Mbinu za Kutengeneza Mtandao wa Ajira

Changamoto kubwa inayowakabili vijana wanaotafuta kazi ni namna ya kupata taarifa sahihi zitakazowasaidia kupata kazi. Ingawa vipo vyanzo vingi vya kupata taarifa hizo, watafuta kazi wengi hutegemea matangazo rasmi ya ajira pekee kupitia vyombo vya habari.
Hata hivyo, tafiti za kazi na ajira zinaonyesha kuwa nafasi nyingi za kazi hasa katika sekta binafsi hazitangazwi hadharani. Waajiri wana tabia ya kutafuta mtu  anayeaminika kupitia vyanzo vinavyoaminika. Tafsiri yake ni kuwa kijana anayetegemea kupata taarifa za kazi kupitia matangazo rasmi, anapitwa na taarifa nyingi muhimu.
Ili kukabiliana na changamoto hii, vijana wanahitaji kujifunza namna ya kutengeneza na kudumisha mitandao ya ajira. Mtandao wa ajira, kimsingi, ni mawasiliano ya karibu anayokuwa nayo mtafuta kazi na watu wa kada mbalimbali, kwa lengo la kupata taarifa za ajiri pale zinazopatikana.
Katika makala haya, utajifunza mbinu nne za kutengeneza mtandao wa kiajira utakaokusaidia kupata taarifa za kazi na ajira.


Imarisha uanachama katika makundi uliyomo

Kila mmoja wetu anayo makundi fulani ya kijamii anayojitambulisha nayo. Kuna sehemu za ibada, vyama vya kijamii na kitaaluma, watu uliowahi kusoma nao kwa ngazi mbalimbali za kielimu na makundi mengineyo. Makundi hayo ni hatua ya kwanza rahisi ya kutengeneza mtandao imara wa kiajira.

Unapokuwa sehemu ya kundi ulilonalo, kwa mfano, ukawa mwanachama mwaminifu, unajipa nafasi muhimu ya kuaminiwa bila gharama yoyote. Watu wanapokufahamu na kukuamini unakuwa katika nafasi nzuri ya kujenga uhusiano wa kudumu na watu wanaoweza kukusaidia.

Ili uweze kuaminiwa na watu, una wajibu wa kuwa sehemu kamili ya kundi husika kwa kuonesha bidii na juhudi. Kama ni kanisani, jitoe kwa moyo, fanya bidii. Watu watauona uwezo wako na itakuwa rahisi kukusaidia watakapogundua unahitaji kazi.

Hudhuria mikutano na makongamano

Vijana wengi kutegemea taarifa wanazozipata kwa watu waliosoma nao, majirani, ndugu na marafiki. Hata hivyo, ikiwa watu hawa unaofahamiana nao wanafanana kwa aina ya mitazamo na uelewa, unaweza kujikuta ukijinyima fursa ya kupata taarifa muhimu wasionazo.

Kwa sababu hiyo, unahitaji kukutana na watu muhimu usiowafahamu kwa sasa ili kuongeza mtaji wako wa watu usionao hivi sasa. Nenda kwenye mikutano, warsha na semina zinazoweza kukukutanisha na watu muhimu na hata waajiri wanaoweza kukuona.

Kama unatafuta kazi ya uhasibu, kwa mfano, lenga kukutana na watu wa namna hiyo kwenye mikutano inayokutanisha wahasibu na wafanyabiashara. Kufanya hivyo kunaweza kukugharimu muda na fedha kidogo lakini utaongeza mtaji wa watu unaofahamiana nao.

Jua namna ya kujitambulisha

Unapokuwa kwenye makundi ya watu, hakikisha umejiandaa. Ikiwa una kadi ya wasifu wako (business card) iweke karibu kisha tambua aina ya watu unaolenga kujenga mtandao nao. Nyenzo unayoihitaji ni ujasiri wa kuwafuata na kuanzisha mazungumzo pale unapoona wanaweza kukusikiliza.

Ni muhimu kuelewa mazingira ambayo unaweza kusikilizwa.  Huwezi, kwa mfano, ukamfuata mtu ambaye tayari anaongea na mtu mwingine na ukategemea azingatie mazungumzo yenu. Hakikisha unayetaka kuongea naye yuko katika nafasi ya kukusikiliza.

Kadhalika, fahamu aina ya mazungumzo yanayoweza kumvutia mtu unayetaka kujenga naye mawasiliano. Kwa kawaida, watu muhimu wanapenda kukutana na watu wenye mawazo mapana, watu wenye uelewa wa changamoto fulani zinazoikabili jamii lakini pia wenye majibu ya changamoto hizo. Unapokuwa mtu asiye na malengo yanayoeleweka, ni vigumu kumfanya mtu akuchukulie kwa uzito. Jitambulishe kwa uwezo ulionao.

Tumia dakika moja za mwanzo katika mazungumzo ya awali kujipambanua wewe ni nani na unalenga kufanya nini katika jamii. Onekana ni mtu mwenye ndoto zinazoeleweka na kuelezeka ndani ya dakika moja.

Ni kuzingatia kuwa unapoongea na mtu muhimu, unahitaji kumpa nafasi azungumze kuliko unavyozungumza wewe. Kufanya hivyo kutakupa fursa ya kumwelewa anajishughulisha na mambo gani ili ujue unavyoweza kujitambulisha. Ukiweza kuunganisha shughuli anazozifanya na ujuzi wako, ni rahisi mtu huyo kuona thamani yako kwake.

Endeleza mawasiliano kukuza uhusiano

Baada ya kupata usikivu wa mtu muhimu unayemhitaji, unao wajibu wa kufanya mawasiliano muda mfupi baada ya kuachana naye. Usipofanya mawasiliano naye, ni rahisi kusahaulika. Kama ulichukua mawasiliano, mtafute.

Hata hivyo, unapofanya mawasiliano chukua tahadharani usimchoshe. Kwa kawaida, watu wanapenda uhusiano wa nipe nikupe. Usijenge taswira ya mtu anayetarajia kuliko anavyoweza kuwa wa msaada.

Onekana ni mtu aliyekomaa kifikra na anayeaminika. Badala ya kutaka kusikilizwa muda wote, tafuta namna unavyoweza kusaidia kwa kutumia ujuzi ulionao. Ukifanya hivyo na ukapunguza utegemezi usio wa lazima, watu watakuamini na watasukumwa kukupa msaada pale utakapouhitaji.

Wito kwa waajiri na taasisi za elimu

Kazi ya kutengeneza mtandao wa kiajira inapoachwa mikononi mwa kijana mwenyewe, ufanisi wake unakuwa na changamoto. Ipo haja ya kuwa na mfumo rasmi unaomwandaa kijana anayeingia kwenye soko la ajira kukutana na watu anaowahitaji.

Taasisi za elimu, kwa mfano, zinahitaji kuratibu vizuri zaidi mafunzo kwa vitendo yamwezeshe kijana kujenga mahusiano endelevu ya kikazi. Kadhalika, kuna haja ya kuwa na vitengo maalum vya unasihi katika taasisi za elimu kwa minajili ya kuwaunganisha vijana na mazingira ya kazi.

Waajiri nao, kwa upande mwingine, wasitegemee taasisi za elimu pekee katika kuwakuza vijana kiujuzi. Kama wanufaika wa ujuzi huo, waone wajibu walionao katika kuwainua kiujuzi vijana wanapojiandaa kuingia katika ajira.

Vijana wanahitaji watu wa kuwalea na kuwakuza. Waajiri wawape nafasi za kujitolea, mafunzo kwa vitendo na hata kuwakaribisha kwenye warsa na semina zinazoweza kuchangia kupanua wigo wa mtandao wa ajira kwa vijana.

Makala haya yamechangiwa pia na Albert William, Mratibu wa Ukuuzaji wa Ujuzi, ILO -Dar es salaam na Prosper Mwakitalima wa Brand Exponentials.

Maoni

  1. albert william18/12/16 7:22 AM

    Ahsante sana bwaya kwa makala haya..muhimu pia kwa waajiri kuwa karibu sana na taasisi za elimu..kufadhili miradi ya kiutafiti ili kunufaika na mawazo mapya waliyonayo vijana

    JibuFuta
  2. Kweli kabisa Albert. Unahitajika ushirikiano baina ya wadau mbalimbali kuwasaidia vijana :)

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging