Jinsi ya Kumsaidia Mtoto Kuchagua Masomo

Mfumo wa elimu yetu humtaka mtoto kusoma masomo yote kuanzia darasa la awali mpaka angalao kidato cha pili. Matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yanakuwa kipimo cha aina ya masomo ambayo mtoto anaweza kuyawekea mkazo zaidi.

Mkazo anaouweka katika baadhi ya masomo unaitwa mchepuo. Mchepuo ni njia anayoichagua mtoto kufanya maandalizi ya kuelekea kule anakolenga kwenda baada ya kuhitimu masomo yake.

Kulingana na shule anayosoma mwanao, ipo michepuo kama sayansi, sayansi jamii (sanaa) na biashara. Siku za nyuma ilikuwepo pia michepuo ya kilimo, upishi na ufundi. 

Mtoto anapochagua mchepuo anaoupenda, hiyo ina maana kuwa anaachana na masomo mengine na kutilia mkazo kwenye masomo machache yanayokidhi matarajio yake ya baadae.



Umuhimu wa mchepuo

Maamuzi anayoyafanya mtoto baada ya kidato cha pili yana umuhimu mkubwa. Masomo atakayoyachagua, kwa kiasi kikubwa, yataongoza mustakabali wake katika elimu.

Kwa mfano, wakati anamaliza kidato cha nne, mtoto atalazimika kuchagua masomo matatu pekee atakayoyasoma kwa ngazi ya kidato cha tano na sita. Masomo hayo matatu, kwa kawaida, yanatokana na aina ya mchepuo aliokuwa nao tangu anaingia kidato cha tatu.

Kwa sababu hiyo, ni muhimu mzazi kumsaidia mtoto kufanya maamuzi haya kwa busara na mapema.

Hata hivyo, wapo wazazi ambao kwa sababu mbalimbali hawafahamu maamuzi ya michepuo yanafanywa na mtoto. Kwa wazazi hawa walimu ndio wenye jukumu kuu la kuwasaidia watoto kufanya maamuzi ya kipi wanakihitaji.

Kwa bahati mbaya, walimu nao kwa sababu mbalimbali hushindwa kuwapa watoto msaada wanaouitaji. Katika mazingira kama haya, ni muhimu kwa mzazi kuelewa nafasi yake. Makala haya yanaangazia mambo manne ya msingi ya kuzingatia unapomsaidia mtoto kufanya maamuzi.

Fahamu uwezo wa mwanao

Wakati mwingine wazazi na baadhi ya walimu wanawalazimisha watoto kufanya vitu visivyoendana na uwezo na matakwa yao. Kwamba sasa hivi tunahitaji wanasayansi haimaanishi kila mtoto akasome sayansi. Maamuzi ya kipi mtoto anapaswa kukifanya yanategemea uwezo wake.

Kila mtoto anazaliwa na uwezo wake wa pekee kiakili. Mazingira ya ukuaji wa mwanao, nayo kwa upande mwingine, yamechangia kutengeneza matarajio ya aina fulani ya maisha.

Pia, mtoto huwa na uwezo katika eneo fulani mahususi kuliko maeneo mengineyo. Anaweza kushindwa sayansi lakini akaweza biashara. Anaweza kushindwa vyote lakini akaweza vingine visivyohitaji vyeti.

Ni muhimu basi kwako mzazi kuelewa uwezo unaompambanua mwanao na kumsaidia kufanya maamuzi yanayopalilia uwezo alionao.

Zingatia maoni ya mtoto

Watoto wanazo ndoto binafsi. Ndoto hizi zinaweza zisilete maana yoyote kwa wazazi lakini ni za muhimu kwao. Wakati mwingine ndoto hizi zinatokana na aina ya marafiki na watu wanaomzunguka. 

Mtoto anaweza kuwa na ndoto za kuwa Mhasibu, kwa mfano. Kilichomfanya awe na ndoto hizi ni kumsikia mtu anayemheshimu, aghalabu mwalimu, akipendekeza uzuri wa kuwa Mhasibu.

Pamoja na ukweli kuwa wewe kama mzazi unaweza kuwa na uzoefu na uelewa mzuri zaidi, usifanye haraka kumshauri mtoto njia ipi aifuate. Mpe nafasi ya kujisikia kama mtu mwenye maamuzi na maisha yake.

Usimlazimishe kufikiri vile anavyopaswa kufikiri. Ukifanya hivyo unaweza kujiweka katika mazingira ya kulaumiwa baadae ikiwa mambo hayatakwenda kama ulivyoshauri. Ni muhimu nafasi yako ikabaki kuwa kumsaidia kufikia ndoto zake.

Msaidie kupanua uelewa wake

Kumsaidia mtoto inaweza kuwa pamoja na kumpa taarifa muhimu anazozihitaji ili afanye maamuzi yake mwenyewe. Wakati sahihi wa kumpa taarifa ni pale unapohisi maoni aliyonayo yanampotosha.

Katika mazingira ambayo mtoto anaonekana kufuata njia ambayo wewe kama mzazi huna hakika na mstakabali wake, ni rahisi kumkosoa. Hukosoi kwa nia mbaya. Hapana. Unakuwa na shauku ya kuona mtoto anapita njia unayodhani ina manufaa kwake.

Hata hivyo, huhitaji kumkosoa. Huhitaji kumpa maelekezo ya moja kwa moja kwa kile unachodhani anahitaji kukifanya. Unachoweza kukifanya ni kumpa taarifa zitakazomwongoza kufanya maamuzi.

Kwa mfano, msaidie kuelewa uhusiano uliopo kati ya aina ya masomo anayotaka kuyachagua na mustakabali wa ajira na kazi anakazofanya baadae. Unaweza kukuta, kwa mfano, mtoto anataka kusoma Sayansi akitaka kufanya kazi za Wanyama pori. Muhimu aelewe kazi ya afisa wanyama pori  katika maisha halisi ina maana gani. Akielewa atafanya maamuzi sahihi.

Mtafutie ushauri wa kitaalam

Ni dhahiri si kila jambo utakuwa na uelewa nalo wewe kama mzazi. Msaidie mtoto kupata ushauri wa kitaalamu.

Wataalamu hawa wanawasadia watoto kujitambua na kujua vipaji vyao. Kazi yao kubwa itakuwa ni kumsaidia mtoto kuelewa kazi zipi anaweza kuzifanya ili kuendana na vipaji vyake. Si kila kazi inamfaa yeyote.

Kwa mfano, kijana anaweza kuwa mzuri katika masomo yanayoweza kumfanya awe daktari lakini asifae kuwa daktari. Udaktari ni pamoja na haiba ya jumla ya mtoto.

Fikra kuwa matokeo ya mtoto ndiyo yanayoamua achague uelekeo upi, si sahihi.  Ndio maana tunahitaji kuwekeza katika ushauri wa kitaalam kumsaidia mtoto kufanya uchaguzi utakayosadifu matarajio yake kimaisha, vipaji vyake pamoja na uwezo wake.

Fuatilia Jarida la Maarifa ndani ya gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa Makala kama hizi.

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?