Tunavyoweza Kuboresha Vituo vya Malezi

PICHA: John-Paul Iwuoha


MALEZI katika vituo vya kulelea watoto hayakwepeki. Katika mazingira ambayo wazazi wanafanya shughuli zao mbali na nyumbani kituo cha malezi kinakuwa msaada. Tafiti za malezi zimekuwa zikijaribu kuangalia namna gani huduma hizi zinavyoweza kuboreshwa. Moja wapo ya mashirika maarufu katika eneo hili ni Taasisi ya Marekani ya Mtandao wa Afya ya Mtoto na Maendeleo ya Utafiti wa Malezi ya Watoto (NICHD).

Masuala yanayozingatiwa na tafiti hizi ni ikiwa ubora wa huduma za vituoni unaweza kuhusishwa na ukuaji timamu wa mtoto kiakili, kihisia, kimwili na kistadi; aina ya mazingira ya kituoni yanayoweza kumsisimua mtoto kihisia na kiakili na kiasi salama cha masaa ambayo mtoto anaweza kubaki kituoni bila kupata madhara.

Uwiano wa walezi na watoto

Idadi ya watoto wanaoangaliwa na mlezi mmoja ni muhimu. Ingawa zinaweza kuwepo tofauti kutoka nchi moja mpaka nyingine, kwa ujumla, ni vyema watoto wadogo waangaliwe kwa ukaribu zaidi wanapokuwa kituoni.

Kwa mujibu wa NICHD, watoto wenye miezi 6 hadi mwaka 1½, kwa mfano, uwiano wapaswa kuwa angalau watoto watatu wanaoangaliwa na mlezi mmoja. Kwa mwaka 1½ mpaka 2 uwiano unaopendekezwa ni watoto watano kwa mlezi mmoja, na kwa miaka 2 mpaka 3, uwiano unaopendekezwa ni watoto saba hadi kumi kwa mlezi mmoja.

Watafiti wengine wanashauri kwa umri usiofikia miezi sita, ni vizuri kila mtoto awe na mlezi wake. Lengo la uwiano huu ni kuwasaidia watoto kuangaliwa kwa karibu kuhakikisha kuwa mahitaji yao yanazingatiwa.

Kadhalika, ukubwa wa kituo cha malezi nao ni kigezo kimoja wapo cha ubora wa huduma. Inapendekezwa kuwa watoto wawekwe kwenye makundi madogo yanayoangaliwa na walezi zaidi ya mmoja ili kuwawezesha kufahamiana kwa karibu. Kufahamiana kunasaidia kuwapa watoto utulivu wa kisaikolojia na kuwapa fursa walezi kushirikiana kwa karibu wanapowasaidia watoto.

Hali halisi katika vituo vingi hapa nchini ni tofauti. Walezi wachache huwajibika kuangalia idadi kubwa ya watoto. Mlezi mmoja, kwa mfano, anaweza kuangalia zaidi ya watoto 15 kwa wakati mmoja. Hali hii haiwezi kutosheleza mahitaji ya mtoto.

Mafunzo kwa walezi
 
Ubora wa kituo pia unategemea ubora wa ujuzi walionao walezi. Inashauriwa walezi wawe wamejifunza angalau mambo ya msingi yanayohusu makuzi. Mafunzo hayo yatawasaidia kujua namna ya kufanya kazi na watoto kwa kuzingatia mahitaji yao maalum. Pia, huwasaidia kufahamu aina ya vifaa vinavyowawezesha watoto kujifunza kulingana na mahitaji yao; aina ya michezo inayowafaa watoto na mambo kama hayo.

Vituo vingi katika nchi yetu vinatumia wasichana wasiopatiwa mafunzo maalumu kuwajengea uwezo wa kuelewa mahitaji ya watoto. Vituo vichache vinatumia walezi wenye elimu ya makuzi, ingawa navyo, vinatoza ada ambayo si wazazi wengi wanaweza kumudu.

Ni muhimu watu binafsi na mashirika yanayoendesha huduma hizi kuwaajiri walimu waliofuzu. Tunavyo vyuo vinavyotoa mafunzo ya elimu ya awali kwa ngazi mbalimbali. Hivyo hakuna sababu ya vituo kuajiri walezi wasio na uelewa wa makuzi ya mtoto ambao, mara nyingi, huwa na matarajio makubwa kuliko uwezo halisi wa watoto. Mazingira haya huweza kuwafanya watoto wajenge uadui na shule mapema.

Mazingira sisimushi kwa mtoto

Inashauriwa kituo kiwe na mazingira rafiki yanayomfanya mtoto ajisikie salama. Hiyo ina maana ya kuhakikisha kuwa walezi wanao uwezo wa kujenga mahusiano mazuri na watoto; hawabadiliki kila mara ili watoto wasipate kadhia ya kukutana na sura ngeni mara kwa mara.

Pia, ni muhimu kituo kiwe na vifaa vinavyomsaidia mtoto kujifunza. Mfano, vifaa vya kuchezea, mafumbo, rangi za kuchorea, CD za hadithi kwa lengo la kupanua uwezo wa mtoto kiufahamu. Sambamba na hilo, ni vyema walezi wakaweza utaratibu mzuri wa watoto huwa na uhuru wa kufanya michezo kadri inavyowezekana.

Usalama ni jambo la msingi. Jengo linalotumiwa kwa huduma ya malezi lisiruhusu mtoto kutoka bila uangalizi. Usalama unakwenda sambamba na kupatikana kwa huduma bora za usafi na chakula, malazi safi, michezo na vifaa muhimu vya mtoto kujifunzia kulingana na umri.

Masaa ya mtoto kubaki kituoni

Tafiti nyingi zilizofanyika katika nchi zinazoendelea zinabainisha kuwa mtoto anapotumia muda mrefu kituoni uhusiano wake na wazazi huzorota. Kwa mfano, mtoto chini ya mwaka mmoja anapoachwa kwa zaidi ya masaa sita kwa siku anaweza kujenga tabia hasi kama upweke na kukosa imani na wazazi.

Ingawa hatuna tafiti zilizofanyika kwenye mazingira yetu, ni dhahiri kuwa upo umuhimu wa kupunguza muda wa kumwacha mtoto kituoni. Kadri mtoto anavyoendelea kukua, hata hivyo, muda anaoweza kuachwa kituoni unaweza kuongezeka. Pamoja na hayo, ni vyema kuhakikisha kuwa mtoto anakaa muda mfupi iwezekanavyo kituoni sambamba na jitihada za kujenga uhusiano mzuri na mtoto mara baada ya kuondoka kituoni.

Mahitaji ya kisera


Ni dhahiri manufaa ya malezi vituoni yanategemea, kwa kiasi kikubwa, ubora wa huduma zinazotolewa kwenye vituo hivi. Katika jitihada za kuhakikisha kuwa vituo hivi vinaendeshwa kwa ubora, ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa vituo vinasajiliwa. Wafanyabiashara wanaoanzisha huduma hizi walazimike kutumia majengo yenye ubora, wawe na vifaa muhimu vya michezo na waajiri walezi wenye mafunzo yanayotambuliwa.

Vile vile, tunahitaji sera za kazi na ajira zinazowezesha akina mama kufanya majukumu yao ya kimalezi bila kuathiri kazi. Kwa mfano, kuongeza muda wa likizo ya uzazi anayopewa mfanyakazi wa kike anayejifungua inaweza kusaidia kupunguza changamoto za malezi.


Kadhalika, waajiri waangalie uwezekano wa kuwa na utaratibu wa vituo vya malezi kwa ajili ya wafanyakazi wao. Mama anayenyonyesha, kwa mfano, awe na fursa ya kumwona mwanae baada ya muda fulani akiwa kazini.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?