Vigezo Vinne Unapotafuta Msichana wa Malezi

PICHA: Gumtree South Africa


MALEZI katika enzi tulizonazo hayafanani na vile iliyokuwa hapo zamani. Mambo yamebadilika. Kwa mfano, zamani wazazi wetu hawakuwa na shida ya nani hasa abaki na mtoto nyumbani. Mama alikuwepo nyumbani. Kazi yake kubwa ilikuwa malezi. Hata katika mazingira ambayo mama hakuwepo, bado walikuwepo ndugu na jamaa walioweza kubeba jukumu hili kwa muda.

 Hivi sasa mfumo wa malezi umebadilika. Wazazi ambao wote kwa pamoja wanalazimika kwenda kazini, wanalazimika kuweka utaratibu mzuri wa mtoto kupata malezi yasiyo na mama.

Ulazima wa malezi mbadala

Kwa wazazi wengi, zipo huduma mbili mbadala za malezi. Moja, huduma zisizo rasmi za malezi zinazopatikana katika mazingira ya nyumbani. Kwa mfano, wazazi huwaomba ndugu na jamaa wanaoishi katika mazingira ya nyumbani kumwangalia mtoto ili kuwaruhusu kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.

Pili, zipo huduma rasmi zinazotolewa kwenye vituo maalum vya malezi kwa watoto kwa mujibu wa sheria. Kupitia utaratibu huu, mama humkabidhi mwanae kwa mlezi, aghalabu mwenye utaalamu wa makuzi, kuanzia asubuhi na humfuata mtoto baada ya saa za kazi. Katika kituo cha malezi, wazazi huchagua huduma zinazolingana na mahitaji yao.

Kwanza, wanaweza kuhitaji uangalizi wa mtoto pekee bila matarajio ya elimu rasmi (day care). Lakini wanaweza pia kuhitaji mtoto apatiwe malezi sambamba na elimu rasmi (nursery). Aidha, ikiwa umri wa mtoto tayari unaruhusu, wazazi wanaweza kumwanzisha shule ya msingi kwa mfumo wa kutwa au bweni.

Tutajadili huduma hizi moja baada ya nyingine kwa kuangalia fursa na changamoto za kila moja. Kwa kuanzia, tunaangazia huduma ya malezi rahisi kupatikana kuliko zote kupitia wasichana wa kazi wanaoajiriwa mahususi kwa ajili ya kuwaangalia watoto.

Wanavyopatikana

Wasaidizi wa nyumbani, maarufu kama ‘house girl’ ni watoto au vijana wadogo waliokulia katika mazingira ya kawaida, mara nyingi kijijini, wanaoajiriwa na wazazi kwa lengo la kuwasaidia kumtazama mtoto wakati wao wakiwa kazini. Sambamba na malezi, wasichana hawa husaidia kazi za ndani kama vile usafi, kuandaa chakula, kutunza nyumba na majukumu mengine kadri yanavyojitokeza.

Kwa kawaida walezi hawa hupatikana kwa utaratibu usio rasmi unaotegemea mfumo wa kufahamiana na ndugu, jamaa na marafiki. Ndugu hawa wanaweza kuwaunganisha wazazi wanaomhitaji msichana anayetafuta kazi ya kufanya.

Hakuna utaratibu rasmi unaowawezesha waajiri wenye uhitaji kuwa na uhakika na historia yake, ujuzi wake pamoja na tabia zake kwa ujumla. Hata hivyo, kwa kubahatisha inawezekana wazazi wakampata kupitia watu wanaofahamika.

Wajibu wao kimalezi

Kwa ujumla, msichana wa kazi ndiye mtu anayetumia muda mwingi na mtoto kuliko mtu mwingine yeyote kwenye familia. Ndiye anayefahamiana na mtoto kwa karibu zaidi kwa sababu ndiye anayehakikisha mtoto anapata chakula na huduma nyingine za muhimu wakati wazazi wakiwa kazini.

Kwa upande mwingine, yamekuwepo matukio ya akina dada hawa kudaiwa kuwafundisha watoto tabia zisizofaa. Matukio haya, mara nyingine, hutokea katika mazingira ambayo binti mwenyewe hajui namna nyingine bora zaidi ya kukaa na mtoto. Alivyolelewa yeye ndivyo anavyofanya.

Hata hivyo, wakati mwingine, huwa ni matokeo ya visasi wanapojisikia hawatendewi haki na waajiri wao. Kwa mfano, mara nyingi, wasichana hawa huajiriwa bila mikataba. Malipo yao hayalingani na kazi nyingi wanazozifanya. Wengi wao huwa wa kwanza kuamka na wa mwisho kulala. Hali ya kutokuridhika na mazingira ya kazi huongeza uwezekano wa vitendo visivyotarajiwa.

Kwa kuwa hakuna mzazi angependa nia njema ya kumtafuta msichana wa kazi ilete matatizo, tunapendekeza hatua nne za kuchukua katika kuboresha huduma za malezi kupitia akina dada hawa ambazo, kwa hakika, zinahitajika kwa wazazi wengi.

Mfahamu kabla

Wapo wasichana wanaotoka kwenye familia zilizokuwa na migogoro. Mazingira kama haya huwafanya wawe wepesi kugombana, kukwazwa hata kuwa tayari kuwaumiza wengine. Pia wapo wanaotoka kwenye familia zenye imani za kishirikina.

Fanya jitihada za kumfahamu kabla hujafanya maamuzi. Huwezi kumfahamu mtu kirahisi lakini ni vyema kujua ametoka wapi, aliishi vipi na familia yake, misimamo yake na mambo mengine ya msingi. Ili hayo yawezekane, ni vizuri ukampata kupitia watu wanaomfahamu vizuri.

Mwelimishe ajue wajibu wake

Mitafuruku mingi kati ya waajiri na hawa mabinti wakati mwingine inachangiwa na kutokufahamu majukumu yao ipasavyo. Waajiri wengi huwa na matarajio makubwa kwa akina dada hawa ingawa hawawasaidii kujua kile wanachopaswa kukifanya.

Ni vyema mara baada ya kufanya makubaliano naye, hakikisha anajua utaratibu kamili wa kazi. Afahamu anaamka saa ngapi, anatakiwa kufanya kipi siku nzima na kipi hapaswi kukifanya. Ukifanya hivyo unapunguza uwezekano wa makosa ya kutokujua jambo sahihi la kufanya.

Mtendee haki

Mfanye binti wa kazi awe sehemu ya familia yako. Mfanye ajisikie kupendwa kama mwanafamilia mwingine. Mtu anayependwa huchangamka moyo na hivyo kuwa na hamasa ya kujituma. Sambamba na hilo, epuka mahusiano yasiyo ya kimaadili na msichana wa kazi. Makosa kama hayo hujenga mazingira ya kudharaulika. Ukidharaulika, ni rahisi mwanao kuwa mhanga.

Aidha, mtengenezee mazingira bora ya kazi. Kwa mfano, unaweza kufikiria kumtengenezea utaratibu wa kujiendeleza kitaaluma. Hakikisha unaonesha kutambua kazi anazozifanya. Kutambuliwa ni hitaji la msingi kwa kila mwanadamu. Kutambuliwa kunamjengea ari ya kujituma.

Mfundishe kwa vitendo

Onesha kwa vitendo namna unavyotarajia mtoto ahudumiwe. Binti atajifunza kwa vitendo. Unapopata muda fanya kazi za ndani kama unavyotarajia afanye yeye. Pika, tenga chakula, fua nguo ili kuonesha kuwa unaishi matarajio yako. Unapofanya hivyo, binti atajifunza.


Kadhalika, tambua kuwa upo uwezekano wa mwanao kujifunza tabia usizozitarajia. Unaporudi nyumbani jua maendeleo ya mwanao kitabia. Jitahidi kuzungumza na mwanao kubaini ikiwa yapo yasiyofaa aliyojifunza. Unapoyabaini chukua hatua za haraka kuyarekebisha.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Pay $900? I quit blogging