Upendeleo wa Wazazi Unavyoweza Kuchochea Uadui kwa Watoto

PICHA: Aim Lower Journal


KUNA kisa kimoja kwenye biblia kinachoweza kutufundisha jambo muhimu kama wazazi. Kisa chenyewe ni kile cha Yusufu, mtoto wa mzee Yakobo, aliyejikuta kwenye mtafaruku mkubwa  na ndugu zake. Ugomvi wa Yusufu na kaka zake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba kaka zake waliazimia kwa pamoja kumwuuza Misri kama adhabu. Jambo la kuzingatia ni kwamba ugomvi huu wa Yusufu na ndugu zake haukutokea kwa bahati mbaya. Chanzo cha yote hayo ni upendeleo.

Mzee Yakobo aliyekuwa na watoto 12 alimpenda zaidi Yusufu na kuonesha kumpendelea waziwazi. Kwa mfano, tunaambiwa Yakobo alimshonea kanzu nzuri kijana wake huyo Yusufu. Pia, wakati wenzake wakiungua jua wakichunga porini, Yusufu alitulia nyumbani na wazazi. Huu ulikuwa ni upendeleo wa wazi.

Inawezekana mzee Yakobo alikuwa na nia njema na hakukusudia kuchochea ghasia kwenye familia. Lakini matokeo ya nia hiyo njema yalikuwa ni kujenga ufa mkubwa kati ya Yusufu kipenzi chake na kaka zake waliojiona hawana nafasi kwenye familia hiyo. Upendo wa mzee ulimgharimu Yusufu na alichukiwa vikali na kaka zake.  Chuki ilifanya iwe vigumu kwa Yusufu kuzungumza na kaka zake. Mwisho wake, tunaambiwa, ilipojitokeza fursa ya kulipiza kisasi, ndugu zake wakawa tayari kumwuua.

Hali kama hii hutokea hata leo. Wapo wazazi, ambao bila kujua, wana tabia ya kuonesha upendeleo kwa watoto. Kwa sababu tu mtoto fulani anafanya vizuri na kukidhi matarajio ya mzazi, basi anapendwa kuliko wengine. Kwa wazazi wengi wa siku hizi, ni wazi mtoto anayefaulu darasani, asiyemsumbua mzazi, ndiye anayegeuka kuwa kipendi cha wazazi. Ndivyo ilivyokuwa kwa Yakobo. Ingawa sababu kubwa ya kumpenda Yusufu inayotajwa ni kuwa mtoto wa mke mdogo aliyependwa zaidi, pengine hata ndoto zake kubwa, kuonekana anajitambua kuliko wenzake, ilimfanya mzee akampenda.

Wakati mtoto mwema akipendwa na kila mmoja kwenye familia akishuhudia, anakuwepo mtoto anayekosea na kushindwa kufikia matarajio ya wazazi, ambaye naye, anajikuta matatani. Wazazi wanamchukia, wanaonesha dhahiri kwamba hawana muda naye, na wamemkatia tamaa. Wazazi ndani yao wanafikiri kufanya hivi ni kumfundisha adabu huyu anayekosea ili ajifunze kuwa mtoto mzuri.

Lakini matokeo yake huwa ni kinyume. Mtoto asiyependwa na anayetengwa anajenga chuki na visasi vya ndani kwa ndani dhidi ya wazazi wenyewe na mwenzake anayeonekana kuwa chaguo la wazazi. Hali hii hutengeneza ufa mkubwa katika familia. Hapawezi kuwa na ushirikiano na maelewano katika mazingira kama haya.

Visa kama hivi visiposhughulikiwa mapema, huweza kuhamia kwenye vizazi vinavyofuata miaka mingi baada ya wazazi kuondoka duniani. Kwa kutumia mfano wa Yakobo, tunaambiwa, naye pia alitokea kwenye familia iliyokuwa na matatizo kama hayo. Baba yake aliyeitwa Isaka, alikuwa na tatizo la ubaguzi kwenye familia yake. Alimpenda Esau na akawa tayari kumbariki na kumtamkia maneno mazuri Esau kuliko Yakobo  ambaye naye tunaambiwa alipendwa na mama yake.

Hali hii, ilijenga ufa mkubwa kwenye familia hiyo. Mbali na Yakobo kulazimika kutoroka familia baada ya kufanya udanganyifu na kumzidi ujanja Esau, hatuoni ushahidi wowote wa mawasiliano kati ya ndugu hawa wa tumbo moja. Miaka mingi baadae, ilibidi ifanyike kazi kubwa kuhakikisha mahusiano yanarudi.  Pamoja na hayo, tunaona, hata yeye Yakobo alipopata familia yake, alirudia kufanya yale yale aliyoyaona yakifanywa na wazazi wake.

Tunajifunza hatari ya kupalilia ubaguzi katika familia. Familia inayopalilia ubaguzi wa wazi wazi au kificho huwa haikosi misuguano. Kwa kawaida, kunakuwa na makundi yasiyoaminiana katika familia. Katika mazingira haya ya kutokuaminiana, ni vigumu wanafamilia kuwa na ushirikiano na upendo kati yao.

Kuepusha matatizo kama haya wazazi tunahitaji kujenga mazingira ya watoto kujisikia kutendewa kwa usawa. Asiwepo mtoto anayejisikia kunyang’anywa haki yake na kupewa mwingine. Tunapowatendea kwa haki na kuwafanya wajione kuwa sawa machoni pa wazazi wao, tunawafanya wawe tayari kushirikiana.

Pengine unajiuliza, nitajuaje kama familia yangu ina ushirikiano na kwamba hakuna mtoto anayejisikia kutengwa na kutokutendewa haki? Hapa vipo viashiria kadhaa za familia yenye uhai. Moja, ni hali ya watu kuaminiana. Kuaminiana maana yake kila mmoja anakuwa hana wasiwasi na kile kinachosemwa au kufanywa na mwanafamilia mwingine. Wazazi wana kazi ya kuhakikisha si tu wanatenda haki, lakini pia wanaaminika kwa maneno yao.

Lakini pili ni kuheshimiana. Unaposema unamheshimu mtu maana yake unajali utu wake kama ambavyo nawe ungependa watu wengine wakujali.  Mzazi asiyemheshimu mtoto, kwa mfano, ni mwepesi kumvunjia heshima pale anapokuwa ametenda kinyume na matarajio yake. Unapomtolea mtoto maneno makali kwa sababu ya makosa aliyoyafanya, unamfanya ajisikie kuvunjiwa heshima kama binadamu. Hali hii huongeza ufa kati yako na mtoto.

Pia, kuwa na desturi ya kufanya mambo kwa ushirikiano kunakuza uhai baina ya wanafamilia. Kwamba hakuna anayejisikia kubaguliwa wala kukosewa heshima, inamfanya kila mmoja ajione anawajibika kwa mwenzake. Kinyume chake ni ubinafsi wa kila mwanafamilia. Familia yenye watu wanaofanya mambo bila kushirikiana haiwezi kuwa na uhai.


Kama wazazi tunaotambua umuhimu wa familia kuwa pamoja, tuna kila sababu ya kuhakikisha tunawawekea watoto mazingira ya kushirikiana kufanya mambo. Tuwape watoto kazi zinazowalazimisha kusaidiana kufikia malengo ya pamoja. Kwa kufanya hivyo, tunajengea kizazi kinachothamini ushirikiano katika kufanya mambo yake. 

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia