Namna ya Kupunguza Changamoto za Wasichana wa Kazi
TUMETAJA mambo mawili yanayobadili mfumo wa
malezi. Mosi, ni kubadilika kwa majukumu ya kijinsia yaliyozoeleka katika
jamii. Mama anapoingia kwenye soko la ajira na kwenda kazini kama ilivyozoeleka
kwa baba, changamoto inayojitokeza ni namna wanavyoweza kumlea mtoto wao katika
muda wa kazi.
Pili ni kufifia kwa utamaduni wa familia
tandao unaozorotesha msaada wa kimalezi uliozoeleka kutoka kwa ndugu wa karibu.
Mawili haya yanalazimisha familia za sasa kutafuta namna nyingine ya malezi
kuwapa fursa wazazi kuendelea na kazi.
Katika makala haya, tunatazama huduma ya
akina dada wanaoajiriwa kuwasaidia wazazi kulea watoto wakati wa kazi, maarufu
kama ‘house girls’. Tunaangazia namna tunavyoweza kupunguza changamoto za
huduma zao.
‘House girls’ ni watoto au vijana wadogo waliokulia
katika mazingira ya kawaida, mara nyingi kijijini tena bila elimu kubwa,
wanaoajiriwa na wazazi kwa lengo la kuwasaidia kumtazama mtoto wakati wa kazi.
Sambamba na malezi, wasichana hawa hufanya kazi za ndani.
Kwa kawaida walezi hawa hupatikana kwa
utaratibu usio rasmi unaotegemea mfumo wa kufahamiana na ndugu, jamaa na
marafiki wanaoweza kuwaunganisha wazazi wenye uhitaji na msichana anayetafuta
kazi. Hakuna utaratibu rasmi unaowawezesha waajiri wenye uhitaji kuwa na
uhakika na historia yake, ujuzi wake pamoja na tabia zake kwa ujumla.
Hata hivyo, hutokea wakati mwingine
wakapatikana kupitia kwa watu wanaofahamika. Ingawa utaratibu huu wengine
huuchukulia kama namna nyingine ya usafirishaji wa binadamu, lakini umekuwa
ukiwasaidia wazazi kuwa na uhakika na wapi hasa watoto hawa wanatoka.
Mazingira
yao ya kazi
Mara nyingi, mabinti hawa huajiriwa bila
mikataba inayoeleweka na hulipwa kiasi kidogo cha fedha. Hata hivyo, nje na
malipo ya fedha taslimu, wazazi wengi huwapa marupurupu kama chakula, matibabu
na huduma nyingine za msingi.
Ratiba zao za siku hujaa shughuli nyingi
zisizolingana na kipato chao. Wengi wao huwa wa kwanza kuamka na wa mwisho
kulala. Waajiri wao huwa na matumaini makubwa kupindukia.
Pamoja na kazi kubwa wanayofanya, yamekuwepo
matukio ya wasichana hawa kuonewa na waajiri wao kwa namna mbalimbali. Wapo
wanaotendewa kama watumwa wasiostahili heshima kama binadamu wengine. Wengine
hunyimwa haki zao za msingi.
Katika mazingira haya, wasichana hawa, wakati
mwingine hujenga tabia zisizofaa ambazo huzorotesha uhusiano wao na waajiri
wao. Hali ya kutokuelewana kati ya mwajiri na mtoto huyu wa kazi husababisha
hasira, uchungu na visasi ambavyo, mara nyingi huishia kwa mtoto asiye na
hatia.
Utendaji
wao kimalezi
Kwa kawaida wasichana hawa, ambao mara nyingi ni watoto, huwa hawana uzoefu na malezi. Utendaji wa wengi wao hutegemea maelekezo ya kila mara. Hata hivyo, pamoja na hayo, bado wazazi wenye uwezo mdogo kiuchumi huwaona kama jawabu la changamoto ya malezi.
Kwa upande mwingine yamekuwepo matukio ya
akina dada hawa kuwafundisha watoto tabia zisizofaa kwa kujua au kutokujua.
Haya, hata hivyo, mara nyingi hufanyika kulipiza kisasi kwa hisia za kutokutendewa
haki.
Kwa kuwa huduma za malezi kupitia akina dada hawa zinaweza zisikwepeke kwa wazazi wengi, ni muhimu kujadili namna gani tunaweza kupunguza wa changamoto za malezi yanayosimamiwa na wasichana hawa. Changamoto hizi, kwa kiasi kikubwa, zinazotokana na kutokufahamiana vya kutosha sambamba na mahusiano halifu kati ya mwajiri na msichana. Tunapendekeza yafuatayo:
Kufahamu historia ya binti
Ipo haja ya kujitahidi kufahamu msichana ametoka familia
gani, aliishi vipi na familia yake, misimamo yake, imani, angalau mambo ya
msingi. Ili hayo yawezekane, ni vizuri kumpata kupitia watu wanaomfahamu vizuri.
Unapokuwa na fursa ya kumfahamu binti vizuri binti, unaweza
kufanya maamuzi sahihi mapema ikiwa unaweza kukaa naye ama la.
Mwelimishe majukumu yake mapema
Mitafuruku mingi kati ya waajiri na hawa mabinti wakati
mwingine inachangiwa na kutokufahamika kwa majukumu yake ipasavyo. Waajiri
wengi huwa na matarajio makubwa kwa akina dada na hivyo hawawasaidii kujua
wanachopaswa kukifanya.
Ni vyema mara baada ya kukubaliana naye kuwa anaishi na
familia yako kwa lengo la kumwangalia mtoto, uhakikishe anajua utaratibu kamili
wa kazi. Ukifanya hivyo unapunguza uwezekano wa makosa yanayotokana na
kutokujua jambo sahihi la kufanya.
Kujenga mahusiano mazuri na binti
Mfanye binti wa kazi awe sehemu ya familia yako. Mfanye ajisikie
kupendwa kama mwanafamilia mwingine. Unapofanya hivyo, unamfanya achangamke
moyo na hivyo kuwa na hamasa ya kujituma.
Kwa mfano, unaweza kumtambulisha kwa wageni kama sehemu
ya familia yako na unaweza kufikiria kumweka kwenye picha rasmi za familia
unazoning’iniza ukutani.
Sambamba na hilo, epuka mahusiano yasiyo ya kimaadili na
wasichana hawa. Unapofanya hivyo, unajenga mazingira ya kudharaulika.
Ukidharaulika, ni rahisi mwanao kuwa mhanga.
Mpe huduma anazostahili
Hakuna mfanyakazi hatamani kupata marupurupu. Hata wewe
unahitaji mkubwa wako wa kazi akuangalie kimaslahi, na atambue kazi nzuri
unayomfanyia.
Vivyo hivyo, na wewe fikiria kumpa msichana wako wa kazi
huduma zinazomvutia. Mtengenezee mazingira bora ya kazi.
Kwa mfano, unaweza kufikiria kumtengenezea utaratibu wa kujiendeleza
kitaaluma. Pia unaweza kuhakikisha unatambua kazi anazozifanya kila siku jioni
unaporudi nyumbani. Kwa kufanya hivyo unamjengea ari ya kazi.
Onesha mfano mzuri
Huwezi kutarajia binti wa kazi aishi vizuri na watoto,
wakati wewe mwenyewe huoneshi kuwajali watoto wako. Onesha kwa vitendo namna unavyotarajia
mtoto ahudumiwe. Binti atajifunza kwa vitendo.
Kadhalika, kuwa mfano kwa kufanya kazi za ndani kama
unavyotarajia afanye yeye. Pika, tenga chakula mezani, fua nguo inapobidi ili
kuonesha kuwa unaishi matarajio yako. Unapofanya hivyo, binti atakuheshimu.
Tumia muda wa kutosha na mtoto
Mtu anayetumia muda mrefu na mwanao ndiye mwenye nafasi
zaidi ya kuwekeza. Kwa sababu binti ndiye anayekaa na mwanao kwa muda mrefu,
upo uwezekano wa mwanao kufundishwa mambo usiyoyatarajia.
Ni vizuri kuhakikisha unafuatilia maendeleo ya kitabia ya
mwanao mara unaporudi nyumbani. Jitahidi kuzungumza na mwanao kubaini ikiwa
yapo yasiyofaa aliyojifunza. Unapoyabaini, weka mbadala wake mapema.
Pamoja na kuchukua hatua hizi, hatusemi kuwa mambo yatakuwa sawia. Zinaweza kuwepo changamoto. Lakini, hata hivyo, zinaweza kupungua.
Fuatilia Safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti
la Mtanzania kila Alhamisi kwa makala kama hizi.
Maoni
Chapisha Maoni