Fanana na Unayetaka Asikilize Nasaha Zako

Fikiria mtoto amekuwa na tabia ya kufanya vibaya darasani. Wewe kama mzazi hupendi hali hiyo. Ungetamani mtoto afanye vizuri. Kwa shauku hiyo, unaona uongee na mwanao kumhamasisha afanye juhudi kwenye masomo.

Unamwambia, 'Hebu jitahidi mwanangu. Alama hizi unazopata hazifai. Mimi sijawahi kupata alama hizi. Nilipokuwa na umri kama wako, nilikuwa na bidii sana kwenye masomo. Kwa sababu ya kufanya bidii, siku zote nilishika nafasi kati ya nambari moja na tatu darasani!'

Lengo ni jema kabisa. Unachofikiri hapo ni kuwa mwanao akisikia simulizi la mafanikio yako, atahamasika na kuanza kujitahidi. Unafikiri uwezo wako unaweza kumtia hamasa kijana. Inawezekana ikawa hivyo. Lakini mara nyingi mambo huwa kinyume.

Unapomwambia kijana namna ulivyokuwa ukifanya vizuri, unaweza kuibua hisia mchanganyiko. Kijana wako anaweza kusikia ujumbe tofauti na huo. Kichwa chake kinaweza kuchakata taarifa tofauti kabisa. Ujumbe huo huo ukasikika, 'Mimi baba yako nilikuwa mtu mwenye akili sana. Nashangaa kwa nini wewe ni mjinga kiasi hiki.'

Tafsiri hiyo inafanya nafsi ya mtoto ijisikie kudhalilika. Hakuna mtu anapenda kujisikia dhalili. Ili kukabiliana na udhalili huo, mtoto anafikiri, 'Huyu mzee anajiona kichwa sana. Hapa ameniita kunizodoa tu. Sasa nitakachofanya ni kuachana nae. Kwanza haelewi mambo yalivyo magumu shuleni siku hizi.'


Kufanana ni kuvaa viatu vyake

Kwa kawaida, watu wanavutiwa na wale wanaofanana nao; wanaoishi maisha kama yao; wenye changamoto kama zao. Hujisikia vizuri kuona mtu anayewashauri, anaelewa maisha yao, yuko kama wao.

Ni vigumu kumvutia mtu unayemwonesha ulivyo tofauti nae. Unapomfanya ajione tofauti na wewe, labda kwa kuwa na uwezo asionao yeye, anakata mawasiliano na wewe. Akiisha kukata mawasiliano hayo, anawasha taa itakayomsaidia kumwulika ujumbe wako kwa kuukosoa; kuubatilisha ili kuhalalisha kwa nini yeye anapata matokeo tofauti na hayo unayomsimulia. Matokeo yake hawezi kufurahia kuusikiliza hata kama ujumbe wako ungemsaidia.

Usijitofautishe

Nasaha na ushauri mwingi mzuri hukosa kibali kwa walengwa. Wanaoshauri hutumia nguvu nyingi kujitofautisha na wanaolengwa. Tofauti hiyo inakaribisha shughuli ya ujumbe huo kupigwa.

Mfano, mzazi anaongea na vijana wenye changamoto za mahusiano ya ujana. Pengine kwa kufikiri anaweza kuwahamasisha, anatumia muda mwingi kusimulia namna yeye alivyokuwa na 'ujana mtakatifu.' Vijana hawa ambao tayari hawana huo utakatifu, wanajisikia dhalili. Hawatamsikiliza. Fikra zao zitakata mawasiliano na kuanza kuhoji yasiyolengwa. Watahoji ukweli wa yanayosemwa; tofauti ya mazingira ya wakati huo na haya waliyonayo wao na kwa kweli uwezekano wa wao kupokea ujumbe huo ni mdogo.

Kumwelewa unayemshauri

Vijana hawa ambao tayari wanaishi kwenye changamoto wanahitaji mzazi mwenye ujasiri wa kwanza, kuelewa mazingira yao na waamini kuwa anaelewa. Pili, ili wamwamini mzazi huyu anahitaji kuwa na ujasiri wa kuwaambia namna yeye mwenyewe alivyokuwa kama wao lakini akajifunza kushinda changamoto hizo kama zao.

Kijana mwenye changamoto anapoyaona maisha yake kwa mzazi huyu, atafungua moyo wake kujifunza kwa vipi anaweza kuiga mbinu za kufanikiwa. Ndio kusema, mapungufu, makosa na udhaifu vikisemwa vizuri vinaweza kuwa na nguvu ya kumbadilisha mtu kuliko masimulizi ya mafanikio.


Kwa wazazi, kama kweli unataka kijana wako ahamasike kuchukua hatua za kubadilisha tabia yake, huna sababu ya kumsimulia namna ulivyokuwa bora kuliko yeye. Mfanye ajione kwenye maisha yako. Atahamasika kubadilika.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?