Hatua za Kuchukua Unapoamua Kuacha Kazi -1
Kuacha
kazi si jambo dogo. Lakini zipo sababu kadhaa zinazoweza kukufanya uamue kuacha
kazi. Mosi, kupata kazi mpya. Unapoitwa kuanza rasmi kazi uliyoomba, ni vigumu
kuendelea na kazi uliyonayo. Kwa kuwa ni vigumu kuwa na ajira mbili kwa wakati
moja, mara nyingi utalazimika kuacha kazi uliyonayo.
Pia
inawezekana umeshindwa kuendelea na kazi uliyonayo hivi sasa. Ingawa
haishauriwi kuacha kazi bila kuwa na uhakiki wa kazi nyingine, hutokea mtu
akafikiri kwa kina, akapata ushauri wa kitaalam na kujiridhisha kuwa ugumu wa
mazingira ya kazi haumruhusu kuendelea na kazi aliyonayo.
Mathalani,
kutokuelewana na mkubwa wako wa kazi au wafanyakazi wenzako; kutokuridhika na tija
ya kazi unayoifanya; kukosa motisha na ari ya kazi; kujihisi huna mchango tena
ofisini kwako ni baadhi ya sababu zinazoweza kusababisha maamuzi magumu ya mtu
kuacha kazi.
Lakini
pia inawezekana ukalazimishwa kuacha kazi hata kama bado ungependa kuendelea
nayo. Kama ambavyo mwajiriwa anaweza kuamua kuacha kazi, mwajiri naye anaweza
kuamua kukuachisha kazi kwa sababu anazoona zinafaa.
Vyovyote
vile iwavyo, tukio la kuacha kazi si jambo jepesi. Makala haya yanalenga kujadili hatua
unazoweza kuchukua mara unapoamua kuachana na kazi yako iwe kwa hiari au kwa
kulazimika.
Tafuta ushauri unaoaminika
Usiache
kazi kwa sababu tu unafikiri huhitaji kuendelea kufanya kazi uliyonayo sasa.
Mazingira magumu ya kazi yanaweza kukushawishi kufanya maamuzi utakayoyajutia
baadae. Inawezekana huna mahusiano mazuri na mkubwa wako wa kazi. Unafikiri
kuacha kazi ni kumkomoa na kulipa kisasi.
Inawezekana
unafanya kazi katika maeneo usiyoyapenda. Unafikiri ukienda kwingineko mambo
yatakuwa mazuri. Pengine umevutiwa na mwajiri mwingine anayeahidi kukuongezea
mshahara zaidi. Lakini hujafikiria kuwa mwajiri
wa sasa anayekulipa kidogo, anakupa uhuru wa kufanya mambo mengine yanayoweza
kukuongezea kipato. Huko unakokwenda unaweza usipate muda wa kufanya mambo
hayo. Msisimuko wa kupata kazi unayoipenda unaweza kukufanya ukasahau kufikiria
mambo ya msingi yanayoweza kukugharimu baadae.
Kabla
hujatekeleza azma yako, fanya mawasiliano na watu wasio na maslahi na kazi yako na wenye uzoefu
zaidi yako. Watu hawa watakusaidia kuyatazama mambo kwa mtazamo mpana. Ushauri
wao unaweza kukufanya ugundue kuwa huna sababu ya kuacha kazi uliyonayo
isipokuwa kuangalia namna ya kutatua changamoto ulizonazo hapo ulipo.
Aidha,
inawezekana unaacha kazi kwa sababu umelazimika kufanya hivyo na mwajiri wako.
Kuacha kazi katika mazingira haya kunaweza kuambatana na maumivu makubwa. Hisia
za kuonewa na taasisi au kampuni inayomlazimisha kuacha kazi; hofu ya aina ya maisha
atakayoishi baada ya kuacha kazi;
wasiwasi wa kukosa hadhi aliyokuwa nayo kama mfanyakazi ni baadhi ya
sababu zinazoweza kumfanya mtu aache kazi kwa moyo mzito.
Unahitaji
kuonana na watalaam wa unasihi wakusaidie kuchukuliana na taarifa hizi. Wakati
mwingine, huhitaji ushauri wowote zaidi ya watu wakomavu unaowaamini
watakaokusikiliza tu. Wape nafasi kabla hujachukua hatua zozote.
Onyesha
utulivu wa kihisia
Inawezekana umepata kazi nzuri yenye maslahi makubwa zaidi. Furaha hiyo isikufanye ukakosa busara. Inawezekana mwajiri wako alikunyima haki zako kinyume na makubaliano yenu ya kazi. Unaweza kuchukulia kupata kazi mpya kama namna fulani ya kutoka kifungoni. Hiyo haiwezi kuwa sababu ya kutosha kukunyang’anya hekima.
Tambua
kuwa kampuni au taasisi hiyo unayoiona haina maana leo, ndiyo iliyochangia kukufikisha
hapo. Changamoto ulizokutana nazo katika kipindi chote cha ajira usiyoipenda,
zilikuwa kichocheo cha kukuhamasisha kupambana kwa ari zaidi. Heshimu hilo.
Pia,
pengine usingefanya kazi kwenye taasisi au kampuni hiyo usiyoipenda leo,
mwajiri wako mpya asingekuona. Katika wasifu wako wa kazi ulimtaja mwajiri huyu
usiyempenda leo. Uzoefu na ujuzi aliouvutiwa nao mwajiri mpya umeupata kwa
kufanya kazi na mwajiri huyu unayeachana naye. Hilo angalau likusaidie kuwa mtulivu
kwa maneno na vitendo. Kwamba hata kama ni kweli ulionewa, bado una sababu za
kuthamini mchango wa mwajiri huyu.
Kwa
upande mwingine, inawezekana umeachishwa kazi isivyo haki. Kutokuelewana na
mkubwa wako kazini kumechangia kukuondoa. Katika mazingira haya, unaweza kuwa
na ghadhabu. Una haki ya kukasirika. Lakini tambua kuwa ghadhabu ni dalili moja
wapo ya kukuukana ukweli usioupenda. Kubali ukweli mchungu kuwa umefukuzwa
kazi. Kisha fanya taratibu za kuondoka bila kuongeza maumivu yasiyo ya lazima.
Heshimu mkataba wa kazi
Kupata
kazi bora zaidi ya hiyo uliyokuwa hakupaswi kukupa kiburi cha kuacha kazi bila
kufuata taratibu. Kufukuzwa kazi, kwa upande mwingine, kunaweza kukuchanganya
kiasi cha kukufanya uamue kuacha kazi
kinyume na mkataba wa kazi. Usifanye
hivyo. Rejea mkataba wako na mwajiri.
Mikataba
mingi inamtaka mwajiriwa kutoa notisi ya kuacha kazi kwa muda wa kuanzia mwezi
mmoja hadi miezi mitatu kabla ya tarehe ya mwisho ya kufanya kazi na mwajiri
wako. Kimsingi, notisi ya kuacha kazi inalenga kumpa mwajiri muda wa kumtafuta
mtu atakayechukua nafasi yako. Inakusaidia na wewe kukabidhi majukumu yako
pamoja na vitendea kazi ulivyokabidhiwa.
Vile
vile, inawezekana mwajiri wako wa sasa alikudhamini kupata mkopo katika taasisi
za fedha. Pengine mlikuwa ya makubaliano ya muda maalum wa kufanya kazi kufidia
gharama za masomo yako. Mtu mzima anayejitambua huheshimu makubaliano
anayoyafanya na watu wenine. Usifanye kosa la kuondoka kazini kinyume na
makubaliano uliyokuwa nayo na mwajiri wako.
Inaendelea
Good piece! Hongera mkuu
JibuFutaAsnte kwa makala kaka. Na hii imenisadia mm hasa maana nimeahachukua maamuz haya.
JibuFutaIko vizuri
JibuFutaHongera kaka
JibuFutaNaomba mnisaidi nikipi mtu anatakiwa kufanya pale anapoamua kuacha kazi kwa sababu za kiafya
JibuFutaAsante saan kwa huu ushauri
JibuFutaIla naomba mnisaidie kuandika barua ya kujiuzulu