Mambo Yanayokuza Motisha kwa WafanyakaziPengine umewahi kufanya kitu kwa sababu tu ulilazimika kukifanya. Moyoni hukusikia msukumo wowote isipokuwa hofu ya kushindwa kufikia matarajio ya mtu mwingine. Lakini pia inawezekana umewahi kufanya kitu bila kusukumwa wala kufuatiliwa. Ndani yako unakuwa na furaha na msukumo unaokuhamasisha kutekeleza jambo si kwa sababu ya hofu iliyotengenezwa na wengine bali shauku ya kufikia kiwango kinachokupa kuridhika.

Ndivyo ilivyo kazini.  Wapo wanaofanya kazi kwa sababu wanamwogopa kiongozi wao. Jitihada yao kazini inategemea sheria na vitisho kutoka kwa kiongozi. Inapotokea kiongozi huyo hayupo karibu, watu hawa hukosa msukumo.  

Kwa hakika utendaji kazi wa namna hii hauwezi kuleta tija. Kwanza, mtu anayetegemea msukumo wa nje kufanya kazi hawezi kujituma. Atafanya kazi kwa mazoea. Pili, ni vigumu kuwa mbunifu. Huwezi kuwa na uwezo wa kutafuta majibu ya matatizo kama huna msukumo unaoanzia ndani yako.

Hata hivyo, kiongozi anaweza kuweka mazingira yanayowapa wafanyakazi motisha ya kutekeleza majukumu yao kwa kujituma bila kutegea. Motisha ni hamasa inayomsukuma mtu kufanya jitihada za kufikia malengo. Mtu mwenye motisha hahitaji uangalizi wa karibu kutekeleza wajibu wake.

Makala haya yanaangazia matano yanayosaidia kukuza motisha ya watu wanaofanya kazi chini yako wewe kama kiongozi.

Mazingira bora ya kazi

Hamasa ya kazi inaanzia kwenye namna unavyomwezesha mfanyakazi kutekeleza kazi yake bila vikwazo. Utendaji wa kazi, kwa mfano, unategemea upatikanaji wa vitendea kazi vya msingi. Hakikisha vitendea kazi anavyovihitaji mfanyakazi wako vinatosheleza.

Pia, weka mazingira yanayomwezesha mfanyakazi kutumia vipaji vyake ipasavyo. Moja wapo ya sababu zinazoongeza motisha ya kazi ni mtu kuona mamna gani anaweza kutumia uwezo alionao kikamilifu. Weka mazingira yanayompa fursa hiyo.  

Kadhalika, maslahi mazuri yanampa mfanyakazi utulivu wa nafsi. Mfanyakazi mwenye msongo wa mawazo wa namna atakavyoendesha maisha yake, hawezi kuwa na hamasa ya kufanya kazi kwa kujituma.  Mlipe mfanyakazi wako kiwango kinacholingana na makubaliano mliyojiwekea.

Baadhi ya viongozi wana tabia ya kuzuia stahili za mfanyakazi kwa sababu zisizoeleweka. Mwisho wa mwezi unapofika ndio kwanza wanajifanya wako na mambo mengi kiasi cha kuchelewesha mishahara. Haipendezi. Mpe mtu kile unachojua ni haki yake. Kama huna sababu ya msingi, lipa madai yoyote ya haki kulingana na kazi aliyoifanya.

Kuaminika na kuheshimika

Kila binadamu analo hitaji la kuaminiwa. Unapokuwa na uhakika mtu unayemheshimu anakuamini unakuwa na motisha ya kufanya vizuri zaidi kukidhi imani yake. Kama kiongozi kazini, unahitaji kuwa na tabia ya kuonyesha unaamini utendaji wa watu wako pasipo kuwaingilia bila sababu.

Unaweza kuonyesha imani kwa namna nyingi. Kwa mfano, badala ya kumfuatilia mtu kwa karibu mno, mpe kiasi fulani cha uhuru wa kufanya kazi kwa namna anayoona inafaa muhimu asiharibu kazi. Hitaji kuona matokeo ya kazi badala ya kudhibiti kila kinachofanywa ikiwa si lazima.

Kadhalika, kuwaamini wafanyakazi kunakwenda sambamba na kuwaheshimu. Heshima kwa watu walio chini yako –iwe ni kwa maneno na vitendo vyako –inakutengenezea mazingira ya kuheshimiwa. Epuka kuonekana unawadharau watu kwa kuwatendea kama watoto.

Hata pale wanapokuwa wamekosea onyesha staha kwa namna unavyoshughulika makosa yao. Kwa mfano, huna sababu ya kumfokea mtu kwa sababu tu una madaraka. Jifunze kudhibiti hasira hata pale unapokuwa na sababu ya kuhalalisha kuudhika mbele ya kadamnasi.

Kutambuliwa na kushirikishwa

Kutambuliwa ni kuonyesha kuelewa nafasi ya mfanyakazi wako kwenye ofisi, idara, kampuni au taasisi.  Unapomtambua mfanyakazi, unamfanya ajisikie kuthaminiwa. Kwa mfano, kufahamu jina na kumtambua kwa nafasi aliyonayo inatuma ujumbe kuwa unathamini uwepo wake.

Kadhalika, namna bora ya kuthibitisha kuwa unawatambua wafanyakazi wako ni kuwafanya wajione ni sehemu ya taasisi au kampuni yako. Washirikishe kwenye maamuzi hata kama unajua wewe ndiye mwenye sauti ya mwisho. Omba mawazo ya watu waliochini yako. Onekana ukiandika mawazo unayoyapokea. Kile kinachowezekana kufanyiwa kazi, kitekeleze. Unapofanya hivi kwa dhati watu watakuwa na ari ya kazi.

Kueleweka kwa malengo

Moja wapo ya mambo yanayofanya watu wakose ari ya kazi, wakati mwingine ni kutokueleweka kwa malengo ya taasisi. Hali hii hufanya kila mtu ajikute anafanya kile kinachomjia kichwani ili naye aonekane anachapa kazi.

Fanya jitihada wafanyakazi wajue kampuni au taasisi inalenga kufika wapi. Malengo ya muda mrefu na ya muda mfupi yaeleweke. Kwa mfano, kama ni kampuni, ifahamike mnataka kupata mafanikio gani katika kipindi cha mwaka mmoja. Kila mmoja aelewe mwelekeo wa pamoja.

Lakini ili malengo hayo ya kitaasisi yawe na maana, lazima uhakikishe kila mmoja anajua anapaswa kufanya nini. Ainisha majukumu ya kila mfanyakazi kuepusha mwingiliano usio na sababu. Kila mmoja afanye kazi yake bila kuingilia majukumu ya mwenzake.

Kadhalika, ni vyema na wewe kama kiongozi ukatabirika. Hakikisha waliochini yako wanajua kwa hakika unatarajia nini kwao. Kutabirika kwako kama kiongozi kunarahisisha kazi ya watu kukidhi matarajio uliyonayo.

Usalama wa ajira

Watu wanapenda kuwa na uhakika na kesho. Hofu ya kufutwa kazi, kuonewa, kudhulumiwa, inaondoa motisha kazini. Ukitaka kuongeza ari ya kazi kwa wafanyakazi wako, wafanye wajisikie wako salama.

Njia ya kwanza kumhakikishia mtu usalama wake ni kumpa mkataba. Hili ni sharti la kisheria na kisaikolojia. Mfanyakazi anapokuwa na mkataba anaouridhia anakuwa hana sababu ya kuwa na wasiwasi na kesho.


Sambamba na hilo, jitahidi kuaminika. Epuka kuonekana mtu mwenye tabia ya upendeleo wa namna yoyote ile. Makundi ya wafanyakazi ‘vipenzi’ si tu yanawavunja moyo wasio ‘vipenzi’ lakini pia yanazalisha misuguano inayoweza kufubaza ufanisi wa kampuni, idara au taasisi unayoiongoza. 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Pay $900? I quit blogging