Namna ya Kutambua na Kukuza Kipaji cha Mwanao -1

Kila mtoto ana kipaji. Ingawa ni kweli kuwa watu wengi hawatambui vipaji vyao, hiyo hata hivyo, haimaanishi hawana vipaji. Zipo sababu nyingi zinazofanya watu wasitambue vipaji vyao. Kwanza, ni mfumo rasmi wa elimu unaotumia tafsiri finyu ya uwezo wa kiakili.

Shule, walimu, mitihani na mitaala ya elimu kwa ujumla imetufanya tuamini kuwa usipokuwa na uwezo wa kuchambua mambo fulani fulani, ukayakumbuka sawia na kuyaandika kama ulivyofundishwa, basi wewe huna akili. Matokeo yake, watoto wetu wamepimwa kwa kigezo kimoja kinachofanana. Kigezo chenyewe, kwa bahati mbaya, hakizingatii vipaji mbalimbali walivyo navyo watoto.


Unapotathmini uwezo wa mtoto mwenye kipaji cha kuchora, kwa mfano, kwa kutumia kigezo cha kukumbuka na kuchambua nadharia fulani fulani huwezi kutenda haki. Na kwa sababu mwenye kipaji cha uchoraji anajua uwezo wake hauna nafasi katika mfumo rasmi wa elimu, analazimika kuachana na ndoto za kukuza uchoraji.

Sababu ya pili ni mtazamo kuwa mafanikio katika maisha yanategemea bora wa vyeti tunavyotunukiwa kupitia mfumo rasmi wa elimu. Kwamba, ikiwa huna uwezo unaotambuliwa na mitaala ya elimu basi ni vigumu kwako kuwa na cheti kitakachokusaidia kupata mafanikio unayoyahitaji.

Ni dhahiri kuwa tunatamani kujiweka katika nafasi nzuri ya kujipatia mafanikio. Kwa hiyo tunalazimika kuweka msisitizo katika kukuza uwezo unaotambuliwa na kuheshimiwa na mfumo rasmi wa elimu.

Hata hivyo, kisaikolojia mafanikio ya mtu kwa kiasi kikubwa yanategemea namna anavyoweza kutumia kipaji chake katika maisha halisi. Kwamba unapofanya kazi inayotumia kipaji chako, uwezekano wako wa kufurahia kile kinachokuingizia kipato unakuwa mkubwa.  Kufanikiwa ni zaidi ya kuwa na uhakika wa kipato. Kufanikiwa ni pamoja na kufurahia kile unachokifanya.

Kwa sababu si rahisi kazi ya kubaini na kukuza kipaji kufanywa na mtaala rasmi wa elimu kama tulivyosaili kwa ufupi, mzazi anabeba wajibu mkubwa wa  kufanya kazi hiyo muhimu kwa mafanikio ya mwanae.

Makala haya yanalenga kuangazia mambo yanayochangia kuibua kipaji cha mtoto; namna unavyoweza kukumsaidia kutambua kipaji chake; kuweka mazingira ya kukuza kipaji cha mtoto na kukioanisha na maarifa na ujuzi unaotolewa na mfumo rasmi wa elimu.

Maana ya kipaji

Kipaji ni uwezo wa pekee anaokuwa nao mtoto unaomwezesha kufanya mambo ambayo kwa kawaida si watu wengi wanaweza kuyafanya. Kwa mfano, mtoto anaweza kuwa mchoraji. Hahitaji mwalimu wa kumfundishwa namna ya kutafsiri mawazo yake kuwa mchoro unaoleta maana; namna ya kuweka vivuli vya mchoro kutengeneza umbo linaloeleweka.

Mtoto huyu hahitaji kuelekezwa namna ya kupaka rangi kulingana na tafsiri ya mchoro wake. Mtoto huyu, katika mazingira yasiyoelezeka, anapoweza kuonyesha uwezo mkubwa katika maeneo hayo, tunasema anacho kipaji cha kuchora.

Kuwa na kipaji hakutoshi. Wakati mwingine yanahitajika mazingira ya kukuza kipaji hicho. Kwa mfano, vipaji kama kuimba, michezo, kuigiza ni rahisi kunaonekana bila jitihada kubwa. Lakini vipaji hivyo, vinaweza visikue ikiwa havitakutana na mazingira yanayokuza uwezo huo.

Kadhalika, vipo vipaji vinavyohitaji kuibuliwa kwa kuchochewa na mazingira fulani ili vionekane. Bila mazingira hayo sisimushi, havionekani kwa wepesi. Kwa mfano, mwanao anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kuwa mwandishi wa vitabu, lakini anahitaji mazingira fulani yanayoweza kuwa kichocheo cha uwezo huo. Akiyakosa, anaweza kujikuta ni Injinia au Daktari kwa sababu tu mazingira yamemlazimisha kuwa hivyo.


Kipaji kinarithiwa au kunajengwa?

Tunazaliwa na kipaji. Kama ambavyo hatuchagui rangi ya ngozi, urefu wa mwili na wajihi tulionao, vivyo hivyo, na vipaji ni zawadi tunayozaliwa nayo. Kwa mfano, wapo waliozaliwa na uwezo wa kuimba. Lakini wapo ambao hata wangepata mafunzo ya aina gani, hawataweza kuimba. Kuimba ni kipaji cha kuzaliwa.

Hata hivyo, kisaikolojia ipo nafasi kubwa ya mazingira tunayokulia katika kututengeneza vile tulivyo, ikiwemo vipaji tunavyokuwa navyo. Kama tulivyotangulia kudokeza, kipaji huibuliwa. Kipaji hujengwa. Aina ya familia zinazotulea, aina ya taarifa tunazokutana nazo tangu tukiwa wadogo, aina ya watu tunaotumia muda mwingi kuwa nao, vyote hivyo kwa pamoja vina nafasi ya kujenga haiba tuliyonayo, ikiwamo kipaji.

Kwa mfano, mtoto aliyekulia katika familia ya wanamuziki, anaona baba akicheza kinanda, akifanya mazoezi ya kuimba ni rahisi kuwa mwanamuziki. Ni vigumu, hata hivyo, kujua amerithi uimbaji kwa baba yake au ni mazingira yamemtengeneza kuwa mwimbaji.

Vivyo hivyo kwa mtoto aliyelelewa na mama mwenye kawaida ya kusoma na kuandika vitabu. Anaweza kuwa mwepesi kupenda kushika kalamu, karatasi na hata vitabu. Inawezekana hajarithi kipaji cha kuandika kutoka kwa mzazi wake, lakini kule kufurahia kazi anayoifanya mama yake, kukamvutia kuwa mwandishi na msomaji wa vitabu.

Mtazamo huu wa nafasi ya mazingira katika kutengeneza vipaji vya watoto umefanyiwa utafiti wa kutosha katika nchi zilizoendelea. Tafiti zinabainisha kuwa mtoto anapozungukwa na watu anaowaheshimu, anaowapenda  ni rahisi kujaribu kuwa kama wao. Watu hao wanaweza kuwa  mahali  anapoishi, shuleni, kwenye vyombo vya habari na kwingineko.

Kwa mfano, kama watu ambao mtoto anavutiwa nao wanaonekana kutumia muda mwingi na vifaa vya teknolojia, mtoto anaweza kuvutiwa kujaribu kufanya vivyo hivyo. Matokeo chanya ya jaribio lake, yanakuwa hamasa ya kuendelea na kufanya. Katika mazingira haya, tunaweza kusema, mtoto amekutana na mazingira yanayoibua uwezo ambayo huenda alikuwa nao.

Maelezo hayo hayo yanaweza kutumika kujua kwa nini mtoto anakuwa na kipaji cha ufundi, anapenda na kumudu mchezo fulani, uigizaji, uchekeshaji, ubunifu, biashara na hata uongeaji mbele ya hadhara.

Ndio kusema, mchanganyiko wa matokeo ya vinasaba kutoka kwa wazazi, aina ya mazingira yanayomzunguka mtoto, yanatengeneza uwezo, ujuzi au maarifa ambayo si kila mtu anaweza kuwa nayo ndiyo yanayoitwa kipaji.


Inaendelea

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?