Kanuni Nne za Kufurahia Kazi Yako

Kwa nini unaamka asubuhi kwenda kazini? Kitu gani kinakupa sababu ya msingi ya kwenda kazini?  Ni dhahiri vigezo tunavyovitumia kufurahia kazi haviwezi kufanana. 

Wapo wanaofurahia kiwango kikubwa cha mshahara. Thamani ya kazi inategemea na ukubwa wa kipato. Wengine wanaridhika na kazi inayowajengea hadhi katika jamii. Kazi inayowaongezea hadhi inawapa kuridhika.

PICHA: Dreamstime.com

Pia, wapo wanaoridhika na kazi inayowapa utulivu. Hawa hata kama kazi yenyewe hailipi, wala haiwapi heshima kubwa katika jamii, ikiwa tu inaweza kuwapa uhakika wa kuishi bila kuwa na wasiwasi wa kukosa kazi kesho, wanatulia.

Ingawa kila mmoja ana sababu zake, kwa ujumla, namna gani mwajiri wako amekuwekea mazingira yanayokuwezesha kutekeleza majukumu yako, kwa kukulipa kiwango kinacholingana na thamani yako, kukutambua, kukupa uhakika wa kazi ni baadhi ya mambo yanayoweza kukuongezea furaha ya kazi.

Hata hivyo, tafiti za ajira na kazi zinaonyesha kuwa mtazamo binafsi wa mfanyakazi una nafasi kubwa ya kumwongezea furaha ya kazi anayoifanya. Makala haya yanaangazia kanuni nne unazoweza kuzitumia kufurahia kazi unayofanya na hivyo kuongeza tija yako kazini.

Fahamu kinachokuridhisha

Kuelewa kitu gani kinakufanya uone thamani ya kazi unayoifanya kunaweza kukuongezea furaha ya kazi. Watu wasio na hakika ya kitu mahususi kinachowapa furaha maishani mwao, ni vigumu kuridhika na kazi.

Jiulize, kitu gani kilikuhamasisha kuomba kazi uliyonayo leo? Je, msukumo gani hasa unakufanya uendelee kwenda kazini? Je, usingekuwa na kazi uliyonayo, ungekuwa na furaha zaidi?

Majibu ya maswali haya yanaweza kukusaidia kutathmini kiwango chako cha kuridhika na kazi uliyonayo. Ni dhahiri pia kuwa ari na msisimko wa kazi hupungua kadri mtu anavyoizoea kazi yake. Kadhalika, mahitaji yetu ya kisaikolojia, kiuchumi na kijamii hubadilika kadri miaka inavyokwenda.

Hata hivyo, unapotambua kiwango chako cha kuridhika na kazi, unaweza kuchukua hatua stahiki. Si mara zote unapokosa msisimko wa kazi maana yake uache kazi. Wakati mwingine kubadili namna unavyoitazama kazi yako kunaweza kukusaidia. Kazi unayoona haina maana leo, wapo watu maelfu ambao pengine wanaota siku moja wangeipata. Labda huipendi kwa sababu ya namna unavyoitazama.

Jitambulishe na kazi yako

Ujasiri wa kujitambulisha na kazi yako ya sasa unakusaidia kuipenda zaidi kazi yako. Kufurahia kazi yako ya sasa haimaanishi usiwe na ndoto za kufanya kazi nyingine. Si watu wengi wanafanya kazi walizotamani kuzifanya.

Hata hivyo, kutokuridhika na kazi uliyonayo tayari, kwa kiasi kikubwa, kunaathiri ufanisi wako. Unapokosa furaha na kazi yako, inakuwa rahisi kwako kukosa hamasa ya kuwa mbunifu; hutajituma na inaweza kuwa vigumu kwako kuleta matokeo yanayoweza kukupeleka kule unakotaka kwenda.

Jizoeshe kujitambulisha na kampuni yako. Jione kama sehemu muhimu ya kampuni au taasisi unayoifanyia kazi badala ya kujichukulia kama mpitaji. Kuwa tayari kuitetea kampuni au taasisi yako mbele ya macho ya umma.

Kutokujisikia fahari na kazi unayoifanya kunakuondolea furaha ya kazi. Kadri unavyoendelea kudanganya mahali unakofanya kazi, kwa sababu ya imani kuwa ikifahamika itakupunguzia heshima unayopata kwa kutokufahamika, ndivyo unayokuwa kwenye mazingira ya kukosa amani na hapo ulipo. Fanya kinyume. Jitambulishe wazi wazi hata kama unajua wapo watu wenye mtazamo hasi na aina ya kazi unayoifanya. Kujiamini kutakuongezea furaha.


Kuwa na bidii na ushirikiano

Heshima inayotokana na kazi ya mtu, kwa kawaida, inaongeza furaha ya kazi. Kule kujisikia kuwa mchango wako unatambuliwa, uwepo wako unahitajika, inakupa heshima. Lakini ili uweze kuheshimiwa kazini, unahitaji kujituma. Fanya kazi kwa bidii. Ione kazi yako kama njia halali ya kukusaidia kupata heshima unayohitaji kuwa nayo.

Ni kweli kuwa wakati mwingine unaweza usijikie kujituma kwa sababu labda mazingira ya kazi sio rafiki. Hakuna kazi inaweza kukujengea mazingira yasiyo na kasoro yoyote. Pengine hujioni ukitumia vipaji vyako ipasavyo. Hakuna kazi yoyote unayoweza kuifanya na ikatumia vipaji ulivyonavyo kikamilifu.

Vipaji vyako vinaweza kutumiwa na karibu kila kazi unayoifanya. Labda hujajituma vya kutosha. Ukiweza kujituma kikamilifu kwenye kazi hiyo unayoifanya, unaweza kushangaa namna utakavyotumia vipaji usivyovutumia hivi sasa. Kadri unavyovitumia vipaji vyako, ndivyo utakavyojisikia kuridhika zaidi.

Kadhalika, jenga uhusiano mzuri na wenzako. Mahusiano mabaya kazini yanachangia kuondoa furaha ya kazi. Huwezi kuridhika na kazi inayokukutanisha na watu msioelewana. Shirikiana na wenzako badala ya kushindana nao. Wape msaada wanaouhitaji kukamilisha kazi zao. Kwa kufanya hivyo, utashangaa namna wanavyofurahia kufanya kazi na wewe na hiyo itakuongezea furaha ya kazi.


Rekebisha namna unavyoyachukulia maisha

Mtu asiye na furaha na maisha yake ya kawaida, anakuwa na uwezekano mdogo wa kufurahia kazi yake. Unapokuwa na utulivu na mtazamo chanya na maisha, inakuwa rahisi kwako kuipenda kazi yako. Kinyume chake pia ni kweli. Usipokuwa na furaha na maisha, hutafurahia kazi yoyote utakayopewa.

Tafsiri yake ni kuwa unahitaji kurekebisha mtazamo wako wa jumla na maisha ili uweze kuona thamani ya kazi unayoifanya. Pengine unashindana na watu. Kila unachokifanya unakiweka kwenye mizani ya kile unachofikiri watu wengine wanakifanya.

Pengine unajifikiria mwenyewe kuliko mchango unaoutoa kwa watu wengine. Labda ni wakati wa kufikiri upya. Je, maisha ni kujifikiria mwenyewe? Je, fedha na mali ndilo lengo kuu la maisha? Hakuna kusudi jingine kubwa zaidi ya kupata mahitaji yako ya kila siku?

Pengine vile unavyoyachukulia maisha ndiyo tatizo. Ukibadili mtazamo wako wa jumla wa maisha, unaweza kugundua namna kazi yako ilivyo na thamani kubwa kuliko unavyofikiri.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Mbinu za Kumshirikisha Mwanafunzi Katika Ujifunzaji

Haiba ni nini?