Kwa nini UKIMWI unashika kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara?

Hivi sasa ni wazi kwamba UKIMWI ni janga la dunia. Na kwa hakika, dunia yenyewe ni hii ya tatu hasa iliyo kusini mwa Jangwa la Sahara. Sasa hivi, tutakuwa hatujakosea sana tukisema kila familia kwa namna moja ama nyingine imeathiriwa na UKIMWI.
Katika kudadisi kiini hasa cha tatizo hili hapa uswahilini, niliwahi kusikia wasomi fulani wakifikia mahali pa kuhisi (na kweli ni kuhisi) kwamba virusi vya UKIMWI vimetengenezwa na waropa kwa lengo kututeketeza sie tuliokolea rangi. Pengine hitimisho hilo lilifikiwa kwa kuangalia msambao wa gonjwa lenyewe. Kwamba tarakimu za waathirika zinaongezeka kwetu,wakati kwa wenzetu tarakimu hizo zinapungua.

Hisia hizo niliziona kama jitihada za kawaida za sisi Waafrika kukimbia tatizo. Kila yanapotokea matatizo tunakuwa wa kwanza kukwepa kuwajibika na badala yake tunatafuta mchawi. Huu ni ujinga wa kawaida ambao naamini hatuwezi kuendelea kuuvumilia ikiwa kweli tunataka kuendelea.
Chembechembe nyeupe tulizonazo waswahili (zinazoshambuliwa na virusi vya UKIMWI) ni hizo hizo walizonazo waropa. Na kisayansi, virusi vya UKIMWI vinamshughulikia binadamu yeyote bila kujali rangi yake ya ngozi kwa sababu chembechembe nyeupe za mwanadamu yeyote zinafanana kimaumbile. Lakini ajabu ni kwamba UKIMWI unaanza kuonekana kama ugonjwa unaoangalia rangi ya ngozi kabla ya kumwingia mwanadamu husika. Sababu ni kwamba Afrika inaonekana kuwa kimbilio sahihi la janga hili.

Tukizungumza kwa kuweka mbali hulka ya kujipendelea na kukwepa kuwajibika, tabia ambao imeendelea kuturudisha nyuma kwakasi isiyokubalika, ni vyema kukubali kwamba waswahili wengi bado hatujaweza kuwa watu wenye adabu kitabia na mwenendo kiasi kwamba tunakuwa wahanga muafaka kwa tatizo hili.

Tabia ngono tulizonazo zinaweka mazingira safi zaidi ya kumalizwa na virusi hivi. Bado hatujawa watu wenye adabu katika mienendo yetu.

Ni kawaida kukuta kijana wa kiswahili akijisifia mbele ya wenzake kuwa na wanawake kadhaa kwa wakati mmoja. Kuwa na heshima ya ngono kunaonekana kuwa sawa na kilema. Hali hii, haiwezi kutuweka mbali na mashambulizi ya kweli kweli ya UKIMWI.

Tumeanza kufikia mahali pa kuamini eti ukiisha kumtamani mwanamke yeyote atakayepita machoni pako, ‘kimaumbile’ huwezi kujizuia.

Tumeanza kufika mahali pa kuamini eti huwezi kuwa na mahusiano ya karibu na mwanamke pasipo agenda ya ngono. Tumekuwa watu tusio na nidhamu katika mahusiano ya kimapenzi. Angalia ‘filamu’ za kiswahili zinazoshika kasi kwenye soko hivi sasa. Jambo linaloshabikiwa zaidi ni usaliti wa kimapenzi na ‘urijali bandia ’ wa kutembea holela. (Akili zetu zimebanwa kwenye eneo hilo hilo, kwa hiyo inakuwa kama bila topiki ya mapenzi hakuna filamu.

Si tu kwamba hatuna nidhamu katika mahusiano ya kimapenzi, lakini pia hatuna adabu katika kujilinda. Najua kwamba si kila mtu anaweza kuiamrisha nafsi yake kutulia na mmoja. Hata tungefanyeje, wapo wenzetu ambao kwa makusudi ama vinginevyo hawawezi kuwa na maamuzi ya nidhamu katika mahusiano yao. Hawa, tukisema kweli, wangeamua kuchukua tahadhari wanaporuka ruka huko na huko wangeweza kuisaidia jamii na msambao wa gonjwa hili.

Tujiulize, hivi kwa nini tuwe na tabia za namna hii? Je, ni ‘maumbile’ ama ni kukosekana kwa utashi wa nidhamu ya kimapenzi? Kwa nini waropa ambao tunaowaona kama watu wasio na mkataba wa kudumu kimapenzi wameweza kuulazimisha UKIMWI kuwa ugonjwa unaopungua? Kwa nini hatuwezi kufanya maamuzi ya dhati ya kutusaidia sisi wenyewe na jamii zetu kupambana na maambukizi zaidi ya UKIMWI? Kama sisi Waafrika hatuwezi, mbona waropa wenye utashi kama sisi, mihemuko kama sisi wameweza? Je, kuendelea kusambaa kwa kasi gonjwa hili hapa Afrika, haiwezi kuwa sababu ya kutufanya tuonekane kuwa watu wenye kasoro?

Maoni

 1. sio kweli kwamba waswahili mnapenda ngono kuliko jamii zingine. fanya utafiti wa kutosha kwa hili ili ujue ukweli haisi juu ya ṕungufu'wa ngono miongoni mwa waafrika ukilinganisha na jamii nyingine na kuna uwezekano kuwa kinachotuua kama ukimwi sio ukimwi.

  fanya utafit mzee

  JibuFuta
 2. Asante kwa maoni yako ndugu Kamala. Nitafurahi ukinipa mtazamo wako katika hili ninalolihoji.

  Ninaweza kudhani nimefanya utafiti kumbe ndio kwanza naanza.

  JibuFuta
 3. Kamala unataka utafiti wa haina gani tena mzee, it is true ngono is centre of excellent huku Africa. Imagine hali inavyokuwa kipindi cha summer kule ulaya watu wanatembea almost uchi lakini kila mtu anajihifadhi kwa mambo ya ngono. Kuwa boyfriend or girl friend is not a ticket to make sex. Ila huku kwetu on the spot waja leo waondoka leo. Ni kweli kuna vitu vingi vinachangia ila mimi nakubaliana na Bwaya kwa asilimia mia. Tena sisi wanaume ndo chanzo, maana ndiyo wateja wakubwa na source ya ngono. Hawa maCD kama sisi wanaume tungeacha kuwa wateja nadhani wasinge simama kwenye barabara, we men are evils!

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3