Chuki Unakuumiza Wewe Kuliko Unayemchukia

PICHA: PM Notes


MIAKA kadhaa iliyopita nilikosana na mtu ambaye awali tulikuwa karibu kikazi. Nilimwamini kama rafiki tuliyefanya kazi pamoja. Sikufikiri angeweza kujitafutia sifa binafsi kwa kunihujumu. Kilichoniumiza si tu kutendewa osa la makusudi, bali kuona mtu niliyemheshimu akijaribu kufikia malengo yake kwa kujaribu kuniharibia kazi yangu.

Nakumbuka baadae tulizungumza na nikafikiri nimemsamehe. Hata hivyo, ninapotazama nyuma, ninagundua kwamba sikuwahi kumsamehe kwa karibu miaka miwili baadae. Uhusiano wetu ulizorota na haukuweza kurudi kama ilivyokuwa hapo kabla. Ingawa tuliendelea kuzungumza lakini ule urafiki wa dhati unaoanzia moyoni haukuwepo tena.

Sikuwa na imani naye. Sikuamini aliyoyasema na kuyafanya. Kila nilipokumbuka namna alivyonihujumu, hisia za usaliti zilinirudia. Ingawa nilijiaminisha kwamba nimemsamehe, lakini katika maisha halisi sikuwa nimemsamehe. Kwanza, wakati wote nilikumbuka yale aliyonitendea. Akili yangu ‘ilisamehe’ kwa maneno lakini haikusahau kwa vitendo. Mara kadhaa moyo wangu ulijaa huzuni na ghadhabu. Kwamba sikuwa nimesahau kosa lake maana yake bado nilikuwa nahesabu kosa lake. 

Lakini pili, sikuwa natamani kusikia akipatwa na mema. Kama ningesikia akisifiwa kwa jambo zuri alilolitenda, moyoni nilijisikia vibaya. Mafanikio yake yaliniudhi. Sifa na jitihada zake njema zilikuwa kero kwangu. Moyoni nilitamani kusikia akipata mshahara wa mabaya aliyonitendea. Wahindi wanaita ‘karma’.

Nakumbuka siku moja alipatwa na changamoto fulani kazini. Niliposikia kilichotokea moyo uliruka ruka kwa furaha hata kama sikusema. Niliamini ‘mungu’ hatimaye amemlipa kwa mabaya aliyonitendea. Nilifurahia kwamba sasa amekula matunda ya matendo yake mwenyewe. Sasa nafahamu hiki kilikuwa ni kisasi cha kificho ndani yangu. Huyu bwana aliishi moyoni mwangu hata kama kwa nje niliamini nimemsamehe.

Hali hii ya kutokusamehe ilipanda ngazi na kugeuka kuwa chuki. Ungeniuliza kwa nini nilimchukia, pengine ungeungana na mimi. Nilikuwa na kila sababu sahihi ya 'kuachana naye.' Sikutamani kuwa karibu naye tena. Chuki iliyokuwa inanitafuna moyoni ilinifanya nikawa mwepesi kuamini tetesi za mapungufu yake. Nilijikabidhi kuwa mtumwa wake.

Unapomchukia mtu, kwa hakika, unajibebesha mzigo mzito kihisia kama ilivyokuwa kwangu. Unakuwa na kazi na kupambana na mtu ambaye pengine hana habari na wewe. Wakati wewe ukijiumiza kwa kutamani aharibikiwe, mwenzako ndio kwanza anafanikiwa. Chuki, katika mazingira haya, inakuwa na kazi ya kukuumiza wewe kuliko inavyomwumiza unayemchukia.

Hatimaye nilijifunza kusamehe. Nikagundua unapomsamehe mtu maana yake si tu unaachilia kile alichokufanyia, bali unarejesha uhusiano uliokuwepo kabla ya kosa. Kiashiria kimojawapo kwamba umerejesha uhusiano ni pale unapoanza kufurahia mafanikio yake na kusikitika unaposikia amepatwa na mabaya. Hiki ndicho kipimo cha msamaha wa kweli. Kinyume na hapo ni chuki inayoishi ndani yako.

Inawezekana unaposoma hapa unakumbuka watu waliokukosea. Pengine ni mume wako au mke wako. Pengine ni mwanao. Pengine ni ndugu yako wa karibu, mfanyakazi mwenzako au mshirika wako wa kibiashara. Unapokumbuka aliyokufanyia unajikisia uchungu. Unajiapiza hutakaa usamehe. Huo ndio utumwa ambao chuki inaweza kukutengenezea.

Kuushinda utumwa huu ni kuwaruhusu watu kukukosea. Nilipojifunza kujiondoa kwenye hadhi ya kuwa mtu maalumu asiyepaswa kuguswa na mwingine, ilikuwa rahisi kuanza ukurasa mpya. Nilianza kuachana na gereza la ‘karma’ la kufikiri kwa kuwa mtu amenikosea, lazima na yeye apatwe na mabaya.

Unaweza kufanya hivyo pia. Msamehe yeyote aliyekutendea mabaya. Hufanyi hivyo kumsaidia yeye kwa sababu pengine anafurahia kukuona unateseka. Unasamehe kwa faida yako mwenyewe. Badala ya kujifungia kwenye gereza la kulipiza kisasi, unajiwekea mazingira ya kuushinda ubaya kwa wema.


Ikiwa ni lazima kulipiza kisasi ili ujisikie ahueni moyoni mwako, kisasi sahihi zaidi ni upendo. Mpende mchumba aliyekuacha. Mpende rafiki aliyekusaliti. Mpende mfanyakazi aliyekuhujumu. Kwa kufanya hivyo, unajiweka huru wewe mwenyewe na kujifungulia milango ya kusonga mbele na maisha.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Pay $900? I quit blogging