Namna ya Kutambua na Kukuza Kipaji cha Mtoto -2
Katika makala yaliyopita tuliona mambo yanayoweza
kujenga kipaji cha mtu na uhusiano wa kipaji na mafanikio katika maisha.
Kufurahia kile unachokifanya kazini au katika shughuli nyinginezo kunategemeana
na namna unavyotumia vipawa ulivyozaliwa navyo.
Kadhalika, tulibainisha umuhimu wa wazazi kufanya
kazi ya kuwasaidia watoto kubaini vipaji vyao mapema. Kufanya hivyo ni kujaza
pengo la mitaala yetu ambayo kimsingi haifanyi mengi katika kuibua na kukuza
vipaji vya watoto.
Katika makala haya tunaangalia
mbinu unazoweza kutumia kama mzazi kubaini na kukuza kipaji cha mwanao.
Kuwa karibu na mwanao
Huwezi kumfahamu mtoto vizuri kama huna muda naye.
Unapotumia muda wa kutosha na mtoto, utaweza kufahamu mambo yake mengi.
Uhusiano wa karibu utakupa nafasi ya kufanya mazungumzo,
kucheza na hata kuona mambo ya msingi anayoyapa uzito. Huwezi hufahamu kitu
kinachomvutia mwanao bila kujenga ukaribu naye.
Unapojenga ukaribu na mtoto, ni vyema kumpa nafasi ya kusema
na kufanya yale anayoyapenda bila hofu ya kukosolewa. Mtoto anapokosolewa
anajenga sura anayojua ndiyo inayotarajiwa na mzazi. Ni vigumu kumfahamu mtoto
wa namna hii anayevaa sura isiyo yake.
Jenga mazingira rafiki kujifunza
Mazingira yana mchango mkubwa
katika kukuza vipaji. Hakikisha mtoto anapata fursa ya kujaribu uwezo wa namna
tofauti. Kupitia kujaribu hiki na kile, atapata kile kinachomtambulisha.
Katika kujenga mazingira mpe mtoto
vifaa anavyovihitaji. Tangu akiwa mdogo wekeza katika vifaa vya kukuza uwezo
wowote alionao. Mpe mpira, rangi, vifaa vya kucheza muziki, vitabu na vifaa
kama hivyo. Unapofanya hivyo bila kupendelea uwezo fulani, ni rahisi mtoto kuonesha
wapi uwezo wake unaelemea zaidi.
Changamoto hapa ni mzazi kujaribu
kuweka mazingira yanayosadifu kile anachokipenda yeye. Kwa mfano, mzazi
anayependa muziki, anaweka mazingira yanayohamasisha muziki pekee na sio uwezo
mwingine. Kufanya hivi hakuwezi kumsaidia mtoto kugundua kipaji chake. Kutamshawishi
mtoto kuwa kile asicho.
Ikiwa unatamani kugundua kipaji
cha mwanao, yafanye mazingira yampe fursa ya kutumia uwezo wa aina mbalimbali. Weka
mazingira yanayohimiza maeneo yote kama vile michezo, sayansi, sanaa, lugha,
uhusiano, ufundi na mengineyo.
Mwoneshe mifano ya vipaji tofauti
Mtoto ana tabia ya kuiga mambo
anayoyaona katika mazingira yake. Anaweza kuvutiwa kuwa daktari kwa sababu hao
ndio watu anawaowasikia katika mazingira yake. Lakini kama ungeweza
kumfahamisha vipawa mbalimbali angegundua eneo jingine tofauti.
Ili kuhakikisha kuwa mtoto haishii
kuiga yale anayoyaona katika mazingira yake, unahitaji kupanua uelewa wake kwa
kumpa mifano halisi ya vipaji ambavyo pengine havifahamu. Tafuta watu maarufu
waliofanikiwa katika maeneo yao na mfahamishe mwanao awaelewe.
Kwa mfano, unaweza kumsimulia
mtoto habari za wanasayansi maarufu na kazi walizozifanya. Mtafutie filamu na
vitabu vinavyoelezea namna wanasayansi hao wanavyokumbukwa kwa mafanikio yao. Mpeleke
kwenye maeneo halisi anakoweza kushuhudia namna wanasayansi hao wanavyofanya
kazi zao.
Fanya hivyo kwa fani mbalimbali.
Manesi. Waandishi. Wanaharakati. Wanasheria. Wanamichezo. Wahandisi. Wafanya
biashara. Walimu. Wahasibu. Wahifadhi mazingira. Wanajeshi. Unapomfahamisha aina mbalimbali za vipaji
unalenga kupima hamasa ya mtoto kujitambulisha na watu wanaomgusa zaidi.
Kwa kuwa zoezi la kumfahamisha
mtoto vipaji hivi halifanyiki kwa siku moja, hatua kwa hatua, mtoto anaweza
kuonesha mapenzi na watu wa aina fulani. Mtoto anaweza kuanza kuvutiwa na
vipaji fulani zaidi kuliko vingine. Huo ndio mwanzo wa kubaini kipaji cha
mtoto.
Tambua
uwezo wake
Baada ya kumpa mtoto fursa ya kuchunguza mazingira yake, ni
dhahiri ataanza kuonesha uwezo fulani mahususi. Katika saikolojia uwezo huu mahususi
unaweza kuganywa katika makundi kadhaa.
Kundi la kwanza ni watoto wanaopenda vitu badala ya watu.
Hawa wanatumia muda mrefu kushughulika na vifaa, wanafurahia kuharibu na
kutengeneza. Pia wanapenda ni wakimya, wanapenda kufuata utaratibu
usiobadilika. Vipaji vyao viko katika ufundi na kufanya kazi na vitu.
Lakini wapo watoto wasio na muda na watu lakini hawana muda
na vitu pia. Hawa muda mwingi wanautumia wakiwa pekee yao. Hawana mazungumzo
mengi. Hawa wanaweza kuwa na vipaji vya kuchambua mambo, kudadisi nadharia na
utundu wa akili. Wanauliza maswali yanayofikirisha, ni wachunguzi, hawaamini
mambo kirahisi. Hawa eneo lao ni sayansi.
Vile vile, wapo wenye watoto mapenzi na sanaa. Hawa ni wabunifu,
wanajua kuongea kitu kikaeleweka kwa maneno machache. Wanapenda uhuru wa kuumba
mawazo ambayo wakati mwingine hayapo na ni wabunifu. Kipaji chao ni utunzi,
uimbaji, utamaduni, uchoraji na ushairi.
Kundi la nne ni wapenda watu. Ni marafiki wazuri, wanapenda
kufanya mambo yao kwa ushirikiano na wengine lakini hawana kawaida ya
kuwatawala wengine. Kuwa pekee yao ni kama adhabu lakini wanapokuwa na wenzao
hawajifikirii wenyewe. Wanaridhika kuwasaidia wengine kupata wanachokitaka. Kipaji
chao ni kuwasaidia wengine.
Pia lipo kundi la watoto wanaopenda watu lakini wanakuwa
rahisi kuonekana. Wanapokuwa na wenzao ni rahisi kusikilizwa kwa sababu ni
waongeaji, wanajiamini kupindukia, wanapenda kusikika na kuelekeza. Hawa kipaji
chao kiko kwenye uongozi, usimamizi na siasa.
Kadhalika, wapo
watoto wanaopenda michezo. Ingawa ni kweli katika umri fulani michezo ni hitaji
la kila mtoto, watoto wa kundi hili wana kawaida ya kuonesha uwezo usio wa
kawaida katika ujuzi wa michezo inayohitaji uwezo maalum wa matumizi ya viungo
vya mwili.
Tafuta
ushauri wa kitaalam
Ni vizuri kuelewa kuwa tabia, mitazamo na utashi wa watoto
hubadilika kadri wanavyokua. Kama tulivyosema, mtoto anaweza kuonesha kuvutiwa
na watu fulani kwa sababu za juu juu zisizodumu.
Ni vyema kutafuta msaada wa wataalam wanaoweza kumchunguza
mtoto kitaalam kubaini kipaji chake halisi. Katika nchi yetu, msaada huu
unaweza kutolewa na watu waliobobea kwenye masuala ya saikolojia na unasihi.
Maoni
Chapisha Maoni