Ni wakati wa kukiasi kivuli cha ukweli…

Hutokea mtu akaishi maisha fulani duni sana lakini asijue kabisa kuwa yu duni. Wengine wetu tutakumbuka, angalau wakati ule tukiishi katika umasikini mkubwa wa familia zetu lakini hatukulifahamu hilo. Tuliishi maisha ambayo tunaamini kabisa kuwa hayo ndiyo yalikuwa yenyewe pasi hofu na mashaka. Maisha yalisonga mbele hata kama tulivaa fulana ndefu iliyosaidia kuondoa ulazima wa kuvaa kaputula. Tulipangana kitandani kila mmoja kwa welekeo wake, na bado hatukuuhisi umasikini.

Umasikini wetu tulikuja kuujua baadae sana tukiisha kuwa tushahama maisha hayo kwa namna hii au ile. Tukaangalia nyuma na kujisikitikia kwamba “kweli” tulikuwa masikini.

Kwa mfano huo, ukweli tulioishi nao ulikuja batilishwa na kugeuka ukweli mwingine tofauti na ule wa mwanzo. Namaanisha, kipindi kile cha umasikini usioonekana, ukweli haukuwa huu tulionao leo kwamba tulikuwa masikini siku zile. Bila shaka unanipata kwa kadiri ninavyotaka unipate, sivyo?

Tafakari watu walioishi katika pango lenye giza nene maisha yao yote, wakiishi kwa kupapasana. Kijitundu kidogo kilicho katika pango hilo kikiwasaidia “kuwaona” binadamu wenzao wanaopita kwa nje, japo kwa ugumu na kubabaisha sana. Kwa hali ilivyo, wakaaji wa hilo pango wangeweza kuviona vivuli vya wapitaji hao vikipita. Na kwa sababu hivyo ndivyo ilivyo tangu wamepata fahamu zao, wakajua kwamba watu ni vile vivuli ambavyo hupita nje ya pango lao, nao wakawaona kwa njia ya vivuli.

Itokee siku moja, mmoja wa “wanapango” aje nje ya pango aone sura halisi za watu ambao kimsingi yeye aliwajua kwa njia ya kivuli! Fikiria mshangao atakaokuwa nao huyu bwana. Halafu baada ya kuubaini uhalisi kwamba alichokuwa akikiona mle pangoni si halisi bali kivuli, na itokee arudi pangoni alimozaliwa na ajaribu kuwasaidia wakaaji yaani “wanapango” wenzie ambao hawakubahatika kupata fursa hiyo ya kuuona ukweli kwamba wanachokiona si watu halisi, bali vivuli! Nani atakuwa nani katika mafungu mawili ya mkweli na mwongo? Fikiria purukushani nzito itakayotokea katika majadiliano yale! Kila mmoja akiaamini kuwa akisemacho yeye ndiyo muhuri wa ofisi ya ukweli!

Kumbe ukweli ni kadiri ya tuuonavyo vichwani mwetu. Ukweli na uhalisi ni vitu viwili tofauti. Mengi tuyajuayo, ni kweli lakini si halisi. Twabishana sana kutetea kweli zetu, lakini kimsingi twaishi pangoni, na tuvionavyo ni “vivuli vya ukweli” na ole wake yeye atuambiaye mbadala wa tuvichukuliavyo kuwa kweli tupu.


Nipatapo nafasi nakusudia kulizungumzia hili kwa urefu kujaribu kuonyesha kuwa hata haya niyasemayo huenda ni kivuli cha ukweli mkamilifu.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia