Mkutano wa Copenhagen: Ugaidi wa kimaendeleo

Hivi sasa dunia yetu inapitia kipindi kigumu kuliko wakati mwingine wowote. Joto limeongezeka sana. Barafu inayeyuka. Kina cha maji kinaongezeka kwa kasi na kwa kweli ndani ya kipindi kifupi, baadhi ya visiwa vitafurikwa na maji kikiwamo kile cha Zanzibar.

Majanga haya yote yamesababishwa na akili ya mwanadamu mwenye fikra potofu ya kile kinachoitwa MAENDELEO. Mwanadamu wa sasa (wa kileo) ndiye hasa chanzo cha dhahama yote hii ambayo kwa sasa imefanyiwa Mkutano maalumu kule Copenhagen ambao ninaamini utaishia wale jamaa kupiga picha ya pamoja na kuja na matamko ya kisiasa then maisha yataendelea kama kawaida.

Bonyeza hapa kujua kinachoendelea kwenye mkutano huo na tayari mashindano ya matamko yameanza.


Ningependa tufanye tathmini ndogo ya namna ambavyo akili ya mwanadamu wa leo anayejiona kuwa kaendelea kuliko wengine wote waliopita.

Moja. Mwanadamu wa leo ameshindwa kabisa kutatua tatizo la utumiaji (ukwapuaji) wa vyanzo vya asili. Akikwapua vikaisha, anahamia kwingine. Akikwakupua vikaisha mlolongo ule ule unaendelea. Mifano iko mingi chagua mmoja ulio karibu.

Mbili. Mwanadamu (wa kileo) anazidi kujiweka mbali na maumbile asilia (nature). Watu wanakusudia kutokuyategemea mazingira ya asili (natural environment) na badala yake wanategemea vitengenezwaji. Watu wanataka kuishi maisha yao wenyewe kwa kutumia PESA, kwa gharama ya upya wa teknolojia ya kisasa ambayo kimsingi ni uharibifu mtupu wa mazingira. Zimejengeka fikra kwamba ukiendelea maana yake sahau shamba. Kila kitu nunua. Yaani maisha yanakuwa PESA. Bila pesa, ‘imekula kwako’.

Inasikitisha kuwa hata serikali ambazo zamani ziliamini kuwa pesa si msingi wa maendeleo, leo hii zimekuwa serikali za kibiashara. Ndio maana hazina sera inayozidi UOMBA OMBA.
Kwa namna ambavyo tumejiweka mbali na mazingira, tumejikuta tunaharibu uwiano wa asili uliokuwepo kati ya uwezo wa asili wa dunia yenyewe na kiwango cha madhara inachoweza kukimudu. Matokeo yake hivi sasa, ili tuishi bila matatizo tunahitaji dunia nyingine kama hii.

Tatu. Mwanadamu wa kisasa hajaweza kabisa kupunguza gharama zisizoonekana zinazolipwa na mzingira yetu kwa ajili ya uzalishaji (mara nyingine wa vitu tusivyovihitaji), usafiri na kadhalika.
Mfano mdogo. Angalia msafara wa Waziri Mkuu kwa mfano anapokwenda mikoani. Anasafiri na magari mangapi yanayowabeba watu wangapi anaowahitaji kwa kiasi gani huko anakoenda, kwa kuchoma mafuta kiasi gani? Sahau fedha zinazotumika, fikiria kiasi cha hewa ya ukaa ambayo ziara moja ya Waziri Mkuu mkoani inaizalisha kwa sababu ya faida tu ya kisiasa halafu umwangalie yeye mwenyewe anavyoweza kuwashutumu sana Wamagharibi kwa madhara ya tabia nchi yanayoonekana.

Nne. Mwanadamu wa leo hakubaliani kabisa na kanuni za kimaumbile. Anadhani ujanja ni kupingana nazo. Mfano kufa. Leo hii mwanadamu hataki kabisa kufa wakati anazaa kuliko wanadamu wengine wote waliopita. Tunataka kuishi muda mrefu wakati idadi yetu haituruhusu kuishi kwa muda huo. Ukomo wa maisha ni suala muhimu kwa sababu ya ukomo wa malighafi tunazohitaji ili kuishi. Ni ajabu kuwa tunazaliana sana halafu hatutaki kufa.

Njaa na idadi kubwa kupindukia ya watu (ambao wote wanalindwa kwa Haki za Binadamu; wasihi, wale, na kadhalika) husababisha mvurugano katika matumizi asilia na hivyo kuongeza uwezekano wa migogoro na hata vita isiyo na kichwa wala miguu. Na ili kupigana inabidi kuharibu mazingira ambayo tayari yameshaharibiwa.

Tano. Namna mwanadamu anavyofikiri katika kujiletwa maendeleo yake, inatia shaka. Tunapokuwa na tatizo, tunafikiri utatuzi wake tu pasipo kufikiri namna utatuzi huo unavyoweza kuleta taizo jingine.
Mfano. Mkulima wa Mwanza anadanganywa kutumia mbolea ya kisasa ili apate faida mara dufu kitendo ambacho kitaharibu udongo wake kabisa ndani ya muda mfupi. Hiyo ni kwa sababu mwandamu wa siku hizi anasaka faida (ya hela zaidi) kuliko kitu kingine chochote.

Ni kwa tabia hizi tano, ninadhani matatizo tunayoyaona yataendelea kuongezeka. Ule utaratibu wa dunia kujidhibiti kwa kuondoa adhari zinazotokea unazidi kupotea. Sababu ni nini? Ujinga wetu wa kifikiri kuwa maendeleo ni haya tunayoyaona. Leo hii vijana tunadhani dalili za mapema za ‘kuula’ ni kununua gari. Fine. Tunaula, matokeo yake kutoka Posta mpaka Mwenge unahitaji masaa matatu ukipaisha hewa ya ukaa hewani. Tunadhani maendeleo ni kupanda ndege kubwa kubwa kila wiki kwenda bara jingine.

Labda nihitimishe kwa maswali mawili matatu:

Je, ni mpaka serikali hizi (za kibiashara) zikutane ndipo wananchi wa kawaida tujue cha kufanya? Tunaelekea wapi? Je, maendeleo ni kwenda mwezini na kurudi? Je, maendeleo ni kula nyama za kopo na maziwa kutoka nchi nyingine?
Kama tunadhani hayo ndiyo maendeleo basi HATUNA HAJA ya mkutano wa COP15 Copenhagen. Tutakuwaje na haja ya mkutano ambao inakuwa kama washiriki wanashindana kuonyesha nani katamka kipi, kwa namna gani na ili kumpendeza nani ilihali mambo yataendelea kubaki vilevile?

Tujielewe.

Maoni

  1. sijui kama idadi ya watu ni tatizo. tatizo ni ujinga zaidi wa maendeleo kama ulivyotaja. watu wako bize kutengeneza siraha na wengine kununua siraha kama ulivyoona za Mbagala zikijiripukia na kuuwa iwezekanavyo!

    vita vinaua kila kitu, askari, raia. zinaua ndege, wanyama, wadudu. zinaua majani, miti na kila mmea, zinaharibu udongo nk na sisi tunaona ni vyema.

    tuko katika teknolojia kibao na maneno kibao, tunadhani pesa itatupeleka kwingi na kwa maana zaidi. tunakula wanyama na kuwamaliza na kukosa uvundo wa kutengeneza ardhi kutokana na vilivyokufa! nk nk

    wanasiasa nnao!

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Fumbo mfumbie mwerevu

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3