Haki ni nini?

SIKU hizi haipiti dakika hujasikia haki zikidaiwa mahali. Kuna haki za watoto. Haki za akina mama. Haki za wafanyakazi wa ndani(Koero analizungumzia hili vizuri). Haki za masikini. Haki za vyangudoa. Haki za maalbino. Haki za wasomaji. Haki za mafisadi (hata fisadi naye ana haki ya kusikilizwa/natural justice). Haki. Haki. Haki. Orodha ni ndefu.

Jambo moja. Inapodaiwa haki, ikumbukwe kuwa upo upande ambao utalazimika kunyang'anywa haki zake ili haki ile ya kwanza inayodaiwa ipatikane. Kwa maneno mengine, unajikuta ili kutetea haki, inabidi unyang'anye haki. Na upande huu wa pili unaolazimika kupoteza haki ili kufidia haki inayodaiwa, nao ukiamka, inabidi zoezi liwe mduara. Yaani poteza haki, kuleta haki.

Kwa mfano. Mtoto anapodai haki, maana yake inamlazimu mzazi kupoteza haki zake ili kumpatia mwanae haki. Kwa maneno mengine, haki ya mtoto inakuwa utumwa kwa mzazi. Unapoteza haki kuleta haki.

Mwanafunzi wa kike anapodai haki ya kusoma kwa upendeleo, inabidi mamlaka zinazohusika kubinya haki za wavulana ili haki hiyo inayodaiwa itimie. Hapa, maana yake unapoteza haki ili kuleta haki.

Sasa hapa ndiko liliko swali langu: Haki ni nini?

Na haki hizi ni kwa ajili ya nani, jamii, kikundi cha watu fulani wanaodai rehema ama ni mtu binafsi?

Inakuwaje kama tukiamua kuzivunja haki hizi? Je, haki ni kutii sheria na taratibu zilizopo kwa lengo tu la kuepuka adhabu?

Je, haki ni kile kinachoweza kufanywa na watu wengine ili kutupa faida hata kama kufanya hivyo kunawaumiza wao? (Je, wao hawana haki?)

Je, haki ni kuwa mtu mzuri anayekubalika kwenye jamii? (Vipi kama nikiamua kutafuta haki zangu kwa namna ninayoijua mimi hata kama kwa kufanya hivyo ntaonekana kituko?)

Je, haki ni kutimiza matakwa ya sheria zilizopo hata kama zinaingilia uhuru wangu?

Je, haki ni kutetea matakwa ya wengine, hata kama kufanya hivyo kunakunyima vitu fulani fulani
Je, haki ni matakwa ya kibinafsi yasilazimika kushahibiana na sheria zinazoonekna ni halali katika jamii?

Kumbuka palipo na haki kuna haramu. Pasipo tafsiri nzuri ya haki, tunajikuta kila tunalolifanya ni haramu. Mzunguko wa madai usioisha. Kupoteza haki. Kupata haki. Kupoteza tena. Kuzipata tena. Mwishowe, kila kitu kinakuwa haramu.

Maoni

 1. Swali zuri kwa walimwengu. Haki ni kitu kilicho kwenye sheria...vitabuni tu maanake ukiangalia dunia ya leo, ni unyanyasaji, chuki, uharamia nk. pembe zote.
  Hata haki ya kusema huru haupo na uhuru wake...naachia hapo.

  JibuFuta
 2. Kwa matazamo wangu jamii yetu imeshindwa kuwajibika ndiyo ikaja suala la kusema tunadai haki zetu

  JibuFuta
 3. Chama tawala ndo chanzo cha kufanya watu wadai kile wanachoamini kuwa kimekataliwa wakati wanastahili kukupata.hiyo ndo tafsiri ya haki kwa hapa Tanzania,ila maana halisi ni uhuru wa kufanya kile unachoamini na kukipata kile unachohitaji au kupata kile unachokitaka kwa muda uliojip[nagia

  JibuFuta
 4. Ukipewa haki na unakajua kuwa umepewa haki, kuna haki unazikosa kwa kujua kuwa umependelewa.

  Mfano akina mama wanaong'ang'ania kukalia viti vya bungeni kwa upendeleo. Haki hiyo wanayodhani ni yao kwa kulazimisha, inawafanya wakose haki mbele ya jamii. Kuna haki wanazikosa kwa sababu tu waligawiwa haki.

  Haki usiidai. Iache ije yenyewe.

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?