Mbinu za Kutengeneza Mtandao wa Ajira
Changamoto kubwa inayowakabili
vijana wanaotafuta kazi ni namna ya kupata taarifa sahihi zitakazowasaidia
kupata kazi. Ingawa vipo vyanzo vingi vya kupata taarifa hizo, watafuta kazi wengi
hutegemea matangazo rasmi ya ajira pekee kupitia vyombo vya habari.
Hata hivyo, tafiti za kazi na ajira
zinaonyesha kuwa nafasi nyingi za kazi hasa katika sekta binafsi hazitangazwi
hadharani. Waajiri wana tabia ya kutafuta mtu
anayeaminika kupitia vyanzo vinavyoaminika. Tafsiri yake ni kuwa kijana
anayetegemea kupata taarifa za kazi kupitia matangazo rasmi, anapitwa na
taarifa nyingi muhimu.
Katika makala haya, utajifunza mbinu nne za kutengeneza mtandao wa kiajira utakaokusaidia kupata taarifa za kazi na ajira.
Imarisha uanachama katika makundi uliyomo
Kila mmoja wetu anayo makundi fulani ya kijamii anayojitambulisha nayo. Kuna sehemu za ibada, vyama vya kijamii na kitaaluma, watu uliowahi kusoma nao kwa ngazi mbalimbali za kielimu na makundi mengineyo. Makundi hayo ni hatua ya kwanza rahisi ya kutengeneza mtandao imara wa kiajira.
Unapokuwa sehemu ya kundi ulilonalo,
kwa mfano, ukawa mwanachama mwaminifu, unajipa nafasi muhimu ya kuaminiwa bila
gharama yoyote. Watu wanapokufahamu na kukuamini unakuwa katika nafasi nzuri ya
kujenga uhusiano wa kudumu na watu wanaoweza kukusaidia.
Ili uweze kuaminiwa na watu, una
wajibu wa kuwa sehemu kamili ya kundi husika kwa kuonesha bidii na juhudi. Kama
ni kanisani, jitoe kwa moyo, fanya bidii. Watu watauona uwezo wako na itakuwa
rahisi kukusaidia watakapogundua unahitaji kazi.
Hudhuria mikutano na makongamano
Vijana wengi kutegemea taarifa wanazozipata kwa watu waliosoma nao, majirani, ndugu na marafiki. Hata hivyo, ikiwa watu hawa unaofahamiana nao wanafanana kwa aina ya mitazamo na uelewa, unaweza kujikuta ukijinyima fursa ya kupata taarifa muhimu wasionazo.
Vijana wengi kutegemea taarifa wanazozipata kwa watu waliosoma nao, majirani, ndugu na marafiki. Hata hivyo, ikiwa watu hawa unaofahamiana nao wanafanana kwa aina ya mitazamo na uelewa, unaweza kujikuta ukijinyima fursa ya kupata taarifa muhimu wasionazo.
Kwa sababu hiyo, unahitaji kukutana
na watu muhimu usiowafahamu kwa sasa ili kuongeza mtaji wako wa watu usionao hivi
sasa. Nenda kwenye mikutano, warsha na semina zinazoweza kukukutanisha na watu muhimu
na hata waajiri wanaoweza kukuona.
Kama unatafuta kazi ya uhasibu, kwa
mfano, lenga kukutana na watu wa namna hiyo kwenye mikutano inayokutanisha
wahasibu na wafanyabiashara. Kufanya hivyo kunaweza kukugharimu muda na fedha
kidogo lakini utaongeza mtaji wa watu unaofahamiana nao.
Jua namna ya kujitambulisha
Unapokuwa kwenye makundi ya watu,
hakikisha umejiandaa. Ikiwa una kadi ya wasifu wako (business card) iweke
karibu kisha tambua aina ya watu unaolenga kujenga mtandao nao. Nyenzo
unayoihitaji ni ujasiri wa kuwafuata na kuanzisha mazungumzo pale unapoona
wanaweza kukusikiliza.
Ni muhimu kuelewa mazingira ambayo unaweza kusikilizwa. Huwezi, kwa mfano, ukamfuata mtu ambaye tayari anaongea na mtu mwingine na ukategemea azingatie mazungumzo yenu. Hakikisha unayetaka kuongea naye yuko katika nafasi ya kukusikiliza.
Kadhalika, fahamu aina ya mazungumzo yanayoweza kumvutia mtu unayetaka kujenga naye mawasiliano. Kwa kawaida, watu muhimu wanapenda
kukutana na watu wenye mawazo mapana, watu wenye uelewa wa changamoto fulani
zinazoikabili jamii lakini pia wenye majibu ya changamoto hizo. Unapokuwa mtu
asiye na malengo yanayoeleweka, ni vigumu kumfanya mtu akuchukulie kwa uzito.
Jitambulishe kwa uwezo ulionao.
Tumia dakika moja za mwanzo katika
mazungumzo ya awali kujipambanua wewe ni nani na unalenga kufanya nini katika
jamii. Onekana ni mtu mwenye ndoto zinazoeleweka na kuelezeka ndani ya dakika moja.
Ni kuzingatia kuwa unapoongea na mtu muhimu, unahitaji kumpa nafasi azungumze kuliko
unavyozungumza wewe. Kufanya hivyo kutakupa fursa ya kumwelewa anajishughulisha
na mambo gani ili ujue unavyoweza kujitambulisha. Ukiweza kuunganisha shughuli
anazozifanya na ujuzi wako, ni rahisi mtu huyo kuona thamani yako kwake.
Endeleza mawasiliano kukuza uhusiano
Baada ya kupata usikivu wa mtu muhimu unayemhitaji, unao wajibu wa kufanya mawasiliano muda mfupi baada ya kuachana naye. Usipofanya mawasiliano naye, ni rahisi kusahaulika. Kama ulichukua mawasiliano, mtafute.
Hata hivyo, unapofanya mawasiliano chukua
tahadharani usimchoshe. Kwa kawaida, watu wanapenda uhusiano wa nipe nikupe.
Usijenge taswira ya mtu anayetarajia kuliko anavyoweza kuwa wa msaada.
Onekana ni mtu aliyekomaa kifikra na
anayeaminika. Badala ya kutaka kusikilizwa muda wote, tafuta namna unavyoweza
kusaidia kwa kutumia ujuzi ulionao. Ukifanya hivyo na ukapunguza utegemezi usio
wa lazima, watu watakuamini na watasukumwa kukupa msaada pale utakapouhitaji.
Wito kwa waajiri na taasisi za elimu
Kazi ya kutengeneza
mtandao wa kiajira inapoachwa mikononi mwa kijana mwenyewe, ufanisi wake
unakuwa na changamoto. Ipo haja ya kuwa na mfumo rasmi unaomwandaa kijana
anayeingia kwenye soko la ajira kukutana na watu anaowahitaji.
Taasisi za elimu, kwa
mfano, zinahitaji kuratibu vizuri zaidi mafunzo kwa vitendo yamwezeshe kijana
kujenga mahusiano endelevu ya kikazi. Kadhalika, kuna haja ya kuwa na vitengo
maalum vya unasihi katika taasisi za elimu kwa minajili ya kuwaunganisha vijana
na mazingira ya kazi.
Waajiri nao, kwa upande
mwingine, wasitegemee taasisi za elimu pekee katika kuwakuza vijana kiujuzi.
Kama wanufaika wa ujuzi huo, waone wajibu walionao katika kuwainua kiujuzi
vijana wanapojiandaa kuingia katika ajira.
Vijana wanahitaji watu
wa kuwalea na kuwakuza. Waajiri wawape nafasi za kujitolea, mafunzo kwa vitendo
na hata kuwakaribisha kwenye warsa na semina zinazoweza kuchangia kupanua wigo
wa mtandao wa ajira kwa vijana.
Makala haya yamechangiwa pia na Albert
William, Mratibu wa Ukuuzaji wa Ujuzi, ILO -Dar es salaam na Prosper
Mwakitalima wa Brand Exponentials.
Ahsante sana bwaya kwa makala haya..muhimu pia kwa waajiri kuwa karibu sana na taasisi za elimu..kufadhili miradi ya kiutafiti ili kunufaika na mawazo mapya waliyonayo vijana
JibuFutaKweli kabisa Albert. Unahitajika ushirikiano baina ya wadau mbalimbali kuwasaidia vijana :)
JibuFuta