nayo kila siku
yanayohitaji majibu mapya.
Tafiti zinaonyesha kuwa ubunifu ni uwezo unaotegemea
mazingira ya kimakuzi anayokutana nayo mtoto. Wazazi, kwa sababu hiyo,
wanahitaji kujifunza namna ya kujenga uwezo huu. Vile watoto wanavyoelelewa,
inaweza kudumaza uwezo wao kiubunifu au kuukuza. Makala haya yanapendekeza
mbinu nne kubwa unazoweza kuzitumia kukuza ubunifu wa mwanao.
Mruhusu
mtoto akutane na changamoto
Kwa kawaida, binadamu hatupendi changamoto. Tunazikwepa.
Tunapopata mafanikio, hatutamani tukabiliane na changamoto. Tunayachukulia
mafanikio kama hatua ya juu inayotunusuru na changamoto. Kwa hivyo, tunajitahidi
sana kuwanusuru wanetu wasikutane na changamoto. Tunafikiri changamoto hazipaswi
kuwa sehemu ya maisha ya mtu aliyefanikiwa.
Hata hivyo, kisaikolojia, changamoto zinahitajika.
Changamoto zinajenga hamasa ya kufanya kitu. Changamoto zinaongeza uwezo wa
kufikiri. Akili ya mtu mwenye uhitaji unafanya kazi kwa kasi na ufanisi
kutafuta majibu. Mtu asiye na uhitaji hahitaji kutumia akili nyingi kutafuta
majibu asiyoyahitaji.
Ni kwa sababu hiyo, mzazi unahitaji kuweka mazingira
yanayomhamasisha mtoto kufikiri. Mfano, badala ya kumpatia kila anachokihitaji,
mnyime baadhi ya vitu anavyofikiri ni vya muhimu kwake. Mpe fedha zisizomtosha.
Punguza kumfanya ajione anaweza kupata chochote anachokihitaji.
Unapofanya hivyo, unamjengea kiu ya kutafuta mbinu
za kutumia kisichomtosha. Changamoto, kwa maana hiyo, zinamfanya atafute majibu
yasiyotarajiwa. Huo ndio ubunifu.
Mpe
uhuru, punguza ukosoaji
Ni kawaida kwa wazazi kujaribu kuwadhibiti watoto.
Kuna namna fulani ya hofu kuwa unapompa mtoto uhuru basi anaweza kuutumia
vibaya au kupata matatizo. Kwa sababu hiyo, tunapenda kuwalinda watoto kupita
kiasi.
Tafiti, kwa upande mwingine, zinaonesha kuwa watoto
wanaobanwa sana hawawezi kufikiri vizuri ukilinganisha na watoto wanaokua bila
kudhibitiwa. Kubanwa kuna maana ya kuongozwa kupindukia katika maeneo mengi ya
kimaisha.
Mruhusu mtoto
kuwa huru. Mpe nafasi ya kuchagua kufanya mambo mapya. Sambamba na
uhuru, unashauriwa kupunguza ukosoaji. Usiwe mwepesi wa kuhukumu na kurekebisha
mawazo yake isipokuwa anapofanya makosa ya wazi. Mwache akosee.
Wakati mwingine, makosa yanaweza kuwa kichocheo
kikubwa cha kujifunza kwa urahisi. Mtu asiyeamini anaweza kukosea, huogopa
kujaribu mambo mapya. Huna sababu ya kumnyima mtoto fursa ya kujifunza kwa
vitendo.
Mpe
vifaa changamshi
Mtoto anahitaji vifaa kujifunza ubunifu. Hata hivyo,
wazazi wengi huwanunulia watoto vifaa ambavyo tayari vimeshatengenezwa. Kazi ya
mtoto inabaki kuwa kuvitumia vivyo hivyo vilivyo, bila kuvifanyia mabadiliko
yoyote. Mfano, mtoto ananuliwa ‘gari’ ambalo tayari lina matairi na kila kitu.
Kumpa mtoto vifaa hivi vilivyotengenezwa tayari ni kuviza ubunifu.
Aidha, wazazi wengine huwapatia watoto vifaa vya
kiteknolojia vinavyojenga utegemezi usio wa lazima. Michezo hii, mbali na
kujenga tabia zisizofaa kwa mtoto, inatekeleza muda.
Katika kukuza ubunifu wa mtoto, inashauriwa kumpatia
mtoto malighafi atakazozitumia kutengeneza vifaa vinavyokidhi mahitaji yake.
Badala ya kumnunulia gari lililotengenezwa tayari, mtafutie vipande vya maboksi,
gundi, nyaya, kamba, vizibo vya chupa, misumari, mbao na vifaa vingine
vimsaidie kuunda kitu kinachokuza uwezo wake wa kufikiri.
Mruhusu
kufikiri tofauti na wewe
Wazazi tunapenda watoto wafikiri kama sisi.
Hatupendi wafikiri kinyume na sisi hata kama kufanya hivyo hakuleti madhara
yoyote. Wakati mwingine tunawaadhibu watoto kwa kosa la kutofautiana misimamo
na sisi kwa mambo ya kawaida. Kwa kufanya hivi, tumewakuza watoto kuogopa
kufikiri kwa uhuru. Tumeua ubunifu.
Unashauriwa kuwapa watoto fursa ya kufikiri tofauti.
Inapobidi waruhusu kupingana na wewe. Kwa mfano, hata kama ungetamani mwanao
avae nguo fulani uipendayo, huna sababu ya kumlazimisha kufanya hivyo. Mpe
nafasi ya kuchagua akipendacho almuradi hakiathiri mamlaka yako kama mzazi. Unapofanya
hivyo, unamjenga kuwa mtu mbunifu asiyetegemea uzoefu kufanya mambo yake.
Kadhalika, mpe mtoto nafasi ya kuyatazama mambo kwa
sura tofauti. Kutafuta majibu tofauti kwa matatizo anayokabiliana nayo.
Anapofikiri amepata majibu, mpe nafasi ya kufikiri majibu mengine kwa tatizo
alilonalo. Anapopata majibu yasiyotarajiwa, tambua bila kumpa motisha. Ubunifu
haupaswi kutegemea motisha kutoka nje. Ubunifu unaanza ndani ya mtoto mwenyewe.
Fuatilia Jarida la Maarifa ndani ya gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa Makala kama hizi.
Maoni
Chapisha Maoni