Machapisho

Inaonyesha machapisho kuanzia 2009

Je, tunafikiri kwa kutumia lugha?

Kuna changamoto zimejitokeza kwenye ule mjadala wa tasnifu ya msomi wetu ambayo kwa maoni yaliyotolewa huenda ingekuwa bora kama ingekuwa katika kiswahili. Changamoto kubwa zaidi ni ile iliyoletwa na msomaji Godwin Habib Meghji akihoji ikiwa mwanadamu hufikiri kwa kutumia lugha. Hapa anasema: "Mimi sina uhakika kama binadamu anafikiria kwa kutumia lugha fulani. Viziwi na bubu pia hufikiri". Hii ni changamoto nyingine. Una maoni gani katika hili? Je, tunawezaje kufikiri? Fikra zinauhusiano wowote na lugha? Je, bubu ama kiziwi hana lugha kwa sababu tu hawezi kutamka ama kusikia?

Tembelea Website mpya

Pole na shuguli za kutupasha habari mbali mbali zinazotokea ndani na nje ya Tanzania. Naomba nafasi katika blog yako ili niwajulishe ndugu zangu watanzania kwamba nimetengeneza website www.rusumo.com ambapo wataweza kusikiliza nyimbo mbali mbali za Tanzania kama vile taarab,segere,dance,bongo flava,gospel na nyimbo za kigeni kama vile raggae,za kihindi,pop na nyengine nyingi tu. Pia kuna dictionary ya kisasa kabisa ambayo ina lugha zote za Ulaya na baadhi ya lugha za Asia,katika dictionary hii baada ya kupata tafsiri ya neno pia unaweza kuona picha za neno hilo kwa kubofya upande wa pili wa Ukurasa. Kadhalika wadau wataweza kuona hali ya hewa na wakati wa sehem mbali mbali za dunia. Karibuni sana wadau, ni mimi MSAFIRI ISMAIL RUSUMO. www.rusumo.com

Soma 'tasnifu' ya msomi wa Chuo Kikuu

Mjadala wa lugha gani itumike katika mfumo wetu wa elimu, ni suala la kutia aibu kuliko hata aibu yenyewe. Inadhalilisha sana unaposikia watu wazima hajui tutumie lugha gani kufundishia. Eti tunabishana kipi bora Kiswahili ama Kiingereza, kweli? Fedheha hii inatokana na ukweli kwamba lugha ya kiingereza inayolazimishiwa hivi sasa ni miongoni mwa maajabu saba ya dunia kwa wanafunzi wengi. Leo nimekuja na ushahidi wa karibu kabisa unaonyesha sura halisi ya tatizo. Nimepata bahati ya kupata karabrasha la 'utafiti' uliofanywa na mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu aliyekuwa anajiandaa kuitetea Digrii yake kwa kuandika 'tasnifu'. Baada ya kusoma vipande vichache vya karabrasha hili naomba uamue mwenyewe kuwa Digrii iliyomwezesha kuandika andiko hili ni halali ama ni feki. Halafu fikiri nani wa kumlaumu: yeye mwenyewe asiyejua lugha ambayo ni ya wakoloni na haitumii kuwasiliana na jamii yake au ni serikali yake isiyoelewa makosa ya kugenisha hadi lugha? Inawezekana kabisa ku...

Mkutano wa Copenhagen: Ugaidi wa kimaendeleo

Picha
Hivi sasa dunia yetu inapitia kipindi kigumu kuliko wakati mwingine wowote. Joto limeongezeka sana. Barafu inayeyuka. Kina cha maji kinaongezeka kwa kasi na kwa kweli ndani ya kipindi kifupi, baadhi ya visiwa vitafurikwa na maji kikiwamo kile cha Zanzibar. Majanga haya yote yamesababishwa na akili ya mwanadamu mwenye fikra potofu ya kile kinachoitwa MAENDELEO. Mwanadamu wa sasa (wa kileo) ndiye hasa chanzo cha dhahama yote hii ambayo kwa sasa imefanyiwa Mkutano maalumu kule Copenhagen ambao ninaamini utaishia wale jamaa kupiga picha ya pamoja na kuja na matamko ya kisiasa then maisha yataendelea kama kawaida. Bonyeza hapa kujua kinachoendelea kwenye mkutano huo na tayari mashindano ya matamko yameanza. Ningependa tufanye tathmini ndogo ya namna ambavyo akili ya mwanadamu wa leo anayejiona kuwa kaendelea kuliko wengine wote waliopita. Moja. Mwanadamu wa leo ameshindwa kabisa kutatua tatizo la utumiaji (ukwapuaji) wa vyanzo vya asili. Akikwapua vikaisha, anahamia kwingine. Aki...

Mwezi Desemba na suluba zake

HIVI unajua kuwa mwezi kama huu, mwakani, serikali iliyopo madarakani itakuwa imeenda zake? Hivi hivi tunashuhudia serikali hii ikimaliza muda wake. Namna gani tunalishuhudia hili inategemeana na asomaye mistari hii. Nilisahau hata nilichotaka kusema. Ni bukheri wa afya nasubiria mwisho wa mwaka. Kama kuna mwezi wenye sikukuu kibao ndio huu. Halafu naona kama siku kuu zote hazina mantiki kabisa. Kuanzia hii ya kesho kutwa (ya kusherehekea uhuru usiokuwepo) mpaka zile nyingine za kuadhimisha siku za kiroho kwa ubwabwa na mavazi. Uzuri wa mwezi huu tuna uhakika wa siku kadhaa ambazo tutabaki tumelala nyumbani. Kisa? Hakutakuwa na kazi kwa hivyo ofisi zitafungwa na kama kawaida tutaendeleza kwa kasi umasikini wetu ambao wapo wenzetu wanautumia kuendesha harakati za kuubakiza ili dili lisife. Unakumbuka wakati wa mzee Mwinyi, siku kuu ikiangukia siku za wikendi, basi siku hiyo inahamishiwa Jumatatu ili watu wale raha na kusahau kuhudumia wananchi. Ayaa... nimeenda nje ya pointi. Ni...

Hongera Mzee wa Mshitu

Picha
Mwanablogu Yahya Chaharani (anayesikiliza simu) amepata Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino, Mwanza. Hongera sana kwa kupiga hatua!Hapo ni katika mahafali yaliyofanyika juma lililopita. Picha kutoka blogu ya Mzee wa mshitu

Fikiri zaidi ya dini yako

Picha
Kitabu hiki nilikipata miezi michache iliyopita. Nimekisoma kwa muda mrefu na kujipatia mwanga adhimu kuhusu dini aina aina. Hapa nilipiga baadhi ya kurasa zake, kukuonesha wewe unayetamani kujua zaidi ya dini yako. Ujue kuna watu hawafikiri kabisa nje ya kiberiti cha dini zao. Kitabu hiki nilikipewa na mdogo wangu Fortunatus kama mchango wake kwenye mijadala ya dini ambayo kimsingi sikupata muda wa kuiendeleza. Upatikanaji wake sina hakika nao lakini nipatapo fursa nitawamegea kidogo kidogo wasomaji wangu.

Public victory: Tatizo letu baya

Picha
Ninaendelea kukisoma kitabu cha Stephen Covey. Nimepata changamoto ambazo idadi yake siijui. Kimsingi anachokisema mwandishi ni umuhimu wa kuanza kujitengeneza wewe mwenyewe kiasi cha kujihakikishia ushindi binafsi (private victory)ndipo ufikiri zaidi ya hapo. Tatizo la watu wengi hufanya makosa. Huanza na kutafuta ushindi wa hadharani (kukubalika, kuhusiana na wengine kwa bidii) kabla ya ushindi binafsi. Huko, kwa mujibu wa Covey ni kupoteza muda!

Ni kukosa muda ama kukosa kipaumbele?

Kimya cha blogu hii hakikutarajiwa ila huenda ni matokeo ya uzembe. Ni wazi bado sijaweza kushika mbili bila kuponyokwa na kimoja. Na nasikitika sana kwamba kinachoniponyoka mara kwa mara ni blogu. Nimekuwa nikifikiri inakuwaje huwa sikosi muda wa kula (na kwa kweli napenda kula) hata kama nimebanwa na vitu kedekede? Kwa nini 'sikosagi' muda wa kuzungumza na marafiki zangu kwa kusingizio cha kubanwa? Hitimisho likawa, huenda ni suala la kipaumbele tu na tabia ya kutokujitimizia ahadi ninazojiahidi. Kwamba inakuwa vyepesi kutimiza ahadi ya nje (na watu wengine) badala ya kutimiza ahadi niliyojiwekea na nafsi yangu. Kwamba kwa nini nisithamini ahadi na nafsi yangu kwanza, ndipo nithamini ahadi na wengine? Kwa nini mtu mwingine akinipa kazi ya kufanya ambayo nina uhakika ina maksi, ninakuwa mwepesi wa kuifanya kwa mazingira yoyote yale (hata ikibidi kujinyima mengineyo kwa uchu tu wa alama za mtihani) and yet nashindwa yale yangu binafsi yasiyo na shinikizo lolote la nje (hi...

Mdoti: Mwanablogu wa kufikirisha katua

Nakumbuka miaka ya 2005 na 2006 wakati vugu vugu la blogu likiwa linashika kasi Bongo, ilikuwa ni kawaida kila siku kukutana na 'post' ya kumtambulisha mwanablogu mpya wa kiswahili kwa karibu kila blogu. Kwa sasa, kasi hiyo imepungua sana. Pengine sababu zinaweza kuwa nyingi. Shughuli zimekuwa nyingi na kadhalika. Lakini kwa kutambua umuhimu wake, naomba kumtambulisha mwanablogu mpya Ndugu Mdoti ambaye bila shaka anayo mengi ya kutufikirisha kupitia blogu yake anayoiita tufikiri. Bonyeza hapa kumtembelea mwanablogu huyu , umkaribishe. Ukiweza pia kumtambulisha kwa wasomaji wako kupitia blogu yako, itakuwa poa sana.

Katika hili Mzumbe wana kesi ya kujibu

Kwa muda sasa zimekuwepo shutma (siku hizi zinaitwa kelele nyingi) kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimetengeneza vihiyo wengi. Ni jambo la kusikitisha kwamba shutma hizi, kadri siku zinavyokwenda zinazidi kushika kasi kiasi kwamba sasa jambo hili limechukua ‘urasmi’ fulani hivi ambao kwa hakika si wa kupuuzwa. Juzi tu, mzalendo mmoja alikuja na maelezo yakinifu akidai kwamba kwa utafiti wake, kagundua kwamba ‘kuna matapeli’ kibao ambao wanakula kuku serikalini kwa jina la ‘Dakta’ lakini hawana lolote. Wahusika hawakutujibu (na kwa kweli sikutegemea wajibu kwa sababu) msomaji mfuatialiaji wa mambo atakubaliana nami kwamba habari hizi si za leo. Zimeanza miaka kadhaa iliyopita. Na wahusika hao wanaendelea kudunda mpaka leo. Hivi sasa unaposoma habari hizi, inasemekana baadhi ya ‘madakta’ hawa wamerudi shuleni kwao Mzumbe kurekebisha mambo kimya kimya. Huo ni ushahidi kwamba hata kama wanajidai hawasikii, lakini ‘waimeipata,’ kwamba ujambazi wao wa kitaaluma hatimaye umebainika. Hofu na mas...

Tulitembea kabla hatujatambaa?

Watu wengi tunayo mengi sana tunayoyafahamu. Lakini hayo yote tunayoyajua yanakosa namna ya kutusaidia sisi wenyewe, kwa sababu tuliruka hatua muhimu katika maisha. Hatua yenyewe ni kujifahamu sisi wenyewe. Nikirudi nitafafanua.

Kitafute hiki cha Stephen R. Covey

Picha
Kitabu hiki ni kati ya vitabu ambavyo unahitaji kuvisoma kwa faida yako mwenyewe. Sitangazi biashara, natangaza maarifa ya bure ambayo huhitaji kulipia 'tuition fee' kuyapata. Kama wewe ni kati ya watu wanaopenda kuwa na mafanikio ya kikweli kweli, kitabu hiki cha Seven Habits of Highly Effective People si cha kukikosa. Nilikipata Moshi kwa Sh. 22,000.00, sijajua bei yake kwa maeneo mengine.

Kanuni za maumbile na ufahamu wa mwanadamu

Hewa (ambayo nayo tunaambiwa it just happened) ina mchanganyiko wa gesi mbalimbali ambazo zipo kwa uwiano maalumu. Oksjeni lazima iwe kwa asilimia kadhaa, hewa-ukaa nayo iwe asilimia kadhaa na kadhalika. Uwiano huo ukiharibika kwa nukta chache sana, lazima madhara yatokee. Hoja yangu hapa ni iweje hewa hizi ambazo tunaambiwa zilitoke-ga ziwe kwa mpangilio ambao hautakiwi kabisa kuvurugika? Kama ni kwa habari ya by chance, kwa nini itokee kwamba uwiano huo uwe namna ile tu ulivyo? Niliachana na Fizikia miaka kadhaa iliyopita pengine ningekuwa na mifano mingi katika eneo hilo. Lakini hiyo hainifanyi nisahahu kuwa mwenendo wa dunia yenyewe unaonesha kutawaliwa na nguvu ili kuu zaidi. Mfano rahisi ni namna dunia inavyozunguka kwenye mhimili wake. Hakuna kukosea. Njia ni ile ile miaka nenda miaka rudi. Kama dunia ingekuwa imetokea-ga tu basi lingekuwa jambo linalowezekana kuwa siku moja dunia ingepotea njia na kwenda kusikojulikana. Kanuni zinazoongoza mzingo wa dunia zinaonekana kuheshim...

Ujuzi wa kanuni za maumbile haumkani Mungu

TUMEKWISHA kuona mifano ya upotoshaji uliofanywa na baadhi ya ‘wanasayansi’ ambao kimsingi walioongozwa na imani kuliko uhalisia. Tukaona kwa ufupi sana nafasi ya sayansi katika kutambua (sio kuvumbua) kanuni za maumbile ambazo kimsingi zilikuwepo kabla ya maarifa haya hayajakuwepo. Hapa tunaendelea pale pale kwa mifano zaidi. **************** Sayansi kwa kuzichunguza kanuni hizo, imeweza kuyabadili maisha ya mwanadamu kwa namna mbalimbali. Kwanza maarifa hayo yameweza kutusaidia kuvumbua nyenzo muhimu zilizotuwezesha kufanya mambo ambayo hapo awali hatukuwa na uwezo nayo. Pamoja na manufaa yote tuliyoyapata kwa maarifa haya ya sayansi, bado yapo maeneo ambayo kusema kweli sayansi imeharibu. Kwanza, kwa matumizi mabaya ya maarifa hayo yamefanya maisha ya viumbe yawe ya wasiwasi zaidi kuliko ilivyowahi kuwa katika kipindi cha nyuma. Kwa mfano, kwa maarifa yaliyopo, zimetengenezwa silaha ambazo kwa kweli kichaa mmoja akipandwa na hasira asubuhi moja na akakosekana wa kumdhiti anawez...

Da' Subi kahamia makazi mapya

Naomba nafasi katika blogu yako kuwataarifu wasomaji kuwa tovuti ya mpya ya wavuti.com imechukua nafasi ya iliyokuwa nukta77.com na nukta77.blogspot.comNaomba yeyote aliyekuwa ameweka linki ya nukta77 aihariri na kuweka wavuti.com Karibuni sana kutembelea kwa taarifa za nafasi za masomo na kazi kwa burudani na bila kusahau habari na porojo!Asanteni.wavuti.com ************ Kuanzia sasa pata habari zote kwa kubonyeza hapa . Na kama utapenda kufanya kama nilivyofanya mimi, unaweza kujiandikisha uwe unatumiwa habari kila anapoziweka pale.

Sayansi itufunze kuwa hatujui

Ushahidi mwingine kwamba viumbe hawawezi kuwa wamebadilika kama wanavyodai mashabiki wa nadharia za Darwin upo kwenye stadi za chembechembe hai za viumbe (seli). Kisayansi, ni jambo lililo wazi kwamba msingi wa kiumbe yeyote ni seli. Seli hizi zimeundika kimfumo. (Unakumbuka tafsiri ya mfumo?) Kila seli inayo vipengele vingi vidogovidogo ambavyo hufanya kazi kubwa kuliko kiwanda chochote kinachofahamika kutengenezwa na mwanadamu. Utendaji huu unawezekana kwa sababu kila kipengele kinatengemea kipengele kingine kiasi kwamba kimoja kikiwa na hitilafu hata ndogo sana , hakuna kinachoweza kuendelea. Na hitilafu hii ndogo kwenye seli moja ikiachwa iendelee basi, hatma yake huweza kuwa ‘ugonjwa’ wa kiumbe mzima na hata janga kubwa zaidi. Ni jambo jema kwamba elimu hii ya kujua utendaji muhimu wa kiwango cha seli umewezeshwa na sayansi halisia. Uvumbuzi wa darubini ndio ulimwezesha mwanadamu kuyajua yote haya ambayo hata hivyo yalikuwepo hata kabla ya sisi kuyajua. Mawazo kwamba kiumbe ana...

Evolution ni nadharia isiyo ya kisayansi

Wapo watu ambao waliweza kuitumia sayansi vibaya na kuidanganya dunia kwamba ‘maumbile’ (nature) ndio kila kitu. Kwamba kule kuyajua maumbile yanaongoza na kutawala mfumo wa ulimwengu (universe) ni sababu tosha ya kuyaamini maumbile yenyewe. [Mfumo kwa maana hii, ni uhusiano wa vipengele mbalimbali vya kimaumbile vinavyotegemeana kiasi kwamba pakitokea hitilafu katika kipengele kimoja, basi uhusiano wote unaathiriwa.] Watu hawa ni mafisadi wa kisayansi. Na wengine wao nilishajaribu kuwasema zamani kidogo kuonyesha kwamba walitumia sayansi kutuhadaa sisi tutetemekao tusikiapo neno ‘...kwa uchunguzi wa kisayansi...’ Kabla sijaenda mbali, niliseme hili mapema: Sayansi ilivyo ni maarifa ya muhimu sana. Tupo tunaoamini kwamba bila maarifa ya kweli kweli ya kisayansi, tungeishi kwenye dunia tusiyoielewa vizuri (japo hatujafika mahali pa kuielewa kwa maana halisi ya kuelewa) na wala kuelewa namna dhana mbali mbali za kimaumbile zinavyofanya kazi. Kwa hivyo, maisha yetu yangekuwa magumu s...

Kwa nini UKIMWI unashika kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara?

Hivi sasa ni wazi kwamba UKIMWI ni janga la dunia. Na kwa hakika, dunia yenyewe ni hii ya tatu hasa iliyo kusini mwa Jangwa la Sahara. Sasa hivi, tutakuwa hatujakosea sana tukisema kila familia kwa namna moja ama nyingine imeathiriwa na UKIMWI. Katika kudadisi kiini hasa cha tatizo hili hapa uswahilini, niliwahi kusikia wasomi fulani wakifikia mahali pa kuhisi (na kweli ni kuhisi) kwamba virusi vya UKIMWI vimetengenezwa na waropa kwa lengo kututeketeza sie tuliokolea rangi. Pengine hitimisho hilo lilifikiwa kwa kuangalia msambao wa gonjwa lenyewe. Kwamba tarakimu za waathirika zinaongezeka kwetu,wakati kwa wenzetu tarakimu hizo zinapungua. Hisia hizo niliziona kama jitihada za kawaida za sisi Waafrika kukimbia tatizo. Kila yanapotokea matatizo tunakuwa wa kwanza kukwepa kuwajibika na badala yake tunatafuta mchawi. Huu ni ujinga wa kawaida ambao naamini hatuwezi kuendelea kuuvumilia ikiwa kweli tunataka kuendelea. Chembechembe nyeupe tulizonazo waswahili (zinazoshambuliwa na virusi ...

Wingi wa siku ndio lengo lako?

Wengi wetu hufanya jitihada kubwa na kutumia muda mwingi kuhakikisha kuwa tunaishi maisha marefu. Tunaepuka kula baadhi ya vyakula na hata kufanya mazoezi si kuwa na furaha bali kuepa magonjwa fulani fulani. Lengo hasa likiwa katika kuzidisha wingi wa siku za kuishi duniani na wala si ubora wa siku hizo. Tungefanya vyema kama tungelijishughulisha kutafuta ubora wa siku chache tulizonazo ili tuweze kuziishi kwa furaha badala ya kuhangaika na kuzirefusha siku zetu ziende mbele pamoja na matatizo yake. Kilichobora si kurefusha siku ambazo zaweza kurefusha matatizo kwa upande mwingine...!

Uhai na mashaka ya chanzo chake

NILIWAHI kujadili kuhusu suala la mkinzano uliopo kati ya sayansi na dini. Sayansi siku hizi haina mvuto kwa vijana wa leo. Unahitaji kuwa mwehu kuijadili. Kimsingi, tangu zamani binadamu amekuwa akijaribu kudadisi asili yake yeye mwenyewe na viumbe wengine. Hilo limekuwa ni mjadala wa binadamu wengi. Kujua hasa ulipotokea uhai na kisa cha kuwa na viumbe wengi kiasi tukionacho leo. Suala hili limejaribu kushughulikiwa kwa njia za kiimani, ambapo wanadamu mwanzoni kabisa waliamini kuwa uhai umeasisiwa na nguvu iliyojuu ya ufahamu unaoelezeka, yaani Mungu. Wafuasi wa imani hii hawahesabiki katika sayari tunayoishi. Ni wengi hata kama si wote katika hawa wanasadiki kiukweli kweli hicho wakiaminicho. Katika hao wachache walishindwa kusaidiki kwa dhati dhana ya uumbaji, jumlisha maendeleo ya ukuaji wa maarifa yenye juhudi za kujua yanayohisiwa kujulikana, wapo binadamu ambao walianza kusita kukubaliana na ‘imani’ hii kwa madai kwamba ‘inalirahisisha mno’ suala gumu kwa maelezo ambayo ...

Ni wakati wa kukiasi kivuli cha ukweli…

Hutokea mtu akaishi maisha fulani duni sana lakini asijue kabisa kuwa yu duni. Wengine wetu tutakumbuka, angalau wakati ule tukiishi katika umasikini mkubwa wa familia zetu lakini hatukulifahamu hilo. Tuliishi maisha ambayo tunaamini kabisa kuwa hayo ndiyo yalikuwa yenyewe pasi hofu na mashaka. Maisha yalisonga mbele hata kama tulivaa fulana ndefu iliyosaidia kuondoa ulazima wa kuvaa kaputula. Tulipangana kitandani kila mmoja kwa welekeo wake, na bado hatukuuhisi umasikini. Umasikini wetu tulikuja kuujua baadae sana tukiisha kuwa tushahama maisha hayo kwa namna hii au ile. Tukaangalia nyuma na kujisikitikia kwamba “kweli” tulikuwa masikini. Kwa mfano huo, ukweli tulioishi nao ulikuja batilishwa na kugeuka ukweli mwingine tofauti na ule wa mwanzo. Namaanisha, kipindi kile cha umasikini usioonekana, ukweli haukuwa huu tulionao leo kwamba tulikuwa masikini siku zile. Bila shaka unanipata kwa kadiri ninavyotaka unipate, sivyo? Tafakari watu walioishi katika pango lenye giza nene mais...

Tovuti bure...wahi!

Nimepata ujumbe kutoka wataalamu hawa wa kutengeneza tovuti. Hivi ndivyo wanavyosema: " Pole na kazi ya kuelimisha na kuburudisha jamii yetu. Tumekuja na huduma mpya ya BURE kwa watanzania tu tunaomba uwafahamishe. Kuzingatia umuhimu wa kuwa na tovuti, na ya kwamba ni gharama sana hapa TZ kupata tovuti, na tena watu wanafanya biashara rasmi kwa barua pepe za bure kama yahuu na giimeili, hii yote inaonesha ukosefu au gharama kubwa ya kupata tovuti. Sisi tumedhamiria kubadili uelekeo mzima wa upepo, na tumepata wasamaria wema na sasa rasmi tumefanikiwa kuleta ufumbuzi na neema kwa waTZ kwa suala la tovuti na anuani rasmi za barua pepe. Na sasa kwa awamu ya kwanza kwa kuanzia tu, WATU 100 WATATENGENEZEWA TOVUTI BURE. Watu 100 kwa maana ya mtu binafsi, kampuni, biashara, shirika, asasi zisizochukua faida (NGO), kikundi, duka, mjasiriamali, saluni, shule ama Saccos n.k. BASI KILA ALIYEDHAMIRIA KUWA NA WEBSITE/TOVUTI ajiunge na utaratibu huu wetu atengenezewe TOVUTI MOJA...

Salamu kwako mwanablogu mpenzi

Ni mwaka unakimbia ama ni sisi tunakimbia? Masaa yanakwenda. Majuma yanayakatika. Mwaka huo unayoyomea. Bila kukaa sawa, mtu unajikuta mwaka umekatika ukikuacha unashangaa. Kazi ipo. Mwezi wa kumi huu! Nimeandika kukusalimu ewe mwanablogu. Mie sijambo, nakula asali na maziwa yake kwenye nchi ya ahadi. Ni bukheri wa afya njema.

Nani hushaurika kikweli kweli?

Kila mtu anayo misimamo na imani ambayo kwayo huiishi. Misimamo hii ambayo kimsingi ni falsafa, hujengeka kadiri tukuavyo kulingana na aina ya watu na matukio tunayokumbana nayo. Falsafa hizi ndizo hutawala namna tunavyoishi na watu, tunavyoyachukulia mawazo yao na hata namna tunavyojichukulia sisi wenyewe. Inasemekana, katika umri fulani wa makuzi, falsafa hizi huwa hazibadiliki tena. Tunaposhauriwa jambo, kwa mfano, kabla ya kulikubali, hulipambanisha na falsafa zetu. Ikiwa litashahabiana, hulipokea/assimilate na ikiwa litapingana na falsafa zetu, hulipuuza. Ndio maana kabla hujajitosa kumshauri mtu lolote, chunguza falsafa yake kwanza. Vinginevyo utakuwa unateketeza muda wako bure kumpa 'vidonge vyake' wakati ni wazi hatavielewa hata kama ni kweli unaweza kuwa sahihi kuliko yeye kwa vigezo vyako. Kimsingi, watu huwa hawashauriki, ila hutafuta kuungwa mkono kile wanachowaza.

Nani hushaurika kikweli kweli?

Kila mtu anayo misimamo na imani ambayo kwayo huiishi. Misimamo hii ambayo kimsingi ni falsafa, hujengeka kadiri tukuavyo kulingana na aina ya watu na matukio tunayokumbana nayo. Falsafa hizi ndizo hutawala namna tunavyoishi na watu, tunavyoyachukulia mawazo yao na hata namna tunavyojichukulia sisi wenyewe. Inasemekana, katika umri fulani wa makuzi, falsafa hizi huwa hazibadiliki tena. Tunaposhauriwa jambo, kwa mfano, kabla ya kulikubali, hulipambanisha na falsafa zetu. Ikiwa litashahabiana, hulipokea/assimilate na ikiwa litapingana na falsafa zetu, hulipuuza. Ndio maana kabla hujajitosa kumshauri mtu lolote, chunguza falsafa yake kwanza. Vinginevyo utakuwa unateketeza muda wako bure kumpa 'vidonge vyake' wakati ni wazi hatavielewa hata kama ni kweli unaweza kuwa sahihi kuliko yeye kwa vigezo vyako. Kimsingi, watu huwa hawashauriki, ila hutafuta kuungwa mkono kile wanachowaza.

Je! Yesu ni Mungu?

Haya ni maoni ya mdau asiyependa jina lake lijulikane. Nimeyatundika hapa kwa sababu ya uzito wa anachokisema. Tafadhali soma na kama unaweza changia maoni yako tuelimike. Nimshukuru sana kwa kutumia muda wake kuandika maoni yake na hapa namnukuu: MAKANISA ya Kikristo yanafunza ya kuwa Yesu Kristo si kama kuwa ni Mwana wa Mungu tu, bali hakika ni Mungu khasa. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni mmoja. Watatu katika mmoja, na mmoja katika watatu. Wote ni wa milele, wote ni sawa. Yesu ni Mungu, na Mungu ni Yesu. Hiyo ni imani ya Kikristo, ambayo inaaminiwa na karibu Wakristo wote. Hebu tuifunue Biblia tutazame inasema nini katika jambo hili? Mt Paulo katika barua yake ya kwanza kuwapelekea Wakorintho aliandika: Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. 1 Wakorintho 15.15 Juu ya kuwa Paulo anaambiwa ya kuwa akiamini kuwa Masihi (yaani Kristo) na Mwenyezi Mungu ni ki...

Dini: Matamanio ya kinadharia

Dini hunadi matamanio na taraji za kinadharia, zisizo halisi. Dini zinatangaza hukumu kwa mambo ya kimaumbile (nature) zikilenga kuwafanya watu kuishi maisha ya kimaigizo, yasiyoyao. Kwa mfano, zipo dini zinalazimisha 'makada' wake wenye damu kama sisi kutokuoa, ama kuolewa. Ilani hii ya useja, hata ikiwa nzuri vipi, inabaki kuwa mapendekezo mazuri yasiyotekelezeka. Huwezi kupambana na maumbile na ukanikiwa. Huwezi kuusukuma mwamba na kweli ukasogea ukiona. Kwa hiyo, matokeo yake unakuta wenye dini wanabaki kuzungumza kitu wasichokifanyia kazi. Hadharani wanazuia watu kuoa, gizani wanayatenda yayo hayo wanayoyazuia. Hadharani wana uwezo usioelezeka, sirini ni dhaifu kama wadhaifu wengine. Nini maana yake? Je, ni kweli dini i zaidi ya uhalisi? Je, miujiza inayonadiwa na dini, ni jambo lililo halisi? Je, dini si jumla ya matamanio hafifu yenye mipaka ya kibinadamu?

Dini na maoni ya wadau

Ninazo nyaraka kadhaa zilizotumwa kwangu na wadau wa ule mjadala wa dini. Zinafikia kumi. Wengine hawachelewi. Wamekuja na tuhuma nzima nzima kwa watu, ama vikundi vya watu. Ninatafakari namna muafaka ya kuwasilisha maoni yao bila upendeleo. Hata hivyo, ningependa kuwashauri wadau wa dini, kuzungumza mambo ambayo wana hakika nayo, yenye hoja, ambayo hataibua ugomvi usio na tija katika kutuelimisha. Kwa wale wasioridhika bila kutukana, ujumbe wangu kwao: Dini isipoweza kukusaidia kuitetea kwa lugha rahisi, hiyo haiwezi kuwa pungufu ya ubatili mtupu.

Viziwi wanaosikia tusivyovisikia...

Singida kwema. Nimekuwa na wakati mzuri na marafiki tulioachana kwa kipindi kirefu. Nimekuwa kiguu na njia utadhani kuku mfungwa aliyeachiwa kwa makosa. Jana nilipata fursa ya kutembelea shule ya viziwi na wasioona, Huruma. Nilikutana na walimu waliojitoa kuwasaidia watu hawa kwa moyo. Ilisisimua kuona viziwi wakipiga soga kwa lugha ya ishara. Walikuwa wenye furaha, kiasi kwamba hakuna kilichoonekana kuwapungukia. Nikajifunza. Kumbe furaha ni vile unavyoamua uwe. Huna haja ya kuwa na vyote ili kuipata. Nilimwona kijana asiyeona wala kusikia, lakini mwenye kusema! Ili kuwasiliana nae, unaandika mkononi mwake, anaelewa, halafu anajibu kwa mdomo! Naye huwezi amini kwa jinsi alivyojaa furaha! Nikaonana na wasioona wenye matumaini. Wasioona, wenye kuona tusivyoviona. Wenye furaha bila kutegemea vionekanavyo. Nikaondoka nikiwa na mawazo tele. Upofu na uziwi ni zaidi ya huu wa mwilini!

Shuzi la mwenye nyumba halinuki?

Kwa wale wenye uzoefu huu, tusaidiane kufikiri. Baba akichafua hewa (ashakumu si matusi akijamba) mbele ya wageni na wanae, nani hasa huwajibikia tendo hilo? Yeye, ama wanae? Manake mara nyingi hukosi kusikia mzee akijiwahi: ' Nyie watoto, sipendi kabisa hiyo tabia yenu...nendeni mkacheze nje.' Watoto pamoja na kuujua ukweli kwamba mtumiwa halisi ni baba yao, ambaye anawasingizia wao, huenda nje wakilalamika '...baba sio mimi...mi'shijajamba labda Mangi...!' Je, kuna ulazima wowote wa baba kukiri kuuwajibikia uchafuzi wake huo wa hewa badala ya kuwabebeshea wanawe?

Operesheni ya kilimo cha barabara

Nimerejea tena baada ya kumalizana na Kaizari. Nimepita Moshi kwa ufupi Jumamosi, kisha nikaja Singida, kupitia Arusha. Njiani nilishuhudia 'maendeleo' ya kilimo cha barabara. Barabara ya Minjingu-Babati inaparurwa kwa kasi. Ile ya Babati - Katesh - Singida nayo haiko nyuma, mkandarasi yuko 'saiti.' Nakumbuka tukiwa Magugu, abiria mmoja niliyebahatika kukaa naye, mtu wa makamo akaniambia; 'Kijana hivi unajua kwa nini barabara hii inajengwa kwa kasi hivi?' Nikamjibu; '...mzee sina hakika kama najua' Akafunga gazeti alilokuwa analisoma, akanitazama akisema: '...hii ni operesheni pumbaza kuelekea uchaguzi.' akaendelea; '...Nchi hii haitawaliwi kwa mipango ya muda mrefu. Kila kinachofanywa kina nia ya miaka isiyozidi mitano..' Barabara hii italimwa wee mpaka kampeni zifike, waitumie kama mradi wa kuvunia kura, na usishangae mambo yakiishia hapo hapo...' Niko Singida mpaka mwezi wa tisa.

Kumradhi wadau...

Sitakuwepo kwa siku mbili tatu sita kumi hivi, kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu. Nimefanya hivi nikiamini si vibaya kupeana taarifa. Mpaka hapo nitakaporejea, Amani kwenu nyote!

Soma maoni marefu ya Silas Jeremia

Msomaji aliyejitambulisha kama Silas Jeremia amenitumia waraka mrefu kupitia barua pepe leo. Aliniandikia SMS akiniarifu kuwa ameshindwa kuweka maoni yake kwenye blogu (Nadhani ni kwa sababu mchango wenyewe ulikuwa mrefu kuzidi kiasi cha meneno yanayoruhusiwa kuwa maoni kwenye blogger.) Nami nikamwelekeza kutumia barua pepe ambayo ni njia rahisi kwake. Kwa kuheshimu mchango wake, kama wasomaji wengine, nimeona ni vyema niu –paste mchango wake hapa kusudi upate hadhira inayohusika kwa majadiliano zaidi: " Naomba kutoa maoni yangu kujibu hoja za upotoshaji zilizoletwa na msomaji wako. Kwanza kama yeye alivyojitambulisha kwa hoja zake kuwa ni Mwislamu, mimi ni Mkristo. Nitajibu hoja zake moja baada ya nyingine ili aelewe kama atakuwa tayari. 1. Walioendesha biashara ya utumwa walikuwa Waarabu wa kiislamu. Hawa walikuja Afrika mashariki kufanya biashara mbaya kabisa ya utumwa na kueneza dini yao. Watumwa walisombwa kutoka Afrika kwenda Uarabuni mahali panaposadikika kuwa chan...

Global Voices: Dunia inaongea, unasikiliza?

Picha
Nimeamua kukata shauri na kujiunga na Jamii ya wanablogu wa Global Voices katika ukurasa wa Kiswahili . Ninajitolea kuusogeza ujumbe karibu na wasomaji wa kiswahili kwa kutafsiri makala zinazoandikwa na wanablogu wengine. Global Voices kimsingi ni jamii ya wanablogu kama 200 waliopo duniani kote ambao wanafanya kazi kwa pamoja kukuletea tafsiri na ripoti za yanayojiri kwenye ulimwengu wa blogu na uandishi wa kiraia. Global voices inapaza sauti ambazo kwa kawaida huwa hazisikiki katika vyombo vya habari vya kimataifa. Bonyeza hapa kusoma zaidi kuhusu jamii hiyo, halafu ukaribie kuchangia maoni kwenye ukurasa huo wa Kiswahili na kubadilishana mawazo na wanablogu wengine. Ndesanjo Macha , mtu aliyefanya kazi kubwa kutangaza teknolojia ya blogu kwa lugha ya kiswahili nchini na mmoja wa wahariri waandamizi wa Jamii hiyo, alikuwa na na haya ya kusema.

Soma maoni ya msomaji: Uislamu ulikuwepo tangu mwanzo

Namshukuru msomaji(ambaye hakutaja jina lake) kutupa maoni yake kuhusu hoja ya lini hasa Uislamu ulianza . Ikumbukwe, lengo hasa ni kujadiliana na si mabishano kama baadhi ya wasomaji walivyofikiri (Poleni nyote mliolalamika kwa SMS na e-mail). Hapa ni majibu ya msomaji huyo katika suala hilo: "...Salamu(amani) juu yenu. Naomba watu wafahamu ya kuwa uislamu si dini iliyopewa jina na muasisi fulani na kusema kuwa wafuasi wake waitwe waislamu, la hasha, bali Uislamu jina hili ukilitafsiri kwa lugha ya kiswahili ni amani, kujisalimisha, kunyenyekea ndiyo maana yake. Mtume Muhammad (S.A.W) si muanzilishi wa dini hii, na emeeleza wazi kuwa uislamu upo yaani (kujisalimisha kwa Mungu) toka kuumbwa kwa ulimwengu. Allah aliumba ulimwengu ili vitu vyote vimtii na kujisalimisha kwake, lakini viumbe hawa wawili (majini na watu) walipewa khiari na matamanio, na huo ndiyo mtihani wenyewe tulioumbiwa nao, ambao watu tunaelekezana, kuelimishana, kujadiliana, kuzozana mpaka tunafikia hata ku...

Nini hukifanya kitabu kuwa kitakatifu?

Picha
Niliyapenda maswali ya mwanazuoni Kamala . Sijayajibu, nikisubiri wengine wayajibu kwa haki. Ninaandika kinachotoka moyoni na nimekitafakari muda mrefu. Ninahitaji kuuelewa 'utakatifu' wa vitabu fulani tunavyoviogopa. (picha kwa hisani ya 3.bp.blogspot.com) Vinaongoza 'ushabiki' wetu kidini, na vinafikirika kuwa mamlaka ya ufahamu wetu. Tukiwa wakweli, vitabu hivi viliandikwa na watu. Hata kama wengine walidai kuwa 'mabomba' ya ujumbe kutoka kwa Mungu, lakini walikuwa watu. Tafsiri 'sahihi' ya vitabu hivi inahitaji imani. Akikisoma asiye na imani, anapata ujumbe tofauti na yule mwenye 'imani.' Sentensi zinazoeleweka, zinapindwa-pindwa kukidhi mukhtadha wa kiimani. Ningependa kujua hasa, vipo vitabu vingapi vitakatifu? Utakatifu wa kitabu unatokea wapi na ni nani mwamuzi wa utakatifu huu? Je, kitabu kitakatifu hakiwezi kusomwa bila uumini na kikaeleweka vizuri zaidi? Je, kitabu kitakatifu ni kweli tupu?

Blogu zetu na uhuru wa maoni

Blogu ni nyezo ya kuuwezesha uandishi wa raia. Kutupa fursa ya kupaza sauti zetu bila masharti. Vyombo vya kizamani vya habari havitupi fursa hii. Mengi ya yanayotangazwa na kuandikwa ni yale anayoyataka mmiliki ama Mhariri. Wasomaji, wasikilizaji ama watazamaji hubaki na haki ya 'kumeza' kilichoandaliwa. Na hata maoni yao yanapoletwa, kazi kubwa huwa ni kuyaminya yalingane na msimamo wa mmiliki ama mhariri. Jambo hili ni tofauti katika blogu. Huku, msingi mkuu ni majadiliano. Anayeandika, hufanya hivyo akialika mawazo ya wasomaji yanayoweza kuwa bora kuliko yake. Kwa hivyo, nimwombe msomaji wangu mmoja anayeficha jina lake kuutumia huru huu, kusema kile anachodhani ni sahihi kwa njia yoyote anayoona inafaa lakini sio kujaribu kusitisha mijalada inayomkwaza. Vilevile, si lazima sana kuficha jina. Kama una uhakika na unachosema, kwa nini ujifiche kwenye kichaka cha majina bandia?

Dini ni ajali ya kuzaliwa

Wengi wetu hatukuchagua kufuata dini tulizonazo. Tumejikuta tunarithi dini za wazazi ambazo leo tunatoana nundu kuzitetea. Tumezivaa dini bila maamuzi na tumezishikilia utafikiri tunazijua. Na ajabu tunaamini kuwa dini nyingine zilizobaki kuwa haziko sahihi wakati kama tungezaliwa na wazazi wengine pengine ndizo zingekuwa zetu! Mkristo (ambaye ni mrithi wa dini ya baba yake) anaamini dini zote zilizobaki zimekosea. Mwislam naye (ambaye kajikuta mwislam kwa kuzaliwa) anaamini wote waliobaki ni 'makafri.' Kinachosikitisha ni kwamba tumejengewa uzio wa kutuzuia kujifunza dini za wenzetu. Na tunapojifunza dini hizo, kimsingi hutafuta kasoro na mapungufu yatakayotupa kuridhika kuwa dini zetu ndizo sahihi. Tungelijua kuwa dini ni ajali, basi ikiwa ni lazima, tungezipitia zote ili kuchagua moja au mbili. Vinginevyo tunabaki vipofu jeuri wanaojua kuelezea mkia wakidhani ndiye tembo.

Uislamu ulianza lini?

Picha
YAMEKUWEPO madai kwamba Uislam ulianza tangu kuumbwa kwa dunia. Na wapo watu wanaotuaminisha hayo. Ukweli ni kwamba Uislam ulianzishwa na Nabii Muhammad mwaka 622 BK huko Arabia. Kabla yake, dini zilizokuwepo zilikuwa ni Uyuda ambayo ni dini rasmi ya Wayahudi (Judaism) na Ukristo ambayo ni dini ya mataifa wasio Wayahudi ulioanza miaka kadhaa baada ya Yesu kuwa ameondoka mwaka 33BK. Yesu mwenyewe hakuanzisha Ukristo. Alisali katika misikiti ya Wayahudi. Masinagogi. Maelezo haya yana msingi wa kistoria na sio propaganda za kidini. Ndio ni propaganda kwa sababu dini zote zimekuwa na tabia ya kuonyesha kwamba zenyewe ndizo za kweli kuliko dini nyinginezo hata ikibidi kwa kuichezea historia. Na ni bahati mbaya kwamba Dini zimekuwa na tabia ya kufanana ya kuzima uwezo wa waumini wake kuhoji lolote kwa kuwajengea hofu ya kujitafutia laana. Qur’an inatupa maelezo yanayokinzana kuhusu lini hasa Uislamu ulianza. Baadhi ya mistari katika kitabu hicho zinadai kwamba ‘nabii’ Muhammad ndiye ...

Kulikoni mambo ya dini

Picha
Ule mjadala hatujauhitimisha. Kama unayo maoni unaweza kuyaacha pale. Kwa sasa ningependa kudurusu baadhi ya mambo yaliyojitokeza kwenye mjadala ule ambao ulipata maoni ya wasomaji mbalimbali. Ikumbukwe kwamba blogu zina maana hasa yanapokuwepo maoni ya wanaosoma na sio kuendeleza tu yale ya aliyeandika. Jambo la kwanza lililojitokeza katika majibizano ya wasomaji wawili walioficha majina yao, ni kuhusu historia ya Uislamu. Kwamba mmoja anadhani Uislamu ulianza tangu kuumbwa kwa Dunia, na mwingine anadhani Uislamu haukuwepo hata miaka 2000 iliyopita. Nijuavyo mimi, kabla ya miaka 2000 iliyopita, haukuwepo Ukristo wala Uislamu. Hizi zote ni dini za juzi juzi. Dini iliyokuwepo enzi hizo katika nchi hizo tunazoiita takatifu ilikuwa ni Judaism. Dini isiyo na uhusiano wa moja kwa moja na Uslamu wala Ukristo. Ibrahimu anayetajwa na msomaji mojawapo kuwa na mila ya dini mojawapo, alikuwa na mila na utamaduni wa Kiyahudi mwenye dini ya Uyuda (Judaism). Maana ya historia hii ni ni...

Nimeikumbuka hii hapa...

Picha
Nimekuwa nikiamini kuwa tofauti ya mawazo ndiyo msingi wa majadiliano. Tofauti hizi ni pamoja na mitazamo na uelewa, namna tunavyo'react' tukiguswa kwenye maeneo tunadhani hayajadiliki, namna tunavyoheshimu mawazo ya wasemaji wengine wanaoamini tofauti na sisi, namna tunavyoweza kuvumiliana na bado tukajadiliana (hata kama inakuwa kama vurugu fulani vile) lakini mwishowe mnajifunza: Hakuna anayejua. Wote mnahitaji kujifunza kwa wengine. Nimefurahi kusoma maoni ya mchangiaji aliyeamua kujificha kwenye kichaka cha jina la 'Natiakasi.' Ni bahati mbaya kwamba alidhani mimi nina chuki na dini yake anayoitetea kwa nguvu zote. Nimeona pengine itafaa nikimwonyesha chuki yangu hasa ni ipi kwa kumpeleka kwenye makala hii , niliyoiandika miaka mitatu iliyopita. Enzi hizo nilikuwa bado naandika makala ndefu ndefu (kwa sasa huwa sioni ulazima wa kurefusha ninachotaka kukisema) kwa hiyo naomba msamaha kwa makala ndefu inayochosha. Pamoja na kwamba wachangiaji wa wakati huo wen...