Unayopaswa Kuzingatia Unapompeleka Mtoto Wako Katika Vituo vya Malezi -1

PICHA: Hope for Bukasa


UTARATIBU wa wazazi kuwapeleka watoto kwenye vituo vya malezi umeanza kuwa maarufu hapa nchini. Karibu kila mji mdogo katika mikoa yote vipo vituo kadhaa mahususi kwa ajili ya kuwatunza watoto wakati wazazi wao wakiwa kazini. Kinachofanya huduma ya malezi ya vituoni kuwa maarufu ni changamoto za akina dada wa kazi, ambao mara nyingi, huwa ni wadogo kiumri na hawana uwezo wala ari ya kuwalea watoto vizuri.

Malezi ya watoto katika vituo maalum hufanyika katika mfumo ulio rasmi kuliko ilivyo nyumbani. Mbali na Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009, ipo Sheria ya Vituo vya Malezi ya Watoto ya mwaka 1981 ambayo, pamoja na kutambua umuhimu wa vituo hivi, imeweka masharti na utaratibu wa kufuata katika utoaji wa huduma hizi.

Ingawa sheria ilitoa fursa kwa yeyote kutoa huduma hizi, masharti yalionekana kuwa magumu kwa mashirika mengi binafsi kuwekeza kwenye eneo hili. Hata hivyo, mashirika ya nje kama UNICEF na CARITAS yaliwahi kufadhili mradi ya vituo vya malezi ya watoto kwa miaka ya nyuma. Bahati mbaya hapakupatikana utaratibu endelevu kuhakikisha miradi hiyo inaendelea.

Vituo vingi vilivyopo hivi sasa vinaendeshwa na watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali. Lengo ni kuwawezesha wazazi wanaofanya kazi mbali na nyumbani kuendelea na shughuli zao bila kuwa na wasiwasi na usalama wa watoto. Matokeo ya tafiti mbalimbali yanaonesha kwamba huduma ya vitu vya malezi ya kutwa kwa watoto yana faida kadhaa kwa watoto.

Uchangamfu wa kiakili

Tafiti zilizofanywa katika nchi zilizoendelea zinathibitisha kuwa watoto waliopelekewa kwenye vituo vya malezi mapema wanakuwa wachangamfu kiakili kuliko wenzao wanaolelewa nyumbani. Katika umri wa miaka miwili, kwa mfano, watoto wanaohudhuria kwenye vituo hivi wanakuwa wepesi zaidi kujifunza lugha kuliko wale wanaolelewa nyumbani katika umri huo.

Sababu kubwa ni kuwa, katika kituo cha malezi, mtoto anakuwa na fursa ya kuchangamana na wenzake wanaotoka kwenye familia nyingine. Kucheza, kuzungumza, kuwasiliana na wenzake ni fursa kwake kujifunza mambo mapya kwa wepesi kuliko anapokuwa kwenye mazingira ya nyumbani.

Lakini pia, malezi katika vituo hufanyika kwa mfumo wa shule zisizo rasmi. Mtoto hupatiwa vifaa vya kujifunzia na kucheza vinavyolingana na mahitaji yake. Shughuli zake hufanyika kwa kufuata mtiririko maalum tangu anapowasili asubuhi mpaka anapoondoka. Wakati mwingine, mtoto hulazimika kuvaa sare za shule na hivyo kujisikia yuko shuleni.

Kuzoea mazingira ya shule

Vituo vya malezi hujenga daraja muhimu kati ya maisha ya nyumbani na shule. Mazingira ya shule yasiyomshinikiza mtoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu humfanya mtoto azoee mazingira ya shule ukilinganisha na mwenzake anayebaki nyumbani.

Ingawa baadhi ya vituo huwalazimisha watoto kuanza kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu kabla ya wakati, kufanya hivi ni kinyume na utaratibu. Kwa mfano, watoto wanaolamishwa kuanza kujifunza masomo katika umri mdogo, hukabiliwa na uwezekano wa kujenga mtazamo hasi na mazingira ya shule.

Kumlazimisha mtoto wa umri mdogo, mfano miaka mitatu, kufanya mahesabu ni kuzidisha matarajio. Uwezo wake wa kiufahamu bado ni mdogo na hauwezi kumudu mafunzo rasmi. Hata hivyo, mara nyingi matarajio makubwa waliyonayo wazazi ndiyo hasa yanayochangia kuwafanya walezi na walimu kuweka msisitizo wa kitaaluma kwa watoto. Badala ya watoto kutumia muda wa kutosha kucheza, kuimba na kufurahia mazingira ya shule, wanabanwa kufanya kazi nyingi zinazochosha akili.

Jambo muhimu ni kwamba vituo hivi vinapoendeshwa na watu wenye uelewa wa masuala ya watoto, vinamsaidia mtoto kujiandaa vizuri na maisha ya shule. Sambamba na hilo, humpa mzazi fursa ya kuendelea na kazi zake kwa utulivu akijua mtoto yuko kwenye mikono salama.

Changamoto nazo zipo

Tafiti zilizofanyika katika nchi zilizoendelea zinabainisha uwezekano wa kuzorota kwa uhusiano kati ya mzazi na mtoto anayepelekwa kwenye kituo cha malezi tangu akiwa mdogo. Kwa mujibu wa tafiti hizi, mtoto anayeanza kuhudhuria malezi ya vituo katika umri mdogo anakuwa kwenye hatari ya kuwa na uhusiano hafifu na wazazi wake.

Hata hivyo, kuzorota kwa uhusiano huu ni suala linalotegemea zaidi tabia ya mama. Utafiti mmoja ulionyesha kwamba kuna uwezekano wa uhusiano huo kuzorota hata katika mazingira ya nyumbani. Maana yake ni kwamba kinachozorotesha uhusiano ni umbali wa kihisia kati ya mama na mwanae. Ikiwa mama ataweza kuwa na ukaribu na mwanae baada ya saa za kituoni, hakuna sababu ya mzazi kuwa na wasiwasi.

Kujifunza yasiyotarajiwa

Vituo vingi hapa nchini vinakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya watoto wasiolingana na idadi ya walezi. Makundi makubwa ya watoto humnyima mtoto mmoja moja fursa ya mahitaji binafsi kushughulikiwa. Tunafahamu, kwa mfano, mtoto wa umri wa kati ya mwaka mmoja na miwili huwa na madai mengi yanayoweza kuwa usumbufu kwa mlei. Mtoto wa umri huu anahitaji mtu anayeweza kumsikiliza kwa karibu. Wingi wa watoto usioendana na idadi ya kutosha ya walezi huweza kufanya hili lisiwezekane.

Katika mazingira ambayo mtoto hapati usikivu wa kibinafsi wa mlezi, anakuwa kwenye hatari ya kutafuta mbadala wa kupata usikivu kwa kulia lia bila sababu, kuwa mbinafsi na wakati mwingine kuwa mgomvi. Kadhalika, mtoto kukaa muda mrefu na watu wengine mbali na familia yake katika umri ambao bado hajajifunza lolote kutoka kwenye familia yake, huongeza uwezekano wa kujifunza tabia ngeni.

Vile vile, zipo tafiti kadhaa zinazohusianisha malezi ya vituoni na changamoto za kiafya kwa watoto. Hili, hata hivyo, linategemea na hali ya usafi ilivyo na mazingira yasiyo na uangalizi mzuri yanayowaweka watoto kwenye hatari ya kuambukizana magonjwa.

INAENDELEA

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Pay $900? I quit blogging