Siri za Watu Wanaotekeleza Maazimio ya Mwaka Mpya
TULIJADILI
baadhi ya sababu zinazofanya watu washindwe kutekeleza maazimio wanayoyaweka
kila mwaka mpya unapoanza. Tuliona sababu kubwa tatu; kuweka maazimio kwa
msisimko tu wa kuingia mwaka mpya usioenda sambamba na tafakari ya kina; kuweka
malengo mapana mno yasiyopimika; na pale malengo yanapohusisha mabadiliko ya
tabia, kutokujua uliko mzizi wa mabadiliko hayo.
Melengo yawe mahususi
Usiweke
malengo mapana yasiyolenga jambo mahususi. Vunja vunja wazo kuu ulilonalo liwe malengo
madogo madogo yanayolenga jambo moja utakaloiishi kila siku.
Kwa
mfano badala ya kuazimia kujenga tabia ya jumla kusoma vitabu, vunja vunja
lengo hilo liwe kusoma kitabu kimoja kwa juma moja. Ukisema unalenga kujenga
tabia ya kusoma, haieleweki unalenga kusoma vitabu vipangi kwa mwezi, miezi
sita na hata miezi 12. Lengo la kusoma kitabu kimoja kila juma ni mahususi na
utaweza kulitathimini.
Kama
unataka kuwa na uhusiano imara na familia yako mwakani, fafanua kwa namna gani.
Je, unataka kujenga mazoea ya kuwahi nyumbani kila siku baada ya kazi? Je,
unataka kutoka na wanao kila mwisho wa juma? Fanya malengo yako yawe madogo
madogo na yapimike kwa muda maalumu. Ukifanya hivyo, utaisaidia akili yako
kujua kitu gani hasa kinakusudiwa na utaongeza uwezekano wa kutekeleza lengo
husika.
Weka mfumo wa kupima
utekelezaji wake
Utekelezaji
wa malengo mengi, kwa kawaida, huhusisha mabadiliko ya tabia. Huwezi kubadili
tabia usiyoweza kuipima. Hakikisha malengo yako yanapimika kadri unavyoendelea
kuyatekeleza.
Ili
uweze kupima, weka muda maalumu wa kuyatekeleza. Deadline. Andika malengo yako
mahali ikusaidie kukumbuka. Malengo yasiyoandikwa yanabaki kuwa ndoto tu. Ndoto
hazitekelezeki kirahisi.
Kama
unalenga kupanua biashara yako kwa mwaka huu, fikiria utakavyoweza kupima
upanuzi huo. Je, utatazama kiasi cha mtaji unaoongezeka? Je, ni kiasi cha
bidhaa unachoouza, idadi ya wateja unaowapata? Utapimaje? Lazima uwe na
utaratibu utakaokusaidia kupima unavyotekeleza malengo yako kadri muda
unavyokwenda.
Waambie watu unaowaamini ulichopanga
Wakati
mwingine ni rahisi kuachana na mipango uliyojiwekea kadri muda unavyokwenda. Sababu
ni kutokuwa na mfumo wa kukuwajibisha pale unapoteleza. Ni muhimu kuwa na watu
watakaokufanya ujisikie vibaya kuachana na mpango wako.
Baada
ya kuhakiki malengo yako, fikiria watu wako wa karibu unaoweza kuwaambia kile
ulichokipanga. Kama maazimio yako yanamhusu mkeo/mumeo, mshirikishe malengo
yako mapema. Kama malengo yanawahusu wanao, waambie.
Kwa
kufanya hivyo, unatengeneza mfumo wa kukuwajibisha pale unapoanza kususua
susua. Itakusaidia kuwa na hamasa ya kufanyia
kazi malengo yao kuliko yanapokuwa siri yako mwenyewe.
Kadhalika,
unapolenga kubadili tabia fulani usizozipenda waambie watu. Ikiwa unataka
kuacha sigara, pombe au tabia fulani wanazozijua rafiki zako, tangaza wazi
wazi. Waambie unataka kuacha sigara, pombe au uzinzi. Wanapojua mpango wako unajiweka
katika mazingira ya kulazimika kutekeleza ili usionekane mtu wa maneno yasiyo
na vitendo.
Muhimu
kuzingatia kuwa watu wanaweza kuwa kikwazo cha malengo yako. Huwezi kuambatana
na watu wanaoshabikia sigara, pombe na uzinzi na ukategemea ufanikiwe kuachana
na tabia hizo. Amua kukaa mbali na watu wenye tabia unazolenga kuachana nazo. Ambatana na watu wenye tabia unazotaka
kuzijenga.
Kama
unataka kuanza kusoma, jenga urafiki na watu wanaopenda kusoma. Kama unataka
kuwa na familia imara, jenga urafiki na watu wenye familia imara. Kama unataka
kuwa na mafanikio kitaaluma, ambatana na watu wenye ari ya kusoma. Watu wenye
tabia unazotaka kuzijenga, watakusaidia kuwa na motisha ya kwenda unakotaka
kwenda.
Usisubiri kesho, anza mara
moja
Mara
nyingi watu husahau malengo yao kwa sababu wanasubiri kuanza kesho. Wanaahirisha
kwa sababu wanajifariji kuwa bado wanajipanga. Lakini kadri muda unavyokwenda, wanajikuta
wakikosa hamasa.
Usisubiri
kesho kuanza kufanya kitu sahihi. Anza mara moja. Kama lengo ni kuanza kusoma,
kanunue kitabu leo anza kukisoma hata kama unafikiri huna muda. Muda
haukusubiri, utengeneze. Azimia kutengeneza muda wa kusoma. Utaweza.
Kama
unalenga kuongeza akiba kila mwezi, usisubiri mwezi ujao. Anza mwezi huu. Weka
akiba kabla ya kufanya matumizi. Ukisubiri mwezi ujao, hutaanza. Ni rahisi
kuahirisha kile usichoona sababu ya kukifanya leo.
Furahia hatua ndogo unayopiga
Huwezi
kutekeleza lengo kubwa bila hatua ndogo. Jifunze kufurahia hatua ndogo
unayopiga almuradi inakusaidia kuelekea kwenye lengo kubwa. Usisubiri
utekelezaji mkubwa ili ufurahie.
Hata
unapokwama, usikate tamaa na kughairi maazimio yako. Songa mbele. Kama unataka
kupunguza uzito, usikate tamaa unapogundua uzito ndio kwanza unaongezeka.
Furahia hatua yoyote ndogo unayopiga.
Watu
wengi hujisikia vibaya wanapoona hawawezi kukiishi kile walichokipanga. Ili
wasijisikie vibaya wanaamua kughairi mipango yao. Usiwe mtu wa namna hiyo. Wakati
mwingine jirihusu kujisikia vibaya ili uwe na motisha ya kupambana kutekeleza
malengo yako. Usikubali kujisikia vizuri kwa kuachana na malengo yako. Fanya
maamuzi.
Fuatilia Gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa Makala kama
hizi.
Asante mkuu kwa makala nzuri imeniongezea uelewa
JibuFuta