Umuhimu wa Kiongozi Kuwa Mnyenyekevu -2

PICHA: entrepreneur.com

JUMA lililopita tuliona kuwa mtu huhitaji sifa fulani kumwezesha kupanda ngazi za uongozi. Mtu anapokuwa na uwezo wa kufanya kazi na watu; kuwasiliana vizuri na wakubwa wake wa kazi na hata walio chini yake na kufuatilia mambo ya msingi kwa makini anakuwa katika nafasi nzuri ya kupewa madaraka.

Kinachompa madaraka, kwa kawaida, ni zile sifa za utu na uwezo wa kusukuma mambo yakaenda kwa ushirikiano wa wengine. Mtu asiye na sifa hizi, kwa hakika, inaweza kumchukua muda mrefu kuaminiwa na kupewa madaraka isipokuwa kwa njia za mkato.

Hata hivyo, baada ya kupata madaraka hayo, uwezekano wa mtu kubadilisha hiba yake huwa ni mkubwa. Sifa zote zilizomwezesha kupanda ngazi hupukutika moja baada ya nyingine na sifa hasi huanza kuchukua nafasi yake.

Kama, mathalani, mtu alikuwa na ushirikiano na wengine, anaanza kujenga tabia ya kupambambana na wanaomzunguka. Majivuno, kiburi, dharau na uonevu vinaanza kuwa sehemu ya maisha yake ya kiuongozi.

Kinachombadilisha

Kimsingi, kiu ya mamlaka humfanya muhusika asijue kile anachokifanya. Hufikiri ili sauti yake isikike, maana yake anahitaji kujikweza awe mbali na wenzake. Mtu wa namna hii ni mwepesi wa kujenga dharau na kiburi na hivyo huwakaripia wanaomzunguka. Katika hatua hii, mtu huyu hugeuka kuwa mnyapara muamrishaji asiyeambilika.

Msingi wa mabadiliko haya ya kitabia ni kule kuona hana sababu tena ya kuwasilikiza waliochini yake. Anaamini kwa namna yoyote watu wa chini yake hawana athari kwake. Huanza kuamini kuwa umbali na hata kutokuelewana na wenzake kunamsaidia kupata heshima na mamlaka yanayostahali nafasi yake mpya.

Hatari ya kubadilika

Ingawa mabadiliko haya yanaweza kuonekana kwa juu juu kama yanamsaidia, katika hali halisi yanaweza kuwa mwanzo wa safari ya anguko lake kwa namna mbili.

Mosi, kujitengenezea maadui wa hiari. Hawa ni watu wanaosikitishwa na vitendo vya kudhalilishwa, kunyanyaswa na kukandamizwa na mtu mwenye madaraka. Kujisikia kudhalilika hujenga chuki inayoweza kuamsha sababu za kupambana naye waziwazi ama kwa siri.

Ni vigumu kwa kiongozi kufanya kazi kwa ufanisi katika mazingira yenye upinzani wa namna hii. Kama kiongozi, anahitaji ushirikiano wa watu kumwezesha kufanya kazi. Watu hawa wanapohujumu juhudi zake hawezi kufika mbali.

Pili, kwa kuwa anajikuta yuko mbali na watu wa kawaida, mtu wa namna hii hujawa woga wa ndani kwa ndani. Hana hakika wanaompiga wanafikiri nini dhidi yake na hivyo hulazimika kujenga ujasiri bandia kwa minajili ya kuwatisha anaohisi wako kinyume nae.

Hatapenda kuona watu wakiongea kwa uhuru, wakijadili mawazo yanayoweza kubainisha mapungufu yake. Ndio maana unakuta viongozi kama hawa makazini huwa hawapendi vikao, hawapendi kuona watu wakikaa pamoja kuzungumza kwa uwazi. Sasa ni woga uliojengeka ndani yake kuwa anapingwa.

Ingawa ndani yake anakuwa na wasiwasi, hadharani hujitahidi kuonesha anajiamini. Utamsikia akisema kwa maneno na vitendo kwamba hana haja ya msaada wa yeyote katika kutekeleza majukumu yake. Matokeo yake ni kujenga sura ya kutokuambilika, kutengeneza makundi ya kimaslahi, na hata kuimarisha visasi na chuki dhidi ya wale anaohisi wanampinga.

Hali ya namna hii huendelea kumsukumizia kwenye maisha ya upweke mbali na watu. Upweke humfanya awe na hasira na watu, hali inayoweza kukomaza kutokuambilika kwake zaidi. Hakuna la maana linaloweza kufanyika kwenye mazingira kama haya.

Heshima kwa unaowaongoza

Kwa kuwa ni dhahiri hakuna kiongozi makini angependa kujikuta kwenye mazingira haya, ni vyema kujifunza kuwa mnyenyekevu. Unyenyekevu ni kuelewa kuwa madaraka hayakufanyi uwe mtu usiye wa kawaida.

Unapopewa madaraka, haina maana unajua kila kitu. Bado unawahitaji watu wa kawaida kukusaidia kufanya kazi yako bila kutumia nguvu. Unapoendelea kuwaheshimu na kuwasikiliza watu hawa unawafanya wawe na msukumo wa ndani wa kukuheshimu.


Makala haya yalichapishwa awali na gazeti la Mtanzania. Fuatilia safu ya Saikolojia kwenye gazeti hilo kila Alhamisi. 

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia