Faida, Hasara za Vituo vya Kulea Watoto
TUMEKUWA tukijadili changamoto zinazowakabili wazazi
wanaofanya kazi mbali na nyumbani. Njia kadhaa zinatumika kukabiliana na
changamoto hizi. Moja wapo, ni kuwaajiri wasichana wa kazi kwa lengo la
kusaidia kuwalea watoto.
Tulipendekeza kuwa msingi mkuu wa kupunguza
changamoto za huduma hizi zinazotolewa na wasichana wa kazi ni kujenga nao mahusiano
mazuri ya kifamilia na kikazi. Mahusiano haya yanawajengea motisha ya kufanya
kazi kwa uadilifu na moyo wa kujituma.
Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo za kujenga
uhusiano wa kifamilia, bado ni vigumu kujihakikishia huduma bora kwa kuwa mara
nyingi huduma hizi zinatolewa katika mazingira yasiyo rasmi.
Kwa mfano yamekuwepo matukio ya wasichana hawa
kuwatendea watoto vitendo visivyokubalika vinavyoathiri tabia na uelewa wa
watoto. Matukio haya yanafanyika katika mazingira ambayo wazazi wamejitahidi
kufanya wajibu wao kuhakikisha kuwa msichana anafanya kazi katika mazingira rafiki.
Kufuatia changamoto hizi, zipo familia zenye uwezo
zinazoamua kutumia malezi rasmi ya watoto kupitia vituo maalumu vya kulelea watoto,
day care. Vituo hivi hupokea watoto
wa majuma kadhaa hadi wa umri wa kuanza shule kwa lengo la kuwalea kwa muda
ambao mama anakuwa kazini.
Aina za vituo
vya malezi
Mara nyingi, katika vituo hivi watoto wa umri
unaokaribiana kati ya umri wa majuma kadhaa hadi miaka sita hulelewa kwa
pamoja. Tofauti na kuwatumia akina dada wa kazi, huduma hii hutumia watu wenye
ujuzi wa malezi ya watoto, waliofunzwa namna ya kumhudumia mtoto kulingana na
umri wake.
Huduma za malezi kituoni zinatofautiana kulingana na umri wa mtoto. Katika umri wa kuanzia mtoto kuzaliwa mpaka miaka miwili, huduma kuu huwa ni sawa na ile inayotolewa na mama au msichana wa kazi. Mkazo ni kumpa mtoto chakula bora, kumtunza mtoto kimwili, kwa maana ya kuhakikisha anakuwa safi na salama. Hakuna mkazo katika mtaala wa elimu.
Kuanzia miaka miwili au mitatu, walezi wa vituo hivi
huanza kudokeza kidogo mambo ya elimu kumkuza mtoto kiufahamu. Kwa baadhi ya
vituo, mtoto huanza kufundishwa kuhesabu, kuandika na kusoma.
Katika umri wa miaka minne hadi
sita, vituo hivi huanza kufahamika kama shule ya awali, kwa kwa kuwa pamoja na
kukutana na mahitaji ya msingi ya mtoto, lengo kuu linakuwa kumpatia mtoto
elimu. Katika hatua hii, walezi hufanya majukumu ya walimu.
Aidha, baada ya mtoto kutimiza
miaka sita na kuanza shule, mfumo wa malezi huweza kufanyika kwa mtindo wa aina
mbili; kuhudhuria masomo kwa mtindo wa kurudi nyumbani jioni; au kuondoka
nyumbani kwa miezi kadhaa kwenda shuleni, mbali na nyumbani, akilelewa na kufundishwa
na walimu kwa ushirikiano na walezi wasio walimu.
Huduma hizi hazikuwa maarufu sana siku za nyuma, lakini kwa sasa uhitaji wake umeanza kuwa mkubwa. Jijini Dar es Salaam, kwa mfano, vituo hivi vya aina zote hizo tulizozitaja vipo katika maeneo mengi. Miji mingine kama Arusha, Mwanza na Moshi, huduma hizi zina umaarufu mkubwa.
Sambamba na vituo hivi,
shule za msingi za kulala zimekuwa maarufu. Pamoja na lengo la kumpatia mtoto
elimu bora, shule hizi humpa mzazi nafasi ya kujikita na kazi nyinginezo bila
wasiwasi wa namna watoto watakavyolelewa.
Faida za malezi ya vituoni
Malezi ya watoto katika vituo maalum hufanyika katika mfumo wenye namna fulani ya urasmi kuliko nyumbani. Ushindani huwalazimisha wafanyabiashara wanaoanzisha vituo hivi kuweka mazingira bora yanayowavutia wazazi na watoa huduma. Mazingira hayo ya kimalezi yanapoboreshwa humnufaisha mtoto kwa namna kadhaa.
Kwanza, yanamsaidia
mtoto kuchangamka kiakili ukilinganisha na watoto wanaolelewa nyumbani. Tafiti
zilizofanywa katika nchi zilizoendelea zinathibitisha kuwa watoto waliopelekwa
kwenye vituo vya malezi mapema wanakuwa wachangamfu kiakili kuliko wenzao
wanaolelewa nyumbani.
Sababu
kubwa ni kuwa katika kituo mtoto anakuwa na fursa ya kuchangamana na wenzake
wanaotoka kwenye familia nyingine. Kucheza, kuzungumza, kuwasiliana na wenzake humfanya
ajifunze mambo mapya kwa wepesi kuliko kama angekuwa mwenyewe nyumbani.
Lakini
pia, malezi haya hufanyika kwa mfumo wa shule zisizo rasmi. Mtoto hupatiwa vifaa
vya kujifunzia na kucheza vinavyolingana na mahitaji yake. Shughuli zake
hufanyika kwa kufuata mtiririko maalum tangu anapowasili mpaka anapoondoka. Wakati
mwingine mtoto hulazimika kuvaa sare za shule na hivyo kujisikia yuko shuleni.
Kwa
sababu hiyo, vituo hivi hujenga daraja muhimu kati ya maisha ya nyumbani na
shule. Mtoto huwa katika mazingira ya kishule shule ambayo hata hivyo
hayamshinikizi kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu. Hali hii humfanya mtoto
azoee mazingira ya shule mapema kuliko anapopelekwa shuleni akitokea nyumbani
moja kwa moja.
Vile vile
kutokana na ukweli kuwa malezi haya hufanywa kibiashara (wakati mwingine) na
watu wenye uelewa wa makuzi ya watoto, mzazi anakuwa na uhakika na huduma
anazopatiwa mwanae. Kwamba mwanae yuko kwenye mikono salama humfanya mzazi aendelee
na kazi zake kwa utulivu kuliko anapomkabidhi msichana wa kazi.
Changamoto za malezi ya
vituoni
Hata hivyo, penye faida
hapakosekani changamoto. Manufaa ya huduma hizi mara nyingi yanategemea zaidi
ubora wa huduma zinazotolewa. Vinginevyo, changamoto kadhaa zinaweza kujitokeza.
Mosi, tafiti zilizofanyika katika
nchi zilizoendelea zimebaini uwezekano
wa kuzorota kwa uhusiano kati ya mzazi na mtoto anayehudhuria vituo hivi tangu
akiwa mtoto. Kwa mujibu wa tafiti hizi, mtoto anayeanza kuhudhuria malezi ya
vituo katika umri mdogo anakuwa kwenye hatari ya kuwa na uhusiano hafifu na
wazazi wake.
Pia, katika vituo hivi mara nyingi
walezi huwaangalia watoto wengi kwa wakati mmoja. Malezi haya ya kimakundi humfanya
mtoto mmoja moja kukosa mtu wa kushughulika na mahitaji yake binafsi.
Kwa mfano, mtoto wa umri wa mwaka
mmoja kwa kawaida ana madai mengi. Anapohitaji kitu, anahitaji awepo mtuanayeweza
kumsikiliza kwa wakati. Wingi wa watoto usioendana na idadi ya kutosha ya
walezi huweza kufanya hili lisiwezekane.
Katika mazingira ambayo mtoto hapati
usikivu wa mlezi, anakuwa kwenye hatari ya kutafuta mbadala kwa lengo la kupata
usikivu huo kama vile kulia bila sababu, ubinafsi na ugomvi.
Mbali na hayao, upo uwezekano wa
mtoto kuanza kujifunza tabia zisizotarajiwa. Kukaa muda mrefu na watu wengine
mbali na familia yake katika umri ambao bado hajajifunza lolote kutoka kwenye
familia yake, hukaribisha uwezekano wa kujifunza tabia ngeni zinazoweza kumstua
mzazi.
Vile vile, zipo tafiti
zinazohusianisha huduma hizi na matatizo ya afya kwa watoto. Kwamba
wanapolelewa katika mazingira ya pamoja bila uangalizi makini, watoto huwa
kwenye hatari ya kuambukizana magonjwa.
Inaendelea
Fuatilia Safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa makala kama hizi.
Asante sana kwa kutupa tafiti nzuri kuhusu watoto na makuzi yao.
JibuFutaTaiga ili liendelee lazima Lowe na misingi mizuri tokea makuzi awali ya mtoto kwenye familia.