Umuhimu wa Kujenga Tabia ya Kujitolea

Kujitolea ni kutoa sehemu ya muda wako, ujuzi na maarifa uliyonayo na wakati mwingine nguvu zako kufanya kazi ya watu wengine bila kupata malipo ya moja kwa moja. Kazi unayoifanya kwa kujitolea mara nyingi ungeweza kuifanya kwa kudai ujira lakini unaamua kuifanya bure.  Mathalani, mwajiriwa anayetamani kuleta mabadiliko nje ya ajira yake, anapotumia ujuzi wake kufanya kazi za jamii bila kudai malipo, anakuwa amejitolea. Tuangalie kwa mhutasari kwa nini ni muhimu kujenga tabia ya kujitolea.


PICHA: jimmyscambridge.net
Kusaidia kutatua matatizo ya jamii

Maisha ni zaidi ya fedha. Mtazamo huu unaweza kuzua mjadala mrefu kutokana na tofauti za kimatazamo, lakini upo ukweli kwamba fedha si kila kitu. Hatuishi kwa lengo la kujikusanyia fedha kujiletea faida binafsi na iishie hapo ingawa ni kweli tunahitaji fedha.  

Kujitolea, kwa mantiki hii, ni kuelewa kuwa si lazima ubadilishane ujuzi na muda wako kwa vipande vya fedha. Wakati mwingine waweza kutoa ujuzi, maarifa na nguvu zako kwa lengo tu la kujisikia furaha ya kutoa mchango wako katika kuboresha maisha ya wengine ambao katika hali ya kawaida wasingeweza kunufaika na ujuzi huo bila kukulipa.

Mhitimu wa chuo cha ualimu, kwa mfano, wakati akisubiri ajira ya ualimu anaweza kuamua kuomba kujitolea kufundisha katika shule ya kata iliyoko kijijini kwake bila malipo anayostahili. Kwa kujitolea huko, kijana huyu anajisikia kutoa mchango muhimu katika kukabiliana na tatizo sugu la ukosefu wa walimu kijijini kwake badala ya kusubiri wengine watafute majibu ya tatizo hili.


Kujifunza ujuzi bila gharama

Si kila ujuzi tunaouhitaji makazini tunaupata vyuoni. Mara nyingi vyuo hutufunza maarifa ya jumla yanayoweza yasioane kabisa na matakwa ya soko la ajira. Hii ni kwa sababu si rahisi vyuo kufanya utafiti wa mara kwa mara kubaini mahitaji ya soko la ajira kwa minajili ya kurekebisha mitaala yao.

Kadhalika, ni vigumu kwa mfumo wa elimu kukidhi mahitaji mahususi ya kila mhitimu na kila mwajiri. Kwa sababu hiyo, vyuo hujikuta vikifundisha maarifa ya jumla ambayo katika hali halisi yanaweza yasikidhi mahitaji ya waajiri.

Katika mazingira haya, kujitolea hutusaidia kujifunza ujuzi mahususi tunaouhitaji ili kuajirika kirahisi  bila kulazimika kuulipia kwa fedha isipokuwa kwa kutumia nguvu na muda wetu. Kwa mfano, mhitimu wa teknolojia ya mawasiliano anaweza kujitolea kufanya kazi katika kampuni ya mawasiliano na hivyo kujifunza mambo mengi ambayo huenda hakujifunza akiwa chuoni. Kwa kutoa muda na nguvu zake bila kutarajia malipo, mhitimu huyu hupata faida ya kujiongezea nafasi ya kuajirika pale nafasi za kazi zinapojitokeza.

Kujitafutia uzoefu unaohitajika

Waajiri wengi huweka sharti la waombaji kuonesha uzoefu wa kazi wanayoiomba kama ushahidi wa uwezo wa kumudu kazi husika. Hiki, kwa hakika, ni kikwazo kwa waombaji wengi hasa wanaotoka vyuoni moja kwa moja kwa sababu ni kweli huwa hawajawahi kuajiriwa na hivyo hawana uzoefu. Pamoja na ugumu wa sharti hili la uzoefu, bado litaendelea kuwa sehemu muhimu ya matangazo ya ajira. 

Kuwasaidia wasioweza kukulipa kunakupa furaha PICHA: goingabroad.org
Kujitolea kwaweza kuwa sehemu ya suluhisho la sharti hili. Unapojitolea bila malipo, unajitengenezea uzoefu utakaouhitaji na mwajiri bila kulazimika kuajiriwa. Kujenga tabia ya kujitolea ni kuchukua hatua za makusudi kupambana na sharti hili. 

Kwa kutokutambua umuhimu wa kujitolea, wahitimu wengi wamekuwa walitumia muda mwingi kulalamikia sharti la uzoefu wakati katika hali halisi hawafanyi chochote kukabiliana na changamoto hiyo. Wanabaki kusoma magazeti na kuulizia nafasi za kazi ambazo hata wanapoomba wanajikuta hawakidhi vigezo vya uzoefu

Ni vyema kutambua kuwa waajiri huvutiwa na mwombaji kazi aliyetayari kujitolea. Mwombaji mwenye historia ya kujitolea muda na ujuzi wake kuwanufaisha wengine anakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushindana na wenzake wasiojitolea. Kujitolea kwaweza kuwa namna ya kuongeza uwezekano wa kuajirika.

Kujiongezea mtandao wa kiajira

Katika siku za leo, mtandao wa kiajira ni hitaji muhimu. Mtu anayefahamiana na watu wengi kwenye maeneo mbalimbali ya kikazi anajiongezea fursa ya kuunganishwa na taarifa za kiajira. Siku hizi wanasema watu ni mtaji.

Aina ya mitandao ya kiajira tunayoijenga, mara nyingi hutegemea tunafahamiana na watu  wa aina gani. kwa hiyo si kazi nyepesi, kwa mfano, kijana anayetoka kwenye familia za tabaka la chini kijijini kufahamiana na watu wengi mjini wanaoweza kumpa taarifa za kiajira anazozihitaji. Ili kupata taarifa hizo muhimu kijana huyu hujikuta akitumia nguvu nyingi sana zisizolingana na matokeo.

Kujitolea kwaweza kumsaidia mtafuta ajira wa aina hii kujiongeza kimtandao. Unapokuwa tayari kufanya kazi za kujitolea kwa bidii na maarifa katika maeneo mbalimbali, mathalani, unakutana na watu wa kada na wenye uzoefu tofauti. Ingawa ni kweli hupati kipato unachokihitaji (sana) kwa wakati huo, lakini bado unakuwa na fursa ya kujitengenezea mtandao muhimu wa watu wanaoweza kukufaa katika safari yako ya kutafuta ajira.

Changamoto za kujitolea

Pamoja na faida za kujenga utamaduni wa kujitolea, zipo changamoto kadhaa. Kwa mfano, zipo taasisi za kinyonyaji zinaopenda kutumia nguvu za watu bure kwa mwamvuli wa kujenga utamaduni wa kujitolea. Taasisi hizi hutumia shida za watu wasio na ajira kutafuta nguvu kazi itakayowawezesha kufikia malengo yao bila gharama kubwa ya kifedha (cheap labour). Ni vizuri kutambua 'unyonyaji' wa taasisi zenye tabia hii na kufanya maamuzi sahihi yatakayokunufaisha na wewe kiujuzi na kiuzoefu. Tuliwahi kuaswa na kiongozi mmoja kuwa wakati mwingine ni lazima kukubali kupoteza kidogo ili kupata.

Kadhalika, upo mtazamo hasi dhidi ya kujitolea. Wapo wanaofikiri kujitolea ni kutokuwa na kazi ya kufanya. Katika mazingira yaliyojaa umasikini, ni vigumu watu kuelewa inakuwaje mtu anaweza 'kupoteza muda wake' kujitolea badala ya kuchapa kazi zinazomwingizia kipato. Wengine wanafikiri  kufanya kazi bila malipo ni kujidhalilisha utu wako. 

Hata hivyo, tunaweza kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto hizi kulingana na mazingira yetu yalivyo ili tuweze kufikia malengo yetu kwa wepesi. Kwa mfano, yako maeneo mengi tunayoweza kujitolea bila kukabiliana na vizuizi vingi. Kuna shule zisizo na walimu katika kila pembe ya nchi yetu, zipo taasisi nyingi zisizojiendesha kibiashara zinazojaribu kusaidia kutatua matatizo mbalimbali katika jamii yetu. Tunaweza kutumia taasisi hizi kama  kianzio muhimu cha kujenga ari ya kujitolea.

Waajiri nao, kwa upande wao wanahitaji kubadilisha mitazamo yao na kuweka mazingira yanayoruhusu wenye nia ya kujitolea kupata fursa hiyo. Kwa kufanya hivyo, wanatoa mchango wa kujenga daraja zuri linaunganisha maarifa ya darasani na hali halisi na hivyo kujenga ujuzi ambao wao wenyewe wanalalamika kuwa wahitimu hawanao.

Tuone fahari kujitolea 

Ni muhimu kwa jamii yetu kujenga tabia ya kujitolea. Tujitolee kuwasaidia wengine. Tujitolee muda na raslimali tulizo nazo kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu. Upo ukweli wa kiutafiti kwamba unapowafanya wengine wawe na furaha, unakuwa na furaha zaidi. Unapochangia kutatua changamoto za wengine, unajiwekea akiba ya mbeleni. Tuache hulka za kimaskini kwamba kila unalolifanya lazima likuingizie fedha. Hatuwezi kubadilisha mambo mengi kwa ujira.

Soma gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa mada kama hizi kwenye safu ya Saikolojia.

Maoni

 1. Safi sana sir Bwaya!! Mungu akuongoze na kukupa nguvu katika kuelimisha umma!! I appreciate you!!!

  JibuFuta
 2. Safi sana sir Bwaya!! Mungu akuongoze na kukupa nguvu katika kuelimisha umma!! I appreciate you!!!

  JibuFuta
 3. PROMO DELIMA
  poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

  Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
  Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

  Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
  Livechat_____: delimapoker
  BBM__________: 7B960959
  Facebook_____: delimapoker
  Phone number_: +85595678845
  pendaftaran___

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu