Namna ya Kujenga Uhusiano Mzuri na Wafanyakazi Wenzako -1

PICHA: tovoy.se

Moja ya sababu zinazowafanya wafanyakazi wengi wakose ari ya kazi ni mahusiano mabaya na watu kazini. Kimsingi, tafiti nyingi zinabainisha kuwa, mbali na kutokuridhishwa na maslahi ya kazi zao, wafanyakazi wengi hufikia huacha kazi kwa sababu ya kutokuelewana na watu kazini.

Unapokuwa na watu wengi ofisini kwako wasiofurahia kukuona; watu wanaokerwa na kazi nzuri unazozifanya; watu wanaokuonea wivu; watu wanaojenga uadui na wewe, ni rahisi kukosa amani na mazingira ya kazi unayoifanya. Kukosa amani kazini kunakuondolea ujasiri na uchangamfu wa kuchangamana na wenzako. Hali hii, kwa kiasi kikubwa, inaweza kupunguza ufanisi wako kazini.

Kama ilivyo mitaani, wapo watu kazini huwezi kuwaridhisha. Unaweza kufanya jitihada za kuwatendea yaliyo mema lakini bado wakakuchukulia kama adui.  Pamoja na hayo, ni vizuri kuelewa kuwa si mara zote watu hujenga chuki na wewe kwa sababu tu hawakupendi. Wakati mwingine, tabia ulizonazo zinaweza kuchochea hisia za wivu, uadui na hata mashindano yanayoweza kuathiri mahusiano yako na watu.

Katika makala haya, tunajifunza tabia mbili zitakazokusaidia kuwa na uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzako. Ukizisoma kwa haraka unaweza kuzichukulia kama mbinu za kucheza na akili za watu. 

Hata hivyo, ukiweza kuzifanya zikawa sehemu ya maisha yako ya kila siku, zitakujengea tabia ya unyenyekevu unaoanzia ndani na zitakupunguzia misuguano isiyo na msingi katika mazingira yako ya kazi.


Wafanye watu wajione wanakuzidi

Kwa kawaida tunapenda kujisikia tunawazidi watu. Kupenda kuwazidi wengine ni moja wapo ya misikumo iliyojificha nyuma ya mengi tunayoyafanya. Tunapojiona tuna hadhi ya juu kuliko wengine, hiyo peke yake inatosha kutupa namna fulani ya utoshelevu wa nafsi.

Katika mazingira ya kazi hisia hizi za kuzidiana hazikosekani. Watu huweza kushindana kimya kimya kwa viwango vya elimu; utendaji wa kazi; tija waliyoiletea taasisi na mambo mengine kama hayo.

Unapoingia kwenye mfumo wa kazi, unajikuta bila wewe kujua, ukiwa sehemu ya mfumo huu wa mashindano yasiyo rasmi. Msisimko wa kuanza kazi mpya unaweza, mathalani, kukusukuma kutaka kuthibitisha kuwa wewe ni mtu mwenye uwezo pengine kuliko wengine. Vyeti ulivyonavyo vinaweza kukupa kiburi cha kujiona kuwa wewe ni mtu bora na mweledi kuliko wengine wote uliowakuta kazini.

Wakati mwingine, hutokea ukalazimika kuwajibika kwa mtu asiye na sifa kama ulizonazo. Kwa kuwa unataka kuonekana bora, unajisikia kufedheheka nafsi. Unatamani kuwaonyesha watu hapo ofisini kuwa unamzidi mkuu wako wa kazi.

Ukikubali hali hiyo ya kujiona unawazidi watu, utajitengenezea mazingira ya kupishana na watu bila sababu. Utajikuta ukiongea kama mtu anayejua kila kitu. Utashauri mahali ambapo ushauri wako haujaombwa. Utafanya mambo kwa papara ili tu uonekane unaweza. Hutakuwa tayari kujifunza kwa wengine. Haya yote yatakutengenezea ufa wa kimahusiano kati yako na wenzako na utajiweka kwenye hatari ya kutengwa kimya kimya.

Unahitaji kubadilisha mtazamo. Mosi, sahau imani uliyonayo kuwa ‘najua…hawa wengine hawajui.’ Mengi uliyojifunza shuleni ni nadharia tu zinazoweza kushindwa kukidhi matakwa ya uhalisia wa kazi. Kimsingi, mazingira ya kazi ni darasa jipya linalokulazimu kuwa mwanafunzi endelevu.

Ukishaelewa hivyo, utafanya jitihada za kujenga taswira ya mtu asiye na ujuaji. Fanya kazi kwa ushirikiano na wenzako. Weka mazingira ya makusudi kuomba msaada kwa watu wanaokuzidi uzoefu. Lakini fanya hivyo kwa uangalifu bila kuwafanya watu waanze kuwa na wasiwasi na uwezo wako.  

Sambamba na hilo, usiwe mwepesi wa kushauri kama ushauri wako haujahitajika. Unapomshauri mtu ambaye hajakuomba ushauri, anakuona mjuaji. Akikukuona hivyo, hutaweza kufanya nae kazi kwa ufanisi. Badala ya kupenda kushauri, jenga weledi utakaowafanya watu wakufuate wenyewe kwa ushauri.

Ukiweza kufanya hivyo, watu hawatakuwa na sababu ya kukuonea wivu, kushindana na wewe kwa sababu huonyeshi mashindano yasiyo ya lazima. Badala yake watakuchukulia kama rafiki asiye  mshindani. Utajipunguzia maadui na mapambano yasiyo ya lazima.

Wasaidie watu kufikia malengo yao




Ni dhahiri nafasi uliyopewa kazini inakutarajia kufikia malengo fulani. Labda ni kuongeza uzalishaji wa kampuni. Labda ni kupunguza malalamiko ya wateja au hata kuongeza siha ya bidhaa mnazozalisha. Hayo, kwa hakika, yanakuwa ni malengo yako rasmi kikazi. Ndiyo dira ya shughuli unazotarajiwa kuzifanya kama mfanyakazi wa taasisi iliyokuajiri.

Vile vile, unaweza kuwa na malengo yako binafsi. Mfano, unatamani kupanda cheo baada ya muda mfupi; kujenga heshima kazini kwako ili ufikie malengo yako binafsi. Si jambo baya kuwa na malengo yako kama mfanyakazi anayejitambua.

Unapofanya hivyo, hata hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa kila mfanyakazi naye ana malengo yake. Wakati mwingine malengo yako yanaweza kuingilia na malengo ya mwingine. Kwa kuwa watu wana tabia ya kujipenda, unapoonekana unatishia malengo yao, unaweza kujikuta kwenye mgogoro usio rasmi.

Ukifanya kosa la kuonyesha wazi wazi kuwa unajijali wewe na malengo yako, tena wakati mwingine ukiwatumia wao, utapoteza watu wengi. Watu, kwa kawaida, hawapendi mtu anayejifikiria yeye muda wote. Wakigundua unafikiria maslahi yako mwenyewe, watajitenga na wewe kimya kimya. Mazingira ya namna hii yatakuletea matatizo mbeleni.

Badala yake, jaribu kudhibiti ubinafsi wako. Fikiria namna unavyoweza kuwasaidia wenzako kufikia malengo yao. Unapowasaidia kufikia malengo yako, unawajengea hali ya kukuhitaji.

Chukulia, kwa mfano, umebaini kuna mwenzako anapata shida kuandaa ripoti na wewe ujuzi huo unao. Jitolee kumsaidia afanikiwe. Ujisikie vibaya kuwa atafanikiwa. Kufanikiwa kwake, kutakuwa akiba kwako. Siku nyingine mtu huyo huyo atajisikia kudaiwa fadhila kwa kukusaidia na wewe.

Jambo la kukumbuka ni kuwa katika kuwasaidia wengine kufikia malengo yao, unaweza kujikuta wakati mwingine watu wakijipatia sifa kwa mgongo wako. Usiumie wala kujiona umetumika. Huo ni uwekezaji unaolipa. Kwanza, watu hao watadaiwa kukulipa fadhila siku ukihitaji msaada wao. Lakini pili, kwa kuwasaidia, unawafanya wasiwe na sababu ya kushindana na wewe.

Makala haya yalichapishwa kwanza kwenye Jarida la Ajira na Kazi, linaloandaliwa na gazeti la MWANANCHI. Itaendelea Ijumaa ijayo.

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Pay $900? I quit blogging