Kwa Nini Maazimio Mengi ya Mwisho wa Mwaka Huwa Hayatekelezeki?
Kila
mwaka mpya unapoanza, ni kawaida kwa watu wengi kuweka maazimio fulani ya
kutekeleza. Wapo ambao huazimia kubadili tabia wasizozipenda. Wengine huazimia kuanzisha
mwenendo mpya wa maisha wanayoyatamani. Wengine hufikiria kutekeleza malengo
fulani ya kijamii na kiuchumi yatakayobadili maisha yao kwa mwaka unaoanza.
Ingawa
ukweli ni kuwa mwaka unapoanza kinachobadilika huwa ni tarehe tu, watu huwa na
imani kuwa wanaingia kwenye zama za maisha mapya. Imani hiyo huambatana na
jitihada za kujaribu kubadili maisha yao yaendane na zama hizo mpya. Wanasema,
‘mwaka mpya na mambo mapya!’
Tafiti
zinasema asilimia kati ya 8 na 10 tu ya watu wanaoweka malengo ya mwaka mpya,
ndio hutekeleza malengo hayo kufikia mwisho wa mwaka. Maana yake asilimia kati
ya 90 na 92 huwa wanaweka maazimio yasiyotekelezeka.
Katika
makala haya, tunajadili kwa nini maazimio mengi mazuri hufa kabla hayajaanza kutekelezwa.
Msisimko wa mwaka mpya
Kuingia
mwaka mpya ni jambo la kusisimua. Watu wengi hutafakari namna watu wengi
walivyoshindwa kuuona mwaka mpya. Kwamba 'wamejaaliwa' huwafanya
wajione kama watu wenye wajibu fulani wa kubadili mtindo wao wa maisha yaendane na mwaka wanaouanza.
Msisimko
huu, kwa hakika, huwa ndio msingi wa maazimio mengi yanayowekwa wakati wa
kuingia mwaka mpya. Kwa
bahati mbaya maazimio yanayoongozwa na msisimko wa namna hii hayawezi kuleta
matokeo yoyote ya maana. Sababu ni kwamba msisimko wa kuingia mwaka mpya unapoyeyuka,
basi na maamizo nayo huyeyuka. Maisha yanarudi kule yalikokuwa.
Malengo yasiyopimika
Sambamba
na kuweka maazimio katika hali ya msisimko, watu wengi huweka malengo
yasiyopimika. Haya ni yale malengo makubwa yanayopendeza masikioni lakini hayana
namna ya kutathmini utekelezaji wake.
Kwa
mfano, mtu anaweza kuwa na malengo ya kufanikiwa kwa mwaka unaoanza. Lakini
unapomwuuliza ana maana gani anapokusudia kufanikiwa, anakwambia basi tu
anataka kufanikiwa.
Lengo
hili, la kufanikiwa, ni pana mno kwa sababu utekelezaji wake hauwezi kupimwa.
Na kwa sababu ni vigumu kupima utekelezaji wake, ni rahisi lengo hili kupoteza uzito
wake siku chache baada ya kuazimiwa.
Kutokujua uliko mzizi wa
mabadiliko
Utekelezaji
wa malengo mengi ni matokeo ya mabadiliko ya tabia. Huwezi kutekeleza lengo la
kuweka akiba kila mwezi kama huwezi kubadili tabia ya kufanya matumizi
yasiyopangiliwa. Kwa mfano inawezekana huwezi kuweka akiba kwa sababu unakuwa mwepesi wa kuwapa watu fedha usizokuwa nazo. Unatoa usichonacho kwa sababu huna uwezo wa kusema hapana.
Kadhalika, huenda unaishiwa kwa sababu una tabia ya kununua vitu usivyovihitaji. Hata unapokuwa huna fedha unatafuta furaha kwa kununua vitu fulani. Usipoweza kubadili tabia hizi, huwezi kutekeleza malengo unayojiwekea.
Vile
vile, watu wengi huwa hawafikirii namna mambo makubwa yanavyochangiwa na mambo
madogo madogo. Na kwa sababu hawaoni mchango wa mambo madogo katika mambo
makubwa, ni rahisi kupuuza mambo hayo ambayo kimsingi ndiyo yanayosaidia kuleta
mabadiliko makubwa.
Kwa
mfano, mtu anayetaka kuacha pombe, anafikiri kile anachotaka kukipata, yaani kuacha
kuacha pombe lakini hafikirii mchango wa mazingira yanayoambatana na unywaji wa
pombe. Mazingira haya, kwa mfano, ni pamoja na kukaa katika maeneo yanayohamasisha
unywaji wa pombe na hata kuambatana na wanywaji wa pombe.
Unapoishi na walevi ni vigumu kubadili tabia unayotaka kuiacha. Kuachana na tabia waliyonayo watu wako wa karibu ni sawa na kuwapinga. Si watu wengi wanaweza kukubali kuwapinga watu wao wa karibu.
Unapoishi na walevi ni vigumu kubadili tabia unayotaka kuiacha. Kuachana na tabia waliyonayo watu wako wa karibu ni sawa na kuwapinga. Si watu wengi wanaweza kukubali kuwapinga watu wao wa karibu.
Kuogopa hatia ya kushindwa
Watu
wengi hawapendi kujisikia hatia. Wanapoona hawawezi kufanya kitu fulani
wanatafuta namna ya kukwepa hatia yao. Mara nyingi, hatia hukwepwa kwa
kuwabebesha lawama watu wengine. Hii ni hulka ya mwanadamu.
Ili
uweze kutimia malengo yako, unahitaji kuwa na kifua cha kuvumilia hatia. Katika safari ya kutimiza malengo, unaweza kufika wakati kile unachokiishi kinaonekana kwenda kinyume kabisa na kile
unachokitamani. Usiruhusu kukata tamaa na kuamua kuachana na malengo yako. Unahitaji
kuendelea kusimamia kile unachokiamini hata kama uhalisia unakuwa kinyume.
Kwa
mfano, badala ya kuamua kuendelea kunywa pombe kwa sababu tu umerudia tabia hiyo baada
ya jaribio la kuacha kwa juma moja, usikate tamaa. Kubali kujisikia hatia, na azimia kuendelea
kujitahidi kujizuia.
Kama
ulilenga kuanza mazoezi kila siku asubuhi na unajikuta umeshindwa kufanya hivyo
kwa siku kadhaa, hatia isikufanye uachane na mpango wako. Kuwa na kifua cha
kuvumilia hatia na amua ksonga mbele na mpango wako. Hiyo inaitwa nguvu ya
maamuzi.
Kukata tamaa, mara nyingi, hutokana na imani kuwa unapolenga kutekeleza jambo, basi lazima ulitimize kwa asilimia mia. Hakuna malengo hufikiwa kwa asilimia hizo. Kubali
kufanikiwa hata kwa asilimia 10 na uendelee mbele. Kuwa na maamuzi yanayoweza kuvumilia kushindwa. Usikate tamaa.
Inaendelea
Fuatilia Gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa Makala kama
hizi.
Maoni
Chapisha Maoni