Yatambue Madhara ya Adhabu ya Bakora

INGAWA wazazi wengi huwachapa watoto wakiamini wanafanya hivyo kwa lengo la kuwaadabisha, tulibainisha sababu zilizojificha. Kwa ujumla, tunaweza kusema mzazi aliyelelewa kwa fimbo hujikuta na yeye akiamini fimbo ndio suluhu ya matatizo ya kinidhamu anayoyaona kwa mwanae.

Aidha, mzazi mwenye hasira kwa sababu yoyote, anakuwa na uwezekano mkubwa wa kutumia fimbo anapofikiria kumwadhibu mwanae. Matumizi ya fimbo katika mukhtadha huu, ni namna ya kujisaidia yeye mwenyewe kukabiliana na hasira na msongo wa mawazo na sio kumsaidia mtoto kama inavyoaminika.

Ndio kusema, mzazi anapokuwa na changamoto zinazomkosesha amani, iwe ni hali duni ya kiuchumi, migogoro ya ndoa, kutokuwa na utulivu wa maisha, anakuwa na uwezekano mkubwa wa kutumia adhabu kama namna ya kujituliza bila yeye mwenyewe kughamua.

Kuna jambo muhimu la kuzingatia kabla hatujatazama madhara ya kumwadhibu mtoto. Ingawa watoto wote bila kujali jinsia ni wahanga wa adhabu ya viboko katika jamii, watoto wa kiume huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuchapwa kuliko wenzao wa kike.

Imejengeka imani isiyowazi kuwa adhabu kwa mtoto wa kiume ni lazima iwe nzito na yenye kuleta maumivu zaidi kuliko ile anayopewa msichana. Kwamba unapomwadhibu mtoto wa kiume unaweza kutumia mabavu zaidi kuliko unapomwadhibu mtoto wa kike.

Katika mazingira ya shule, mathalani, watoto wa kike walichapwa viganjani wakati watoto wa kiume walichapwa kwa namna inayowadhalilisha zaidi.

Tunaweza kuwa na tafsiri nyingi kuelezea tofauti hii. Lakini mojawapo, jamii inaelewa maumivu yanayoambatana na mapigo ya fimbo na hutuzitumia kama namna ya kukuza fikra za ubabe na mabavu kwa watoto wa kiume. Fimbo zinakuwa namna fulani ya kuendelea mfumo dume kwenye jamii.

Hata hivyo, viboko vimethibitika kuwaathiri watoto. Tukiachana na madhara ya mwili yanayoweza kutokana na majeraha, yapo matatizo makubwa matatu ya kisaikolojia.

Huharibu uhusiano na mtoto

Adhabu ya fimbo, kama tulivyoona, ina uhusiano mkubwa na hasira anazokuwa nazo mzazi. Tunafahamu mtu aliyekasirika anaweza kufanya lolote ikiwemo kutumia nguvu nyingi kupita kiasi kuliko ambazo angetumia kama angesubiri hasira zipungue.

Upo utafiti mmoja ulioonyesha kuwa mtu mwenye hasira anapopewa nafasi ya kutulia na kupooza hasira zake anakuwa mwepesi kughairi matumizi ya adhabu. Mtu huyo huyo anapotoa adhabu akiwa na hasira, adhabu huwa kali zaidi.

Mara nyingi, mtu anapotumia fimbo hufanya hivyo akiwa na hasira. Kwamba anayeadhibiwa amefanya kosa linalostahili kichapo, hufanya adhabu iwe ya papo kwa hapo. Hakuna kusubiri. Na ilivyo, hawezi kuchapa kimya kimya. Hukazia kichapo anachokitoa kwa maneno ya kushutumu na kulaumu. Lengo ni kuonyesha kuwa amefanya hivyo kwa nia njema.

Matokeo yake adhabu kudhuru uhusiano wa mzazi na mtoto. Mtoto anayechapwa, kwa mfano, hujiona kama mtu asiye thamani kwa mzazi wake hasa kama mzazi hana tabia ya kukarabati mahusiano yake upya na mwanae baada ya kumchapa.

PICHA: parentspartner.com
Vile vile, wakati mwingine wazazi huwachapa watoto wao bila staha. Mtoto huchapwa hadharani mbele ya watu mfano rafiki zake na wadogo zake. Kuchapwa katika mazingira ya namna hii humfanya ajisikie kudhalilishwa na kuonewa. Mtoto hutafsiri kuchapwa kama kutokuthaminiwa na kupewa heshima yake hata kama ni kweli amekosea. Hali hii huathiri uhusiano kati ya mzazi na mtoto.

Pia wazazi wengine hawakumbuki kukaa na watoto baada ya adhabu kufafanua sababu iliyowalazimu kuwachapa na kujadili tabia mbadala. Mzazi mwenye uwezo wa kufanya mazungumzo ya namna hii baada ya fimbo, maana yake angeweza kabisa kuachana na mpango wa fimbo tangu awali. Kwa hiyo, ni nadra mzazi aliyemchapa mwanae kufikiria kurudisha mahusiano baada ya adhabu.

Kukosekana kwa ukaratabu huu baada ya adhabu ya fimbo hufanya watoto waachwe na majeraha moyoni ambayo, pasipo hatua kuchukuliwa, huathiri mitazamo ya watoto na hata namna wanavyowachukulia wazazi wao.

Hukuza tabia ya usugu

Fimbo zina tatizo la kuzoeleka. Kadri inavyotumika kumsababishia maumivu mtoto, ndivyo inavyobidi iwe kali zaidi. Isipokuwa kali na nzito haiwezi tena kuendelea kumfanya mtoto apate maumivu yanayotarajiwa. Kama mtoto alikuwa akichapwa fimbo mbili ndogo, baada ya muda, fimbo mbili hazitshi kumpa wasiwasi. Anajua akikosea, atapata fimbo mbili na mambo yataisha.

Kwa kuwa mzazi hana namna nyingine ya kumrudi mwanae, mtoto hufanya kosa lile lile. Mzazi naye hutumia mbinu ile ile ya kumsababishia mtoto maumivu akifikiri anaweza kumjengea hfu ya kutorudia alichokifanya. Kwa mshangao wake, mzazi anaweza mtoto hufika mahali hatetemeki kama ilivyokuwa awali.

Suluhu inakuwa ni kuongeza mapigo ili kutengeneza woga unaoonekana kupotea. Kadri mapigo yanavyozidi kuongezeka na kuwa makali zaidi, ndivyo adhabu inavyoendelea kupoteza maana yake na kugeuka kuwa ugomvi kati ya mzazi na mtoto.

Watoto wanaozoea hali ya kupigwa, ni watu sugu hata katika mahusiano yao na watu wengine. Wengi wanapokuwa watu wazima hukosa uwezo wa kujua hisia za wengine kwa sababu wamekulia kwenye mazingira yaliyowazoeza kupuuza hisia zao wenyewe.

Hufundisha Ubabe

Fimbo humfundisha mtoto kutumia nguvu katika kutatua migogoro anayokutana nayo. Watoto wanaochapwa, mara nyingi huwa ni wagomvi katika maisha halisi. Hujikuta wakiwa na mazoea ya kupigana na wenzao na hata watu wengine kama namna ya kutatua matatizo yao.

Tabia ya ugomvi anakuwa amejifunza kwa wazazi wake mwenyewe. Amemwona baba akishika fimbo kushughulikia tatizo yanayojitokeza na yeye atamshika shati mtu mwingine anayemkosea. Hawezi kuona njia nyingine bora zaidi. Mtoto wa nyoka anaendelea kuwa nyoka.


Matokeo ya mazoea haya ni kumfanya awe mtu wa mabavu, mchokozi kwa wenzake, asiyeweza kuelewa hisia za wengine na mwisho wake na yeye wenyewe hugeuka kuwa mtu anayeunga mkono fimbo kwa watoto wake. Ni namna fulani ya kuridhisha utamaduni wa ubabe.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu