Jinsi ya Kumsaidia Mtoto Anayefanya Vibaya Shuleni
Si jambo la kufurahisha kwa mzazi unapoona mtoto hajafanya
vizuri masomoni. Unapofahamu kuwa maendeleo ya mwanao si kama vile ulivyotarajia,
ni rahisi kupatwa na simanzi, wasiwasi na hasira.
Ni dhahiri mzazi unatamani mtoto awe na mustakabali mzuri
kimaisha. Matumaini hayo yanakufanya uchukulie kushindwa kwake masomo kama kiashiria
cha kuharibika kwa maisha yake ya baadae. Hakuna mzazi angependa mtoto awe na
maisha yasiyoeleweka.
Kwa sababu ya matarajio makubwa uliyonayo kwake,
kinyume chake kinapotokea kinakuwa na nafasi kubwa kuzorotesha uhusiano wenu.
Kufeli kunaleta maana ya mtoto kujiharibia maisha yake kwa mikono yake mwenyewe.
Wakati mwingine mtoto hufanya vibaya hata baada ya
kuwa umeshaongea naye mara kadhaa. Katika hali kama hii, huwezi kuwa na utulivu
kuona mambo yanaharibika.
Kufeli
ni fursa ya mafanikio zaidi
Katika kila tatizo kuna fursa. Kufanya vibaya darasani
kunaweza kumwamsha mtoto usingizini akajifunza somo muhimu litakalobadilisha
maisha yake.
Inawezekana mwanao alikuaminisha kuwa anafanya
juhudi shuleni. Lakini kumbe anachokifanya shuleni ni tofauti na imani aliyokujengea.
Kufanya vibaya hufunua ukweli unaokusaidia
mzazi kuelewa hali halisi.
Vile vile, kufanya vibaya kunaweza kuwa fursa ya mtoto
kujifunza mapema matokeo ya kutokuweka juhudi masomoni. Hatua madhubuti
zinapochukuliwa mapema zinamnusuru mtoto na matokeo mabaya zaidi siku za usoni.
Ipo mifano mingi ya wasomi maarufu walioanza safari
yao ya kielimu kwa kufanya vibaya darasani. Hawakukata tamaa wala kukubali
kushindwa. Kufanya vibaya kuliwatengenezea njia ya kujikagua na kurekebisha
makosa. Kufeli si mwisho wa mafanikio.
Mruhusu mwanao kufanya vibaya
Kufanya
vibaya darasani humfanya mtoto ajisikie vibaya. Kujiona hajafikia malengo yake
binafsi, matarajio ya wazazi, na viwango vya shule humjengea wasiwasi na hatma
ya maisha yake. Hali hiyo, hata hivyo, yaweza kugeuka kuwa hamasa ya
kukabiliana na changamoto kwa ufanisi zaidi.
Mtoto
huyu anayejisikia vibaya kwa kushindwa kufaulu, hatapenda kujikuta katika
mazingira yayo hayo siku zijazo. Atahamasika kusoma kwa bidii ili aepuke
kujisikia vibaya kwa mara nyingine.
Kadhalika,
matokeo mabaya yanaweza kuwa sehemu ya safari ndefu ya kielimu kwa mwanao.
Kwamba ameshindwa kufikia malengo si tiketi ya kukatisha safari bali fursa ya
kujikagua na kujipanga upya.
Pamoja
na ukweli kuwa ungejisikia fahari mwanao kufanya vizuri darasani, hali halisi
inapokuwa kinyume, usione kuwa huo ndio mwisho wake. Mruhusu afanye vibaya kama
fursa ya kujifunza.
Ajifunze kwa nini amefeli
Mtoto
asipojifunza kwa nini hakufanya vizuri hawezi kubadilika. Lazima kuhakikisha
anatambua wapi alipojikwaa apate somo kupitia kushindwa kwake. Huenda ni kukosa
uzingativu darasani, kushindwa kushirikiana na wenzake darasani na hata
kushindwa kutumia muda wake vizuri. Msaidie kujitathimini.
Kwa
kawaida, ni vigumu mtoto kujitathimini bila kuwabebesha wengine wajibu wake.
Hufanya hivyo kama jitihada za kujinasua na makosa yake. Anaweza kutafuta
kuwabebesha lawama watu wengine kama walimu, wanafunzi wenzake na hata wewe
mzazi. Usiruhusu afanikiwe kujinasua.
Ingawa
anaweza kutoa sababu zinazoshawishi kuhalalisha matokeo mabaya, kukubaliana na
visingizio vyake ni kujenga mazoea yasiyofaa. Ni vyema ajenge uelewa kuwa
hakuna mtu mwingine anayewajibika na mafanikio yake kielimu isipokuwa yeye.
Awajibikie
matokeo yake mabaya
Kumpenda
mtoto si kumdekeza na kumlinda hata pale anapokosea. Unapomdekeza unamjengea
mazoea yasiyofaa ya kuwanyooshea vidole watu wengine kwa makosa yake mwenyewe. Hii,
kwa hakika si tabia ya kufumbia macho.
Kumpenda
mtoto ni pamoja na kufanya ajisikie hatia na kujutia makosa yake. Anaposhindwa
mtihani, aelewe kuwa kufauli ni matokeo ya matendo yake mwenyewe. Kwa mantiki
hiyo, aelewe kuwa hana mtu mwingine wa kuwajibika isipokuwa yeye mwenyewe.
Ikiwa
matokeo yake mabaya yanaambatana na adhabu, hakuna sababu ya kumtetea. Inawezekana
kweli mtoto amefanya vibaya kwa sababu ya mfumo wa elimu, aina ya walimu
wanaomfundisha, mazingira mabaya ya shule na hata tabia za wanafunzi wenzake.
Hata
hivyo, ni muhimu kumfanya mtoto awajibike kwa sehemu yake. Kama shule inamtaka
arudi mapema kabla ya wenzake kumaliza likizo, huko ndiko kuwajibika. Kama
matokeo yake yanamlazimisha kuhama shule, atajifunza vizuri zaidi ikiwa atahama.
Kumtetea mtoto aliyepoteza sifa za kuendelea kusoma mahali alikoshindwa
kuonesha bidii ni kumfundisha tabia ya kuhalalisha makosa. Hatajifunza.
Atengeneze
mikakati ya kujirekebisha
Kuelewa
makosa yake na kuyawajibikia hakuwezi kuwa na faida ikiwa mtoto hataweza kujua
kipi anapaswa kufanya ili kubadilika. Mbinu chanya za kutatua tatizo
aliloligundua zinahitajika.
Hatua
ya kwanza kumwezesha kupata mbinu zinazomfaa, ni kumsaidia kutathimini ari na
motisha yake kimasomo. Mpe fursa ya kutafakari namna anavyojituma na pia namna
anavyoelewa uhusiano wa juhudi zake na mafanikio yake kimasomo.
Tathmini
nzuri itamsaidia kuweka mikakati madhubuti ya kujinusuru na makosa
yaliyochangia kufanya vibaya. Kama anahitaji kutunza muda awapo shuleni, achukue
hatua ya kupanga na kuheshimu ratiba.
Kama
hana ari ya kutosha kujifunza, msaidie kumpa motisha. Motisha ya kwanza ni
kumhakikishia kwa dhati kuwa bado unayo imani na uwezo wake. Kisha mpe mtoto
msaada na ushirikiano anaouhitaji ili kupata mafanikio unayoyatarajia kwake kitaaluma.
Fuatilia Jarida la Maarifa ndani ya Gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa makala kama hizi.
Fuatilia Jarida la Maarifa ndani ya Gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa makala kama hizi.
Maoni
Chapisha Maoni