Mambo ya Kutafakari Unapoanzisha Uhusiano wa Kimapenzi Kazini

PICHA: Shalinii Choudhary 


Sehemu kubwa ya maisha yako kama mfanyakazi unaitumia kwenye eneo la kazi. Ingawa inategemea na aina ya kazi unayoifanya, ni wazi muda mrefu kwa siku unaoutumia kutekeleza majukumu yako unakuweka karibu zaidi na wafanyakazi wenzako kuliko hata familia na marafiki. Mazingira haya ya ukaribu wa kikazi, wakati mwingine, yanatengeneza uwezekano wa uhusiano wa kimapenzi baina ya wafanyakazi.

Kwa kawaida, unapokuwa na mtu mnayefanya naye kitu kinachofanana kwa muda mwingi, ni rahisi kuanza kuvutiwa naye. Kadri mnavyoonana mara kwa mara ndivyo mnavyozidi kufahamiana kwa karibu. Hisia za mapenzi zinaweza kuzaliwa kama tahadhari hazitachukuliwa.

Msomaji mmoja  ambaye hakujitambulisha jina lake aliniandikia ujumbe mfupi wa maneno, ‘Mazingira yanayoweza kuanzisha mapenzi kazini, Da. Nimeyasoma vizuri sana. Nahisi kama hayaepukiki hivi. Tatizo ni muda mwingi watu wanakuwa pamoja katika kufanya kazi… Issue (suala) ya mapenzi katika mazingira ya kazi haiepukiki. Hayo ndio mambo yetu sie vijana.’ Kwa vijana wengi wanaoanza kazi, eneo la kazi linaweza kuwakutanisha na watu wanaoweza kuwa wapenzi wao.

Ni dhahiri ofisi zinakutanisha watu wenye uelewa usiotofautiana sana, wenye mtindo wa maisha usiotofautiana sana na hivyo kuongeza uwezekano wa mahusiano ya karibu. Kukaa pamoja kwa muda mrefu pia inaweza kuwa fursa ya kumfahamu mtu anayeweza kuwa mpenzi wako bila yeye kufahamu kama Mage (27) anavyofafanua.

‘Ukisema nikwepe mapenzi kazini saa nyingine haiwezekani. Mimi karibu kila siku naondoka nyumbani saa 12 asubuhi narudi usiku saa 2. Nitaonana wapi na watu wengine?’

Kwa wafanyakazi wasiopata muda wa kukutana na watu wengine nje ya eneo la kazi kama Mage, ofisi inaweza kuwa fursa ya mahusiano ya kudumu.

Ukaribu unaowatenga na wengine

Upo uwezekano mkubwa wa ofisini kuwa eneo la ‘michepuko.’ Wanandoa wenye matatizo nyumbani wanaweza kutumia ukaribu wa ofisi kujiliwaza kama anavyosimulia Khalid, ‘Kazi zinawezesha michepuko. Unakuta mtu ana mafrustration (matatizo) yake nyumbani. Hapa kazini anakutana na watu wajanja wanaomjali na kumsikiliza kuliko mke wake nyumbani, kuchepuka ni dakika.’

Vyovyote iwavyo, unapokuwa na mpenzi kwenye eneo la kazi, ni vigumu kuficha. Ingawa inategemea na ukomavu wenu, ni suala la muda tu kabla hamjaanza kuonekana karibu kuliko ilivyo kawaida. Tetesi zitakapoanza kuenea kwamba ‘mnatoka’ hamtazifurahia na zinaweza kutengeneza ufa baina yenu na wafanyakazi wenzenu.

Pia, wafanyakazi wenzenu kwa kutambua mapenzi yenu wanaweza kuanza kuwapa nafasi ya kuwa na faragha yenu wenyewe. Hali hii mtaitafsiri kama kutengwa na kuonewa wivu. Katika mazingira kama haya, ni rahisi uhusiano wenu na wafanyakazi wengine kuzorota.

Mgongano wa maslahi

Unapokuwa na uhusiano na mfanyakazi mwenzako, unajiweka kwenye mitihani ya kiutendaji. Fikiria, kwa mfano, mazingira ambayo mmoja wenu kati ya ninyi mlio wapenzi anawajibika kwa mwenzake kikazi. Kibinadamu ni vigumu kuacha kukupendelea. Katika mazingira ambayo wafanyakazi wengine wanashuhudia hilo likiendelea, sifa na maslahi ambayo pengine mmoja wenu angestahili kwa haki, yanaweza kuibua maneno yatakayowaudhi.

Kwa upande mwingine, aliye chini ya mwenzake naye anaweza kuanza kuwa mzembe kazini akiamini mpenzi wake ambaye ndiye bosi atamlinda. Hali kama hii inaweza kuibua changamoto kubwa ya kiutendaji. Mkubwa ataanza kujisikia kudharaulika, na aliye chini ataanza kujisikia hatendewi haki pale atakapokosa kile anachokihitaji.

Inapotokea mmeachana

Tunajua mapenzi yana nyakati zake ngumu pia. Si mara zote unapoanzisha uhusiano na mtu basi maana yake mnaweza kuendelea kuwa wapenzi kwa muda mrefu. Inawezekana mkashindwa kuelewana kwa sababu moja au nyingine na mkaamua kuachana.

Ugomvi wa mapenzi mara nyingi hufanya watu waliokuwa wapenzi wasiendelee kuwa marafiki. Fikiria namna utakavyoendelea kufanya kazi katika mazingira kama haya. Unapofanya kazi na mtu ambaye alikufahamu kwa karibu sana na baadae mkaachana vibaya huwezi kuwa na ujasiri.

Hali hii inaweza kusababisha kuzorota kwa kazi zako, utoro kazini na hata kuchukia kazi bila sababu za msingi. Kinachosababisha yote haya ni kuanza kuyahusisha mazingira ya kazi na mazingira ya ugomvi wenu wa kimapenzi. Katika mazingira kama haya, ni rahisi kupoteza utoshelevu kazini.

Unaweza kupoteza kazi

Mbali na kuathiri mawasiliano yako na wafanyakazi wenzako, mapenzi kazini yanaweza kukuingiza kwenye matatizo. Kumbuka kwamba maisha ya ofisini hayatoshi kumfahamu mtu. Unayefikiri anatafuta mwenza inawezekana ameacha familia nyumbani. Uhusiano wa namna hii unaweza usiwe na mwisho mzuri.

Janeth Urio, Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge anaonya mazingira hatarishi yanayoweza kugharimu mtu kazi. ‘Mahusiano ya kimapenzi kazini yanaweza kuwa na athari kwa mwajiriwa pale atakaposhindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Katika mazingira ya namna hiyo, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini namba 6 ya 2004, mwajiriwa anaweza kujikuta akipoteza kazi kwa sababu ya utendaji usioridhisha.’

Chukua tahadhari

Mkurugenzi wa Raslimali Watu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Fr. Adalbert Donge anatoa tahadhari. ‘Eneo la kazi linapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Mahusiano ya kimapenzi kazini si mahali pake. Mahusiano yanayoruhusiwa kazini ni yale ya kuheshimiana na kusaidiana ili kuboresha utendaji kazi,’ anasema na kisha kutoa ushauri kwa waajiri.

Mahusiano mengi ya muda mrefu ikiwemo maisha ya ndoa msingi wake unaweza kuwa maeneo ya kazi. Ili kuwa na tahadhari na heshima katika suala la mapenzi kazini waajiri wanashauriwa kuwa na miongozo ili kulinda heshima ya ajira na malengo yake.’


Mapenzi ofisini yanaweza kuzaa uhusiano wa kudumu ikiwa hayataharibu kazi na tahadhari za msingi zikichukuliwa. Kupima faida na hasara kabla haujaanzisha uhusiano wa kimapenzi ofisini ni jambo la busara. 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?