Kujenga Tabia ya Kusoma kwa Watoto Wadogo

Kusoma si tabia nyepesi kuijenga katika mazingira ambayo masimulizi na mazungumzo ni vyanzo vikuu vya maarifa kuliko maandishi. Tumelelewa katika utamaduni usiosisitiza sana umuhimu wa kusoma. Lakini, hata hivyo, hatuwezi kukwepa kusoma katika ulimwengu huu unaotulazimisha kuyasaka maarifa kwa njia ya maandishi.

Kadhalika, mafanikio ya mtoto kitaaluma yana uhusiano wa moja kwa moja na utamaduni wa kujisomea. Mtoto asiyependa kusoma anajiweka katika hatari ya kuwa na mafanikio dhaifu kielemu kwa sababu, katika mfumo wa elimu, kusoma si uamuzi binafsi.

Kwa hivyo, ikiwa tunatamani watoto wetu wafanikiwe kielimu sambamba na kujenga utamaduni wa kujisomea bila kushurutishwa, tunao wajibu mkubwa wa kuwajengea utamaduni huo tangu wangali wadogo. Katika makala haya tunaangalia mbinu nne rahisi zinazoweza kuwasaidia watoto wetu kupenda kusoma.

Kuweka mazingira ya kujisomea

Mazingira yanayohamasisha kujisomea ni pamoja na kuhakikisha vitabu vinapatikana nyumbani. Tafiti zinaonesha kuwa watoto wanaokulia katika mazingira yenye vitabu, wana uwezekano wa kuvipenda kuliko wenzao waliokulia katika mazingira yasiyo rafiki kwa maandishi. Mtoto anapoona vitabu nyumbani tangu akiwa mdogo huamini vitabu ni sehemu ya maisha yake ya kila siku.

Kwa kutambua ukweli huo, mzazi anaweza kukusanya vitabu, magazeti, majarida na machapisho mbalimbali na kuyatunza katika sehemu maalum inayoonekana kirahisi nyumbani. 

Sambamba na hilo, tunaweza pia kupunguza muda wa watoto kutazama televisheni. Ni vigumu kudhibiti maudhui ya vipindi vya televisheni lakini tunaweza kudhibiti namna chombo hicho kinavyotumika vyumbani. Kwa hiyo badala ya watoto kukaa muda mwingi wakitazama yanayoendelea kwenye televisheni, tunaweza kuwa na utaratibu maalum wa kutazama mambo yanayofahamika katika chombo hiki. Udhibiti wa televisheni unapokwenda sambamba na upatikanaji wa vitabu vinavyomvutia mtoto, ni rahisi kujenga mazoea mapya ya kupenda maandishi.

Kuwa mfano kwa kusoma

Hatuwezi kumfundisha mtoto tabia ambayo sisi wenyewe hatuna. Kama tunataka mtoto apende kusoma, tunashauriwa sisi wenyewe tujifunze kupenda kusoma. Ni hivyo kwa sababu, kwa kawaida, mtoto hujifunza kwa kile anachokiona mzazi akikifanya kuliko anachokisema. Tunapoonekana tukisoma mara kwa mara, ni rahisi mtoto kuiga mazoea hayo.

Ni mara ngapi sisi wazazi tumeonekana nyumbani tukisoma hata kipande cha gazeti? Mara ngapi watoto wametuona tukisoma biblia, kwa mfano? Sababu rahisi mara nyingi ni kukosekana kwa muda. Inavyoonekana ni kwamba ingawa wazazi hatuna muda wa kusoma bado tuna matarajio makubwa kwa watoto wetu kuwa ni lazima wasome kwa bidii.

lakini hata kama hatuna kawaida ya kusoma, hatulazimiki  kusoma vitabu tusivyovipenda kwa lengo tu la kuigiza utamaduni tusiouzoea. Kuna magazeti, majarida na vitabu rahisi ambavyo kila mzazi anaweza kuvisoma awapo nyumbani akitaka. Tabia zote zinajengwa. Tunaweza kuanza na magazeti na baadae tukaanza kusoma vitabu mbalimbali bila kujisikia adhabu.

Kadhalika, vipo vitabu vya lazima kiimani, ambavyo kwa hakika hatuwezi kuwa waamini imara bila kujenga tabia ya kuvisoma. Ni jambo jema kwa mtoto kuona tukivisoma tuwapo nyumbani. Anapoona sisi wenyewe tukisoma Biblia, ni rahisi na yeye kuiga.

Kumsomea hadithi

Mtoto hawezi kuthamini tu kile anachokiona bila kuona umaana wake katika maisha yake. Kuona mzazi anasoma kunaleta maana kama mtoto anaweza kuelewa thamani ya kinachosomwa. Ili kuleta maana ya vitabu, ni muhimu kujenga mazoea ya kumsomea mtoto  yale anayoyapenda tangu akiwa mdogo.
Baba akiwasomea wanae hadithi. PICHA: verywell.com

Kwa kawaida, watoto wadogo wanapenda sana hadithi zenye visa mbalimbali vinavyowakuza uelewa wao. Kwa hivyo, kuwasomea hadithi zinazowavutia kuliko kuwasimulia husaidia kutambua thamani ya vitabu kimaudhui.

Kwa mfano, yapo masimulizi mengi katika vitabu vitakatifu tunayoweza kutafuta vitabu vyake na kuwasomea watoto wetu. Mazoea ya kuwasomea hadithi, hata kwa dakika chache wakati wanapojiandaa kulala kila siku, mbali na kusaidia kujenga ukaribu na mtoto, yanamfanya mtoto ajenge shauku ya kujua kusoma mwenyewe ili aweze asome hadithi hizo yeye mwenyewe. Anapokua na tabia hii, haitakuwa kazi ngumu kuwa msomaji mzuri wa vitabu atakapokuwa mtu mzima.

Kumpa motisha anapojisomea

Kwa kufanya matatu tuliyoyaona, ni rahisi mtoto kuanza kuiga tabia ya kusoma. Mara anapoanza kuonesha kupenda vitabu, tunahitaji kumpa motisha ili kuiendeleza tabia hiyo. Kwa mfano, anapodai kusomewa hadithi jioni kwa mazoea yaliyoanza kujengeka, motisha ni kutimiza shauku hiyo kwa kumsomea pasipo kutoa visingizio vyovyote.

Ni kweli wakati mwingine tunarudi nyumbani tukiwa wenye uchovu wa kazi nyingi za siku. Lakini kusomea mtoto haihitaji dakika kumi. Watoto hasa wadogo hawawezi kuzingatia kitu kwa muda mrefu. Hatuna sababu ya kutumia visingizio vya uchovu wa mambo mengi kama sababu ya kushindwa kuwasomea watoto.

Kadhalika, badala ya kuwaletea watoto zawadi za pipi na vitu vingine vya kawaida, tunaweza pia kuwaletea vitabu vya hadithi wanazozipenda na kuwasomea. Tunapofanya hivyo, tangu wakiwa wadogo, tunawajengea hamasa ya kuwafanya wathamini vitabu kama wanavyothamini zawadi nyingine. Mazoea haya yanajenga tabia imara ya mtoto kupenda kujisomea.

Pamoja na changamoto za kujenga tabia hii tangu utotoni, bado tunaweza kabisa kuwajenga watoto kuwa wasomaji wazuri. Kilicho muhimu katika yote ni sisi wazazi kuona umuhimu wa kujisomea kwa kuwa mfano wa usomaji wa vitabu tuwapo nyumbani. 


Unaweza kusoma zaidi makala kama hizi kwenye safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti la Mtanzania kila Alhamisi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging