Shirikiana na Mtoto, Usishindane Nae

Tunaendelea kujibu swali linaloulizwa na wazazi wengi, ‘kwa nini watoto hukosa adabu?’ ‘Kwa nini wakati mwingine watoto hawasikii hata pale wanapoadhibiwa?’ ‘Inakuwaje mtoto anakuwa na nidhamu mbele ya mzazi lakini akiwa mbali na mzazi anakuwa na tabia nyingine?’

Jibu la maswali haya ni mjadala mrefu. Hata hivyo, tumejaribu kuonyesha kwamba mtoto kukosa adabu haitokei kwa bahati mbaya. Kwanza, hazaliwi na msukumo wa kushindana wala kumkosea adabu mzazi. Badala yake, huzaliwa na fahari ya kumpendeza na kushirikiana na mzazi. Kwa mfano, mtoto hufurahia mzazi anapocheza nae, anapomkumbatia, anapomrusha rusha kwa furaha na hata anapomtania.

PICHA: Atum Azzahir

Matendo yanayoimarisha ukaribu huu na mzazi, kwa kawaida, humsaidia mtoto kujisikia salama. Anakuwa hana sababu ya kuwa na wasiwasi na usalama wake akiamini wanaomzunguka ni watu wanaoaminika. Utulivu wa namna hii hujenga ari ya kushirikiana na mzazi inayomfanya kuwa msikivu.

Lakini kadri mtoto anavyokua kimwili, mara nyingi mzazi hupunguza jitihada za kushirikiana nae. Kama alizoea kucheza nae, anaanza kusita kufanya hivyo. Wakati mwingine, mtoto mwingine huzaliwa. Mzazi huyu hujikuta akitumia muda mwingi kumpa ushirikiano mtoto mchanga aliyeongezeka kwenye familia. Jitihada hizo za kumfurahia mtoto mchanga hufanyika katika mazingira ambayo mtoto ‘mkubwa’ anayeanza kujisikia umbali na wazazi wake, akishuhudia.

Hali kama hizi, zinamjengea uhitaji mkubwa wa ndani kwa ndani. Mtoto anakuwa na shauku ya ukaribu usiopatikana. Ukaribu unapokosekana huchochea jitihada za kuziba pengo. Moja wapo ya jitihada hizi ni kufanya vituko ambavyo mzazi anaweza kuvitafsiri kama kukosa nidhamu.

Ni vizuri kutambua kuwa mtoto anapofanya hivyo, nia yake hasa si kumuudhi mzazi. Hapana. Hawezi kutaka kumuudhi mzazi kwa sababu, kwa asili, ana shauku ya kushirikiana nae.

Usipuuze hisia za mwanao

Kama tulivyoona, mara nyingi mtoto hutafsiri yale anayotendewa kwa namna inayoweza kuwa na upotofu. Unaweza kufanya kitu kidogo pasipo nia mbaya. Labda umeahidi zawadi na hujatekeleza. Labda umemkejeli mbele ya wenzake. Labda umemwambia mtoto mwingine maneno mazuri na hujamwambia yeye. Kwako uliye mtu mzima, huoni tatizo. Kwa kujua hukuwa na nia mbaya, unaweza ukaamua kupuuza vile anavyojisikia mtoto kwa sababu unajua hayo anayoyafikiri hayana ukweli wowote.

Jambo la kuzingatia ni kuwa hisia hata kama zimejengwa kwenye dhana potofu zinaathiri kwa kiasi kikubwa mtazamo wa mtoto. Mtazamo potofu huongoza maamuzi potofu anayoyafanya mtoto. Mathalani, mtoto anayeamini hapendwi hata kama kiukweli anapendwa atakuwa tayari kushindana na mzazi. Kushindana na mtoto mwenye mtazamo potofu kunaweza kuchangia kukuza tabia mbovu.

Makala haya yanalenga kusisitiza umuhimu wa kuvaa viatu vya mtoto na kuelewa hisia zake, anafikiri nini, anaamua nini na kwa sababu gani. Hata hivyo, katika kufanya hivyo, ni muhimu kuchukua tahadhari tatu kubwa. Kuepuka kumdekeza mno mtoto, kumdhibiti na kumwadhibu kupita kiasi.

Kumdekeza mtoto

Kudekeza ni kumlinda mtoto kupita kiasi kwa lengo la kumfanya ajione mtu mwenye umaalum usio wa kawaida. Wazazi wenye mtoto mmoja, mathalani, wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kumchukulia mtoto kwa umaalum. Mtoto anayedekezwa hufikia kujiona bora kuliko watu wengine.

Unapomdekeza mwanao kumbuka kuwa unatengeneza hatari ya kumfanya aamini usalama wake unategemea kiasi gani anajidekeza kwako. Pia, anaweza kujiona mtawala anayeweza kuwaendesha wengine atakavyo yeye.

Kwa upande mwingine, mtoto huyu ana uwezekano mkubwa wa kushindwa kufanya vitu vingi bila msaada wa mtu mwingine, upungufu unaoweza kufanya maisha yake yawe magumu pindi atakapoondoka nyumbani.

Ili kuepuka kumdekeza mtoto, punguza kumwonea huruma. Mpe nafasi ya kukabiliana na magumu na hata ikibidi kuumia kidogo kwa lengo la kujifunza maisha halisi. Usimnyime mwanao maumivu, lakini pia usimwumize bila sababu.


Kumdhibiti kupita kiasi

Kumdhibiti mtoto ni kumwongoza kupita kiasi na kutompa nafasi ya kushiriki kufanya maamuzi. Kila anachofanya mtoto ni matokeo ya amri zisizotoa nafasi ya majadiliano. Atakwenda wapi, asoma nini, atapenda nini, yote hayo ni juu ya mzazi.

Mtoto anayedhibitiwa namna hii anaweza kuonekana ni mtu mwenye nidhamu kwa nje. Lakini kama mwanadamu mwingine, ndani yake kunakuwa na kiu ya kujiona ni mtu mwenye maamuzi na maisha yake. Mtoto huyu anapopata nafasi ya kufanya vitu vyake mara nyingi hufanya makosa mengi.

Papara ya maamuzi ambayo mara nyingi huwa kinyume na matakwa ya wazazi, inatokana na ukweli kuwa hajiamini. Hajajengewa kuuamini uwezo wake ingawa ndani kunawaka shauku ya kuthibitisha kuwa anaweza kufanya maamuzi.

Ili kukabiliana na athari za kumdhibiti mno mwanao, jitahidi kumpa uhuru wenye mipaka kulingana na umri wake. Mpe nafasi ya kufanya maamuzi yanayolingana na umri wake. Nafasi yako kama mzazi ibaki kuwa kumhakikisha usalama wake na kuhakiki maamuzi yake.
Unavyomwadhibu

Mtoto anapoanza kushindwa kushirikiana na wazazi, ni kawaida kwa mzazi kutumia adhabu. Mfano, kumkemea, kumfokea, kumchapa, kumfinya na hata kumnyima vile anavyovihitaji.

Lakini unapomwadhibu hususani kwa adhabu kali, mtoto hujenga dhana potofu. Kwake, adhabu maana yake ni ‘naonewa, sieleweki.’ Hisia hizi mara nyingi huambatana na woga wa kuogopa adhabu, hali inayoweza kumfanya alazimike kufanya vitu anavyojua vinahitajika hata kama havianzii ndani yake.

Mtoto anayeadhibiwa mara kwa mara, hujenga sura isiyo yake kwa lengo la kumridhisha mzazi. Sura hii inaweza kupotea atakapokuwa mtu mzima, au atakapoondoka nyumbani na kuanza kujitegemea.

Upande mwingine wa adhabu ni mtoto huanza kujenga hisia za kisasi ndani yake. Anaweza kufanya vitu kwa lengo la kushindana na matokeo yake kuathiri ukaribu wake na mzazi.

Ni vyema kutumia adhabu kama njia ya mwisho ya kumsaidia mwanao. Mwadhibu mtoto kwa upendo, na rudisha uhusiano baada ya adhabu. Kadhalika, usijenge mazoea ya kumwadhibu mwanao ukiwa na hasira.


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Fumbo mfumbie mwerevu

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3