Tabia Saba Zitakazokuwezesha Kutekeleza Malengo Unayojiwekea

KUANZA kwa mwaka mpya kunaambatana na matarajio mengi. Tunapoingia mwaka mpya tunamani kubadili maeneo mengi katika maisha yetu. Tunatamani kuwa na maisha bora yenye tija kiuchumi, kijamii, kiimani na kwenye maeneo mengine.

Hata hivyo, katika kutekeleza malengo yako, ni dhahiri kuwa zipo baadhi ya tabia ulizonazo zinazoweza kuwa kikwazo katika kutekeleza malengo ya mwaka huu. Unahitaji kubadili tabia ili uweze kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutekeleza malengo yako.

Katika makala haya tunajadili tabia saba muhimu unazohitaji kuzibadili ili uweze kufanikiwa kwa mwaka huu. Katika hizi, zipo ambazo ni rahisi kuzibadili, lakini nyingine zinahitaji bidii zaidi kuzibadili. 



Kuyatazama maisha kwa malengo ya muda mfupi

Malengo yanayoweza kubadili uelekeo wa maisha yako, mara nyingi, yanahitaji uwezo wa kuyatazama mambo kwa jicho la muda mrefu. Huwezi kufanikiwa kwa kuendeleza mtazamo mfupi. Huwezi kufanikiwa kwa kutazama kile unachohitaji leo.

Unafanikiwa kwa kufikiria namna gani mambo unayofanya leo yanaweza kuathiri mwelekeo wa maisha yako kwa masafa marefu. Kama wewe ni mwanafunzi, kwa mfano, lazima uelewe namna gani uvivu unaojisikia leo, unaweza kuathiri matokeo yako mwishoni mwa masomo. Usipoona uhusiano huo, ni rahisi kuyatelekeza (kuyaghairi) malengo.

Hata hivyo, kutekeleza malengo ya muda mrefu kunahitaji mabadiliko ya mienendo yako ya kila siku. Kwamba ili mipango yako ya muda mrefu itekelezeke, lazima uishi kwa namna inayosadifu mipango hiyo. Badili unavyoishi leo ili uweze kufikia malengo ya muda mrefu.

Kuacha visingizio

Huwezi kufanikiwa kwa kuwategemea watu wengine watekeleze wajibu wako. Unahitaji kufikiria nafasi uliyonayo wewe katika kufikia malengo yao mwenyewe. Usitegee malengo yako mwenyewe kwa kusubiri watu wengine wafanye.

Unapokuwa na mtazamo wa kutegemea kufanikiwa kwa jitihada za wengine, hutakuwa na motisha ya kutosha kufanya bidii zitakazokusaidia kutekeleza malengo yako. Jipe wajibu mkamilifu. Elewa kuwa hakuna mtu mwingine atakayewajibika kukusaidia kutekeleza malengo yako.

Unapojiona kuwa una wajibu mkamilifu wa chochote kinachotokea katika maisha yako, unajiweka katika nafasi bora zaidi ya kutia jitihada zitakazotekeleza ndoto zako.

Usifanye mambo mengi kwa wakati mmoja


Huwezi kukimbiza sungura wawili kwa wakati mmoja na ukawapa. Utawakosa wote. Ndivyo ilivyo mara nyingi tunavyotekeleza mipango yetu. Tunataka kufanya mambo yote kwa wakati ule ule. Hasara yake ni kujikuta tukiyafanya mambo yote nusu nusu.

Jifunze kuelekeza nguvu zako kwenye jambo moja na ulikamilishe. Iwe ni kwenye mazungumzo, kazi, biashara, uhusiano, elekeza uzingativu wako wote kwenye jambo moja.

Sasa hiyo, hata hivyo, haimaanishi usiwe na mipango mingi. Unaweza kuwa na mipango mingi kadri inavyowezekana. Lakini ni busara kuhakikisha kuwa hufanyi mambo mawili kwa wakati ule ule. Hakikisha unaelekeza nguvu zako zote kukamilisha jambo unalolifanya.


Jifunze kusema hapana

Katika maisha yetu tunakutana na watu wenye mahitaji na maombi fulani kwetu. Wanaweza kuwa marafiki, wafanyakazi wenzetu, ndugu zetu, waumini wenzetu na hata majirani. Ni rahisi kuogopa kutokueleweka, kwa kukubaliana na maombi fulani yasiyo na tija.


Usiwe mwepesi kusema kusema ‘sawa’ kwa mambo yasiyo ya lazima. Mara nyingi ‘sawa’ unazozitoa kwa lengo la kuwaridhisha watu wengine zinaweza kukwamisha malengo yako kwa kiasi kikubwa. Jifunze kusema hapana kwa maombi yanayoingiliana na malengo uliyonayo.

Kama wewe ni mwanafunzi unayetaka kufaulu, usiruhusu watu wasiojitambua kuingilia ratiba yako. Sema ‘hapana’ kwa ratiba isiyoendana na malengo yako. Kama wewe ni baba unayetaka kujenga familia yako, sema ‘hapana’ kwa wenye kukuhitaji katika ratiba zisizojenga familia. Wakati mwingine unahitaji hapana tu kutekeleza malengo yako.

Jitenge na watu wasiokujenga

Upo ukweli kuwa  kila mmoja wetu ni wastani wa watu wanne tunaotumia nao muda mwingi. Huwezi kuwa tofauti na watu wanaokuzunguka. Watu unaowasiliana nao kila siku ndio wanaotengeza wajihi wako. Kuwa makini na aina ya watu unaowapa nafasi ya kuhusiana na wewe katika maisha halisi na hata mitandao ya kijamii.

Chagua watu wanaofanana na malengo yako. Tafuta watu wanaoyaishi malengo uliyonayo. Kama unataka kuwa na familia imara mwaka huu, jenga urafiki na watu wenye familia imara. Utajifunza kwao. Kama unataka kufanya biashara fulani, jenga urafiki na watu wanaofanya biashara hiyo.

Usipoteze muda na watu wasiosaidia kutekeleza malengo yako. Usipoteze muda na watu walio kinyume na malengo yako. Huwezi kuwa na familia imara kwa kutumia muda mwingi na watu wasiojali familia zao. Utajikuta unabadilika hatua kwa hatua bila kujua. Maji ya moto hayawezi kuendelea kuwa moto yakichanganywa na maji ya baridi. Chagua marafiki kwa kuangalia malengo yako.

Hiyo, hata hivyo, haimaanishi usiwe na uhusiano na watu wote. Unaweza kuhusiana na watu bila kuwafanya marafiki zako.

Usitumikishwe na mitandao ya kijamii

Tunaishi katika wakati ambao mawasiliano yamerahisishwa kuliko wakati mwingine wowote. Ni rahisi, kwa mfano, ndani ya dakika tano tangu unapoamka, kujua nini kimetokea duniani kote. Ukiwa kwenye mitandao kama Facebook, Twitter, Instagram na Whatsapp, huna sababu ya kuzitafuta taarifa. Zinakufuata uliko.

Katika mazingira kama hayo, ni rahisi kupoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii. Tafiti zinazonesha kuwa watu wengi wanapoteza muda mwingi kwenye mitandao hii. Mrejesho wa papo kwa hapo unaowezeshwa na mitandao hii, unajenga utegemezi. Ni aina fulani ya ulevi.

Usiposhinda utegemezi unaojengwa na mitandao hii, itakuwa vigumu sana kutekeleza malengo yako. Isipokuwa kama kazi zako zinategemea mitandao hii, jiwekee muda maalumu wa kuingia kwenye mitandao.

Usikate tamaa unaposhindwa


Wakati mwingine tunashindwa kutekeleza malengo yetu kwa sababu tunakuwa wepesi kukataa tamaa mambo yanapokwenda vile tusivyotarajia. Tabia hii ya kughairi mambo kirahisi haiwezi kukusaidia kutekeleza mipango yako. Jifunze kuwa imara hata pale mambo yanapoharibika.

Kama ulipanga kuanza kuweka akiba mwaka huu, si lazima uweze kuweka kiasi kamili cha fedha ulichopanga kuanzia mwezi Januari. Ukweli ni kuwa unaweza kufanikiwa kuweka kiasi kidogo au ushindwe kabisa. Usiwe mwepesi kughairi mpango huo kwa sababu tu ulifikiri ungeweza kuweka kiasi cha fedha ulichokipanga kirahisi.

Jifunze kuwa na nguvu ya maamuzi isiyoyumbishwa na matokeo hasi. Jipange upya kwa kutathimini kile ulichokosea na rudia tena na tena. Nguvu ya maamuzi ndiyo inayowatofautisha watu wanaotekeleza malengo yao na watu wanaoachana na mipango yao mara tu wanapoona dalili za kushindwa.

Wakati mwingine watu watakukatisha tamaa. Kwamba unachokifanya hakiwezekani. Usikubali kukatishwa tamaa.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia